/1 Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo; Sisi tumepata 
kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa 
mikono yetu wenyewe. 
Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni 
juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. 
Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate 
kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. 
Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike. 
Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni 
mwanga na hamna giza lolote ndani yake. 
Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa 
tumesema uongo kwa maneno na matendo. 
Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa 
na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi 
zote. 
Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani 
yetu. 
Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye 
atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote. 
Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno 
lake halimo ndani yetu. 

/2 Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi; Lakini, 
ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye 
Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa. 
Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali 
pia dhambi za ulimwengu wote. 
Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua. 
Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, 
na ukweli haumo ndani yake. 
Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili 
wa Mungu ndani yake; Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana 
naye. 
Mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama 
alivyoishi Yesu Kristo. 
Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya 
zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo; Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe 
mliousikia. 
Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana 
ndani ya Kristo na ndani yenu pia; Maana giza linatoweka, na mwanga wa ukweli 
umekwisha anza kuangaza. 
Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu 
huyo bado yumo gizani. 
Yeyote ampendaye ndugu yake, yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake 
kiwezacho kumkwaza mtu mwingine. 
Lakini anayemchukia ndugu yake, yumo gizani; anatembea gizani, na hajui 
anakokwenda, maana giza limempofusha. 
Ninawaandikieni ninyi watoto, kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la 
Kristo. 
Nawaandikieni ninyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu 
mwanzo, Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu. 
Nawaandikieni ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba; Nawaandikieni ninyi kina 
baba, kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo; Nawaandikieni ninyi 
vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mmemshinda yule 
Mwovu. 
Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu; Mtu anayeupenda 
ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake. 
Vitu vyote vya ulimwengu-tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na 
kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali-vyote hivyo havitoki kwa Baba, 
bali vyatoka kwa ulimwengu. 
Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu 
atendaye atakalo Mungu, anaishi milele. 
Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba adui wa Kristo anakuja, na 
sasa adui wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u 
karibu. 
Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana 
walituacha; Kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi; Lakini waliondoka, 
wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu. 
Ninyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua 
ukweli. 
Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamuujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na 
pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli. 
Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha; Mtu wa namna hiyo ni 
adui wa Kristo, anamkana Baba na Mwana. 
Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali 
Mwana, anampata Baba pia. 
Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu; Kama ujumbe 
huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika 
umoja na Mwana na Baba. 
Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uzima wa milele. 
Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha ninyi. 
Lakini, kwa upande wenu ninyi, Kristo aliwamiminieni Roho wake; Na kama 
akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote; Maana Roho 
wake anawafundisheni kila kitu na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo; 
Basi shikeni mafundisho ya huy o Roho na kubaki katika muungano na Kristo.
Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila 
kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu Siku ya kuja kwake. 
Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila 
mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu. 

/3 Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na 
kweli, ndivyo tulivyo; Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui 
Mungu. 
Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi 
jinsi tutakavyokuwa; Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, 
tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. 
Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile 
Kristo alivyo safi kabisa. 
Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa 
sheria. 
Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna 
dhambi yoyote. 
Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu 
atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo. 
Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote; Mtu atendaye matendo 
maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. 
Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu 
mwanzo; Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi. 
Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani 
yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. 
Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si 
mtoto wa Mungu; Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto 
wa Ibilisi. 
Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana!. 
Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake; Na, 
kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu 
yake yalikuwa mema!. 
Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi. 
Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima 
kwa sababu tunawapenda ndugu zetu; Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. 
Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule 
hana uzima wa milele ndani yake. 
Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa 
ajili yetu; Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu 
zetu. 
Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, 
lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba 
anampenda Mungu?. 
Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa 
vitendo. 
Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na 
hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. 
Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu 
zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. 
Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na 
uthabiti mbele ya Mungu. 
Na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na 
kufanya yale yanayompendeza. 
Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama 
alivyotuamuru. 
Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi 
katika muungano naye; Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua 
kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi. 

/4 Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali 
chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, Maana 
manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. 
Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri 
kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu. 
Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu; 
Mtu huyo ana roho ambaye ni wa Adui wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba 
anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni!. 
Lakini ninyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa 
uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu zaidi kuliko roho aliye ndani ya 
hao walio wa ulimwengu. 
Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa 
ulimwengu. 
Lakini sisi ni wake Mungu; Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa 
Mungu hatusikilizi; Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho 
wa ukweli na roho wa uongo. 
Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu; Kila mtu aliye na 
upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. 
Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. 
Na Mungu alionyesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, 
ili tuwe na uzima kwa njia yake. 
Hivi ndivyo upendo ulivyo: si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, 
bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea 
dhambi zetu. 
Wapenzi wangu, ikiwa Mungu alitupenda hivyo, basi, nasi tunapaswa kupendana. 
Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana Mungu 
anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu. 
Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja 
nasi, kwani yeye ametupa Roho wake. 
Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa 
ulimwengu. 
Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika 
muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu. 
Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi; Mungu ni 
upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, 
na Mungu anaishi katika muungano naye. 
Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri Siku ile ya 
Hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo. 
Palipo na upendo hapana uoga; naam, upendo kamili hufukuza uoga wote; Basi, 
mtu mwenye uoga hajakamilika bado katika upendo, kwani uoga huhusikana na 
adhabu. 
Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. 
Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni 
mwongo; Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda 
Mungu ambaye hamwoni. 
Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda 
ndugu yake. 

/5 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ni Kristo, huyo ni mtoto wa Mungu; na, 
anayempenda mzazi humpenda pia mtoto wa huyo mzazi. 
Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu: Kwa kumpenda Mungu 
na kuzitii amri zake. 
Maana kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake; Na, amri zake si ngumu. 
Maana kila aliye mtoto wa Mungu anaweza kuushinda ulimwengu; Hivi ndivyo 
tunavyoushinda ulimwengu: kwa imani yetu. 
Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni 
Mwana wa Mungu. 
Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo 
chake; Hakuja kwa maji tu, bali kwa maji na kwa damu; Naye Roho anashuhudia 
kwamba ni kweli, kwani Roho ni ukweli. 
Basi, wako mashahidi watatu. 
Roho, maji na damu; na ushahidi wa hawa watatu waafikiana. 
Ikiwa twaukubali ushahidi wa binadamu, ushahidi wa Mungu una uzito zaidi; na 
huu ndio ushahidi alioutoa Mungu mwenyewe juu ya Mwanae. 
Anayemwamini mwana wa Mungu anao ushahidi huo ndani yake; lakini asiyemwamini 
Mungu, anamfanya yeye kuwa mwongo, maana hakuamini ushahidi alioutoa Mungu juu 
ya Mwanae. 
Na, ushahidi wenyewe ndio huu: Mungu alitupatia uzima wa milele, na uzima huo 
uko kwa Bwana. 
Yeyote, aliye na Mwana wa Mungu anao uzima huo; asiye na Mwana wa Mungu, hana 
uzima. 
Nawaandikieni mpate kujua kwamba mnao uzima wa milele ninyi mnaoamini kwa jina 
la Mwana wa Mungu. 
Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba 
chochote kadiri ya mapenzi yake, yeye hutusikiliza. 
Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye 
hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba atupatia yote tunayomwomba. 
Mtu akimwona ndugu yake ametenda dhambi isiyompeleka kwenye kifo anapaswa 
kumwombea kwa Mungu, naye Mungu atampatia uzima; Nasema jambo hili kuhusu wale 
waliotenda dhambi ambazo si za kifo; Lakini ipo dhambi yenye kumpeleka mtu 
kwenye kifo nami sisemi kwa mba mnapaswa kumwomba Mungu kwa ajili ya hiyo.
Kila tendo lisilo adilifu ni dhambi, lakini kuna dhambi isiyompeleka mtu 
kwenye kifo. 
Tunajua kwamba kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, kwa sababu Mwana wa 
Mungu humlinda salama, na yule Mwovu hawezi kumdhuru. 
Tunajua kwamba sisi ni wake Mungu ingawa ulimwengu wote unatawaliwa na yule 
Mwovu. 
Twajua pia kwamba Mwana wa Mungu amekuja, akatupa elimu ili tumjue Mungu wa 
kweli; tuishi katika muungano na Mungu wa kweli, katika muungano na Mwanae, 
Yesu Kristo; Huyu ndiye Mungu wa kweli, na huu ndio uzima wa milele. 
Watoto wangu, epukaneni na sanamu za miungu.