The Old Testament of the Holy Bible

Mwanzo 1

1 Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. 3 Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. 4 Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. 6 Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. 7 Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. 8 Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. 9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. 10 Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 11 Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo. 12 Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 13 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. 14 Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka; 15 tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. 17 Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi 18 na kuutawala mchana na usiku na kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 19 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. 20 Mungu akasema, Maji na yajawe kwa wingi na kitu kiendacho chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga la mbingu. 21 Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa wingi kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 22 Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkayajaze maji ya baharini, ndege na wazidi katika nchi. 23 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. 24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, nacho kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. 28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. 29 Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; 30 na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche, ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. 31 Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.

Mwanzo 2

1 Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. 2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. 3 Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. 4 Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi 5 hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi; 6 ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi. 7 Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. 8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya. 9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. 10 Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne. 11 Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; 12 na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham. 13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. 14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati. 15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. 16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. 18 Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. 19 Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake. 20 Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye. 21 Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, 22 na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu. 23 Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume. 24 Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. 25 Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.

Mwanzo 3

1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. 4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. 6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. 7 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. 8 Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. 9 Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? 10 Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. 11 Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? 12 Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. 13 Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. 14 Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; 15 nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. 16 Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. 17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; 18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; 19 kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. 20 Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. 21 Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. 22 Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; 23 kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. 24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

Mwanzo 4

1 Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. 2 Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. 3 Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. 4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. 6 Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? 7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. 8 Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. 9 Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? 10 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. 11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; 12 utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. 13 Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. 14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. 15 Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. 16 Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni. 17 Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe. 18 Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki. 19 Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila. 20 Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. 21 Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. 22 Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama. 23 Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua; 24 Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba. 25 Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua. 26 Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.

Mwanzo 5

1 Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya; 2 mwanamume na mwanamke aliwaumba, akawabariki akawaita jina lao Adamu, siku ile walipoumbwa. 3 Adamu akaishi miaka mia na thelathini, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita jina lake Sethi. 4 Siku za Adamu baada ya kumzaa Sethi zilikuwa miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake. 5 Siku zote za Adamu alizoishi ni miaka mia kenda na thelathini, naye akafa. 6 Sethi akaishi miaka mia na mitano, akamzaa Enoshi. 7 Sethi akaishi baada ya kumzaa Enoshi miaka mia nane na saba, akazaa wana, waume na wake. 8 Siku zote za Sethi ni miaka mia kenda na kumi na miwili, akafa. 9 Enoshi akaishi miaka tisini, akamzaa Kenani. 10 Enoshi akaishi baada ya kumzaa Kenani miaka mia nane na kumi na mitano, akazaa wana, waume na wake. 11 Siku zote za Enoshi ni miaka mia kenda na mitano, akafa. 12 Kenani akaishi miaka sabini, akamzaa Mahalaleli. 13 Kenani akaishi baada ya kumzaa Mahalaleli miaka mia nane na arobaini, akazaa wana, waume na wake. 14 Siku zote za Kenani ni miaka mia kenda na kumi, akafa. 15 Mahalaleli akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Yaredi. 16 Mahalaleli akaishi baada ya kumzaa Yaredi miaka mia nane na thelathini, akazaa wana, waume na wake. 17 Siku zote za Mahalaleli ni miaka mia nane na tisini na mitano, akafa. 18 Yaredi akaishi miaka mia na sitini na miwili, akamzaa Henoko. 19 Yaredi akaishi baada ya kumzaa Henoko miaka mia nane, akazaa wana, waume na wake. 20 Siku zote za Yaredi ni miaka mia kenda na sitini na miwili, akafa. 21 Henoko akaishi miaka sitini na mitano, akamzaa Methusela. 22 Henoko akaenda pamoja na Mungu baada ya kumzaa Methusela miaka mia tatu, akazaa wana, waume na wake. 23 Siku zote za Henoko ni miaka mia tatu na sitini na mitano. 24 Henoko akaenda pamoja na Mungu, naye akatoweka, maana Mungu alimtwaa. 25 Methusela akaishi miaka mia na themanini na saba, akamzaa Lameki. 26 Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na miwili, akazaa wana, waume na wake. 27 Siku zote za Methusela ni miaka mia kenda na sitini na kenda, akafa. 28 Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana. 29 Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani Bwana. 30 Lameki akaishi baada ya kumzaa Nuhu miaka mia na tisini na mitano, akazaa wana, waume na wake. 31 Siku zote za Lameki ni miaka mia saba na sabini na saba, akafa. 32 Nuhu alikuwa mwenye miaka mia tano, Nuhu akawazaa Shemu, na Hamu, na Yafethi.

Mwanzo 6

1 Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, 2 wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. 3 Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. 4 Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile;tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana;hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani ,watu wenye sifa. 5 Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. 6 Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. 7 Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. 8 Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana. 9 Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu. 10 Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu, na Hamu, na Yafethi. 11 Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma. 12 Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mwenye mwili amejiharibia njia yake duniani. 13 Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia. 14 Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami. 15 Hivi ndivyo utakavyoifanya; mikono mia tatu urefu wa safina, mikono hamsini upana wake, na mikono thelathini kwenda juu kwake. 16 Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu. 17 Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa. 18 Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe. 19 Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke. 20 Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi. 21 Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao. 22 Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.

Mwanzo 7

1 Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. 2 Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke. 3 Tena katika ndege wa angani saba saba, mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. 4 Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilicho hai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. 5 Nuhu akafanya kama vile Bwana alivyomwamuru. 6 Naye Nuhu alikuwa mtu wa miaka mia sita hapo hiyo gharika ya maji ilipokuwa juu ya nchi. 7 Nuhu akaingia katika safina, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; kwa sababu ya maji ya gharika. 8 Na katika wanyama walio safi, na wanyama wasio safi, na ndege, navyo vyote vitambaavyo juu ya nchi, 9 wakaingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, mume na mke, kama vile Mungu alivyomwamuru Nuhu. 10 Ikawa baada ya siku hizo saba, maji ya gharika yakawa juu ya nchi. 11 Katika mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, mwezi wa pili, siku ya kumi na saba ya mwezi, siku ile chemchemi zote za vilindi vikuu zilibubujika kwa nguvu, madirisha ya mbinguni yakafunguka. 12 Mvua ikanyesha juu ya nchi, siku arobaini mchana na usiku. 13 Siku ile ile Nuhu akaingia katika safina, yeye, na Shemu na Hamu na Yafethi, wana wa Nuhu, na mkewe Nuhu, na wake watatu wa wanawe pamoja naye; 14 wao na kila mnyama wa mwitu kwa jinsi yake, na kila mnyama wa kufugwa kwa jinsi yake, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi, kwa jinsi yake, na kirukacho kwa jinsi yake, kila ndege wa namna yo yote. 15 Waliingia katika safina alimo Nuhu, wawili wawili, wa kila chenye mwili kilicho na pumzi ya uhai ndani yake. 16 Na walioingia, waliingia mume na mke, wa kila kitu chenye mwili, kama vile alivyomwamuru Mungu; Bwana akamfungia. 17 Ile gharika ilikuwako juu ya nchi siku arobaini; nayo maji yakazidi, yakaieleza safina, ikaelea juu ya nchi. 18 Maji yakapata nguvu, yakazidi sana juu ya nchi; na ile safina ikaelea juu ya uso wa maji. 19 Maji yakapata nguvu sana sana juu ya nchi; na milima mirefu yote iliyokuwako chini ya mbingu ikafunikizwa. 20 Maji yakapata nguvu, hata ikafunikwa milima kiasi cha mikono kumi na mitano. 21 Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu; 22 kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. 23 Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina. 24 Maji yakapata nguvu juu ya nchi siku mia na hamsini.

Mwanzo 8

1 Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua; 2 chemchemi za vilindi zikafungwa, pia na madirisha ya mbinguni, mvua kutoka mbinguni ikazuiliwa; 3 maji yakadumu kuondoka katika nchi; na mwisho wa siku mia na hamsini maji yakapunguka. 4 Mwezi wa saba, siku ya kumi na saba ya mwezi, safina ikatua juu ya milima ya Ararati. 5 Maji yakapunguka-punguka hata mwezi wa kumi; mwezi huo wa kumi, siku ya kwanza ya mwezi, vilele vya milima vikaonekana. 6 Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; 7 akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. 8 Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; 9 bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. 10 Akangoja na siku saba tena; kisha akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, 11 njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. 12 Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. 13 Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. 14 Na mwezi wa pili, siku ya ishirini na saba ya mwezi, nchi ilikuwa kavu. 15 Mungu akamwambia Nuhu, akisema, 16 Toka katika safina, wewe, na mkeo, na wanao, na wake za wanao pamoja nawe. 17 Utoe pamoja nawe kila kilicho hai kilichomo pamoja nawe, chenye mwili, ndege, na mnyama, na kila kitambaacho, chenye kutambaa juu ya nchi; wajae katika nchi, wawe na uzazi, wakaongezeke katika nchi. 18 Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye; 19 kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina. 20 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. 22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

Mwanzo 9

1 Mungu akambariki Nuhu na wanawe, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi. 2 Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani: pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. 3 Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote. 4 Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. 5 Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. 6 Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu. 7 Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake. 8 Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, 9 Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; 10 tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. 11 Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. 12 Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; 13 Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. 14 Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, 15 nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili. 16 Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi. 17 Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi. 18 Wana wa Nuhu waliotoka katika safina, ni Shemu, na Hamu, na Yafethi; na Hamu ndiye baba wa Kanaani. 19 Hawa watatu walikuwa wana wa Nuhu na kwa hao nchi yote ikaenea watu. 20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; 21 akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake. 22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake, akawaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23 Shemu na Yafethi wakatwaa vazi, wakalitanda mabegani mwao wote wawili, wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao; na nyuso zao zilielekea nyuma, wala hawakuuona uchi wa baba yao. 24 Nuhu akalevuka katika ulevi wake, akajua mwana wake mdogo alivyomtendea. 25 Akasema,Na alaaniwe Kaanani;Atakuwa mtumwa kabisa kwa ndugu zake. 26 Akasema,Na atukuzwe Bwana,Mungu wa Shemu;Na kaanani awe mtumwa wake. 27 Mungu akamnafisishe Yafethi,Na akae katika hema za Shemu; Na kaanani awe mtumwa wake. 28 Na Nuhu akaishi baada ya ile gharika miaka mia tatu na hamsini. 29 Siku zote za Nuhu zilikuwa miaka mia kenda na hamsini, akafa.

Mwanzo 10

1 Hivi ndivyo vizazi vya wana wa Nuhu, Shemu, na Hamu, na Yafethi. Na kwao walizaliwa wana wa kiume baada ya gharika. 2 Wana wa Yafethi ni Gomeri, na Magogu, na Madai, na Yavani, na Tubali, na Mesheki, na Tirasi. 3 Na wana wa Gomeri ni Ashkenazi, na Rifathi, na Togama. 4 Na wana wa Yavani ni Elisha, Tarshishi, Kitimu, na Warodani. 5 Kwa hao nchi za pwani za mataifa ziligawanyikana kuwa nchi zao, kila moja kwa lugha yake, kwa jamaa zao, kufuata mataifa yao. 6 Na wana wa Hamu ni Kushi, na Misri, na Putu, na Kanaani. 7 Na wana wa Kushi ni Seba, na Havila, na Sabta, na Raama, na Sabteka. Na wana wa Raama ni Sheba, na Dedani. 8 Kushi akamzaa Nimrodi, akaanza kuwa mtu hodari katika nchi. 9 Alikuwa hodari kuwinda wanyama mbele za Bwana. Kwa hiyo watu hunena, Kama Nimrodi, hodari wa kuwinda wanyama mbele za Bwana. 10 Mwanzo wa ufalme wake ulikuwa Babeli na Ereku, na Akadi, na Kalne, katika nchi ya Shinari. 11 Akatoka katika nchi ile akaenda mpaka Ashuru, akajenga Ninawi, na Rehoboth-iri, na Kala; 12 na Reseni, kati ya Ninawi na Kala, nao ni mji mkubwa. 13 Misri akazaa Waludi, na Waanami, na Walehabi, na Wanaftuhi, 14 na Wapathrusi, na Wakasluhi; huko ndiko walikotoka Wafilisti na Wakaftori. 15 Kanaani akamzaa Sidoni, mwanawe wa kwanza, na Hethi, 16 na Myebusi, na Mwamori, na Mgirgashi, 17 na Mhivi, na Mwarki, na Msini, 18 na Mwarvadi, na Msemari, na Mhamathi. Baadaye jamaa za Wakanaani walitawanyikana. 19 Na mpaka wa Wakanaani ulianza kutoka Sidoni kwa njia ya Gerari hata Gaza; tena kwa njia ya Sodoma, na Gomora, na Adma, na Seboimu, hata Lasha. 20 Hao ndio wana wa Hamu, kufuata jamaa zao, kwa lugha zao, katika nchi zao, kufuata mataifa yao. 21 Naye Shemu ambaye ni baba wa wana wote wa Eberi, na ndugu mkubwa wa Yafethi, akazaliwa wana. 22 Wana wa Shemu ni Elamu, na Ashuru, na Arfaksadi, na Ludi, na Aramu. 23 Na wana wa Aramu ni Usi, na Huli, na Getheri, na Mashi. 24 Arfaksadi akamzaa Sela, Sela akamzaa Eberi. 25 Eberi akazaliwa wana wawili wa kiume; jina la wa kwanza ni Pelegi maana katika siku zake nchi iligawanyika; na jina la nduguye ni Yoktani. 26 Yoktani akamzaa Almodadi, na Shelefu, na Hasarmawethi, na Yera, 27 na Hadoramu, na Uzali, na Dikla, 28 na Obali, na Abimaeli, na Seba, 29 na Ofiri, na Havila, na Yobabi. Hao wote ndio wana wa Yoktani. 30 Makao yao yalikuwa kutoka Mesha kwa njia ya Sefari, mlima wa mashariki. 31 Hao ndio wana wa Shemu, kufuata jamaa zao, na lugha zao, katika nchi zao, kufuata mataifa yao. 32 Hizo ndizo jamaa za wana wa Nuhu, kufuata vizazi vyao, katika mataifa yao; na kwa hao mataifa yaligawanyika katika nchi baada ya gharika.

Mwanzo 11

1 Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. 2 Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. 3 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. 4 Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. 5 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. 6 Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. 7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. 8 Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. 9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote. 10 Hivi ndivyo vizazi vya Shemu; Shemu alikuwa mtu wa miaka mia akamzaa Arfaksadi miaka miwili baada ya gharika. 11 Shemu akaishi baada ya kumzaa Arfaksadi miaka mia tano, akazaa wana, waume na wake. 12 Arfaksadi akaishi miaka thelathini na mitano, akamzaa Sela. 13 Arfaksadi akaishi baada ya kumzaa Sela miaka mia nne na mitatu, akazaa wana, waume na wake. 14 Sela akaishi miaka thelathini, akamzaa Eberi. 15 Sela akaishi baada ya kumzaa Eberi miaka mia nne na mitatu, akazaa wana, waume na wake. 16 Eberi akaishi miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi. 17 Eberi akaishi baada ya kumzaa Pelegi miaka mia nne na thelathini, akazaa wana, waume na wake. 18 Pelegi akaishi miaka thelathini, akamzaa Reu. 19 Pelegi akaishi baada ya kumzaa Reu miaka mia mbili na kenda, akazaa wana, waume na wake. 20 Reu akaishi miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi. 21 Reu akaishi baada ya kumzaa Serugi miaka mia mbili na saba, akazaa wana, waume na wake. 22 Serugi akaishi miaka thelathini, akamzaa Nahori. 23 Serugi akaishi baada ya kumzaa Nahori miaka mia mbili, akazaa wana, waume na wake. 24 Nahori akaishi miaka ishirini na kenda, akamzaa Tera. 25 Nahori akaishi baada ya kumzaa Tera miaka mia na kumi na kenda, akazaa wana, waume na wake. 26 Tera akaishi miaka sabini, akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani. 27 Na hivi ndivyo vizazi vya Tera. Tera akamzaa Abramu, na Nahori, na Harani. Harani akamzaa Lutu. 28 Harani akafa kabla ya baba yake Tera katika nchi aliyozaliwa, yaani, katika Uru wa Wakaldayo. 29 Abramu na Nahori wakajitwalia wake. Jina la mkewe Abramu aliitwa Sarai, na jina la mkewe Nahori aliitwa Milka, binti Harani, ambaye alikuwa baba wa Milka na wa Iska. 30 Na Sarai alikuwa tasa, hakuwa na mtoto. 31 Tera akamtwaa Abramu mwanawe, na Lutu mwana wa Harani, mwana wa mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka wote katika Uru wa Wakaldayo, waende nchi ya Kanaani, wakafika mpaka Harani wakakaa huko. 32 Siku za Tera zilikuwa miaka mia mbili na mitano; Tera akafa katika Harani.

Mwanzo 12

1 Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; 2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; 3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa. 4 Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani. 5 Abramu akamchukua Sarai mkewe, na Lutu mwana wa nduguye, na vitu vyao vyote walivyokuwa wamejipatia na hao watu waliowapata huko Harani, wakatoka ili kwenda nchi ya Kanaani; nao wakaingia katika nchi ya Kanaani. 6 Abramu akapita katikati ya nchi mpaka mahali patakatifu pa Shekemu; mpaka mwaloni wa More. Na Wakanaani siku zile walikaa katika nchi hiyo. 7 Bwana akamtokea Abramu, akasema, Uzao wako nitawapa nchi hii. Naye huko akamjengea madhabahu Bwana aliyemtokea. 8 Kisha akaondoka huko akaenda mpaka mlima ulio upande wa mashariki wa Betheli, akaipiga hema yake; alikuwa na Betheli upande wa magharibi, na Ai upande wa mashariki, akamjengea Bwana madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. 9 Naye Abramu akasafiri, akazidi kwenda pande za kusini. 10 Basi kulikuwa njaa katika nchi ile; Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi. 11 Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; 12 basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. 13 Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. 14 Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. 15 Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao. 16 Naye akamtendea Abramu mema kwa ajili yake; naye alikuwa na kondoo na ng'ombe, na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia. 17 Lakini Bwana akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu. 18 Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? 19 Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. 20 Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.

Mwanzo 13

1 Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini. 2 Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu. 3 Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai; 4 napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la Bwana hapo. 5 Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng'ombe na kondoo, na hema. 6 Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. 7 Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi. 8 Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. 9 Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto. 10 Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. 11 Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. 12 Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma. 13 Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya Bwana. 14 Bwana akamwambia Abramu, alipokwisha kutengana na Lutu, Inua sasa macho yako, ukatazame kutoka hapo ulipo, upande wa kaskazini, na wa kusini na wa mashariki na wa magharibi; 15 maana nchi hii yote uionayo, nitakupa wewe na uzao wako hata milele. 16 Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako nao utahesabika. 17 Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo. 18 Basi Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea Bwana madhabahu huko.

Mwanzo 14

1 Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, 2 walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. 3 Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. 4 Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. 5 Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, 6 na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. 7 Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. 8 Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; 9 wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. 10 Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. 11 Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. 12 Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. 13 Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. 14 Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. 15 Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. 16 Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. 17 Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. 18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. 19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. 20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote. 21 Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. 22 Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi, 23 ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu; 24 isipokuwa hivyo walivyokula vijana, na sehemu za watu waliokwenda nami, yaani, Aneri, na Eshkoli, na Mamre; na watwae wao sehemu zao.

Mwanzo 15

1 Baada ya mambo hayo neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. 2 Abramu akasema, Ee Bwana MUNGU, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? 3 Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. 4 Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. 5 Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. 6 Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. 7 Kisha akamwambia, Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi. 8 Akasema, Ee Bwana MUNGU, nipateje kujua ya kwamba nitairithi? 9 Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. 10 Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. 11 Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. 12 Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. 13 Bwana akamwambia Abramu, Ujue hakika ya kwamba uzao wako utakuwa mgeni katika nchi isiyo yake, watawatumikia watu wale, nao watateswa muda wa miaka mia nne. 14 Hata na taifa lile, watakaowatumikia, nitawahukumu; baadaye watatoka na mali mengi. 15 Lakini wewe utakwenda kwa baba zako kwa amani, utazikwa katika uzee mwema. 16 Na kizazi cha nne kitarudi hapa, maana haujatimia uovu wa Waamori bado. 17 Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. 18 Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati, 19 Mkeni, na Mkenizi, na Mkadmoni, 20 na Mhiti, na Mperizi, na Mrefai, 21 na Mwamori, na Mkanaani, na Mgirgashi, na Myebusi.

Mwanzo 16

1 Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. 2 Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, Bwana amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. 3 Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. 4 Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake. 5 Sarai akamwambia Abramu, Ubaya ulionipata na uwe juu yako; nimekupa mjakazi wangu kifuani mwako, naye alipoona kwamba amepata mimba, mimi nimekuwa duni machoni pake. Bwana na ahukumu kati ya mimi na wewe. 6 Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. 7 Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. 8 Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. 9 Malaika wa Bwana akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. 10 Malaika wa Bwana akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. 11 Malaika wa Bwana akamwambia, Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Ishmaeli, maana Bwana amesikia kilio cha mateso yako. 12 Naye atakuwa kama punda-mwitu kati ya watu, mkono wake utakuwa juu ya watu wote na mkono wa watu wote utakuwa juu yake, naye atakaa mbele yao ndugu zake wote. 13 Akaliita jina la Bwana aliyesema naye, Wewe U Mungu uonaye, kwani alisema, Hata hapa nimemwona yeye anionaye? 14 Kwa hiyo kisima kile kiliitwa Beer-lahai-roi.Tazama,kiko kati ya kadeshi na beredi. 15 Hajiri akamzalia Abramu mwana wa kiume; Abramu akamwita jina lake Ishmaeli, yule mwanawe, ambaye Hajiri alimzaa. 16 Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka themanini na sita, hapo Hajiri alipomzalia Abramu Ishmaeli.

Mwanzo 17

1 Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. 2 Nami nitafanya agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. 3 Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, 4 Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, 5 wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. 6 Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. 7 Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako. 8 Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao. 9 Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako. 10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. 11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi. 12 Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako. 13 Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele. 14 Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu. 15 Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. 16 Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake. 17 Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? 18 Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako. 19 Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. 20 Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu. 21 Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao. 22 Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu. 23 Ibrahimu akamtwaa Ishmaeli mwanawe, na wote waliozaliwa nyumbani mwake, na wote walionunuliwa kwa fedha yake, wanaume wote wa watu wa nyumba ya Ibrahimu, akawatahiri nyama ya magovi yao siku ile ile, kama Mungu alivyomwambia. 24 Naye Ibrahimu alikuwa mwenye umri wa miaka tisini na kenda alipotahiriwa nyama ya govi lake. 25 Na Ishmaeli mwanawe alikuwa mtu wa miaka kumi na mitatu, alipotahiriwa nyama ya govi lake. 26 Siku ile ile akatahiriwa Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe. 27 Na watu wote wa nyumba yake, wazaliwa nyumbani, na wanunuliwa kwa fedha katika mkono wa mgeni, wakatahiriwa pamoja naye.

Mwanzo 18

1 Bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. 2 Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, 3 akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. 4 Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. 5 Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. 6 Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. 7 Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. 8 Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. 9 Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. 10 Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. 11 Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? 13 Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? 14 Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. 15 Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka. 16 Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. 17 Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, 18 akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? 19 Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. 20 Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, 21 basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. 22 Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. 23 Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? 24 Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? 25 Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? 26 Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. 27 Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. 28 Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. 29 Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. 30 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. 31 Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. 32 Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. 33 Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.

Mwanzo 19

1 Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. 2 Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha. 3 Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala. 4 Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote. 5 Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua. 6 Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake. 7 Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi. 8 Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu. 9 Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, anataka kuhukumu! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango. 10 Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango. 11 Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango. 12 Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; 13 maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za Bwana; naye Bwana ametupeleka tupaharibu. 14 Lutu akatoka akasema na wakweze, waliowaposa binti zake, akasema, Ondokeni mtoke katika mahali hapa kwa sababu Bwana atauharibu mji huu. Lakini akawa kama achezaye machoni pa wakweze. 15 Hata alfajiri ndipo malaika wakamhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. 16 Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi Bwana alivyomhurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. 17 Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. 18 Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu! 19 Tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. 20 Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. 21 Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. 22 Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. 23 Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. 24 Ndipo Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa Bwana. 25 Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waliokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. 26 Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. 27 Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za Bwana, 28 naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru. 29 Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu. 30 Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili. 31 Yule mkubwa akamwambia mdogo, Baba yetu ni mzee, wala hakuna mtu mume katika nchi atuingilie kama ilivyo desturi ya dunia yote. 32 Haya, na tumnyweshe baba yetu mvinyo, tukalale naye, ili tumhifadhie baba yetu uzao. 33 Wakamnywesha baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka huyo mkubwa akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. 34 Ikawa siku ya pili, mkubwa akamwambia mdogo, Tazama, nimelala jana na baba yangu, tumnyweshe mvinyo tena usiku huu, ukaingie ukalale naye. 35 Wakamnywesha tena baba yao mvinyo usiku ule, akaondoka mdogo akalala naye, wala yeye hana habari alipolala wala alipoondoka. 36 Basi hao binti wote wawili wa Lutu wakapata mimba kwa baba yao. 37 Yule mkubwa akazaa mwana, akamwita jina lake Moabu; huyo ndiye baba wa Wamoabi, hata leo. 38 Na yule mdogo naye akazaa mwana akamwita jina lake Benami; huyo ndiye baba wa Waamoni hata leo.

Mwanzo 20

1 Ibrahimu akaondoka huko kwenda nchi ya kusini, akakaa kati ya Kadeshi na Shuri, naye akatembea katika Gerari. 2 Ibrahimu akamnena Sara mkewe, Huyu ni ndugu yangu. Basi Abimeleki mfalme wa Gerari akapeleka watu akamtwaa Sara. 3 Lakini Mungu akamjia Abimeleki katika ndoto ya usiku, akamwambia, Umekuwa mfu wewe kwa sababu ya mwanamke huyu uliyemtwaa, maana ni mkewe mtu. 4 Basi Abimeleki alikuwa hakumkaribia, akasema, Ee Bwana, Je! Utaua hata taifa lenye haki? 5 Je! Hakuniambia mwenyewe, Huyu ni ndugu yangu? Na mwanamke mwenyewe naye alisema, Huyu ni ndugu yangu. Kwa ukamilifu wa moyo wangu, na kwa kuwa safi mikono yangu, nimefanya hivi. 6 Mungu akamwambia katika ndoto, Nami nimejua ya kwamba kwa ukamilifu wa moyo wako umefanya hivi, ndipo nami nikakuzuia usinitendee dhambi, kwa hiyo sikukuacha umguse. 7 Basi sasa umrudishe mwanamke kwa mtu huyo, maana yeye ni nabii, naye atakuombea, upate kuishi. Bali usipomrudisha, fahamu ya kwamba kwa hakika utakufa wewe na watu wote ulio nao. 8 Abimeleki akaamka asubuhi na mapema, akawaita watumwa wake wote, akawaambia maneno hayo yote masikioni mwao, nao watu hao wakaogopa sana. 9 Kisha Abimeleki akamwita Ibrahimu, akamwambia, Umetutenda nini? Nimekukosa nini, hata ukaleta juu yangu na juu ya ufalme wangu dhambi kuu? Umenitenda matendo yasiyotendeka. 10 Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Umeona nini hata ukatenda jambo hili? 11 Ibrahimu akasema, Kwa sababu naliona, Yakini hapana hofu ya Mungu mahali hapa, nao wataniua kwa ajili ya mke wangu. 12 Naye kweli ni ndugu yangu, binti wa baba yangu ila siye mwana wa mama yangu, ndipo akawa mke wangu. 13 Ikawa hapo Mungu aliponisafirisha kutoka nyumba ya baba yangu, nikamwambia, Hii ndiyo fadhili yako, utakayonifanyia. Kila mahali tuingiapo, useme, Huyu ni ndugu yangu. 14 Basi Abimeleki akatwaa kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi, akampa Ibrahimu, akamrudishia Sara mkewe. 15 Abimeleki akasema, Nchi yangu iko mbele yako, kaa upendapo. 16 Naye akamwambia Sara, Tazama! Nimempa ndugu yako fedha elfu, itakuwa kifunika macho kwako mbele ya wote walio pamoja nawe, nawe utakuwa na haki mbele ya watu wote. 17 Ibrahimu akamwomba Mungu, Mungu akamponya Abimeleki, na mkewe, na wajakazi wake, nao wakazaa wana. 18 Maana Bwana alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.

Mwanzo 21

1 Bwana akamjia Sara kama alivyonena, na Bwana akamfanyia kama alivyosema. 2 Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. 3 Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. 4 Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru. 5 Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. 6 Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami. 7 Akasema, N'nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake. 8 Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. 9 Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. 10 Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. 11 Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. 12 Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. 13 Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. 14 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. 15 Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. 16 Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia. 17 Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. 18 Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. 19 Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. 20 Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde. 21 Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri. 22 Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda. 23 Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake. 24 Ibrahimu akasema, Nitaapa. 25 Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang'anya. 26 Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu. 27 Ibrahimu akatwaa kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano. 28 Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao. 29 Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini? 30 Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki. 31 Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili. 32 Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti. 33 Ibrahimu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la Bwana Mungu wa milele. 34 Ibrahimu akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.

Mwanzo 22

1 Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. 3 Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. 4 Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. 5 Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena. 6 Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja. 7 Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? 8 Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja. 9 Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe. 11 Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. 12 Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. 13 Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana. 15 Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni 16 akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, 17 katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; 18 na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. 19 Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba. 20 Ikawa baada ya mambo hayo, Ibrahimu akaambiwa ya kwamba, Tazama, Milka naye amemzalia Nahori ndugu yako wana; 21 Usi, mzaliwa wa kwanza wake, na Buzi nduguye, na Kemueli, baba wa Aramu; 22 na Kesedi, na Hazo, na Pildashi, na Yidlafu, na Bethueli. 23 Bethueli akamzaa Rebeka; hao wanane Milka alimzalia Nahori ndugu wa Ibrahimu. 24 Na suria wake Reuma naye alizaa Teba na Gahamu na Tahashi na Maaka.

Mwanzo 23

1 Basi umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba ndio umri wake Sara. 2 Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. 3 Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na wazawa wa Hethi, akinena, 4 Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. 5 Wazawa wa Hethi wakamjibu Ibrahimu, wakamwambia, 6 Utusikie, Ee bwana, ndiwe mtu mkuu sana kwetu, uzike maiti wako katika kaburi lile utakalochagua katika makaburi yetu. Hapana mtu kwetu atakayekuzuilia kaburi lake, usizike maiti wako. 7 Ibrahimu akaondoka, akainama mbele ya watu wa nchi, mbele ya hao wazawa wa Hethi. 8 Naye akazungumza nao, akisema, Ikiwa nia yenu nimzike maiti wangu atoke mbele yangu, mnisikie, mkaniombee kwa Efroni bin Sohari, 9 ili kwamba anipe pango ya Makpela, iliyo katika mpaka wa shamba lake, na anipe kwa kima kilicho kamili, katikati yenu, iwe milki yangu ya kuzikia. 10 Basi Efroni alikuwa akiketi kati ya wazawa wa Hethi. Efroni Mhiti akamjibu Ibrahimu, na wazawa wa Hethi wanasikiliza, hata watu wote waingiao mlango wa mji wake, akisema, 11 Sivyo, bwana wangu, unisikilize. Lile shamba nakupa, na pango iliyomo nakupa; mbele ya wana wa watu wangu nakupa, uzike maiti wako. 12 Ibrahimu akainama mbele ya watu wa nchi. 13 Akamwambia Efroni, na watu wa nchi wanasikiliza, akisema, Tafadhali unisikilize; nitatoa kima cha shamba, nawe ukipokee kwangu, nami nitamzika humo maiti wangu. 14 Efroni akamjibu Ibrahimu, akamwambia, 15 Bwana wangu, unisikilize. Sehemu ya nchi, ambayo thamani yake ni shekeli za fedha mia nne, n'nini hii baina yako na yangu? Basi uzike maiti wako. 16 Ibrahimu akakubali maneno ya Efroni. Ibrahimu akampimia Efroni ile fedha aliyotaja masikioni mwa wazawa wa Hethi, shekeli za fedha mia nne za namna inayotumika na wenye biashara. 17 Basi shamba la Efroni lililokuwa katika Makpela kuelekea Mamre, shamba, na pango iliyokuwamo, na miti yote iliyokuwamo shambani, iliyokuwa katika mipaka yake pande zote, vyote viliyakinishwa 18 kuwa mali yake Ibrahimu, mbele ya wazawa wa Hethi, mbele ya watu wote waingiao katika mlango wa mji wake. 19 Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. 20 Na lile shamba, na pango iliyomo, iliyakinishwa kuwa mali yake Ibrahimu na wazawa wa Hethi, kuwa mahali pa kuzikia.

Mwanzo 24

1 Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. 2 Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, 3 nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; 4 bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. 5 Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? 6 Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. 7 Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; 8 na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. 9 Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo. 10 Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. 11 Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. 12 Naye akasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. 13 Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, 14 basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. 15 Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. 16 Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. 17 Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. 18 Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. 19 Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. 20 Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. 21 Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba Bwana ameifanikisha safari yake ama sivyo. 22 Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, 23 akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? 24 Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. 25 Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. 26 Yule mtu akainama akamsujudu Bwana. 27 Akasema, Na atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. Bwana akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu. 28 Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo. 29 Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani. 30 Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani. 31 Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na Bwana, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. 32 Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye. 33 Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema. 34 Akasema, Mimi ni mtumwa wa Ibrahimu, 35 na Bwana amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng'ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda. 36 Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo. 37 Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao. 38 Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke. 39 Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami. 40 Akaniambia, Bwana, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu. 41 Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu. 42 Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi, 43 tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe, 44 naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke Bwana aliyemwekea mwana wa bwana wangu. 45 Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe. 46 Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao. 47 Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake. 48 Nikainama, nikamsujudia Bwana, nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake. 49 Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto. 50 Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa Bwana, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya. 51 Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema Bwana. 52 Ikawa mtumishi wa Ibrahimu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za Bwana. 53 Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia. 54 Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. 55 Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende. 56 Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi Bwana amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu. 57 Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe. 58 Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda. 59 Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake. 60 Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao. 61 Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake. 62 Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini. 63 Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. 64 Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. 65 Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. 66 Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. 67 Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.

Mwanzo 25

1 Ibrahimu alioa mke mwingine jina lake akiitwa Ketura. 2 Akamzalia Zimrani, na Yokshani, na Medani, na Midiani, na Ishbaki, na Sua. 3 Yokshani akamzaa Sheba, na Dedani; na wana wa Dedani walikuwa Waashuri na Waletushi, na Waleumi. 4 Na wana wa Midiani walikuwa, Efa, na Eferi, na Hanoki, na Abida, na Eldaa. Hao wote walikuwa ni wana wa Ketura. 5 Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. 6 Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. 7 Hizi ndizo siku za miaka ya maisha ya Ibrahimu alizoishi, miaka mia, na sabini na mitano. 8 Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake. 9 Isaka na Ishmaeli wanawe wakamzika katika pango ya Makpela, katika shamba la Efroni bin Sohari Mhiti, lielekealo Mamre. 10 Katika lile shamba alilolinunua Ibrahimu kwa wazawa Hethi, huko ndiko alikozikwa Ibrahimu na Sara mkewe. 11 Ikawa, baada ya kufa kwake Ibrahimu, Mungu akambariki Isaka mwanawe. Naye Isaka akakaa karibu ya Beer-lahai-roi. 12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli, mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri, Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu. 13 Na haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, kwa majina yao, na kwa vizazi vyao. Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli, ni Nebayothi, na Kedari, na Abdeeli, na Mibsamu, 14 na Mishma, na Duma, na Masa, 15 na Hadadi, na Tema, na Yeturi, na Nafishi, na Kedema. 16 Hao ndio wana wa Ishmaeli, na hayo ni majina yao, katika miji yao, na katika vituo vyao, maseyidi kumi na wawili kwa kufuata jamaa zao. 17 Na hii ndiyo miaka ya maisha ya Ishmaeli, miaka mia na thelathini na saba. Akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake. 18 Wakakaa toka Havila mpaka Shuri, unaoelekea Misri, kwa njia ya kwenda Ashuru. Akakaa katikati ya ndugu zake wote. 19 Na hivi ndivyo vizazi vya Isaka, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu alimzaa Isaka. 20 Isaka akawa mwenye miaka arobaini alipomtwaa Rebeka binti Bethueli, Mshami, wa Padan-aramu, ndugu wa Labani, Mshami, kuwa mke wake. 21 Isaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, maana alikuwa tasa. Naye Bwana akamwitikia, na Rebeka mkewe akachukua mimba. 22 Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana. 23 Bwana akamwambia,Mataifa mawili yamo tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo. 24 Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. 25 Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. 26 Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. 27 Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa hemani. 28 Basi Isaka akampenda Esau, kwa sababu alikula mawindo yake, na Rebeka akampenda Yakobo. 29 Yakobo akapika chakula cha dengu. Esau akaja kutoka nyikani, naye alikuwa amechoka sana. 30 Esau akamwambia Yakobo, Tafadhali, unipe hicho chakula chekundu nile, kwa kuwa ninazimia mimi. Kwa hiyo walimwita jina lake Edomu. 31 Yakobo akamwambia, Kwanza niuzie leo haki yako ya mzaliwa wa kwanza. 32 Esau akasema, Tazama, mimi ni karibu kufa, itanifaa nini haki hii ya uzazi? 33 Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. 34 Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

Mwanzo 26

1 Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Ibrahimu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari. 2 Bwana akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia. 3 Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Ibrahimu baba yako. 4 Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia. 5 Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu. 6 Isaka akakaa katika Gerari. 7 Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso. 8 Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anacheza-cheza na Rebeka mkewe. 9 Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni ndugu yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nalisema, Nisife kwa ajili yake. 10 Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani. 11 Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa. 12 Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, Bwana akambariki. 13 Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. 14 Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. 15 Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. 16 Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. 17 Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. 18 Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye. 19 Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika. 20 Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye. 21 Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna. 22 Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa Bwana ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi. 23 Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba. 24 Bwana akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubarikia, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Ibrahimu mtumishi wangu. 25 Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la Bwana. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko. 26 Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake. 27 Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu? 28 Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba Bwana alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe 29 ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa Bwana. 30 Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa. 31 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani. 32 Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji. 33 Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo. 34 Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti. 35 Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.

Mwanzo 27

1 Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Naye akamwitikia, Mimi hapa. 2 Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. 3 Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; 4 ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. 5 Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. 6 Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, akisema, Angalia, nimemsikia baba yako akisema na Esau, ndugu yako, akinena, 7 Niletee mawindo, ukanifanyie chakula kitamu ili nile, na kukubariki mbele za Bwana kabla ya kufa kwangu. 8 Basi, mwanangu, sikiliza sauti yangu kama nitakavyokuagiza. 9 Enenda sasa kundini ukanitwalie wana-mbuzi wawili walio wema, nami nitawafanya chakula kitamu kwa baba yako, namna ile aipendayo. 10 Kisha utampelekea baba yako, apate kula, ili akubariki kabla ya kufa kwake. 11 Yakobo akamwambia Rebeka mamaye, Esau ndugu yangu ni mtu mwenye malaika, na mimi ni mtu laini. 12 Labda baba yangu atanipapasa, nami nitakuwa machoni pake kama mdanganyifu; nami nitaleta juu yangu laana wala si mbaraka. 13 Mamaye akamwambia, Laana yako na iwe juu yangu, mwanangu, usikie sauti yangu tu, enenda ukaniletee wana-mbuzi. 14 Akaenda, akawatwaa, akamletea mamaye. Mamaye akafanya chakula kitamu namna ile aliyopenda babaye. 15 Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. 16 Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. 17 Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu, na mkate alioufanya. 18 Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? 19 Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondoka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. 20 Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu Bwana, Mungu wako, amenifanikisha. 21 Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. 22 Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau. 23 Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki. 24 Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. 25 Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogezea karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. 26 Isaka, baba yake, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu. 27 Akakaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. 28 Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo. 29 Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, Na wana wa mama yako na wakusujudie. Atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe. 30 Ikawa Isaka alipokwisha kumbariki Yakobo, na alipokuwa Yakobo ndiyo kwanza ametoka mbele ya Isaka, baba yake, mara Esau ndugu yake akaja kutoka katika kuwinda kwake. 31 Naye pia amefanya chakula kitamu akamletea babaye, akamwambia baba yake. Babangu na aondoke, ale mawindo ya mwanawe, ili roho yako inibariki. 32 Isaka, baba yake, akamwuliza, U nani wewe? Akasema, Mimi ni mwanao, Esau, mzaliwa wako wa kwanza. 33 Isaka akatetemeka tetemeko kuu sana, akasema, Ni nani basi yule aliyetwaa mawindo akaniletea? Nami nimekwisha kula kabla hujaja wewe, nikambariki; naam, naye atabarikiwa. 34 Esau aliposikia maneno ya babaye, akalia kilio kikubwa cha uchungu sana, akamwambia babaye, Nibariki na mimi, mimi nami, Ee babangu. 35 Akasema, Nduguyo amekuja kwa hila, akauchukua mbaraka wako. 36 Akasema, Je! Hakuitwa Yakobo kwa haki, maana amejitia mahali pangu mara mbili hizi? Alichukua haki yangu ya mzaliwa wa kwanza, na sasa amechukua mbaraka wangu. Akasema, Je! Hukuniwekea na mimi mbaraka? 37 Isaka akajibu, akamwambia Esau, Tazama, nimemfanya awe bwana wako, na ndugu zake wote nimempa kuwa watumishi wake; kwa nafaka na mvinyo nimemtegemeza, nami nikufanyie nini sasa, mwanangu? 38 Esau akamwambia babaye, Una mbaraka mmoja tu, babangu? Unibariki mimi, mimi nami, Ee babangu. Esau akapaza sauti yake, akalia. 39 Isaka, baba yake, akajibu, akamwambia,Angalia,penye manono ya nchi patakuwa makao yako,Na penye umande wa mbingu unaotoka juu. 40 Kwa upanga wako wewe utaishi, nawe utamtumikia nduguyo; Na itakuwa utakapoponyoka, Utalivunja kongwa lake katika shingo yako. 41 Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo. 42 Rebeka akaarifiwa maneno ya Esau, mwanawe mkubwa. Akapeleka mtu kumwita Yakobo, mwanawe mdogo, akamwambia, Tazama, katika habari zako Esau, ndugu yako, anajifariji moyo wake, maana anakusudia kukuua. 43 Na sasa, mwanangu, sikia sauti yangu, uondoke, ukimbilie kwa Labani, ndugu yangu huko Harani; 44 ukae kwake siku chache, hata ghadhabu ya ndugu yako igeuke; 45 hata ikuondokee ghadhabu ya ndugu yako, akasahau uliyomtenda. Ndipo nitakapopeleka watu kukuchukua kutoka huko. Kwa nini nifiwe nanyi nyote wawili siku moja? 46 Rebeka akamwambia Isaka, Rohoni mwangu sina raha kwa sababu ya hao binti za Hethi. Kama Yakobo akitwaa mke katika binti za Hethi, kama hawa binti za nchi, maisha yangu yatanifaidia nini?

Mwanzo 28

1 Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani. 2 Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako. 3 Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila. 4 Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu. 5 Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau. 6 Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usitwae mke wa binti za Kanaani, 7 na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu. 8 Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake. 9 Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao. 10 Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani. 11 Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. 12 Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. 13 Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. 14 Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. 15 Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. 16 Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. 17 Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. 18 Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. 19 Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. 20 Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; 21 nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. 22 Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

Mwanzo 29

1 Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki. 2 Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima. 3 Makundi yote hukusanyika huko, watu wakafingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake. 4 Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi. 5 Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua. 6 Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo. 7 Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha. 8 Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo. 9 Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga. 10 Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye. 11 Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia. 12 Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari. 13 Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote. 14 Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja. 15 Labani akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni ndugu yangu, basi, je! Unitumikie bure? Niambie mshahara wako utakuwa nini? 16 Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. 17 Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. 18 Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo. 19 Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu. 20 Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda. 21 Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake. 22 Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu. 23 Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake. 24 Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake. 25 Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda? 26 Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa; 27 timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine. 28 Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye akampa Raheli binti yake kuwa mkewe. 29 Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi wake. 30 Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine. 31 Bwana akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai. 32 Lea akapata mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa Bwana ameona teso langu; sasa mume wangu atanipenda. 33 Akapata mimba tena akazaa mwana, akasema, Kwa kuwa Bwana amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu; akamwita jina lake Simeoni. 34 Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi. 35 Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu Bwana; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.

Mwanzo 30

1 Naye Raheli alipoona ya kuwa hamzalii Yakobo mwana, Raheli alimwonea ndugu yake wivu. Akamwambia Yakobo, Nipe wana; kama sivyo, nitakufa mimi. 2 Yakobo akamghadhibikia Raheli, akasema, Je! Mimi ni badala ya Mungu, aliyekuzuilia uzao wa mimba? 3 Akasema, Yuko mjakazi wangu, Bilha, uingie kwake ili kwamba azae juu ya magoti yangu, nami nipate uzao kwa yeye. 4 Basi akampa Bilha mjakazi wake kuwa mkewe. Yakobo akaingia kwake. 5 Naye Bilha akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana. 6 Raheli akasema, Mungu amenipa haki yangu, naye amesikia sauti yangu, akanipa mwana. Kwa hiyo akamwita jina lake Dani. 7 Bilha, mjakazi wa Raheli, akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa pili. 8 Raheli akasema, Kwa mashindano makuu nimeshindana na ndugu yangu, nikashinda. Akamwita jina lake Naftali. 9 Lea alipoona ya kuwa ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mjakazi wake, akampa Yakobo kuwa mkewe. 10 Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana. 11 Lea akasema, Bahati njema! Akamwita jina lake Gadi. 12 Zilpa, mjakazi wa Lea, akamzalia Yakobo mwana wa pili. 13 Lea akasema, Ni heri mimi, maana wanawake wataniita heri. Akamwita jina lake Asheri. 14 Reubeni akaenda siku za mavuno ya ngano akaona tunguja kondeni, akazileta kwa Lea mamaye. Ndipo Raheli akamwambia Lea, Nipe mimi baadhi ya tunguja za mwanao. 15 Naye akamwambia, Je! Ni jambo dogo kuninyang'anya mume wangu; hata wataka kuzitwaa tunguja za mwanangu pia? Raheli akamwambia, Kwa hiyo atalala kwako usiku huu kwa tunguja za mwanao. 16 Yakobo akaja kutoka kondeni jioni, Lea akatoka kumlaki, akasema, Lazima uje kwangu, kwa sababu nimekuajiri, kwa tunguja za mwanangu; akalala kwake usiku ule. 17 Mungu akamsikia Lea, naye akapata mimba, akamzalia Yakobo mwana wa tano. 18 Lea akasema, Mungu amenipa ujira wangu, kwa sababu nimempa mume wangu mjakazi wangu. Akamwita jina lake Isakari. 19 Lea akapata mimba tena, akamzalia Yakobo mwana wa sita. 20 Lea akasema, Mungu amenipa mahari njema, sasa mume wangu atakaa nami, kwa kuwa nimemzalia wana sita. Akamwita jina lake Zabuloni. 21 Baadaye akazaa binti, akamwita jina lake Dina. 22 Mungu akamkumbuka Raheli; Mungu akamsikia, akamfungua tumbo. 23 Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, Mungu ameondoa aibu yangu. 24 Akamwita jina lake Yusufu, akisema, Bwana aniongeze mwana mwingine. 25 Ikawa Raheli alipomzaa Yusufu, Yakobo akamwambia Labani, Nipe ruhusa niende kwetu, na kwenye nchi yangu. 26 Nipe wake zangu na watoto wangu, niliokutumikia, niende zangu, maana umejua utumishi wangu niliokutumikia. 27 Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba Bwana amenibariki kwa ajili yako. 28 Akasema, Sema mshahara wako utakao, nami nitatoa. 29 Akamwambia, Umejua jinsi nilivyokutumikia, na jinsi wanyama wako walivyokuwa kwangu. 30 Maana mali yako ilikuwa haba kabla sijaja, nayo imezidi kuwa nyingi, Bwana akakubariki kila nilikokwenda. Basi sasa, nitaangalia lini mambo ya nyumba yangu mwenyewe? 31 Akamwuliza, Nikupe nini? Yakobo akasema, Usinipe kitu; ukinifanyia neno hili, nitalisha wanyama wako tena na kuwalinda. 32 Nitapita katika wanyama wako wote leo, na kutoa huko kila mnyama aliye na madoadoa na marakaraka, na kila mnyama mweusi katika hao kondoo, na aliye na marakaraka na madoadoa katika mbuzi; nao watakuwa mshahara wangu. 33 Na haki yangu itanishuhudia katika siku zijazo, utakapokuja kwa habari ya mshahara wangu ulioko kwako. Kila asiye madoadoa au marakaraka katika mbuzi, au asiye mweusi katika kondoo, akionekana kwangu, itahesabiwa kuwa ameibiwa. 34 Labani akasema, Tazama, na iwe hivi kama usemavyo. 35 Basi akatoa siku ile mbuzi waume walio na milia na madoadoa, na mbuzi wake walio na madoadoa na marakaraka, kila aliye na doa jeupe, na kondoo wote waliokuwa weusi, akawatia mikononi mwa wanawe. 36 Akajitenga na Yakobo mwendo wa siku tatu; naye Yakobo akachunga wanyama wa Labani waliosalia. 37 Yakobo akatwaa fito za mlubna mbichi, na mlozi, na mwaramoni, akazibambua maganda, mistari myeupe ionekane ndani ya hizo fito. 38 Akazisimamisha fito hizo alizozibambua katika mabirika ya kunyweshea maji, pale walipokuja wanyama wanywe; wakachukua mimba walipokuja kunywa. 39 Wanyama wakapata mimba mbele ya hizo fito, wakazaa wanyama walio na milia, na madoadoa, na marakaraka. 40 Na Yakobo akawatenga wana-kondoo, akazielekeza nyuso za makundi zielekee wale waliokuwa na milia, na kila aliyekuwa mweusi katika wanyama wa Labani. Akaweka kando wanyama wake mwenyewe, wala hakuwachanganya pamoja na wanyama wa Labani. 41 Ikawa kila walipopata mimba wanyama wenye nguvu, Yakobo akaziweka zile fito mbele ya macho ya hao wanyama katika mabirika ili kwamba wachukue mimba kati ya zile fito, 42 lakini wanyama walipodhoofika hakuziweka zile fito. Basi wale dhaifu walikuwa wa Labani, na wenye nguvu walikuwa wa Yakobo. 43 Kwa hiyo mtu huyo akazidi mno, akawa na wanyama wengi, na vijakazi, na watumwa, na ngamia, na punda.

Mwanzo 31

1 Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote. 2 Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi. 3 Bwana akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe. 4 Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia, 5 Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami. 6 Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu. 7 Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru. 8 Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia. 9 Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi. 10 Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka. 11 Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa. 12 Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani. 13 Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa. 14 Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu? 15 Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa? 16 Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye. 17 Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia. 18 Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa ameyapata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani. 19 Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye. 20 Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia. 21 Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi. 22 Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia, 23 akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi. 24 Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. 25 Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi. 26 Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. 27 Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi? 28 Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu. 29 Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari. 30 Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu? 31 Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang'anya binti zako kwa nguvu. 32 Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli ameiiba. 33 Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia katika hema ya Raheli. 34 Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona. 35 Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago. 36 Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo akajibu, akamwambia Labani, N'nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata ukanifuatia namna hii? 37 Umepapasa-papasa vyombo vyangu vyote; ni kitu gani ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu zako, wakaamue kati yetu. 38 Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala. 39 Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku. 40 Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu. 41 Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi. 42 Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu. 43 Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea? 44 Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe. 45 Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo. 46 Yakobo akawaambia ndugu zake, Kusanyeni mawe. Wakatwaa mawe, wakafanya chungu, nao wakala huko karibu na ile chungu. 47 Labani aliiita Yegarsahadutha, lakini Yakobo aliiita Galedi. 48 Labani akasema, Chungu hii ni shahidi kati ya mimi na wewe hivi leo. Kwa hiyo likaitwa jina lake Galedi, 49 na Mispa, maana alisema, Mungu avizie kati ya mimi na wewe, wakati tusipoonana. 50 Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe. 51 Labani akamwambia Yakobo, Tazama chungu hii utazame na nguzo niliyoitia kati ya mimi na wewe. 52 Chungu hii na iwe shahidi, na nguzo hii na iwe shahidi, ya kuwa mimi sitapita chungu hii kuja kwako, wala wewe hutapita chungu hii na nguzo hii uje kwangu, kwa madhara. 53 Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba yao, ahukumu kati yetu. 54 Yakobo akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani. 55 Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.

Mwanzo 32

1 Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye. 2 Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu. 3 Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu. 4 Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa, 5 nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako. 6 Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye. 7 Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili. 8 Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka. 9 Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Bwana, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema; 10 mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili. 11 Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana. 12 Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi. 13 Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye; 14 mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini; 15 ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi. 16 Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi. 17 Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako? 18 Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu. 19 Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta. 20 Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu. 21 Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini. 22 Akaondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. 23 Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo. 24 Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. 25 Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. 26 Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. 27 Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo. 28 Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. 29 Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko. 30 Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka. 31 Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake. 32 Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.

Mwanzo 33

1 Yakobo akainua macho yake, akaona, na tazama, Esau anakuja na watu mia nne pamoja naye. Akawagawanyia Lea, na Raheli, na wale vijakazi wawili, wana wao. 2 Akawaweka hao vijakazi na wana wao mbele, na Lea na wanawe nyuma yao, na Raheli na Yusufu mwisho. 3 Akapita mwenyewe mbele yao, akainama mpaka nchi mara saba, hata alipomkaribia ndugu yake. 4 Esau akaja mbio kumlaki, akamkumbatia, na kumwangukia shingoni, akambusu; nao wakalia. 5 Akainua macho yake, akawaona wale wanawake na watoto, akauliza, Ni nani hawa walio pamoja nawe? Akasema, Ni watoto Mungu aliompa mtumwa wako kwa neema yake. 6 Ndipo wale vijakazi, na wana wao, wakakaribia wakainama. 7 Lea naye, na wanawe, wakakaribia wakainama. Baadaye Yusufu na Raheli wakakaribia, wakainama. 8 Akasema, Kundi hili lote nililolikuta, maana yake ni nini? Akasema, Kunipatia kibali machoni pa bwana wangu. 9 Esau akasema, Ninayo tele, ndugu yangu, uliyo nayo na yawe yako. 10 Yakobo akasema, Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu, iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami. 11 Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote Akamshurutisha, naye akapokea. 12 Kisha Esau akamwambia, Twende zetu, tusafiri, nami nitakutangulia. 13 Akamjibu, Bwana wangu anajua ya kuwa watoto ni wachanga, tena kondoo na ng'ombe nilio nao wanyonyesha. Hao wanyama wakiharakishwa siku moja, watakufa wote. 14 Tafadhali bwana wangu na apite mbele ya mtumwa wake; nami nitawaongoza polepole kwa kadiri ya mwendo wa wanyama walio mbele yangu, na kwa kadiri ya mwendo wa watoto, hata nitakapofika kwa bwana wangu huko Seiri. 15 Esau akasema, Nikuachie, basi, baadhi ya watu walio pamoja nami. Akasema, Pana haja gani? Na nione kibali tu machoni pa bwana wangu. 16 Basi Esau akarudi siku ile ile akishika njia yake mpaka Seiri. 17 Yakobo akaendelea mpaka Sukothi. Akajijengea nyumba, akawafanyia makundi yake vibanda. Kwa hiyo jina la mahali pale pakaitwa Sukothi. 18 Yakobo akaja kwa amani mpaka mji wa Shekemu, ulio katika nchi ya Kanaani, alipokuja kutoka Padan-aramu; akapiga kambi mbele ya huo mji. 19 Akainunua sehemu ya nchi, alipopiga hema yake, kwa mkono wa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. 20 Akajenga huko madhabahu, akaiita, El-elohe-Israeli.

Mwanzo 34

1 Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. 2 Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. 3 Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. 4 Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. 5 Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja. 6 Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. 7 Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka. 8 Hamori akasema nao, akinena, Roho ya Shekemu, mwanangu, inamtamani binti yenu, tafadhalini, mpeni amwoe. 9 Mkaoane na sisi, mtupe sisi binti zenu, nanyi mkatwae binti zetu. 10 Nanyi mtakaa nasi, na nchi hii itakuwa mbele yenu; kaeni, na kufanya biashara humo, mkapate mali humo. 11 Shekemu akamwambia babaye yule msichana na nduguze, Na nikubalike machoni penu, na mtakavyoniambia nitatoa. 12 Mjapoongeza sana mahari na zawadi, nitatoa kadiri ya mtakavyoniambia, lakini mnipe huyu msichana, awe mke wangu. 13 Wana wa Yakobo wakawajibu Shekemu na Hamori babaye, kwa hila, maana amemharibu Dina, umbu lao, 14 wakawaambia, Hatuwezi kufanya neno hili, tumpe umbu letu mtu asiyetahiriwa; ingekuwa aibu kwetu. 15 Lakini kwa sharti hii tu tutapatana nanyi; mkiwa kama sisi, akitahiriwa kila mwanamume wenu, 16 ndipo tutawapa ninyi binti yetu, na sisi tutatwaa binti zenu tutakaa pamoja nanyi, nasi tutakuwa watu wamoja. 17 Lakini kama hamtusikii na kutahiriwa, basi tutamtwaa umbu letu, nasi tutakwenda zetu. 18 Maneno yao yakawa mema machoni pa Hamori, na machoni pa Shekemu, mwana wa Hamori. 19 Na yule kijana hakukawia kulifanya neno lile, maana amependezewa na binti Yakobo, naye alikuwa mwenye heshima kuliko wote nyumbani mwa babaye. 20 Hamori, na Shekemu mwanawe, wakaja langoni pa mji wao, wakasema na watu wa mji wao, wakinena, 21 Watu hawa wana amani nasi, basi na wakae katika nchi, na kufanya biashara humo; kwa maana nchi ni kubwa, yawatosha; na tuwatwae binti zao kuwa wake zetu, na binti zetu tuwape wao. 22 Lakini kwa sharti hiyo moja tu watapatana nasi wakae wote kwetu, tuwe watu wamoja, kama tukitahiriwa kila mwanamume, kama hawa walivyotahiriwa. 23 Je! Kondoo zao, na mali zao, na wanyama wao wote hawatakuwa mali zetu? Basi na tupatane nao tu, nao watakaa kwetu. 24 Wakawasikia Hamori na Shekemu mwanawe, wote watokao katika lango la mji wake. Wakatahiriwa kila mwanamume, wote watokao katika lango la mji wake. 25 Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wakiumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, nduguze Dina, wakatwaa kila mtu upanga wake, wakaujia mji kwa ujasiri, wakawaua waume wote. 26 Wakawaua Hamori, na Shekemu mwanawe, kwa makali ya upanga, wakamtwaa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakatoka. 27 Wana wa Yakobo wakawajilia hao waliouawa, wakauteka nyara mji kwa sababu wamemharibu umbu lao. 28 Wakachukua kondoo zao, na ng'ombe zao, na punda zao, na vitu vilivyokuwamo mjini, navyo vilivyokuwako kondeni. 29 Wakatwaa na mali zao zote, na watoto wao wote, na wake zao, na vyote vilivyokuwamo nyumbani mwao wakavichukua mateka. 30 Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, Mmenitaabisha, kunifanya ninuke vibaya kati ya watu wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi; na mimi, kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu. 31 Nao wakasema, Je! Ni vema amtendee umbu letu kama kahaba?

Mwanzo 35

1 Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. 2 Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu. 3 Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. 4 Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. 5 Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo. 6 Basi Yakobo akafika Luzu, ulio katika nchi ya Kanaani, ndio Betheli, yeye na watu wote waliokuwa pamoja naye. 7 Akajenga huko madhabahu, akapaita mahali pale, El-Betheli; kwa sababu huko Mungu alimtokea, hapo alipomkimbia ndugu yake. 8 Akafa Debora mlezi wa Rebeka, akazikwa chini ya Betheli, chini ya mwaloni; na jina lake likaitwa Alon-bakuthi. 9 Mungu akamtokea Yakobo tena, aliporudi kutoka Padan-aramu akambariki. 10 Mungu akamwambia, Jina lako ni Yakobo; hutaitwa tena Yakobo, lakini Israeli litakuwa jina lako. Akamwita jina lake, Israeli. 11 Mungu akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uzidi ukaongezeke. Taifa na kundi la mataifa watatoka kwako, na wafalme watatoka viunoni mwako. 12 Na nchi hii niliyowapa Ibrahimu na Isaka nitakupa wewe, na uzao wako baada yako nitawapa nchi hiyo. 13 Mungu akakwea juu kutoka kwake mahali hapo aliposema naye. 14 Yakobo akasimamisha nguzo mahali aliposema naye, nguzo ya mawe, akamimina juu yake sadaka ya kinywaji, akamimina mafuta juu yake. 15 Yakobo akapaita mahali pale, Mungu aliposema naye, Betheli. 16 Wakasafiri kutoka Betheli, hata ukabaki mwendo wa kitambo tu kufika Efrathi, Raheli akashikwa na utungu wa kuzaa, na utungu wake ulikuwa mzito. 17 Ikawa alipokuwa anashikwa sana na utungu, mzalisha akamwambia, Usiogope, maana sasa utamzaa mwanamume mwingine. 18 Ikawa hapo katika kutoa roho yake, maana alikufa, akamwita jina lake Benoni, lakini babaye alimwita Benyamini. 19 Akafa Raheli, akazikwa katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu. 20 Yakobo akasimamisha nguzo juu ya kaburi lake, ndiyo nguzo ya kaburi la Raheli hata leo. 21 Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili wa mnara wa Ederi. 22 Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; Israeli akasikia habari. Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili. 23 Wana wa Lea ni Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo, na Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Zabuloni. 24 Wana wa Raheli, ni Yusufu na Benyamini. 25 Wana wa Bilha, kijakazi wa Raheli, ni Dani na Naftali. 26 Wana wa Zilpa, kijakazi wa Lea, ni Gadi na Asheri. Hawa ndio wana wa Yakobo aliozaliwa katika Padan-aramu. 27 Yakobo akaja kwa Isaka, babaye, huko Mamre, mji wa Arba, ndio Hebroni, walipokaa ugenini Ibrahimu na Isaka. 28 Siku za Isaka zilikuwa miaka mia na themanini. 29 Naye Isaka akakata roho, akafa, akakusanyika kwa watu wake, ni mzee, ameshiba siku. Esau na Yakobo, wanawe, wakamzika

Mwanzo 36

1 Hivi ndivyo vizazi vya Esau, ndiye Edomu. 2 Esau alitwaa binti za Kanaani, kuwa wakeze; Ada, binti Eloni, Mhiti, na Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, Mhivi; 3 na Basemathi, binti Ishmaeli, nduguye Nebayothi. 4 Ada akamzalia Esau Elifazi; na Basemathi alizaa Reueli. 5 Oholibama alizaa Yeushi, na Yalamu, na Kora. Hao ndio wana wa Esau aliozaliwa katika nchi ya Kanaani. 6 Esau akawatwaa wakeze, na wanawe, na binti zake, na watu wote wa nyumbani mwake, na ng'ombe zake, na wanyama wake wote, na mali yake yote, aliyoyapata katika nchi ya Kanaani; akaenda mpaka nchi iliyo mbali na Yakobo nduguye. 7 Maana mali yao yalikuwa mengi wasiweze kukaa pamoja, wala haikuweza nchi ya kusafiri kwao kuwachukua, kwa sababu ya wanyama wao. 8 Esau akakaa katika mlima Seiri, Esau ndiye Edomu. 9 Hivi ni vizazi vya Esau, baba ya Edomu katika mlima Seiri. 10 Haya ndiyo majina ya wana wa Esau; Elifazi, mwana wa Ada mkewe Esau. Reuli, mwana wa Basemathi, mkewe Esau. 11 Na wana wa Elifazi, ni Temani na Omari, na Sefo, na Gatamu, na Kenazi. 12 Na Timna alikuwa suria wa Elifazi, mwana wa Esau; naye akamzalia Elifazi Amaleki. Hao ndio wana wa Ada, mkewe Esau. 13 Na hawa ni wana wa Reueli, Nahathi, na Zera, na Shama na Miza. Hao walikuwa wana wa Basemathi, mkewe Esau. 14 Na hawa ni wana wa Oholibama, binti Ana, binti Sibeoni, mkewe Esau; akamzalia Esau, Yeushi, na Yalamu, na Kora. 15 Hawa ndio majumbe wao wana wa Esau; wana wa Elifazi, mzaliwa wa kwanza wa Esau; jumbe Temani, jumbe Omari, jumbe Sefo, jumbe Kenazi, 16 jumbe Kora, jumbe Gatamu, jumbe Amaleki. Hao ndio majumbe, waliotoka kwa Elifazi katika nchi ya Edomu. Hao ni wana wa Ada. 17 Na hawa ni wana wa Reueli, mwanawe Esau; jumbe Nahathi, jumbe Zera, jumbe Shama, jumbe Miza. Hao ndio majumbe waliotoka kwa Reueli katika nchi ya Edomu. Hao ni wana wa Basemathi, mkewe Esau. 18 Na hawa ni wana wa Oholibama, mkewe Esau; jumbe Yeushi, jumbe Yalamu, jumbe Kora. Hao ndio majumbe waliotoka kwa Oholibama, binti Ana, mkewe Esau. 19 Hao ni wana wa Esau, na hao ndio majumbe wao; naye Esau ndiye Edomu. 20 Hawa ni wana wa Seiri, Mhori, wenyeji wa nchi ile; Lotani, na Shobali, na Sibeoni, na Ana, 21 na Dishoni, na Eseri, na Dishani. Hao ndio majumbe waliotoka katika Wahori, wana wa Seiri, katika nchi ya Edomu. 22 Na wana wa Lotani, ni Hori, na Hemamu; na umbu lake Lotani ni Timna. 23 Na hawa ni wana wa Shobali, Alvani, na Manahathi, na Ebali, na Shefo, na Onamu. 24 Na hawa ni wana wa Sibeoni, Aya, na Ana; ni yule Ana aliyeona chemchemi za maji ya moto katika jangwa, alipokuwa akichunga punda za Sibeoni babaye. 25 Na hawa ni wana wa Ana, Dishoni, na Oholibama, binti Ana. 26 Na hawa ni wana wa Dishoni, Hemdani, na Eshbani, na Ithrani, na Kerani. 27 Na hawa ni wana wa Eseri, Bilhani, na Zaawani, na Akani. 28 Na hawa ni wana wa Dishani, Usi, na Arani. 29 Hawa ndio majumbe waliotoka katika Wahori; jumbe Lotani, jumbe Shobali, jumbe Sibeoni, jumbe Ana, 30 jumbe Dishoni, jumbe Eseri jumbe Dishani. Hao ndio majumbe waliotoka katika Wahori, kwa habari za majumbe yao, katika nchi ya Seiri. 31 Na hawa ndio wafalme waliomiliki katika nchi ya Edomu, kabla ya kumiliki mfalme ye yote juu ya wana wa Israeli. 32 Bela wa Beori alimiliki katika Edomu, na jina la mji wake ni Dinhaba. 33 Akafa Bela, akamiliki Yobabu mwana wa Zera, wa Bosra, badala yake. 34 Akafa Yobabu, akamiliki Hushamu, wa nchi ya Watemani, badala yake. 35 Akafa Hushamu, akamiliki Hadadi wa Bedadi badala yake, naye ndiye aliyepiga Midiani katika nyika ya Moabu, na jina la mji wake ni Avithi. 36 Akafa Hadadi, akamiliki Samla wa Masreka badala yake. 37 Akafa Samla, na Shauli wa Rehobothi, ulio karibu na mto, akamiliki badala yake. 38 Akafa Shauli, akamiliki Baal-hanani, mwana wa Akbori, badala yake. 39 Akafa Baal-hanani, mwana wa Akbori, akamiliki Hadadi badala yake; na jina la mji wake ni Pau; na jina la mkewe ni Mehetabeli, binti Matredi, binti Mezahabu. 40 Na hayo ndiyo majina ya majumbe waliotoka kwa Esau, kufuata jamaa zao, na mahali pao, kwa majina yao. Jumbe Timna, jumbe Alva, jumbe Yethethi, 41 jumbe Oholibama, jumbe Ela, jumbe Pinoni, 42 jumbe Kenazi, jumbe Temani, jumbe Mibsari, 43 jumbe Magdieli, jumbe Iramu. Hao ndio majumbe wa Edomu, kufuata makao yao, katika nchi ya mamlaka yao. Naye huyo ndiye Esau, baba ya Edomu.

Mwanzo 37

1 Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani. 2 Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. 3 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. 4 Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. 5 Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; 6 akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. 7 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. 8 Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. 9 Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. 10 Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? 11 Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili. 12 Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. 13 Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa. 14 Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu. 15 Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini? 16 Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga. 17 Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. 18 Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. 19 Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. 20 Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake. 21 Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. 22 Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake. 23 Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, 24 wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. 25 Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. 26 Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? 27 Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. 28 Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri. 29 Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake. 30 Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi? 31 Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu. 32 Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo. 33 Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa. 34 Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi. 35 Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia. 36 Nao Wamidiani wakamwuza huko Misri, kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari.

Mwanzo 38

1 Ikawa wakati ule, Yuda akashuka kutoka kwa ndugu zake, akamfikia mtu Mwadulami, jina lake Hira. 2 Yuda akaona huko binti wa mtu Mkanaani, jina lake Shua. Akamtwaa, akaingia kwake. 3 Naye akapata mimba, akazaa mwana, akamwita jina lake Eri. 4 Akapata mimba tena, akazaa mwana, akamwita jina lake Onani. 5 Akaendelea, akazaa tena mwana mwingine, akamwita jina lake Shela. Naye Yuda alikuwako huko Kezibu, alipomzaa. 6 Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari. 7 Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa Bwana; na Bwana akamwua. 8 Yuda akamwambia Onani, Uingie kwa mke wa nduguyo, ukamwoe, ukamwinulie nduguyo uzao. 9 Onani alijua ya kwamba huo uzao hautakuwa wake, ikawa, alipoingia kwa mke wa nduguye, akamwagia chini asimpe nduguye uzao. 10 Neno hili alilolifanya likawa baya machoni pa Bwana, basi akamwua yeye naye. 11 Yuda akamwambia Tamari mkwewe, Ukae mjane nyumbani mwa baba yako hata Shela mwanangu atakapokuwa mtu mzima, maana alisema, Asipate kufa yeye kama nduguze. Basi Tamari akaenda, akakaa nyumbani mwa babaye. 12 Siku nyingi zikapita, akafa binti Shua, mkewe Yuda. Yuda akafarijika, akaenda kwa watu wake wawakatao manyoya kondoo huko Timna, yeye na mwenzake Hira, Mwadulami. 13 Huyo Tamari akapewa habari, kusema, Mkweo anakwenda Timna, akate manyoya ya kondoo zake. 14 Basi akavua nguo za ujane wake, akajivika utaji, akajifunika uso, akakaa mlangoni pa Enaimu, karibu na njia ya kuendea Timna. Maana aliona ya kwamba Shela amekuwa mtu mzima, wala hakuozwa awe mkewe. 15 Yuda alipomwona alimdhania kuwa ni kahaba, maana amejifunika uso. 16 Akamgeukia kando ya njia, akasema, Niruhusu niingie kwako. Maana hakujua ya kuwa ni mkwewe. Akamwuliza, Utanipa nini, ukiingia kwangu? 17 Akasema, Nitakuletea mwana-mbuzi wa kundini. Naye akamwuliza, Je! Utanipa rehani hata utakapomleta? 18 Akasema, Nikupe rehani gani? Akamjibu, Pete yako ya muhuri, na kamba yake, na fimbo yako iliyo mkononi mwako. Basi akampa, akaingia kwake, naye akapata mimba. 19 Akaondoka, akaenda zake, akavua utaji wake, na kuvaa mavazi ya ujane wake. 20 Yuda akapeleka yule mwana-mbuzi kwa mkono wa rafiki yake Mwadulami, ili aipate rehani mkononi mwa huyo mwanamke lakini hakumkuta. 21 Akauliza watu wa mahali pale, akisema, Yuko wapi yule kahaba aliyekuwapo Enaimu kando ya njia? Wakasema, Hakuwako hapa kahaba. 22 Akamrudia Yuda akasema, Sikumwona; hata na watu wa mahali hapo walisema, Hakuwako kahaba. 23 Yuda akasema, Na aichukue yeye, tusije tukatiwa aibu; tazama, nimempelekea mbuzi huyu, wala hukumkuta. 24 Ikawa baada ya miezi mitatu Yuda akapewa habari kwamba, Mkweo, Tamari, amefanya uzinifu, naye ana mimba ya haramu. Yuda akasema, Mtoeni ateketezwe. 25 Alipotolewa, alipeleka watu kwa mkwewe, akisema, Mimi nimepewa mimba na mtu mwenye vitu hivi. Akasema, Tambua basi, vitu hivi ni vya nani, pete hii, na kamba hii, na fimbo hii. 26 Yuda akavikiri, akasema, Yeye ni mwenye haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumpa Shela, mwanangu. Wala hakumjua tena baada ya hayo. 27 Ikawa, wakati wake wa kuzaa walikuwapo mapacha tumboni mwake. 28 Ikawa alipokuwa akizaa, mtoto mmoja akatoa mkono, mzalisha akautwaa uzi mwekundu akaufunga mkononi mwake, huku akisema, Huyu ametoka kwanza. 29 Ikawa aliporudisha mkono wake, tazama, ndugu yake akatoka. Akasema, Mbona umepita kwa nguvu wewe? Mambo ya nguvu na yakuandame. Kwa hiyo jina lake likaitwa Peresi. 30 Akatoka ndugu yake baadaye, ana uzi mwekundu mkononi mwake; naye akaitwa jina lake Zera.

Mwanzo 39

1 Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko. 2 Bwana akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. 3 Bwana wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa Bwana anafanikisha mambo yote mkononi mwake. 4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. 5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. 6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. 7 Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. 8 Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. 9 Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? 10 Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. 11 Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; 12 huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. 13 Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, 14 akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. 15 Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. 16 Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. 17 Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. 18 Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. 19 Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. 20 Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani. 21 Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza. 22 Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya. 23 Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa Bwana alikuwa pamoja naye. Bwana akayafanikisha yote aliyoyafanya.

Mwanzo 40

1 Ikawa, baada ya mambo hayo, mnyweshaji wa mfalme wa Misri, na mwokaji wake, wakamkosa bwana wao, mfalme wa Misri. 2 Farao akawaghadhibikia maakida wake wawili, mkuu wa wanyweshaji na mkuu wa waokaji. 3 Akawatia katika lindo nyumbani mwa mkuu wa askari, humo gerezani, mahali alipofungwa Yusufu. 4 Mkuu wa askari akamwekea Yusufu watu hao, naye akawahudumu, nao wakakaa siku kadha wa kadha katika kifungo. 5 Wakaota ndoto wote wawili, kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri waliofungwa gerezani. 6 Yusufu akawajia asubuhi, akawaona wamefadhaika. 7 Akawauliza hao maakida wa Farao, waliokuwa pamoja naye katika kifungo, nyumbani mwa bwana wake, akisema, Mbona nyuso zenu zimekunjamana leo? 8 Wakamwambia, Tumeota ndoto wala hapana awezaye kuifasiri. Yusufu akawaambia, Kufasiri si kazi ya Mungu? Tafadhalini mniambie. 9 Mnyweshaji mkuu akamhadithia Yusufu ndoto yake; akamwambia, Katika ndoto yangu nimeota, uko mzabibu mbele yangu. 10 Na katika mzabibu mlikuwa na matawi matatu, nao ulikuwa kana unamea, unachanua maua, vishada vyake vikatoa zabibu zilizoiva. 11 Na kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, nikampa Farao kikombe mkononi mwake. 12 Yusufu akamwambia, Tafsiri yake ndiyo hii. Matawi matatu ni siku tatu. 13 Baada ya siku tatu Farao atakiinua kichwa chako, atakurudisha katika kazi yako; nawe utampa Farao kikombe mkononi mwake, kama desturi ya kwanza, ulipokuwa mnyweshaji wake. 14 Ila unikumbuke mimi, utakapopata mema, ukanifanyie fadhili, nakuomba, ukanitaje kwa Farao, na kunitoa katika nyumba hii. 15 Kwa sababu hakika naliibiwa kutoka nchi ya Waebrania, wala hapa sikutenda neno lo lote hata wanitie gerezani. 16 Mkuu wa waokaji alipoona ya kwamba hiyo tafsiri ni ya mema, akamwambia Yusufu, Mimi kadhalika nilikuwa katika ndoto yangu, na tazama, ziko nyungo tatu za mikate myeupe juu ya kichwa changu. 17 Na katika ungo wa juu, mlikuwa na kila namna ya chakula kwa Farao, kazi za mwokaji; ndege wakavila katika ungo juu ya kichwa changu. 18 Yusufu akajibu, akasema, Tafsiri yake ndiyo hii Nyungo tatu ni siku tatu. 19 Baada ya siku tatu Farao atakiinua na kukuondolea kichwa chako, na kukutundika juu ya mti, na ndege watakula nyama yako. 20 Ikawa siku ya tatu, siku ya kuzaliwa kwake Farao, akawafanyia karamu watumwa wake wote; akakiinua kichwa cha mkuu wa wanyweshaji, na cha mkuu wa waokaji, miongoni mwa watumwa wake. 21 Akamrudisha mkuu wa wanyweshaji katika kazi yake ya kunywesha, naye akampa Farao kikombe mkononi mwake. 22 Bali akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyowafasiria. 23 Lakini huyo mkuu wa wanyweshaji hakumkumbuka Yusufu, alimsahau.

Mwanzo 41

1 Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. 2 Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. 3 Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto. 4 Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. 5 Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. 6 Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. 7 Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. 8 Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo. 9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo. 10 Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji. 11 Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota. 12 Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake. 13 Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa. 14 Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao. 15 Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri. 16 Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani. 17 Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto; 18 na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini. 19 Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu. 20 Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono. 21 Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka. 22 Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa. 23 Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. 24 Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake. 25 Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. 26 Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja. 27 Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa. 28 Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu. 29 Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri. 30 Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi. 31 Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana. 32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi. 33 Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri. 34 Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba. 35 Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji. 36 Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. 37 Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote. 38 Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake? 39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. 40 Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. 41 Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri. 42 Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake. 43 Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri. 44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri. 45 Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri. 46 Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri. 47 Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi. 48 Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake. 49 Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu. 50 Kabla ya kuja miaka ya njaa, Yusufu akazaliwa wana wawili, ambao Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia. 51 Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu. 52 Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu. 53 Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri, 54 ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula. 55 Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. 56 Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. 57 Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.

Mwanzo 42

1 Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana? 2 Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife. 3 Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka. 4 Walakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate. 5 Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. 6 Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. 7 Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula. 8 Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye. 9 Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi. 10 Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula. 11 Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi. 12 Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi. 13 Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko. 14 Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi. 15 Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo. 16 Mpelekeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa, hata maneno yenu yahakikishwe, kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao, ninyi ni wapelelezi. 17 Akawatia wote gerezani siku tatu. 18 Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. 19 Kama ni wa kweli ninyi ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, 20 mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. 21 Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata. 22 Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. 23 Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. 24 Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao. 25 Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. 26 Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko. 27 Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake. 28 Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N'nini hii Mungu aliyotutendea? 29 Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema, 30 Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi. 31 Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi. 32 Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani. 33 Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu. 34 Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii. 35 Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa. 36 Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi. 37 Reubeni akamwambia babaye, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako. 38 Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini.

Mwanzo 43

1 Njaa ikawa nzito katika nchi. 2 Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. 3 Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. 4 Ukimpeleka ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula. 5 Ila usipompeleka, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. 6 Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine? 7 Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tuliweza kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu? 8 Yuda akamwambia Israeli babaye, Mpeleke kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu. 9 Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima; 10 maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili. 11 Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi. 12 Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa. 13 Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule. 14 Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa. 15 Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu. 16 Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje na kuandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri. 17 Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu. 18 Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutuangukia, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda zetu. 19 Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba. 20 Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula. 21 Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu. 22 Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu. 23 Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu ziliniwasilia. Kisha akawatolea Simeoni. 24 Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakatawadha miguu, akawapa punda zao chakula. 25 Wakaiweka tayari ile zawadi hata atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. 26 Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka nchi. 27 Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? 28 Wakasema, Mtumwa wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu. 29 Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mamake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu. 30 Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulia, akaingia chumbani mwake, akalia humo. 31 Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula. 32 Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri. 33 Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa cheo cha kuzaliwa kwake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao. 34 Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafanya furaha pamoja naye.

Mwanzo 44

1 Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake. 2 Na kikombe changu, kikombe kile cha fedha, ukitie kinywani mwa gunia la yule mdogo pamoja na fedha ya nafaka yake. Akafanya kama vile alivyomwambia Yusufu. 3 Asubuhi kulipopambazuka, hao watu wakapewa ruhusa, wao na punda zao. 4 Na walipotoka mjini, wala hawajaendelea sana, Yusufu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake, Ondoka, uwafuate watu hawa, nawe utakapowapata, waambie, Kwa nini mmelipa mabaya kwa mema? 5 Je! Kikombe hiki, sicho anyweacho bwana wangu? Naye hufanya uaguzi kwa hicho. Mmefanya vibaya kwa kufanya hivi. 6 Akawafuata, akawapata, na kuwaambia maneno hayo. 7 Wakamwambia, Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? 8 Hasha! Watumwa wako wasifanye hivi; tazama, hizo fedha mlizoziona kinywani mwa magunia yetu, tumekuletea tena kutoka nchi ya Kanaani. Tuwezeje sisi kuiba nyumbani mwa bwana wako fedha au dhahabu? 9 Atakayeonekana kuwa nacho miongoni mwa watumwa wako, na afe, na sisi nasi tutakuwa watumwa wa bwana wangu. 10 Akasema, Basi na iwe hivyo kama mlivyosema, Mtu atakayeonekana kuwa nacho atakuwa mtumwa wangu, na ninyi mtakuwa hamna hatia. 11 Wakafanya haraka, wakashusha kila mtu gunia lake, na kufungua kila mtu gunia lake. 12 Naye akatafuta, akaanza kwa mkubwa na kuisha kwa mdogo. Kikombe kikaonekana katika gunia la Benyamini. 13 Wakararua nguo zao, wakaweka kila mtu mzigo wake juu ya punda wake, wakarudi mjini. 14 Akaja Yuda na ndugu zake nyumbani kwa Yusufu, naye mwenyewe alikuwamo, nao wakamwangukia kifudifudi. 15 Yusufu akawaambia, Ni tendo gani hili mlilolitenda? Hamkujua ya kwamba mtu kama mimi naweza kufanya uaguzi? 16 Yuda akasema, Tumwambie nini bwana wangu? Tusemeje! Tujivutieje haki? Mungu ameona uovu wa watumwa wako. Tazama, sisi ni watumwa wa bwana wangu, sisi na yeye ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake. 17 Akasema, Hasha! Nisifanye hivi; mtu ambaye kikombe kilionekana mkononi mwake, ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Nanyi enendeni zenu kwa amani kwa baba yenu. 18 Ndipo Yuda akamkaribia, akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. 19 Wewe, bwana wangu, ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! Mnaye baba, au ndugu? 20 Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. 21 Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. 22 Tukakuambia, bwana wangu, Kijana hawezi kumwacha babaye, maana akimwacha babaye, babaye atakufa. 23 Ukatuambia watumwa wako, Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena 24 Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. 25 Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. 26 Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka, maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. 27 Mtumwa wako, baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alinizalia wana wawili; 28 mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. 29 Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. 30 Basi, nikienda kwa mtumwa wako, baba yangu, na huyu kijana hayupo pamoja nasi, iwapo roho yake imeshikamana na roho ya kijana; 31 itakuwa atakapoona ya kwamba huyu kijana hayuko, atakufa; na watumwa wako watashusha mvi za mtumwa wako, baba yetu, kwa huzuni kaburini. 32 Kwa maana mtumwa wako alijifanya mdhamini wa huyu kijana kwa baba yangu, nikisema, Nisipomrudisha kwako, nitakuwa na hatia kwa baba yangu sikuzote. 33 Basi, sasa nakusihi, uniache mimi mtumwa wako nikae badala ya huyu kijana kuwa mtumwa wa bwana wangu; na huyu kijana umwache aende pamoja na nduguze. 34 Kwa maana nitawezaje kumwendea baba yangu, na huyu kijana hayuko pamoja nami? Nisije nikayaona mabaya yatakayompata baba yangu.

Mwanzo 45

1 Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. 2 Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. 3 Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. 4 Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. 5 Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. 6 Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. 7 Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. 8 Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri. 9 Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie. 10 Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng'ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko; 11 maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo. 12 Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi. 13 Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu. 14 Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake. 15 Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye 16 Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake. 17 Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani; 18 kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi. 19 Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje. 20 Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu. 21 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani. 22 Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. 23 Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani. 24 Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani. 25 Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao. 26 Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki. 27 Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka. 28 Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.

Mwanzo 46

1 Akasafiri Israeli, pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. 2 Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. 3 Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. 4 Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha tena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. 5 Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua. 6 Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. 7 Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri. 8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli walioingia Misri, Yakobo na wanawe: Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Yakobo. 9 Na wana wa Reubeni; Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi. 10 Na wana wa Simeoni; Yemueli na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli, mwana wa mwanamke Mkanaani. 11 Na wana wa Lawi; Gershoni, na Kohathi, na Merari. 12 Na wana wa Yuda; Eri, na Onani, na Shela, na Peresi, na Zera; lakini Eri na Onani walikufa katika nchi ya Kanaani. Na wana wa Peresi, ni Hesroni, na Hamuli. 13 Na wana wa Isakari; Tola, na Puva, na Yashubu, na Shimroni. 14 Na wana wa Zabuloni; Seredi, na Eloni, na Yaleeli. 15 Hao ndio wana wa Lea, aliomzalia Yakobo katika Padan-aramu, na Dina, binti yake. Nafsi zote za wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu. 16 Na wana wa Gadi; Sefoni, na Hagi, na Shuni, na Esboni, na Eri, na Arodi, na Areli. 17 Na wana wa Asheri; Imna, na Ishva, na Ishvi, na Beria, na Sera, umbu lao. Na wana wa Beria ni Heberi, na Malkieli. 18 Hao ndio wana wa Zilpa, ambaye Labani alimpa Lea, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao, nafsi kumi na sita. 19 Wana wa Raheli, mkewe Yakobo Yusufu na Benyamini. 20 Walizaliwa kwake Yusufu katika nchi ya Misri, Manase na Efraimu, aliomzalia Asenathi binti Potifera, kuhani wa Oni. 21 Na wana wa Benyamini; Bela, na Bekeri, na Ashbeli, na Gera, na Naamani, na Ehi, na Roshi, na Mupimu, na Hupimu, na Ardi. 22 Hao ndio wana wa Raheli, aliomzalia Yakobo, nafsi zote walikuwa kumi na wanne. 23 Na wana wa Dani; Hushimu. 24 Na wana wa Naftali; Yaseeli, na Guni, na Yaseri, na Shilemu. 25 Hao ndio wana wa Bilha, ambaye Labani alimpa Raheli, binti yake, naye akamzalia Yakobo hao; nafsi zote walikuwa saba. 26 Nafsi zote waliokuja pamoja na Yakobo mpaka Misri waliotoka viunoni mwake, bila wake za wanawe Yakobo, nafsi zote walikuwa sitini na sita. 27 Na wana wa Yusufu aliozaliwa katika Misri walikuwa nafsi wawili. Nafsi zote za nyumba ya Yakobo walioingia Misri walikuwa sabini. 28 Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. 29 Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake kitambo kizima. 30 Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai. 31 Yusufu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, Nitapanda mimi nimpashe Farao habari; nitamwambia, Ndugu zangu, na watu wa nyumbani mwa baba yangu, waliokuwa katika nchi ya Kanaani, wamenijia. 32 Na watu hao ni wachungaji, maana wamekuwa watu wa kuchunga wanyama, nao wameleta kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo. 33 Itakuwa Farao atakapowaita, na kuwauliza, Kazi yenu ni nini? 34 Semeni, Watumwa wako tumekuwa wachunga wanyama tangu ujana wetu, na hata leo, sisi, na baba zetu; mpate kukaa katika nchi ya Gosheni; maana kila mchunga wanyama ni chukizo kwa Wamisri.

Mwanzo 47

1 Ndipo Yusufu akaja akamwarifu Farao, akasema, Baba yangu, na ndugu zangu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo, wamekuja kutoka nchi ya Kanaani, nao wako katika nchi ya Gosheni. 2 Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao. 3 Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu. 4 Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni. 5 Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia; 6 nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu. 7 Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao. 8 Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi? 9 Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao. 10 Yakobo akambariki Farao, akatoka mbele ya Farao. 11 Yusufu akawakalisha babaye na nduguze, na kuwapa milki katika nchi ya Misri, katika mahali pazuri pa nchi, katika nchi ya Ramesesi, kama Farao alivyoamuru. 12 Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao. 13 Wala hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, hata nchi ya Misri, na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa. 14 Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao. 15 Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha. 16 Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha. 17 Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng'ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule. 18 Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu. 19 Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee. 20 Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao. 21 Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu. 22 Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao. 23 Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi. 24 Itakuwa wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu. 25 Wakasema, Umetulinda hai, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao. 26 Yusufu akaifanya sheria kwa habari ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao. 27 Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana. 28 Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi siku za miaka ya maisha yake Yakobo ilikuwa miaka mia moja na arobaini na saba. 29 Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri. 30 Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema. 31 Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda.

Mwanzo 48

1 Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako hawezi; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye. 2 Naye akaarifiwa Yakobo ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda. 3 Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki, 4 akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele. 5 Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni. 6 Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao. 7 Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrathi. Nikamzika katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu. 8 Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa? 9 Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki. 10 Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia. 11 Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionyesha na uzao wako pia. 12 Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi 13 Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye. 14 Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza. 15 Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo, 16 naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi. 17 Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase. 18 Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake. 19 Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa. 20 Akawabariki siku ile akasema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase. 21 Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu. 22 Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.

Mwanzo 49

1 Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho. 2 Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni Israeli, baba yenu. 3 Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. 4 Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu. 5 Simeoni na Lawi ni ndugu; Panga zao ni silaha za jeuri. 6 Nafsi yangu, usiingie katika siri yao, Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao, Maana katika ghadhabu yao walimuua mtu, Na kwa ukaidi wao walikata mshipa wa ng'ombe; 7 Ghadhabu yao na ilaaniwe, maana ilikuwa kali, Na hasira yao, maana ilikuwa haina huruma. Nitawagawa katika Yakobo, Nitawatawanya katika Israeli. 8 Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia. 9 Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha? 10 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii. 11 Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwana-punda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu. 12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa. 13 Zabuloni atakaa pwani ya bahari, Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu, Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni. 14 Isakari ni punda hodari, Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo; 15 Akaona mahali pa raha, kuwa pema, Na nchi, ya kuwa ni nzuri, Akainama bega lake lichukue mizigo, Akawa mtumishi kwa kazi ngumu. 16 Dani atahukumu watu wake, Kama moja ya makabila ya Israeli; 17 Dani atakuwa nyoka barabarani, Bafe katika njia, Aumaye visigino vya farasi, Hata apandaye ataanguka chali. 18 Wokovu wako nimeungoja, Ee Bwana. 19 Gadi, jeshi litamsonga, Lakini atawasonga wao mpaka visigino. 20 Asheri, chakula chake kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme. 21 Naftali ni ayala aliyefunguliwa; Anatoa maneno mazuri. 22 Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matwi yake yametanda ukutani. 23 Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamtupia, wakamwudhi, 24 Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye jiwe la Israeli, 25 Naam, kwa Mungu wa baba yako atakaye kusaidia; Kwa mibaraka ya mbinguni juu. Mibaraka ya vilindi vilivyo chini, Mibaraka ya maziwa, na ya mimba. 26 Mibaraka ya baba yako Imepita mibaraka ya milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliye mkuu kati ya ndugu zake. 27 Benyamini ni mbwa-mwitu mwenye kurarua-rarua Asubuhi atakula mawindo, Na jioni atagawanya mateka. 28 Hizo zote ndizo kabila za Israeli kumi na mbili. Na hayo ndiyo aliyowaambia baba yao, na kuwabariki; mmoja mmoja kwa mbaraka wake aliwabariki. 29 Akawaamuru, akasema, Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; 30 katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia. 31 Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea; 32 shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa wazawa wa Hethi. 33 Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake.

Mwanzo 50

1 Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu. 2 Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga, kwamba wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli. 3 Siku zake arobaini zikaisha, maana hivyo hutimizwa siku za kupaka dawa. Wamisri wakamlilia siku sabini. 4 Siku za kumlilia zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema, 5 Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi. 6 Farao akasema, Uende, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha. 7 Basi Yusufu akaenda amzike babaye, na watumwa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri. 8 Na nyumba yote ya Yusufu, na nduguze, na nyumba ya babaye; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, katika nchi ya Gosheni. 9 Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana. 10 Wakaja mpaka sakafu ya Atadi, iliyo ng'ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya babaye siku saba. 11 Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng'ambo ya Yordani. 12 Wanawe wakamfanyia kama alivyo waagiza; 13 kwa kuwa wanawe wakamchukuwa mpaka nchi ya Kanaani, nao wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia. 14 Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliyokwenda pamoja naye kumzika babaye, baada ya kumzika babaye. 15 Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. 16 Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, 17 Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. 18 Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. 19 Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu? 20 Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. 21 Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. 22 Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi Yusufu miaka mia na kumi. 23 Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. 24 Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. 25 Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. 26 Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

Kutoka 1

1 Basi majina ya wana wa Israeli walioingia Misri ni haya; kila mtu pamoja na jamaa zake walikuja pamoja na Yakobo. 2 Reubeni, na Simeoni na Lawi, na Yuda; 3 na Isakari, na Zabuloni, na Benyamini; 4 na Dani, na Naftali, na Gadi, na Asheri. 5 Na nafsi zile zote zilizotoka viunoni mwa Yakobo zilikuwa ni nafsi sabini; na huyo Yusufu alikuwa huko ndani ya Misri tangu hapo. 6 Yusufu akafa, na ndugu zake wote, na watu wote wa kizazi kile. 7 Na wana wa Israeli walikuwa na uzazi sana, na kuongezeka mno, na kuzidi kuwa wengi, nao wakaendelea na kuongezeka nguvu; na ile nchi ilikuwa imejawa na wao. 8 Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. 9 Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. 10 Haya! Na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, ikitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii. 11 Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. 12 Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. 13 Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; 14 wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. 15 Kisha mfalme wa Misri akasema na wazalisha wa Waebrania, mmoja jina lake aliitwa Shifra, na wa pili jina lake aliitwa Pua; 16 akasema, Wakati mwazalishapo wanawake wa Kiebrania na kuwaona wa katika kuzaa, ikiwa ni mtoto mwanamume, basi mwueni, bali ikiwa ni mtoto mwanamke, na aishi. 17 Lakini wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, wasifanye kama walivyoamriwa na huyo mfalme wa Misri, lakini wakawahifadhi hai wale wanaume. 18 Basi mfalme wa Misri akawaita wale wazalisha na kuwauliza, Kwa nini kufanya jambo hili, na kuwahifadhi watoto waume wawe hai? 19 Wazalisha wakamwambia Farao, Ni kwa sababu hao wanawake wa Kiebrania si kama wanawake wa Kimisri; kwa kuwa ni hodari hao, nao huzaa kabla mzalisha hajapata kuwafikilia. 20 Basi Mungu akawatendea mema wale wazalisha; na hao watu wakaongezeka sana, wakaendelea na kuzidi kuwa na nguvu nyingi. 21 Ilikuwa kwa sababu wale wazalisha walikuwa wakimcha Mungu, akawasimamishia nyumba. 22 Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai.

Kutoka 2

1 Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. 2 Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. 3 Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka sifa na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto. 4 Umbu lake mtoto akasimama mbali ili ajue yatakayompata. 5 Basi binti Farao akashuka, aoge mtoni, na vijakazi wake wakatembea kando ya mto; naye akakiona kile kisafina katika majani, akamtuma kijakazi wake kwenda kukileta. 6 Akakifungua, akamwona mtoto, na tazama, mtoto yule analia. Basi akamhurumia, akasema, Huyu ni mmojawapo wa watoto wa Waebrania. 7 Basi umbu lake mtoto akamwambia binti Farao, Je! Niende nikamwite mlezi katika wanawake wa Kiebrania, aje kwako, akunyonyeshee mtoto huyu? 8 Binti Farao akamwambia, Haya! Enenda. Yule kijana akaenda akamwita mama yake yule mtoto. 9 Binti Farao akamwambia, Mchukue mtoto huyu, ukaninyonyeshee, nami nitakupa mshahara wako. Yule mwanamke akamtwaa mtoto, akamnyonyesha. 10 Mtoto akakua, naye akamleta kwa binti Farao, akawa mwanawe. Akamwita jina lake Musa, akasema, Ni kwa sababu nalimtoa majini. 11 Hata siku zile, Musa alipokuwa mtu mzima, akatoka kuwaendea ndugu zake, akatazama mizigo yao. Akamwona Mmisri anampiga Mwebrania, mmojawapo wa ndugu zake. 12 Basi akatazama huko na huko, na alipoona ya kuwa hapana mtu, akampiga Mmisri yule, akamficha ndani ya mchanga. 13 Akatoka siku ya pili, na tazama, watu wawili wa Waebrania walikuwa wakipigana. Akamwambia yule aliyemdhulumu mwenzake, Mbona unampiga mwenzako? 14 Yule akasema, Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mkuu wetu, na mwamuzi juu yetu? Je! Wataka kuniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri? Musa akaogopa, akasema, Kumbe! Jambo lile limejulikana. 15 Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima. 16 Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao. 17 Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao. 18 Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo? 19 Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi. 20 Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula. 21 Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora. 22 Huyo akamzalia mwana, akamwita jina lake Gershomu, maana alisema, Nimekuwa mgeni katika nchi ya ugeni. 23 Hata baada ya siku zile nyingi mfalme wa Misri akafa; wana wa Israeli wakaugua kwa sababu ya ule utumwa, wakalia; kilio chao kikafika juu kwa Mungu kwa sababu ya ule utumwa. 24 Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. 25 Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia. Print this page Top | Next Chapter | Index | Home Full online version here [with search engine, multilingual display and audio Bible]

Kutoka 3

1 Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. 2 Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. 3 Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. 4 Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. 5 Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. 6 Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. 7 Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; 8 nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. 9 Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. 10 Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri. 11 Musa akamwambia Mungu, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? 12 Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. 13 Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, Jina lake n'nani? Niwaambie nini? 14 Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO;akasema,Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli;MIMI NIKO amenituma kwenu. 15 Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote. 16 Enenda, ukawakusanye wazee wa Israeli pamoja, ukawaambie, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenitokea, akaniambia, Hakika nimewajilieni, tena nimeyaona mnayotendewa huko Misri; 17 Nami nimesema, Nitawapandisha kutoka katika mateso ya Misri na kuwaingiza katika nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, nchi ijaayo maziwa na asali. 18 Nao watakusikia sauti yako; nawe utakwenda, wewe na wazee wa Israeli kwa mfalme wa Misri, na kumwambia, Bwana Mungu wa Waebrania, amekutana nasi; basi sasa twakuomba, tupe ruhusa twende mwendo siku tatu jangwani, ili tumtolee dhabihu Bwana Mungu wetu. 19 Nami najua ya kuwa huyo mfalme wa Misri hatawapa ruhusa mwende zenu, la, hata kwa mkono wa nguvu. 20 Nami nitaunyosha mkono wangu, na kuipiga Misri kwa ajabu zangu zote, nitakazofanya kati yake, kisha baadaye atawapa ruhusa kwenda. 21 Nami nitawapa watu hao kufadhiliwa mbele ya Wamisri; hata itakuwa, hapo mtakapokwenda zenu hamtakwenda kitupu; 22 Lakini kila mwanamke ataomba kwa jirani, na kwa huyo akaaye naye nyumbani, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi; nanyi mtawavika wana wenu na binti zenu; nanyi mtawateka nyara Wamisri.

Kutoka 4

1 Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, Bwana hakukutokea. 2 Bwana akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. 3 Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. 4 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;) 5 ili kwamba wapate kusadiki ya kwamba Bwana, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amekutokea. 6 Bwana akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! Mkono wake ulikuwa una ukoma, umekuwa mweupe kama theluji. 7 Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake. 8 Basi itakuwa, wasipokusadiki, wala kuisikiliza sauti ya ishara ya kwanza, wataisikiliza sauti ya ishara ya pili. 9 Kisha itakuwa wasipoamini hata ishara hizo mbili, wala kuisikiliza sauti yako, basi, yatwae maji ya mtoni uyamwage juu ya nchi kavu, na yale maji uyatwaayo mtoni yatakuwa damu juu ya nchi kavu. 10 Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. 11 Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana? 12 Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena. 13 Akasema, Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake huyo utakayemtuma. 14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Najua ya kuwa yeye aweza kusema vizuri. Pamoja na hayo, tazama, anakuja kukulaki; naye atakapokuona, atafurahi moyoni mwake. 15 Nawe utasema naye, na kuyatia maneno kinywani mwake; nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayofanya. 16 Naye atakuwa msemaji wako kwa watu, hata yeye atakuwa mfano wa kinywa kwako, nawe utakuwa mfano wa Mungu kwake. 17 Nawe utatwaa fimbo hii mkononi mwako, na kwa hiyo utazifanya zile ishara. 18 Basi Musa akaenda na kurejea kwa Yethro mkwewe, na kumwambia, Nipe ruhusa niende, nakusihi, niwarudie hao ndugu zangu walioko Misri, nipate kuwaona kwamba wako hai hata sasa. Yethro akamwambia Musa, Haya, nenda kwa amani. 19 Bwana akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa. 20 Basi Musa akamchukua mkewe na wanawe, na kuwapandisha juu ya punda, naye akarudi mpaka nchi ya Misri; na Musa akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake. 21 Bwana akamwambia Musa, Hapo utakaporudi Misri, angalia ukazifanye mbele ya Farao zile ajabu zote nilizozitia mkononi mwako; lakini nitaufanya mgumu moyo wake, naye hatawapa ruhusa hao watu waende zao. 22 Nawe umwambie Farao, Bwana asema hivi, Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu; 23 nami nimekuambia, Mpe mwanangu ruhusa aende, ili apate kunitumikia, nawe umekataa kumpa ruhusa aende; angalia basi, mimi nitamwua mwanao, mzaliwa wa kwanza wako. 24 Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, Bwana akakutana naye akataka kumwua. 25 Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema. Hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi. 26 Basi akamwacha. Ndipo huyo mkewe akanena, U bwana arusi wa damu wewe, kwa ajili ya kutahiri. 27 Bwana akamwambia Haruni, Nenda jangwani uonane na Musa. Naye akaenda, akamkuta katika mlima wa Mungu, akambusu. 28 Musa akamwambia Haruni hayo maneno yote ya Bwana ambayo alimtuma aende nayo, na ishara hizo zote alizomwagiza. 29 Musa na Haruni wakaenda, wakawakusanya wazee wote wa watu wa Israeli. 30 Haruni akawaambia maneno yote Bwana aliyonena na Musa akazifanya zile ishara mbele ya watu. 31 Watu wakaamini, na waliposikia ya kuwa Bwana amewajilia wana wa Israeli, na ya kuwa ameyaona mateso yao, wakainama vichwa vyao wakasujudu.

Kutoka 5

1 Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani. 2 Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao. 3 Wakasema, Mungu wa Waebrania amekutana nasi; twakuomba, tupe ruhusa twende safari ya siku tatu jangwani, tumtolee dhabihu Bwana, Mungu wetu; asije akatupiga kwa tauni, au kwa upanga. 4 Mfalme wa Misri akawaambia Enyi Musa na Haruni, mbona mnawaachisha watu kazi zao? Enendeni zenu kwa mizigo yenu. 5 Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha, wasichukue mizigo yao. 6 Na siku ile ile Farao akawaamuru wasimamizi wa watu, na wanyapara wao, akisema, 7 Msiwape watu tena majani ya kufanyia matofali, kama mlivyofanya tangu hapo; na waende wakatafute majani wenyewe. 8 Lakini hesabu ya matofali waliyokuwa wakifanya tokea hapo, wawekeeni iyo hiyo, msiipunguze hata kidogo, kwa maana ni wavivu hao; kwa hiyo wanapiga kelele, wakisema, Tupe ruhusa twende kumtolea Mungu wetu dhabihu. 9 Wapeni watu hao kazi nzito zaidi, waitaabikie; wala wasiangalie maneno ya uongo. 10 Hao wasimamizi wa watu na wanyapara wao wakatoka, wakasema na watu, wakanena, Farao asema hivi, Mimi siwapi majani. 11 Enendeni wenyewe, jipatieni majani hapo mtakapoyaona; kwa maana kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo. 12 Basi hao watu wakatawanyika katika nchi yote ya Misri ili wapate kukusanya matakataka ya mashamba badala ya majani. 13 Wasimamizi wao wakawahimiza, wakisema, Timizeni kazi zenu, shughuli zenu za kila siku, kama wakati ule majani yalipokuwapo. 14 Na wanyapara wa wana wa Israeli, ambao wasimamizi wa Farao wamewaweka juu yao, wakapigwa, wakiambiwa, Kwa nini hamkutimiza kazi yenu jana na leo; kwa kufanya matofali kama hapo kwanza? 15 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaenda, wakamlilia Farao, wakisema, Mbona umetutendea hivi, sisi watumwa wako? 16 Watumwa wako hawapewi majani, nao wanatuambia, Fanyeni matofali; na tazama, watumwa wako wapigwa; lakini kosa hilo ni la watu wako mwenyewe. 17 Akasema, Wavivu ninyi; wavivu; kwa ajili hii mwasema, Tupe ruhusa twende kumtolea Bwana dhabihu. 18 Basi, enendeni sasa, mkafanye kazi; kwa maana hamtapewa majani, na pamoja na hayo mtaleta hesabu ile ile ya matofali. 19 Basi wanyapara wa wana wa Israeli wakaona ya kwamba wa katika hali mbaya, walipoambiwa, Hamtapunguza hesabu ya matofali yenu hata kidogo; ndizo shughuli zenu za kila siku. 20 Wakakutana na Musa na Haruni, waliokuwa wanasimama njiani, hapo walipotoka kwa Farao; 21 wakawaambia, Bwana awaangalie na kuamua; kwa kuwa mmefanya harufu yetu kuwa chukizo mbele ya Farao, na mbele ya watumishi wake, mkatia upanga mikononi mwao, watuue. 22 Musa akarudi kwa Bwana, akasema, Bwana, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi? 23 Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo.

Kutoka 6

1 Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. 2 Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; 3 nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. 4 Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. 5 Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. 6 Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; 7 nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. 8 Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA. 9 Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu. 10 Bwana akasema na Musa, akamwambia, 11 Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake. 12 Musa akanena mbele ya Bwana, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara? 13 Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri. 14 Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni. 15 Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni. 16 Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, sawasawa na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. 17 Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, sawasawa na jamaa zao. 18 Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na mitatu. 19 Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi sawasawa na vizazi vyao. 20 Huyo Amramu akamwoa Yokebedi ndugu ya baba yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. 21 Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri. 22 Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri. 23 Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, umbu lake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. 24 Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora. 25 Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi sawasawa na jamaa zao. 26 Hawa ni Haruni ye yule, na Musa ye yule, Bwana aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao. 27 Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa ye yule, na Haruni ye yule. 28 Ilikuwa siku hiyo Bwana aliponena na Musa katika nchi ya Misri, 29 Bwana akamwambia Musa, akasema, Mimi ni Bwana; mwambie Farao mfalme wa Misri maneno yote nikuambiayo. 30 Musa akanena mbele ya Bwana, Mimi ni mtu mwenye midomo isiyo tohara, Farao atanisikizaje?

Kutoka 7

1 Bwana akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. 2 Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. 3 Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. 4 Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. 5 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. 6 Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama Bwana alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. 7 Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. 8 Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaambia, 9 Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. 10 Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama Bwana alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. 11 Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. 12 Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. 13 Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama Bwana alivyonena. 14 Bwana akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. 15 Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. 16 Nawe umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. 17 Bwana asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi Bwana; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. 18 Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. 19 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. 20 Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama Bwana alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. 21 Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. 22 Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama Bwana alivyonena. 23 Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. 24 Wamisri wote wakachimba-chimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. 25 Zikatimia siku saba, baada ya Bwana kuupiga ule mto.

Kutoka 8

1 Bwana akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, Bwana asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia. 2 Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura; 3 na huo mto utafurika vyura, nao watakwea juu na kuingia ndani ya nyumba yako, na ndani ya chumba chako cha kulala, na juu ya kitanda chako, na ndani ya nyumba ya watumishi wako, na juu ya watu wako, na ndani ya meko yako, na ndani ya vyombo vyako vya kukandia unga. 4 Kisha hao vyura watakwea juu yako wewe, na juu ya watu wako, na juu ya watumishi wako wote. 5 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri. 6 Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri. 7 Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri. 8 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu. 9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu. 10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu. 11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu. 12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao. 13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba. 14 Wakawakusanya chungu chungu; na nchi ikatoa uvundo. 15 Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama Bwana alivyonena. 16 Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri. 17 Nao wakafanya; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri. 18 Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama. 19 Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni chanda cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama Bwana alivyonena. 20 Bwana akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, Bwana asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi. 21 Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta wingi wa mainzi juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na wingi wa mainzi, na nchi nayo ambayo wa juu yake. 22 Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao mainzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi Bwana kati ya dunia. 23 Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho. 24 Bwana akafanya; wakaja wingi wa mainzi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa kwa ajili ya wale mainzi. 25 Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii. 26 Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka Bwana, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe? 27 La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu Bwana, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza. 28 Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu Bwana, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni. 29 Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba Bwana ili hao mainzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia Bwana dhabihu. 30 Musa akatoka kwa Farao, akamwomba Bwana. 31 Bwana akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale mainzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja. 32 Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.

Kutoka 9

1 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao, umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, yuasema, Wape ruhusa watu wangu ili waende wanitumikie. 2 Kwani ukikataa kuwapa ruhusa waende, na kuzidi kuwazuia, 3 tazama, mkono wa Bwana u juu ya wanyama wako wa mifugo walioko kondeni, juu ya farasi, na juu ya punda, na juu ya ngamia, na juu ya ng'ombe, na juu ya kondoo; kutakuwa na tauni nzito sana. 4 Kisha Bwana atawatenga wanyama wa Israeli na wanyama wa Misri; wala hakitakufa kitu cho chote cha wana wa Israeli. 5 Naye Bwana akaweka muda, akasema, Kesho Bwana atalifanya jambo hili katika nchi. 6 Bwana akalifanya jambo hilo siku ya pili, na wanyama wote wa kufugwa wa Misri wakafa; lakini katika wanyama wa wana wa Israeli hakufa hata mmoja. 7 Farao akatuma watu, na tazama, hapana mmoja aliyekufa katika wanyama wa wana wa Israeli. Lakini moyo wa Farao ulikuwa mzito, wala hakuwapa hao watu ruhusa waende zao. 8 Bwana akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuuni, kisha Musa na ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao. 9 Nayo yatakuwa ni mavumbi membamba juu ya nchi yote ya Misri, nayo yatakuwa majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama, katika nchi yote ya Misri. 10 Basi wakatwaa majivu ya tanuuni, na kusimama mbele ya Farao; na Musa akayarusha juu mbinguni nayo yakawa ni majipu yenye kufura na kutumbuka juu ya wanadamu na juu ya wanyama. 11 Nao wale waganga hawakuweza kusimama mbele ya Musa kwa sababu ya hayo majipu, kwa maana hao waganga walikuwa na majipu, na Wamisri wote walikuwa nayo. 12 Bwana akaufanya mgumu moyo wa Farao, asiwasikize; vile vile kama Bwana alivyomwambia Musa. 13 Bwana akamwambia Musa, Ondoka asubuhi na mapema, ukasimame mbele ya Farao, umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema, Wape watu wangu ruhusa waende ili wanitumikie. 14 Kwani wakati huu nitaleta mapigo yangu yote juu ya moyo wako, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako; ili upate kujua ya kuwa hapana mmoja mfano wa mimi ulimwenguni mwote. 15 Kwa kuwa wakati huu ningekwisha kuunyosha mkono wangu, na kukupiga wewe na watu wako, kwa tauni, nawe ungekatiliwa mbali na kuondolewa katika nchi; 16 lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. 17 Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao? 18 Tazama, kesho wakati kama huu, nitanyesha mvua ya mawe nzito sana, ambayo mfano wake haujakuwa huko Misri tangu siku ile ilipoanza kuwa hata hivi sasa. 19 Basi sasa tuma wahimize waingie ndani wanyama wako na hayo yote uliyo nayo mashambani; kwani kila mtu na kila mnyama apatikanaye mashambani, wasioletwa nyumbani, hiyo mvua ya mawe itanyesha juu yao, nao watakufa. 20 Yeye aliyelicha neno la Bwana miongoni mwa watumishi wa Farao aliwakimbiza watumishi wake na wanyama wake waingie nyumbani; 21 na yeye asiyelitia moyoni neno la Bwana akawaacha watumishi wake na wanyama wake mashambani. 22 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, ili iwe mvua ya mawe katika nchi yote ya Misri, juu ya wanadamu na juu ya wanyama, na juu ya mboga zote za mashamba, katika nchi yote ya Misri. 23 Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; na Bwana akaleta ngurumo na mvua ya mawe, na moto ukashuka juu ya nchi; Bwana akanyesha mvua ya mawe juu ya nchi yote ya Misri. 24 Basi palikuwa na mvua ya mawe, na moto uliochanganyikana na ile mvua ya mawe, nzito sana, ambayo mfano wake haukuwapo katika nchi yote ya Misri tangu ilipoanza kuwa taifa. 25 Na ile mvua ya mawe ikapiga kila kilichokuwako mashambani, binadamu na mnyama, katika nchi yote ya Misri; hiyo mvua ya mawe ikapiga kila mmea wa mashambani, na kuuvunja kila mti wa mashamba. 26 Katika nchi ya Gosheni peke yake, walikokaa wana wa Israeli, haikuwako mvua ya mawe. 27 Farao akatuma watu, na kuwaita Musa na Haruni, na kuwaambia, Mimi nimekosa wakati huu; Bwana ni mwenye haki, na mimi na watu wangu tu waovu. 28 Mwombeni Bwana; kwa kuwa zimekuwa za kutosha ngurumo hizo kuu na hii mvua ya mawe; nami nitawapa ninyi ruhusa mwende zenu, msikae zaidi. 29 Musa akamwambia, Mara nitakapotoka mjini nitamwinulia Bwana mikono yangu; na hizo ngurumo zitakoma, wala haitanyesha mvua ya mawe tena; ili upate kujua ya kuwa dunia hii ni ya Bwana. 30 Lakini, wewe na watumishi wako, najua ya kuwa ninyi hamtamcha Bwana Mungu bado. 31 Kitani na shayiri zilipigwa; maana shayiri zilikuwa na masuke na kitani zilikuwa katika kutoa maua. 32 Lakini ngano na kusemethu hazikupigwa; maana, zilikuwa hazijakua bado. 33 Musa akatoka mjini, kutoka kwa Farao, akamwinulia Bwana mikono yake; na zile ngurumo na ile mvua ya mawe zikakoma, wala mvua haikunyesha juu ya nchi. 34 Farao alipoona ya kwamba mvua na mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akazidi kufanya dhambi, na kuufanya moyo wake mzito, yeye na watumishi wake. 35 Moyo wa Farao ukawa ni mgumu naye hakuwapa wana wa Israeli ruhusa waende zao; kama Bwana alivyonena kwa kinywa cha Musa.

Kutoka 10

1 Bwana akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao; kwa kuwa mimi nimeufanya moyo wake mzito, nipate kuzionyesha ishara zangu hizi kati yao; 2 nawe upate kusema masikioni mwa mwanao, na masikioni mwa mjukuu wako, ni mambo gani niliyotenda juu ya Misri, na ishara zangu nilizozifanya kati yao; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana. 3 Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, na kumwambia, Bwana, Mungu wa Waebrania, asema hivi, Je! Utakataa hata lini kujinyenyekeza mbele zangu? Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie. 4 Au, kwamba wakataa kuwapa hao watu wangu ruhusa waende zao, tazama, kesho nitaleta nzige waingie ndani ya mipaka yako; 5 nao wataufunika uso wa nchi, mtu asipate kuona hiyo nchi; nao watakula mabaki ya hayo yaliyopona yaliyowasalia baada ya ile mvua ya mawe, watakula kila mti umeao kwa ajili yenu mashambani; 6 na nyumba zako, na nyumba za watumishi wako, na nyumba za Wamisri wote zitajawa na nzige; mfano wake baba zako wala baba za baba zako hawakuona, tangu siku walipoanza kuwapo juu ya nchi hata hivi leo. Basi akageuka na kutoka kwa Farao. 7 Ndipo watumishi wa Farao wakamwambia, Mtu huyu atakuwa tanzi kwetu sisi hata lini? Wape hawa watu ruhusa waende zao, wamtumikie Bwana, Mungu wao; hujatambua bado ya kuwa Misri imekwisha haribika? 8 Musa na Haruni wakaletwa tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie Bwana, Mungu wenu; lakini ni kina nani watakaokwenda? 9 Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia Bwana sikukuu. 10 Lakini akawaambia, Ehe, Bwana na awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu; angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. 11 Sivyo; endeni ninyi mlio watu wazima, mkamtumikie Bwana; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni pa Farao. 12 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya nchi ya Misri kwa hao nzige, ili wakwee juu ya nchi ya Misri, waile mimea yote ya nchi, yaani, vyote vilivyosazwa na ile mvua ya mawe. 13 Basi Musa akainyosha fimbo yake juu ya nchi ya Misri, na Bwana akaleta upepo kutoka mashariki juu ya nchi, mchana kutwa, na usiku kucha; kulipopambazuka ule upepo wa mashariki ukawaleta nzige. 14 Na hao nzige wakakwea juu ya nchi yote ya Misri, wakatua ndani ya mipaka yote ya Misri, walikuwa wabaya mno; hawajakuwapo nzige kama hao majira yo yote, wala baada yao hawatakuwa wengine jinsi hiyo. 15 Kwa kuwa waliufunika uso wote wa nchi, hata nchi iliingia giza; wakala mimea yote ya nchi, na matunda yote ya miti yaliyosazwa na ile mvua ya mawe; hapakusalia hata jani moja, mti wala mmea wa mashamba, katika nchi yote ya Misri. 16 Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni haraka; akasema, Nimemfanyia dhambi Bwana, Mungu wenu na ninyi pia. 17 Basi sasa, nawasihi, nisameheni dhambi yangu mara hii moja tu, mkamwombe Bwana, Mungu wenu, aniondolee kifo hiki tu. 18 Akatoka kwa Farao, na kumwomba Bwana. 19 Bwana akaugeuza upepo wa magharibi wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka katika Bahari ya Shamu; hakusalia hata nzige mmoja ndani ya mipaka yote ya Misri. 20 Lakini Bwana akaufanya ule moyo wa Farao uwe mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa waende zao. 21 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani. 22 Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu; 23 hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao. 24 Farao akamwita Musa, na kumwambia, Haya, nendeni, mkamtumikie Bwana; kondoo zenu na ng'ombe zenu tu na waachwe; watoto wenu nao na waende pamoja nanyi. 25 Musa akasema, Ni lazima utupe mikononi mwetu na wanyama wa dhabihu na wa sadaka za kuteketezwa, ili tupate kumchinjia Bwana Mungu wetu dhabihu. 26 Makundi yetu pia watakwenda pamoja nasi; hautasalia nyuma hata ukwato mmoja; kwa maana inampasa kutwaa katika hao tupate kumtumikia Bwana, Mungu wetu; nasi hatujui, hata tutakapofika huko, ni kitu gani ambacho kwa hicho inatupasa kumtumikia Bwana. 27 Lakini Bwana akaufanya kuwa mgumu moyo wa Farao, asikubali kuwapa ruhusa waende zao. 28 Farao akamwambia Musa, Nenda zako, ujiangalie, usinione uso tena; kwani siku hiyo utakayoniangalia uso wangu utakufa. 29 Musa akasema, Umenena vema; mimi sitakuangalia uso wako tena.

Kutoka 11

1 Bwana akamwambia Musa, Liko pigo moja bado, nitakaloleta juu ya Farao na juu ya Misri; baadaye atawapa ninyi ruhusa mtoke huku; naye hapo atakapowapa ruhusa, atawafukuza mtoke huku kabisa kabisa. 2 Basi nena wewe masikioni mwa watu hawa, na kila mtu mume na atake kwa jirani yake, na kila mwanamke atake kwa jirani yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu. 3 Bwana akawapa watu hao kibali machoni pa Wamisri. Zaidi ya hayo, huyo Musa alikuwa ni mkuu sana katika nchi ya Misri, machoni pa watumishi wa Farao, na machoni pa watu wake. 4 Musa akasema, Bwana asema hivi, Kama usiku wa manane mimi nitatoka nipite kati ya Misri; 5 na wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri watakufa, tangu yule mzaliwa wa kwanza wa Farao aketiye katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa huyo kijakazi aliye pale nyuma ya jiwe la kusagia; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. 6 Ndipo kutakuwa na kilio kikuu katika nchi yote ya Misri, ambacho mfano wake haujakuwa bado majira yo yote, wala hautakuwako mfano wake tena kabisa. 7 Lakini katika wana wa Israeli hapana hata mbwa atakayetoa ulimi juu yao, juu ya mtu wala juu ya mnyama; ili kwamba mpate kujua jinsi Bwana anavyowatenga Wamisri na Waisraeli. 8 Tena hao watumishi wako wote watanitelemkia kwangu mimi, nao watanisujudia, wakisema, Toka wewe, na hawa watu wote wakufuatao; na baada ya hayo nitatoka. Basi akatoka kwa Farao na hasira kuu. 9 Bwana akamwambia Musa, Farao hatawasikiza ninyi; kusudi ajabu zangu ziongezeke katika nchi ya Misri. 10 Musa na Haruni walifanya ajabu hizo zote mbele ya Farao; Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, asiwape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake.

Kutoka 12

1 Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, 2 Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. 3 Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; 4 na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. 5 Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. 6 Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. 7 Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. 8 Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. 9 Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. 10 Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. 11 Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. 12 Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. 13 Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. 14 Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele 15 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli. 16 Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu. 17 Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele. 18 Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni. 19 Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi. 20 Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote. 21 Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka. 22 Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. 23 Kwa kuwa Bwana atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, Bwana atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi. 24 Nanyi mtalitunza jambo hili kuwa ni amri kwako na kwa wanao milele. 25 Itakuwa hapo mtakapoifikilia hiyo nchi, Bwana atakayowapa, kama alivyoahidi, ndipo mtakapoushika utumishi huu. 26 Kisha itakuwa, hapo watoto wenu watakapowauliza, N'nini maana yake utumishi huu kwenu? 27 Ndipo mtawaambia, Ni dhabihu ya pasaka ya Bwana, kwa kuwa alipita juu ya nyumba za wana wa Israeli huko Misri, hapo alipowapiga Wamisri, akaziokoa nyumba zetu. Hao watu wakainama vichwa na kusujudia. 28 Basi wana wa Israeli wakaenda na kufanya mambo hayo; vile vile kama Bwana alivyowaamuru Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya. 29 Hata ikawa, usiku wa manane Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, tangu mzaliwa wa kwanza wa Farao aliyeketi katika kiti chake cha enzi, hata mzaliwa wa kwanza wa mtu aliyefungwa katika nyumba ya wafungwa; na wazaliwa wa kwanza wote wa wanyama. 30 Farao akaondoka usiku, yeye na watumishi wake wote, na Wamisri wote; pakawa na kilio kikuu katika Misri; maana hapakuwa na nyumba hata moja asimokufa mtu. 31 Akawaita Musa na Haruni usiku, akasema, Ondokeni tokeni katika watu wangu, ninyi na wana wa Israeli; enendeni, kamtumikieni Bwana kama mlivyosema. 32 Twaeni kondoo zenu na ng'ombe zenu kama mlivyosema, enendeni zenu, mkanibariki mimi pia. 33 Wamisri nao wakawahimiza watu, kuwatoa katika nchi kwa haraka, maana walisema, Tumekwisha kufa sote. 34 Watu wakauchukua unga wa mikate yao kabla haijatiwa chachu, na vyombo vyao vya kukandia wakavitia ndani ya nguo zao mabegani. 35 Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. 36 Bwana akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka. Nao wakawateka Wamisri nyara. 37 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi mpaka Sukothi, walipata hesabu yao kama watu sita mia elfu watu waume waliokwenda kwa miguu, bila kuhesabu watoto. 38 Na kundi kubwa la watu waliochangamana mno wakakwea pamoja nao; na kondoo na ng'ombe, wanyama wengi sana. 39 Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. 40 Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini. 41 Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya Bwana yalitoka nchi ya Misri. 42 Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za Bwana kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa Bwana, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao. 43 Bwana akawaambia Musa na Haruni, Amri ya pasaka ni hii; mtu mgeni asimle; 44 lakini mtumishi wa mtu awaye yote aliyenunuliwa kwa fedha, ukiisha kumtahiri, ndipo hapo atamla pasaka. 45 Akaaye kwenu hali ya ugeni, na mtumishi aliyeajiriwa, wasimle pasaka. 46 Na aliwe ndani ya nyumba moja; usiichukue nje ya nyumba nyama yake yo yote; wala msivunje mfupa wake uwao wote. 47 Na wafanye jambo hili mkutano wa Israeli wote. 48 Na mgeni atakapoketi pamoja nawe, na kupenda kumfanyia Bwana pasaka, waume wake wote na watahiriwe, ndipo hapo akaribie na kufanya pasaka; naye atakuwa mfano mmoja na mtu aliyezaliwa katika nchi; lakini mtu ye yote asiyetahiriwa asimle. 49 Sheria ni hiyo moja kwa mtu aliyezaliwa kwenu, na kwa mgeni akaaye kati yenu ugenini. 50 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli wote; kama Bwana alivyowaagiza Musa na Haruni, ndivyo walivyofanya. 51 Ilikuwa siku ile ile moja, Bwana akawatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri kwa majeshi yao.

Kutoka 13

1 Bwana akasema na Musa, akamwambia, 2 Nitakasie mimi wazaliwa wa kwanza wote, kila afunguaye tumbo katika wana wa Israeli, wa binadamu na wa mnyama; ni wangu huyo. 3 Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa Bwana aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa. 4 Ninyi mwatoka leo katika mwezi wa Abibu. 5 Itakuwa hapo Bwana atakapowaleta mpaka nchi ya Wakanaani, na Wahiti, na Waamori, na Wahivi, na Wayebusi, nchi hiyo aliyowaapia baba zako kwamba atakupa wewe, ni nchi imiminikayo maziwa na asali, ndipo mtakapoushika utumishi huu katika mwezi huu. 6 Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba, nayo siku ya saba itakuwa ni sikukuu ya Bwana. 7 Mikate isiyochachwa italiwa katika hizo siku saba; mkate uliotiwa chachu usionekane kwako, wala chachu isionekane kwako, ndani ya mipaka yako yote. 8 Nawe utamwambia mwanao siku hiyo, ukisema, Ni kwa sababu ya hayo Bwana aliyonifanyia hapo nilipotoka Misri. 9 Nayo itakuwa ishara kwako katika mkono wako, na kwa ukumbusho kati ya macho yako, ili kwamba sheria ya Bwana ipate kuwa kinywani mwako; kwani Bwana alikutoa utoke Misri kwa mkono wenye uwezo. 10 Kwa hiyo utaitunza amri hii kwa wakati wake mwaka baada ya mwaka. 11 Itakuwa hapo Bwana atakapokuleta katika nchi ya Wakanaani, kama alivyokuapia wewe na baba zako, na kukupa, 12 ndipo utamwekea Bwana kila afunguaye tumbo, na kila mzaliwa wa kwanza uliye naye, azaliwaye na mnyama; hao waume watakuwa ni wa Bwana. 13 Kila mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; na kwamba hutaki kumkomboa, utamvunja shingo; na kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu katika wanao utamkomboa. 14 Kisha itakuwa hapo mwanao atakapokuuliza keshoni, akisema, Ni nini hivi? Utamwambia, Bwana alimtoa Misri, kutoka ile nyumba ya utumwa, kwa uwezo wa mkono wake; 15 basi ilikuwa hapo Farao alipojifanya kuwa mgumu ili asitupe ruhusa kuondoka, Bwana akawapiga wazaliwa wa kwanza wote waliokuwa katika nchi ya Misri, wa binadamu na wa mnyama; kwa ajili ya hayo namtolea Bwana wote wafunguao tumbo, wakiwa waume; lakini wazaliwa wa kwanza wote wa wana wangu nawakomboa. 16 Jambo hilo litakuwa ni ishara mkononi mwako, na utepe katikati ya macho yako; kwa kuwa Bwana alitutoa Misri kwa uwezo wa mkono wake. 17 Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; 18 lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. 19 Musa akaichukua ile mifupa ya Yusufu pamoja naye; maana, alikuwa amewaapisha sana wana wa Israeli, akisema, Mungu hana budi atawajilia ninyi; nanyi mtaichukua mfupa yangu kutoka hapa pamoja nanyi. 20 Nao wakasafiri kutoka Sukothi, wakapiga kambi Ethamu, kwenye mpaka wa ile jangwa. 21 Bwana naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru; wapate kusafiri mchana na usiku; 22 ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu.

Kutoka 14

1 Bwana akasema na Musa, akamwambia, 2 Waambie wana wa Israeli, kwamba warudi na kupiga kambi yao mbele ya Pi-hahirothi, kati ya Migdoli na bahari, kukabili Baal-sefoni; mtapanga mbele yake karibu na bahari. 3 Naye Farao atasema katika habari za wana wa Israeli, Wametatanishwa katika nchi, ile jangwa imewazuia wasitoke. 4 Nami nitaufanya uwe mgumu moyo wa Farao, naye atafuata nyuma yao; nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote; na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana. Basi wakafanya hivyo. 5 Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? 6 Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; 7 tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari yote ya Wamisri, na maakida juu ya magari hayo yote. 8 Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. 9 Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. 10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. 11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? 12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. 13 Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. 14 Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. 15 Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. 16 Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. 17 Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. 18 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake. 19 Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao; 20 ikafika kati ya jeshi la Misri na jeshi la Israeli; napo palikuwa na lile wingu na lile giza, lakini lilitoa nuru wakati wa usiku; na hawa hawakuwakaribia hawa usiku kucha. 21 Musa; akanyosha mkono wake juu ya bahari; Bwana akaifanya bahari irudi nyuma kwa upepo wa nguvu utokao mashariki, usiku kucha, akaifanya bahari kuwa nchi kavu, maji yakagawanyika. 22 Wana wa Israeli wakaenda ndani kati ya bahari katika nchi kavu; nayo maji yalikuwa ukuta kwao mkono wa kuume, na mkono wa kushoto. 23 Na wale Wamisri wakawafuatia, wakaingia ndani kati ya bahari, farasi zote za Farao, na magari yake, na wapanda farasi wake. 24 Ikawa katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. 25 Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri. 26 Bwana akamwambia Musa, Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi tena juu ya Wamisri, juu ya magari yao, na juu ya farasi zao. 27 Musa akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka, bahari ikarudi kwa nguvu zake; Wamisri wakakimbia mbele yake; na Bwana akawakukutia mbali hao Wamisri kati ya bahari. 28 Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja. 29 Lakini wana wa Israeli wakaenda katika nchi kavu katikati ya bahari; na hayo maji yalikuwa ni kuta upande wao wa kuume, na upande wao wa kushoto. 30 Ndivyo Bwana alivyowaokoa Israeli siku ile mikononi mwa Wamisri; Waisraeli wakawaona Wamisri ufuoni kwa bahari, wamekufa. 31 Israeli akaiona ile kazi kubwa aliyoifanya Bwana juu ya Wamisri, ndipo hao watu wakamcha Bwana, wakamwamini Bwana, na Musa mtumishi wake.

Kutoka 15

1 Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 2 Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu; Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza. 3 Bwana ni mtu wa vita, Bwana ndilo jina lake. 4 Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. 5 Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe. 6 Bwana, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, Bwana, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui. 7 Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokuondokea, Wapeleka hasira yako, nayo huwateketeza kama mabua makavu. 8 Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa, Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa chungu, Vilindi vikagandamana ndani ya moyo wa bahari. 9 Adui akasema, Nitafuatia, nitapata, nitagawanya nyara, Nafsi yangu itashibishwa na wao; Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza. 10 Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza; Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu. 11 Ee Bwana, katika miungu ni nani aliye kama wewe? Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu, Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu? 12 Ulinyosha mkono wako wa kuume, Nchi ikawameza. 13 Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa, Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu. 14 Kabila za watu wamesikia, wanatetemeka, Wakaao Ufilisti utungu umewashika. 15 Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa, Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata, Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka. 16 Hofu na woga umewaangukia; Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe; Hata watakapovuka watu wako, Ee Bwana, Hata watakapovuka watu wako uliowanunua. 17 Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono yako. 18 Bwana atatawala milele na milele. 19 Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari. 20 Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza. 21 Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. 22 Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji. 23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 24 Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini? 25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko; 26 akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye. 27 Wakafikilia Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapanga hapo, karibu na maji.

Kutoka 16

1 Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. 2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung'unikia Musa na Haruni, huko barani; 3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote. 4 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. 5 Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. 6 Musa na Haruni wakawaambia wana wote wa Israeli, Jioni ndipo mtakapojua ya kuwa Bwana amewaleta kutoka nchi ya Misri; 7 na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wa Bwana; kwa kuwa yeye asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia Bwana; na sisi tu nani, hata mkatunung'unikia? 8 Musa akasema, Ndilo litakalokuwa, hapo Bwana atakapowapa nyama wakati wa jioni mle, na asubuhi mikate hata mkakinai; kwa kuwa Bwana asikia manung'uniko yenu mliyomnung'unikia yeye; na sisi tu nani? Manung'uniko yenu hayakuwa juu yetu sisi, ila juu ya Bwana. 9 Musa akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli, Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa kuwa yeye ameyasikia manung'uniko yenu. 10 Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli, wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwana ukaonekana katika hilo wingu. 11 Bwana akasema na Musa, akinena, 12 Nimeyasikia manung'uniko ya wana wa Israeli; haya sema nao, ukinena, Wakati wa jioni mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 13 Ikawa wakati wa jioni, kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa juu ya nchi pande zote za kituo. 14 Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. 15 Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa ninyi, mle. 16 Neno hili ndilo aliloagiza Bwana, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi,kama hesabu ya watu wenu ilivyo ;ndivyo mtakavyotwaa,kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake. 17 Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua. 18 Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa. 19 Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi. 20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana. 21 Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka. 22 Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. 23 Akawaambia, Ndilo neno alilonena Bwana Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa Bwana; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi. 24 Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu. 25 Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani. 26 Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. 27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. 28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? 29 Angalieni, kwa kuwa Bwana amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. 30 Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba. 31 Na nyumba ya Israeli wakakiita jina lake Mana; nacho kilikuwa mfano wa chembe za mtama, nyeupe; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya maandazi membamba yaliyoandaliwa kwa asali. 32 Musa akasema, Hili ni neno Bwana aliloliamuru, Pishi moja ya kitu hicho na kiwekwe kwa ajili ya vizazi vyenu; ili kwamba wao wapate kukiona kile chakula nilichowalisha ninyi barani, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri. 33 Basi Musa akamwambia Haruni, Twaa kopo, ukatie pishi moja ya hiyo Mana ndani yake, uiweke mbele ya Bwana, ilindwe kwa ajili ya vizazi vyenu. 34 Kama vile Bwana alivyomwagizia Musa ndivyo Haruni alivyoiweka hapo mbele ya Ushahidi, ili ilindwe. 35 Na wana wa Israeli walikula Mana muda wa miaka arobaini, hata walipofikilia nchi iliyo na watu, wakala ile Mana, hata walipofikilia mipakani mwa nchi ya Kanaani. 36 Hiyo omeri ni sehemu kumi ya efa.

Kutoka 17

1 Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe. 2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana? 3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung'unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu? 4 Musa akamlilia Bwana, akisema, Niwatendee nini watu hawa? Bado kidogo nao watanipiga kwa mawe. 5 Bwana akamwambia Musa, Pita mbele ya watu, ukawachukue baadhi ya wazee wa Israeli pamoja nawe; na ile fimbo yako ambayo uliupiga mto kwayo, uitwae mkononi mwako, ukaende. 6 Tazama, nitasimama mbele yako huko, juu ya lile jabali katika Horebu; nawe utalipiga jabali, na maji yatatoka, watu wapate kunywa. Musa akafanya hivyo mbele ya wazee wa Israeli. 7 Akapaita mahali pale jina lake Masa, na Meriba; kwa sababu ya mateto ya wana wa Israeli, na kwa sababu walimjaribu Bwana, wakisema, Je! Bwana yu kati yetu au sivyo? 8 Wakati huo Waamaleki wakatokea, wakapigana na Israeli huko Refidimu. 9 Musa akamwambia Yoshua, Tuchagulie watu, ukatoke upigane na Waamaleki; kesho nitasimama juu ya kilele kile, na ile fimbo ya Mungu nitakuwa nayo mkononi mwangu. 10 Basi Yoshua akafanya kama Musa alivyomwambia, akapigana na Amaleki; na Musa na Haruni na Huri wakapanda juu ya kile kilima. 11 Ikawa, Musa alipouinua mkono wake, Israeli walishinda; na alipoushusha mkono wake, Amaleki walishinda. 12 Lakini mikono ya Musa ilikuwa mizito; basi wakatwaa jiwe, wakaliweka chini yake akalikalia. Haruni na Huri wakaitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu; mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa. 13 Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga. 14 Bwana akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. 15 Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake Yehova-nisi; 16 akasema, Bwana ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi.

Kutoka 18

1 Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi Bwana alivyowaleta Israeli watoke Misri. 2 Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha, 3 pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini; 4 na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao. 5 Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu; 6 naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye. 7 Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani. 8 Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote Bwana aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi Bwana alivyowaokoa. 9 Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote Bwana aliowatendea Israeli, kwa alivyo waokoa mikononi mwa Wamisri. 10 Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe Bwana aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri. 11 Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti. 12 Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu. 13 Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni. 14 Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni? 15 Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu; 16 wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake. 17 Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema. 18 Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako. 19 Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao; 20 nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya. 21 Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi; 22 nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe. 23 Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani. 24 Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia. 25 Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi. 26 Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe. 27 Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.

Kutoka 19

1 Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai. 2 Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. 3 Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; 4 Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. 5 Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, 6 nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli. 7 Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, Bwana aliyokuwa amemwagiza. 8 Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu. 9 Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. 10 Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, 11 wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. 12 Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa. 13 Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima. 14 Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. 15 Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke. 16 Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. 17 Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. 18 Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana. 19 Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. 20 Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. 21 Ndipo Bwana akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa Bwana kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia. 22 Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase, Bwana asije akawafurikia. 23 Musa akamwambia Bwana, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga. 24 Bwana akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia Bwana, asije yeye akawafurikia juu yao. 25 Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo.

Kutoka 20

1 Mungu akanena maneno haya yote akasema, 2 Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 3 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. 7 Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. 8 Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. 9 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 10 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa. 12 Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. 13 Usiue. 14 Usizini. 15 Usiibe. 16 Usimshuhudie jirani yako uongo. 17 Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako. 18 Watu wote wakaona umeme na ngurumo na sauti ya baragumu, na ule mlima kutoka moshi; na watu walipoona hayo wakatetemeka, wakasimama mbali. 19 Wakamwambia Musa, Sema nasi wewe, nasi tutasikia, bali Mungu asiseme nasi, tusije tukafa. 20 Musa akawaambia watu, Msiogope, maana Mungu amekuja ili awajaribu, na utisho wake uwe mbele yenu, ili kwamba msifanye dhambi. 21 Basi hao watu wakasimama mbali, naye Musa akalikaribia lile giza kuu Mungu alipokuwapo. 22 Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli hivi, Ninyi wenyewe mmeona ya kuwa nimenena nanyi kutoka mbinguni. 23 Msifanye miungu mingine pamoja nami; miungu ya fedha, wala miungu ya dhahabu, msijifanyie. 24 Utanifanyia madhabahu ya udongo, nawe utatoa dhabihu zako juu yake; sadaka za kuteketezwa, na sadaka za amani, kondoo zako, na ng'ombe zako, kila mahali nitakapotia ukumbusho wa jina langu, hapo ndipo nitakapokujilia na kukubarikia. 25 Nawe ukinifanyia madhabahu ya mawe, hutaijenga ya mawe yaliyochongwa; kwa kuwa ukiwa wewe umetumia chombo chako katika kuichonga umeitia unajisi. 26 Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.

Kutoka 21

1 Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi 2 Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure. 3 Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye. 4 Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake. 5 Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; 6 ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote. 7 Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo. 8 Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu. 9 Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake. 10 Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia. 11 Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali. 12 Mtu awaye yote ampigaye mtu, hata akafa, hana budi atauawa huyo. 13 Lakini kama hakumvizia, ila Mungu amemtia mkononi mwake; basi nitakuonyesha mahali atakapopakimbilia. 14 Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe. 15 Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. 16 Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo 17 Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. 18 Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake; 19 atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa. 20 Mtu akimpiga mtumwa wake, au kijakazi chake, kwa fimbo, naye akifa mkononi mwake, hana budi ataadhibiwa. 21 Lakini akipona siku moja au mbili hataadhibiwa; maana, ni mali yake. 22 Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema. 23 Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai, 24 jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, 25 kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko. 26 Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake. 27 Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake. 28 Ng'ombe akipiga pembe mtu mume au mtu mke, nao wakafa, huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, nyama yake isiliwe; lakini mwenye huyo ng'ombe ataachiliwa. 29 Lakini kwamba huyo ng'ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameonyeshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mtu mume au mwanamke; huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa. 30 Lakini akiandikiwa ukombozi, ndipo atakapotoa kwa ajili ya uhai wake hicho atakachoandikiwa. 31 Akiwa ng'ombe amempiga pembe mtoto wa kiume na kumtumbua, au akiwa amempiga mtoto wa kike, atatendwa kama hukumu hiyo. 32 Ng'ombe akimtumbua mtumwa mume au kijakazi; mwenye ng'ombe atampa bwana wao shekeli thelathini za fedha, naye ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe. 33 Kwamba mtu atafunua shimo, au kuchimba shimo, naye asilifunike, kisha ikawa ng'ombe au punda kutumbukia humo, 34 mwenye shimo atalipa; atampa huyo mwenye mnyama fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa ni wake. 35 Ng'ombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine hata akafa; ndipo watamwuza huyo ng'ombe aliye hai na kugawanya thamani yake; na ng'ombe aliyekufa pia watamgawanya. 36 Au kwamba ilijulikana ya kuwa ng'ombe tangu hapo amezoea kupiga kwa pembe, wala mwenyewe asimzuie; ndipo atakapolipa yeye, ng'ombe kwa ng'ombe, na huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa ni wake.

Kutoka 22

1 Mtu akiiba ng'ombe au kondoo, na kumchinja, au kumwuza; atalipa ng'ombe watano badala ya ng'ombe mmoja, na kondoo wanne badala ya kondoo mmoja. 2 Mwivi akipatikana akiwa yu hali ya kuvunja mahali, naye akapigwa hata akafa, hapatakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake. 3 Lakini kama jua limekucha juu yake, ndipo patakuwa na malipizo ya damu kwa ajili yake; ingempasa kutoa malipo kamili; akiwa hana kitu, na auzwe kwa ajili ya wivi wake. 4 Kama hicho kitu kilichoibwa chapatikana hai mkononi mwake, kama ni ng'ombe, au punda, au kondoo; atalipa thamani yake mara mbili. 5 Mtu akilisha katika shamba, au shamba la mizabibu, akimwacha mnyama wake, akala katika shamba la mtu mwingine; atalipa katika vitu vilivyo vizuri vya shamba lake mwenyewe, au vya mizabibu yake. 6 Ukiwaka moto, na kushika penye miiba, na ngano zilizofungwa miganda, au ngano ambazo hazijakatwa, au shamba, likateketea; yeye aliyeuwasha huo moto lazima atalipa. 7 Mtu akimpa mwenziwe amana ya fedha au vitu vingine amtunzie, na vitu vile vikaibwa katika nyumba ya mtu huyo; mwivi akipatikana, atalipa thamani yake mara mbili. 8 Mwivi asipopatikana, ndipo mwenye nyumba atakaribia mbele ya Mungu, ionekane kwamba si yeye aliyetia mkono na kutwaa vyombo vya mwenziwe. 9 Kila jambo la kukosana, kama ni la ng'ombe, au la punda, au la kondoo, au la mavazi, au la kitu cho chote kilichopotea, ambacho mtu mmoja asema ni chake, hilo jambo la watu wote wawili litaletwa mbele ya Mungu; na yeye atakayehukumiwa na Mungu kuwa ni mkosa atamlipa mwenziwe thamani yake mara mbili. 10 Mtu akimpa mwenziwe punda, au ng'ombe, au kondoo, au mnyama ye yote, ili amtunzie; yule mnyama akafa, au akaumia, au akachukuliwa mtu asione; 11 patakuwa na kiapo cha Bwana katikati ya watu hao wawili, kwamba alipeleka mkono wake kutwaa mali ya mwenziwe, na mwenyewe atakubali hayo, wala hatalipa. 12 Lakini kwamba aliibiwa mnyama huyo, sharti amlipe yule mwenyewe. 13 Kwamba aliraruliwa na mnyama mkali, na amlete uwe ushahidi; hatalipa kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa. 14 Mtu akiazima mnyama kwa mwenziwe, naye akaumia huyo mnyama, au akafa, mwenyewe asipokuwapo, lazima atalipa. 15 Kama huyo mwenyewe alikuwapo pamoja na mnyama wake, hatalipa; kama ni mnyama aliyeajiriwa, alikwenda kwa ajili ya ujira wake. 16 Mtu akimshawishi mwanamwali, aliyeposwa na mume, na kulala naye, lazima atatoa mahari kwa ajili yake ili awe mkewe. 17 Ikiwa baba yake huyo mwanamwali akataa kabisa kumpa, atalipa fedha kama hesabu ya mahari ya mwanamwali ilivyo. 18 Usimwache mwanamke mchawi kuishi. 19 Mtu awaye yote alalaye na mnyama sharti atauawa. 20 Mtu atakayemchinjia sadaka mungu ye yote, isipokuwa ni yeye Bwana peke yake, na angamizwe kabisa. 21 Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. 22 Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. 23 Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, 24 na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima. 25 Ukimkopesha mtu aliye maskini, katika watu wangu walio pamoja nawe; usiwe kwake mfano wa mwenye kumdai; wala hutamwandikia faida. 26 Ikiwa wewe kwa njia yo yote wapokea nguo ya jirani yako rehani, lazima utamrudishia mbele ya jua kuchwa; 27 maana hiyo nguo ni kifuniko chake, hiyo peke yake ni nguo ya ngozi yake; je! Atalalia nini? Itakuwa, hapo atakaponililia mimi, nitasikia; kwa kuwa mimi ni mwenye rehema. 28 Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako. 29 Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na ya vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao waume utanipa mimi. 30 Nawe utafanya vivyo katika ng'ombe zako, na kondoo zako; utamwacha siku saba pamoja na mama yake; siku ya nane utanipa mimi. 31 Nanyi mtakuwa watu watakatifu kwangu mimi; kwa hiyo msiile nyama yo yote iliyoraruliwa huko kondeni na mnyama wa mwitu; mtawatupia mbwa nyama hiyo.

Kutoka 23

1 Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu. 2 Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu; 3 wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake. 4 Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena. 5 Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye hali ameanguka chini ya mzigo wake, nawe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie. 6 Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake. 7 Jitenge mbali na neno uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu. 8 Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki. 9 Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. 10 Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake; 11 lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni. 12 Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika. 13 Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako. 14 Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu. 15 Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu; 16 tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani. 17 Mara tatu katika mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU. 18 Usisongeze damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hata asubuhi. 19 Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya Bwana, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake. 20 Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. 21 Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. 22 Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. 23 Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali. 24 Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande. 25 Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. 26 Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza. 27 Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao. 28 Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako. 29 Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. 30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi. 31 Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hata bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako. 32 Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. 33 Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako.

Kutoka 24

1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Kweeni wewe, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini wa wazee wa Israeli, mkamfikilie Bwana; mkasujudie kwa mbali; 2 na Musa peke yake ndiye atakayekaribia karibu na Bwana; lakini hao hawatakaribia karibu; wala hao watu hawatakwea pamoja naye. 3 Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. 4 Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, 5 akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng'ombe. 6 Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. 7 Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. 8 Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote. 9 Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; 10 wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. 11 Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa. 12 Bwana akamwambia Musa, Njoo huku juu kwangu mlimani, uwe huku; nami nitakupa mbao za mawe na ile sheria na hiyo amri niliyoiandika ili uwafundishe. 13 Musa akaondoka na Yoshua, mtumishi wake, Musa akapanda mlimani kwa Mungu. 14 Akawaambia hao wazee, Tungojeeni hapa, mpaka tutakaporudi kwenu; na tazameni, Haruni na Huri wapo pamoja nanyi; kila mtu aliye na neno na awaendee. 15 Musa akapanda mlimani, lile wingu likaufunikiza mlima. 16 Na huo utukufu wa Bwana ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. 17 Na kuonekana kwake ule utukufu wa Bwana kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli. 18 Musa akaingia ndani ya lile wingu, akapanda mlimani; Musa akawa humo katika ule mlima siku arobaini, mchana na usiku.

Kutoka 25

1 Bwana akanena na Musa, akamwambia, 2 Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. 3 Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba, 4 na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani safi, na singa za mbuzi; 5 na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na miti ya mshita, 6 na mafuta ya ile taa, na viungo vya manukato kwa yale mafuta ya kupaka, na kwa ule uvumba wenye harufu nzuri; 7 na vito vya shohamu, na vito vingine vya kutiwa kwa ile naivera, na kwa kile kifuko cha kifuani. 8 Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. 9 Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya. 10 Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. 11 Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. 12 Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili. 13 Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. 14 Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku. 15 Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa. 16 Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. 17 Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu. 18 Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. 19 Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. 20 Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema. 21 Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku. 22 Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli. 23 Nawe fanya meza ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa dhiraa mbili, na upana wake dhiraa moja, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. 24 Uifunike dhahabu safi, na kuifanyia ukingo wa dhahabu wa kuizunguka pande zote. 25 Kisha ifanyie upapi wa kuizunguka pande zote, upana wake utakuwa nyanda nne, nawe uufanyie ule upapi ukingo wa urembo wa dhahabu wa kuuzunguka pande zote. 26 Uifanyie vikuku vinne vya dhahabu, na kuvitia vile vikuku katika pembe zake nne, katika miguu yake minne. 27 Vile vikuku na viwe karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza. 28 Fanya ile miti ya mti wa mshita, na kuifunika dhahabu, kwamba ile meza ichukuliwe kwayo. 29 Nawe fanya sahani zake, na miiko yake, na makopo yake, na vikombe vyake vya kumiminia; vifanye vyote vya dhahabu safi. 30 Nawe utaiweka mikate ya wonyesho juu ya meza mbele yangu daima. 31 Nawe fanya kinara cha taa cha dhahabu safi; hicho kinara na kifanywe cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake, vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vitakuwa vya kitu kimoja nacho; 32 nacho kitakuwa na matawi sita yenye kutoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara upande wake mmoja, na matawi matatu ya kinara upande wake wa pili 33 vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi moja; tovu na ua; na vikombe vitatu vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi katika tawi la pili, tovu na ua; vivyo hivyo hayo matawi yote sita yatokayo katika kile kinara; 34 na katika hicho kinara vikombe vinne vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake, na maua yake; 35 na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, na tovu chini ya matawi mawili la kitu kimoja nacho, kwa hayo matawi sita yatokayo katika kile kinara. 36 Matovu yake na matawi yake yatakuwa ya kitu kimoja nacho; kiwe chote pia kazi moja ya kufua, ya dhahabu safi. 37 Nawe zifanye taa zake saba; nao wataziwasha hizo taa zake, zitoe nuru mbele yake. 38 Na makoleo yake, na visahani vyake, vyote vitakuwa vya dhahabu safi. 39 Kitafanywa cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo hivi vyote. 40 Nawe angalia ya kwamba uvifanye kama mfano wake, ulioonyeshwa mlimani.

Kutoka 26

1 Kisha fanya hiyo maskani iwe na mapazia kumi; ifanye ya nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, pamoja na makerubi; kazi ya fundi stadi. 2 Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; mapazia yote yatakuwa ya kipimo kimoja. 3 Mapazia matano yataungwa pamoja, hili na hili; na mapazia matano mengine yataungwa pamoja, hili na hili. 4 Kisha utafanya tanzi za rangi ya samawi upande wa mwisho wa pazia moja katika ule upindo wa fungu lake, vivyo utafanya upande wa mwisho wa ile pazia iliyo, katika fungu la pili. 5 Fanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upande wa mwisho wa ile pazia iliyo katika kuungana kwa pili; hizo tanzi zitaelekeana. 6 Kisha ufanye vifungo hamsini vya dhahabu, na kuunganya hayo mapazia pamoja kwa vile vifungo; na hiyo maskani itakuwa ni moja. 7 Nawe fanya mapazia ya singa za mbuzi yawe hema juu ya maskani; fanya mapazia kumi na moja. 8 Urefu wa kila pazia utakuwa dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia utakuwa dhiraa nne; hayo mapazia kumi na moja yatakuwa ya kipimo kimoja. 9 Kisha utaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali, na lile pazia la sita utalipeta hapo upande wa mbele wa ile hema. 10 Fanya tanzi hamsini upande wa mwisho wa pazia lile lililo la mwisho katika hayo yaliyounganywa pamoja, na tanzi hamsini upande wa mwisho wa lile pazia lililo nje katika hayo ya pili yaliyounganywa pamoja. 11 Tena ufanye vifungo hamsini vya shaba, na kuvitia vile vifungo katika zile tanzi, na kuiunganya ile hema pamoja, ili iwe hema moja. 12 Na kipande kile kilichosalia, kile kiangukacho, cha yale mapazia ya hema, ile nusu ya pazia iliyosalia, itaanguka huko upande wa nyuma wa maskani. 13 Na hiyo dhiraa moja upande mmoja, na ile dhiraa moja upande wa pili, ya urefu wa mapazia ya hema uliosalia, zitaanguka katika ubavu wa maskani upande huu na upande huu, ili kuifunika. 14 Nawe fanya kifuniko cha ile hema, cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na juu yake kifuniko cha ngozi za pomboo. 15 Nawe fanya hizo mbao za maskani za mti wa mshita, zenye kusimama. 16 Kila ubao utakuwa na urefu wa dhiraa kumi, na upana wake kila ubao utakuwa dhiraa moja na nusu. 17 Kila ubao utakuwa na ndimi mbili, zenye kuunganywa huu na huu; ndivyo utakavyozifanya mbao zote za maskani. 18 Kisha ufanye zile mbao za maskani, mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini. 19 Nawe ufanye matako arobaini ya fedha chini ya zile mbao ishirini, matako mawili chini ya ubao mmoja, kupokea zile ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kupokea zile ndimi zake mbili; 20 na upande wa pili wa maskani, upande wa kaskazini, mbao ishirini; 21 na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine. 22 Kisha ufanye mbao sita kwa ajili ya upande wa nyuma wa maskani kuelekea magharibi. 23 Tena ufanye mbao mbili kwa ajili ya hizo pembe za maskani zilizo upande wa nyuma. 24 Upande wa chini zitakuwa ni mbili mbili; vivyo zitaungwa pamoja mbao pacha hata ncha ya juu katika pete ya kwanza; zote mbili ndivyo zitakavyokuwa; zitakuwa kwa ajili ya hizo pembe mbili. 25 Mbao zitakuwa ni nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao wa pili. 26 Nawe fanya mataruma ya mti wa mshita; mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa maskani, 27 na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa ajili ya mbao za upande wa maskani ulio nyuma kuelekea magharibi. 28 Na hilo taruma la katikati, lililo katikati ya zile mbao litapenya toka mwisho huu hata mwisho huu. 29 Na hizo mbao utazifunika dhahabu, na pete zake za kutilia yale mataruma utazifanya za dhahabu; na hayo mataruma utayafunika dhahabu. 30 Nawe utaisimamisha hiyo maskani sawasawa na mfano wake ulioonyeshwa mlimani. 31 Nawe fanya pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na nguo za kitani nzuri zenye kusokotwa, litafumwa na kutiwa makerubi, kazi ya fundi stadi; 32 kisha litungike katika nguzo nne za mti wa mshita zilizofunikwa dhahabu, vifungo vyake vitakuwa vya dhahabu, katika matako ya fedha manne. 33 Nawe tungika lile pazia chini ya vile vifungo, nawe lete lile sanduku la ushuhuda na kulitia humo nyuma ya pazia; na lile pazia litawagawanyia kati ya patakatifu, na mahali patakatifu sana. 34 Nawe utaweka kiti cha rehema juu ya lile sanduku la ushuhuda ndani ya mahali pale patakatifu sana. 35 Na ile meza utaiweka nje ya pazia, na kinara cha taa kuikabili ile meza upande wa maskani wa kuelekea kusini; na ile meza utaiweka upande wa kaskazini. 36 Kisha utafanya kisitiri kwa mlango wa Hema, cha nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza. 37 Nawe fanya nguzo tano za mti wa mshita kwa kile kisitiri, na kuzifunika dhahabu; kulabu zake zitakuwa za dhahabu; nawe utasubu matako ya shaba matano kwa ajili yake.

Kutoka 27

1 Nawe fanya madhabahu ya mti wa mshita; urefu wake utakuwa ni dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano; hiyo madhabahu itakuwa mraba; na kwenda juu kwake kutakuwa dhiraa tatu. 2 Nawe fanya pembe nne katika pembe zake nne; hizo pembe zitakuwa za kitu kimoja na madhabahu; nawe utayafunika shaba. 3 Na vyombo vyake vya kuyaondoa majivu yake utavifanya, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote utavifanya vya shaba. 4 Nawe uifanyie hiyo madhabahu wavu wa shaba; kisha utie pete nne za shaba katika hizo pembe nne za ule wavu. 5 Nawe tia huo wavu chini ya kizingo kiizungukacho madhabahu upande wa chini, ili huo wavu ufikilie katikati ya hiyo madhabahu. 6 Nawe fanya miti kwa ajili ya madhabahu, miti ya mshita, na kuifunika shaba. 7 Na hiyo miti itatiwa katika pete, na ile miti itakuwa katika pande mbili za madhabahu, wakati wa kuichukua. 8 Uifanye ya mbao, yenye mvungu ndani yake; kama ulivyoonyeshwa mlimani, ndivyo watakavyoifanya. 9 Nawe fanya ua wa maskani; upande wa kusini wa kuelekea kusini kutakuwa na chandarua ya nguo ya kitani nzuri yenye kusokotwa, kwa huo ua, urefu wake upande mmoja utakuwa ni dhiraa mia; 10 na nguzo zake zitakuwa nguzo ishirini, na matako yake ishirini, matako yake yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 11 Ni vivyo upande wa kaskazini, urefu wake hiyo chandarua utakuwa ni dhiraa mia, na nguzo zake ishirini, na matako yake ishirini yatakuwa ya shaba; kulabu za zile nguzo na vitanzi vyake vitakuwa vya fedha. 12 Na upande wa magharibi, upana wa ua kutakuwa na chandarua ya dhiraa hamsini; nguzo zake kumi, na matako yake kumi. 13 Na upana wa ule ua upande wa mashariki kuelekea mashariki utakuwa ni dhiraa hamsini. 14 Chandarua upande mmoja wa lango itakuwa dhiraa kumi na tano upana wake; nguzo zake zitakuwa tatu na matako yake matatu. 15 Upande wa pili ni vivyo chandarua ya dhiraa kumi na tano; nguzo zake tatu, na matako yake matatu. 16 Na kwa lile lango la ua patakuwa na kisitiri cha dhiraa ishirini, kitakuwa cha nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa, kazi ya mshona taraza; nguzo zake zitakuwa nne, na matako yake manne. 17 Nguzo zote za ule ua ziuzungukazo pande zote zitakuwa na vitanzi vya fedha; kulabu zake za fedha, na matako yake ya shaba. 18 Urefu wa huo ua utakuwa dhiraa mia, na upana wake utakuwa dhiraa hamsini kotekote, na kwenda juu kwake dhiraa tano; yawe ya nguo ya kitani nzuri, na matako yake yatakuwa ya shaba. 19 Vyombo vyote vya maskani vitumiwavyo katika utumishi wake wote, na vigingi vyake vyote, na vigingi vyote vya ule ua, vitakuwa vya shaba. 20 Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima. 21 Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele ya Bwana; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.

Kutoka 28

1 Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni. 2 Nawe utamfanyia Haruni ndugu yako mavazi matakatifu, kwa utukufu na kwa uzuri. 3 Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Haruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani. 4 Na mavazi watakayoyafanya ni haya; kifuko cha kifuani, na naivera, na joho, na kanzu ya kazi ya urembo; na kilemba, na mshipi; nao watawafanyia Haruni nduguyo, na wanawe, mavazi matakatifu ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. 5 Nao wataitwaa dhahabu, na nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, na nguo ya kitani nzuri. 6 Nao waifanye naivera kwa nyuzi za dhahabu, na za samawi, na za zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa kwa kazi ya mstadi. 7 Itakuwa na vipande viwili vya mabegani, vilivyoungana kwenye ncha zake mbili; ili ipate kuunganywa. 8 Na mshipi wa kazi ya ustadi ulio juu yake, ili kuifunga mahali pake; utakuwa wa kazi kama ile ya naivera, ya vitu vile vile ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri yenye kusokotwa. 9 Nawe utatwaa vito viwili vya shohamu, ya rangi ya chani-kiwiti, nawe utachora juu yake majina ya wana wa Israeli; 10 majina yao sita katika kito kimoja, na majina sita yaliyosalia katika kile kito cha pili, kwa utaratibu wa kuzaliwa kwao. 11 Kwa kazi mtu mwenye kuchora mawe kama vile muhuri ichorwavyo, utavichora hivi vito viwili, sawasawa na majina ya wana wa Israeli, nawe utavitia katika vijalizo vya dhahabu. 12 Nawe utavitia vile vito viwili juu ya vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli; naye Haruni atayachukua majina yao mbele za Bwana juu ya mabega yake mawili ili kuwa ukumbusho. 13 Nawe fanya vijalizo viwili vya dhahabu; 14 na mikufu miwili ya dhahabu safi; utaifanya iwe mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa; nawe uitie ile mikufu ya kazi ya kusokotwa katika vile vijalizo. 15 Nawe utafanya kifuko cha kifuani cha hukumu, kazi ya fundi stadi; utakifanya kwa kuiandama ile kazi ya hiyo naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani safi yenye kusokotwa, ndivyo utakavyokifanya. 16 Kitakuwa mraba, tena cha kukunjwa; urefu wake utakuwa shibiri moja, na upana wake shibiri moja. 17 Nawe ukijaze viweko vya vito, safu nne za vito; safu moja itakuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, hivi vitakuwa safu ya kwanza; 18 na safu ya pili itakuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi; 19 na safu ya tatu itakuwa hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto; 20 na safu ya nne itakuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi; vito hivyo vitakazwa ndani ya dhahabu kwa kujaa mahali pake. 21 Na vile vito vitakuwa sawasawa na majina ya wana wa Israeli, kumi na viwili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora kwa muhuri kila kimoja sawasawa na jina lake, vitakuwa vya hizo kabila kumi na mbili. 22 Nawe utie katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa, ya dhahabu safi. 23 Nawe utie pete mbili za dhahabu katika kile kifuko cha kifuani, na kuzitia hizo pete mbili katika ncha mbili za kifuko cha kifuani. 24 Nawe utie hiyo mikufu miwili ya dhahabu iliyosokotwa katika zile pete mbili zilizo katika ncha za kifuko cha kifuani. 25 Na ncha zile nyingine za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa utazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera upande wa mbele. 26 Nawe utafanya pete mbili za dhahabu, uzitie katika hizo ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani. 27 Nawe fanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya mabegani vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi. 28 Nao watakikaza kile kileso kwa zile pete zake kwenye pete za naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kwamba kikae pale juu ya ule mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, ili kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera. 29 Na Haruni atayachukua majina ya wana wa Israeli katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu juu ya moyo wake, hapo atakapoingia ndani ya mahali patakatifu, kuwa ukumbusho mbele ya Bwana daima. 30 Nawe utie hizo Urimu na Thumimu katika kile kifuko cha kifuani cha hukumu; nazo zitakuwa juu ya moyo wa Haruni, hapo atakapoingia ndani mbele ya Bwana; na Haruni atachukua hukumu ya hao wana wa Israeli juu ya moyo wake mbele ya Bwana daima. 31 Nawe fanya hiyo joho ya naivera ya rangi ya samawi yote. 32 Nayo itakuwa na tundu katikati yake kwa kupitisha kichwa; itakuwa na utepe wa kazi ya kusokotwa kuzunguka hilo tundu lake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, ili lisipasuke. 33 Nawe katika pindo zake utatia makomamanga ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na ya rangi nyekundu, kuzunguka pindo zake kotekote; na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga pande zote; 34 njuga ya dhahabu na komamanga, njuga ya dhahabu na komamanga, katika pindo za joho kuizunguka pande zote. 35 Nayo itakuwa juu ya Haruni akitumika; na sauti ya hizo njuga itasikilikana hapo aingiapo ndani ya mahali patakatifu mbele ya Bwana na hapo atokapo nje, ili kwamba asife. 36 Nawe fanya bamba la dhahabu safi na kuchora juu yake, mfano wa machoro ya muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana. 37 Nawe ulitie hilo bamba katika ukanda wa rangi ya samawi, nalo litakuwa katika kile kilemba; litakuwa upande wa mbele wa kile kilemba. 38 Nalo litakuwa katika kipaji cha uso cha Haruni, na Haruni atauchukua uovu wa vile vitu vitakatifu, watakavyovitakasa hao wana wa Israeli katika vipawa vyao vyote vitakatifu, nalo litakuwa katika kipaji chake cha uso sikuzote, ili kwamba vipate kukubaliwa mbele za Bwana. 39 Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza. 40 Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri. 41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani. 42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani; 43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.

Kutoka 29

1 Nawe uwafanyie jambo hili, ili kuwatakasa, wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani; twaa ng'ombe mmoja mume kijana, na kondoo waume wawili walio wakamilifu, 2 na mkate usiotiwa chachu, na maandazi yasiyotiwa chachu yaliyokandwa kwa mafuta, na kaki zisizotiwa chachu zilizotiwa mafuta; utazifanya za unga mzuri mwembamba wa ngano. 3 Nawe vitie vyote katika kikapu, uvilete ndani ya kikapu, pamoja na huyo ng'ombe, na hao kondoo waume wawili. 4 Kisha mlete Haruni na wanawe hata mlangoni pa hema ya kukutania, ukawaoshe kwa maji. 5 Kisha twaa hayo mavazi na kumvika Haruni; itie kanzu, na joho ya naivera, na naivera, na kifuko cha kifuani, na kumkaza kwa huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi; 6 nawe mvike kile kilemba kichwani, na ile taji takatifu utaitia katika kile kilemba. 7 Ndipo utakapotwaa hayo mafuta ya kutiwa, na kummiminia kichwani mwake, na kumtia mafuta. 8 Kisha walete hao wanawe na kuwavika kanzu. 9 Nawe uwakaze mishipi, Haruni na wanawe, na kuwavika kofia; nao watakuwa na huo ukuhani kwa amri ya milele; nawe utawaweka Haruni na wanawe kwa kazi takatifu. 10 Kisha utamleta huyo ng'ombe mbele ya hema ya kukutania; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa cha huyo ng'ombe. 11 Kisha utamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania. 12 Kisha twaa baadhi ya damu ya ng'ombe, uitie katika pembe za madhabahu kwa kidole chako; na kuimimina damu yote chini ya madhabahu. 13 Kisha twaa mafuta yote yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo juu yake, uyateketeze yote juu ya madhabahu. 14 Lakini nyama yake huyo ng'ombe, na ngozi yake, na mavi yake, utayachoma kwa moto nje ya marago; ni sadaka kwa ajili ya dhambi. 15 Pia mtwae kondoo mume mmoja; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo mume. 16 Kisha utamchinja huyo kondoo mume, na kuitwaa damu yake, na kuinyunyiza katika madhabahu kuizunguka kando-kando. 17 Kisha utamkata-kata kondoo vipande vyake, na kuyaosha matumbo yake na miguu yake, na kuiweka pamoja na vipande vyake na kichwa chake. 18 Nawe mteketeze kondoo mzima juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Bwana; ni harufu nzuri, sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 19 Kisha mtwae huyo kondoo wa pili; na Haruni na wanawe wataweka mikono yao juu ya kichwa chake huyo kondoo. 20 Kisha utamchinja kondoo, na kuitwaa damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la Haruni la upande wa kuume, na katika ncha za masikio ya kuume ya wanawe, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vikuu vya miguu yao ya kuume, na kuinyunyiza hiyo damu katika madhabahu kuizunguka kando-kando. 21 Kisha twaa katika hiyo damu iliyo juu ya madhabahu, na katika hayo mafuta ya kutiwa, na kumnyunyizia Haruni, juu ya mavazi yake, na wanawe, na mavazi yao pia, pamoja naye; naye atatakaswa, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye. 22 Tena yatwae mafuta ya huyo kondoo mume, na mkia wake wa mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, na kitambi kilicho katika ini, na figo mbili, na mafuta yaliyo katika hizo figo, na paja la kuume; kwani ni kondoo ambaye ni wa kuwekwa kwa kazi takatifu; 23 utwae na mkate mmoja wa unga, na mkate mmoja ulioandaliwa kwa mafuta, na kaki moja katika kile kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichowekwa mbele ya Bwana; 24 nawe utavitia hivi vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe; nawe utavitikisa-tikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana. 25 Kisha uvitwae vile vitu mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya ile sadaka ya kuteketezwa, viwe harufu nzuri mbele ya Bwana; ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 26 Kisha twaa kidari cha huyo kondoo wa kuwekwa kwake Haruni kwa kazi takatifu, na kukitikisa-tikisa kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; nacho kitakuwa ni sehemu yako. 27 Nawe kitakase kile kidari cha ile sadaka ya kutikiswa, na lile paja la sadaka ya kuinuliwa, lililotikiswa, na lililoinuliwa juu, vya yule kondoo wa kuwekwa kwa kazi takatifu, huyo aliyekuwa kwa ajili ya Haruni, na huyo aliyekuwa kwa ajili ya wanawe; 28 navyo vitakuwa vya Haruni na wanawe posho ya lazima sikuzote itokayo kwa hao wana wa Israeli; kwa kuwa ni sadaka ya kuinuliwa; nayo itakuwa ni sadaka ya kuinuliwa itokayo kwa hao wana wa Israeli katika dhabihu zao za sadaka za amani, ni sadaka yao ya kuinuliwa kwa ajili ya Bwana. 29 Na hayo mavazi matakatifu ya Haruni yatakuwa ya wanawe baada yake, wayavae watakapotiwa mafuta, na watakapowekwa kwa kazi takatifu. 30 Huyo mwanawe atakayekuwa kuhani badala yake atayavaa muda wa siku saba, hapo atakapoingia ndani ya hiyo hema ya kukutania, ili atumike ndani ya mahali patakatifu. 31 Nawe twaa huyo kondoo mume aliyekuwa wa kuwekwa kwa kazi takatifu, na kuitokosa nyama yake katika mahali patakatifu. 32 Na Haruni na wanawe wataila ile nyama ya kondoo, na mikate iliyo katika kile kikapu, hapo mbele ya mlango wa hema ya kukutania. 33 Nao watakula vile vitu ambavyo upatanisho ulifanywa kwa hivyo, ili kuwaweka kwa kazi takatifu na kuwatakasa; lakini mgeni asivile, maana, ni vitu vitakatifu. 34 Na kwamba kitu cho chote cha ile nyama, iliyo kwa ajili ya kuweka kwa kazi takatifu, au cho chote cha hiyo mikate, kikisalia hata asubuhi, ndipo utavichoma kwa moto hivyo vilivyosalia; havitaliwa, maana, ni vitu vitakatifu. 35 Ni hivyo utakavyowatendea Haruni na wanawe, sawasawa na hayo yote niliyokuagiza; utawaweka kwa kazi takatifu siku saba. 36 Kila siku utamtoa ng'ombe wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya upatanisho; nawe utaisafisha hiyo madhabahu, hapo utakapofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu; nawe utaitia mafuta, ili kuitakasa. 37 Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu. 38 Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja wawili siku baada ya siku daima. 39 Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni; 40 tena, pamoja na mwana-kondoo mmoja utatoa vibaba vitatu vya unga mzuri uliochanganyika na mafuta yenye kupondwa, kiasi cha kibaba na robo kibaba; na divai kiasi cha kibaba na robo kibaba, iwe sadaka ya kinywaji. 41 Na huyo mwana-kondoo wa pili utamchinja wakati wa jioni, nawe utamfanyia vivyo kama ile sadaka ya unga ya asubuhi, na kama ile sadaka yake ya kinywaji, iwe harufu nzuri, ni dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 42 Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya Bwana; hapo nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo. 43 Nami nitakutana na wana wa Israeli hapo, na hiyo Hema itafanywa takatifu na utukufu wangu. 44 Nami nitaitakasa hiyo hema ya kukutania, na hiyo madhabahu; pia Haruni na wanawe nitawatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 45 Na mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao. 46 Nao watanijua kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao, niliyewaleta watoke katika nchi ya Misri, nipate kukaa kati yao; ni mimi Bwana Mungu wao.

Kutoka 30

1 Nawe fanya madhabahu ya kufukizia uvumba; utaifanyiza kwa mti wa mshita. 2 Urefu wake utakuwa dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; itakuwa mraba; na kwenda juu kwake dhiraa mbili; pembe zake zitakuwa za kitu kimoja nayo. 3 Nawe utaifunikiza dhahabu safi juu yake, na mbavu zake kando kando, na pembe zake; nawe utaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka. 4 Kisha utaifanyia pete mbili za dhahabu, chini ya ukingo wake katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili utazifanya; nazo zitakuwa mahali pa kuitia miti ya kuichukulia. 5 Na ile miti utaifanya kwa mti wa mshita, na kuifunikiza dhahabu safi. 6 Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe. 7 Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza. 8 Na Haruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Bwana katika vizazi vyenu vyote. 9 Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji. 10 Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa Bwana. 11 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 12 Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa Bwana kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu. 13 Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya Bwana. 14 Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya Bwana. 15 Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu. 16 Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania; ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele ya Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu. 17 Bwana akanena na Musa, na kumwambia 18 Fanya na birika la shaba, na tako lake la shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji. 19 Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo; 20 hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea Bwana sadaka ya moto; 21 basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote. 22 Kisha Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 23 Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na kane shekeli mia mbili na hamsini, 24 na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano; 25 nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa. 26 Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda, 27 na hiyo meza, na vyombo vyake vyote, na kinara cha taa, na vyombo vyake, na madhabahu ya kufukizia uvumba, 28 na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na tako lake. 29 Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu. 30 Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, na kuwatakasa, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 31 Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote. 32 Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu. 33 Mtu awaye yote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu awaye yote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. 34 Bwana akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja; 35 nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenazaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu; 36 nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana. 37 Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya Bwana. 38 Mtu ye yote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.

Kutoka 31

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; 3 nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, 4 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, 5 na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote. 6 Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza; 7 yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema; 8 na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba; 9 na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; 10 na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani; 11 na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao. 12 Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 13 Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi. 14 Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. 15 Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa. 16 Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. 17 Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika. 18 Hapo Bwana alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.

Kutoka 32

1 Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. 2 Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee. 3 Watu wote wakazivunja pete za dhahabu zilizo katika masikio yao, wakamletea Haruni. 4 Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. 5 Naye Haruni alipoona jambo hili, akajenga madhabahu mbele yake; Haruni akatangaza akasema, Kesho itakuwa sikukuu kwa Bwana. 6 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakatoa dhabihu, wakaleta sadaka za amani, watu wakaketi kula na kunywa, wakaondoka wacheze. 7 Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, 8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. 9 Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu 10 basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. 11 Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? 12 Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. 13 Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. 14 Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake. 15 Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. 16 Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. 17 Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. 18 Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi. 19 Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima. 20 Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. 21 Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? 22 Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. 23 Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. 24 Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu. 25 Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao, 26 ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, Mtu awaye yote aliye upande wa Bwana, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia 27 Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake. 28 Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu. 29 Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa Bwana leo, naam, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo. 30 Hata asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. 31 Musa akarejea kwa Bwana akasema, Aa! Watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. 32 Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao -- na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. 33 Bwana akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. 34 Basi sasa uende ukawaongoze watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekwambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia; pamoja na hayo siku nitakayowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao. 35 Bwana akawapiga hao watu, kwa walivyoifanya ile ndama, ambayo Haruni aliifanya.

Kutoka 33

1Bwana akanena na Musa, Haya, ondokeni, katokeni hapo, wewe na hao watu uliowaleta wakwee kutoka nchi ya Misri, waende nchi hiyo niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, niliposema, Nitakipa kizazi chako nchi hii; 2 nami nitamtuma malaika aende mbele yako; nami nitawafukuza Mkanaani, na Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; 3 waifikilie nchi imiminikayo maziwa na asali; kwa maana mimi sitakwenda kati yenu; kwa sababu ninyi ni watu wenye shingo ngumu; nisiwaangamize ninyi katika njia. 4 Watu waliposikia habari hizo mbaya wakaomboleza wala hapana mtu aliyevaa vyombo vyake vya uzuri. 5 Bwana akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli, Ninyi ni watu wenye shingo ngumu; kama mimi nikiingia kati yenu dakika moja, nitawaangamiza; basi sasa vueni vyombo vyenu vya uzuri ili nipate kujua nitakalowatenda. 6 Basi wana wa Israeli wakavua vyombo vyao vyote vya uzuri, tangu mlima wa Horebu na mbele. 7 Basi desturi ya Musa, ilikuwa kuitwaa ile hema, na kuikita nje ya marago mbali na hayo marago; akaiita, hema ya kukutania. Hata kila mtu aliyekuwa akitaka neno kwa Bwana, akatoka, akaenda hata hema ya kukutania, iliyokuwa nje ya marago. 8 Hata Musa alipotoka kuiendea ile hema, watu wote waliondoka wakasimama, kila mtu mlangoni pa hema yake, akamtazama Musa, hata alipokwisha kuingia hemani. 9 Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye Bwana akasema na Musa. 10 Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake. 11 Naye Bwana akasema na Musa uso kwa uso, kama vile mtu asemavyo na rafiki yake. Kisha akageuka akarejea hata maragoni; bali mtumishi wake Yoshua, mwana wa Nuni, naye ni kijana, hakutoka mle hemani. 12 Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu. 13 Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. 14 Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. 15 Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. 16 Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? 17 Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. 18 Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako. 19 Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la Bwana mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu. 20 Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi. 21 Bwana akasema, Tazama, hapa pana mahali karibu nami, nawe utasimama juu ya mwamba; 22 kisha itakuwa wakati unapopita utukufu wangu, nitakutia katika ufa wa ule mwamba, na kukufunika kwa mkono wangu hata nitakapokuwa nimekwisha kupita; 23 nami nitaondoa mkono wangu, nawe utaniona nyuma yangu, bali uso wangu hautaonekana.

Kutoka 34

1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; nami nitaandika juu ya mbao hizo maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, hizo ulizozivunja. 2 Nawe uwe tayari asubuhi, na asubuhi ukwee juu katika mlima wa Sinai, nawe hudhurisha nafsi yako kwangu huko katika kilele cha mlima. 3 Asikwee mtu pamoja nawe, wala asionekane mtu awaye yote katika huo mlima; wala kondoo na ng'ombe wasilishe mbele ya huo mlima. 4 Naye akachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza; na Musa akainuka na mapema asubuhi, naye akakwea katika mlima wa Sinai, kama Bwana alivyomwamuru, akazichukua hizo mbao mbili za mawe mkononi mwake. 5 Bwana akashuka ndani ya lile wingu, akasimama pamoja naye huko, akalitangaza jina la Bwana. 6 Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; 7 mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne. 8 Musa akafanya haraka, akainamisha kichwa chake hata nchi, akasujudu. 9 Akasema, Ikiwa sasa nimepata neema mbele zako, Bwana, nakuomba, Bwana, uende kati yetu, maana ni watu wenye shingo ngumu; ukasamehe uovu wetu na dhambi yetu, ukatutwae tuwe urithi wako. 10 Akasema, Tazama, nafanya agano; mbele ya watu wangu wote nitatenda miujiza, ya namna isiyotendeka katika dunia yote, wala katika taifa lo lote; na watu wote ambao unakaa kati yao wataona kazi ya Bwana, kwa maana ni neno la kutisha nikutendalo. 11 Liangalie neno hili ninalokuamuru leo; tazama, mbele yako namtoa Mwamori, na Mkanaani, na Mhiti, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. 12 Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. 13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao. 14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu. 15 Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake. 16 Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao. 17 Usijifanyizie miungu ya kuyeyusha. 18 Hiyo sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu utaitunza. Utakula mikate isiyotiwa chachu muda wa siku saba, kama nilivyokuagiza, kwa majira yaliyoaganwa katika mwezi wa Abibu; kwa kuwa ulitoka Misri katika mwezi huo wa Abibu. 19 Kila kifunguacho mimba ni changu mimi; na wanyama wako wote walio waume, wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na wa kondoo. 20 Na mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana-kondoo; tena kwamba hutaki kumkomboa, ndipo utamvunja shingo. Wazaliwa wa kwanza wote wa wanao utawakomboa. Wala hapana atakayehudhuria mbele zangu mikono mitupu. 21 Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika. 22 Nawe utaitunza sikukuu ya majuma, nayo ni ya malimbuko ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya vitu mwisho wa mwaka. 23 Mara tatu kila mwaka watu waume wako wote watahudhuria mbele za Bwana MUNGU, Mungu wa Israeli. 24 Kwa kuwa mimi nitazitupa nje taifa za watu mbele yako, na kuipanua mipaka yako; wala hapana mtu ye yote atakayeitamani nchi yako, hapo utakapokwea kwenda kuhudhuria mbele za Bwana Mungu wako mara tatu kila mwaka. 25 Usisongeze damu ya sadaka yangu pamoja na mkate uliotiwa chachu; wala hiyo sadaka ya sikukuu ya pasaka haitasazwa hata asubuhi. 26 Vitu vya kwanza vya malimbuko ya nchi yako utavileta na kuvitia ndani ya nyumba ya Bwana Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake. 27 Bwana akamwambia Musa, Andika maneno haya; kwa kuwa mimi nimefanya agano nawe, na pamoja na Israeli, kwa mujibu wa maneno haya. 28 Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi. 29 Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. 30 Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia. 31 Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. 32 Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo Bwana amemwambia katika mlima Sinai. 33 Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. 34 Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. 35 Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.

Kutoka 35

1 Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia Bwana ni haya, kwamba myafanye. 2 Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yo yote katika siku hiyo atauawa. 3 Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. 4 Kisha Musa akanena na mkutano wote wa wana wa Israeli, akawaambia, Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema, 5 Katwaeni kati yenu matoleo kwa Bwana; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba; 6 na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi; 7 na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, na mbao za mshita; 8 na mafuta kwa hiyo taa, na viungo vya manukato kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri; 9 na vito vya shohamu, na vito vya kutiwa kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani. 10 Na kila mtu kati yenu aliye na moyo wa hekima na aje, na kuyafanya hayo yote ambayo Bwana ameyaagiza; 11 yaani, hiyo maskani na hema yake, na kifuniko chake, na vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na viguzo vyake, na matako yake; 12 hilo sanduku, na miti yake, na hicho kiti cha rehema, na lile pazia la sitara; 13 na hiyo meza, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hiyo mikate ya wonyesho; 14 na hicho kinara cha taa kwa mwanga, na vyombo vyake, na taa zake, na hayo mafuta kwa nuru; 15 na hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba, na miti yake, na hayo mafuta ya kupaka, na huo uvumba mzuri, na hicho kisitiri cha mlango, mlangoni mwa hiyo maskani; 16 na hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, pamoja na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na hilo birika na tako lake; 17 na hizo kuta za nguo za ua, na viguzo vyake, na matako yake, na pazia la lango la ua; 18 na vile vigingi vya maskani, na vigingi vya ua, na kamba zake 19 na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, kwa ajili ya kutumika ndani ya mahali patakatifu, hayo mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani. 20 Basi mkutano wote wa wana wa Israeli wakaondoka hapo mbele ya Musa. 21 Wakaja kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza, na kila mtu ambaye roho yake ilimfanya kuwa apenda, nao wakaleta sadaka za kumpa Bwana, kwa kazi ya hema ya kukutania, na kwa utumishi wake, na kwa hayo mavazi matakatifu. 22 Nao wakaja, waume kwa wake, wote waliokuwa na moyo wa kupenda, wakaleta vipini, na hazama, na pete za muhuri, na vikuku, na vyombo vyote vya dhahabu; kila mtu aliyetoa toleo la dhahabu la kumpa Bwana. 23 Tena kila mtu aliyeona kwake nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na singa za mbuzi, na ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na ngozi za pomboo, akavileta. 24 Kila mtu aliyetoa toleo la fedha, na la shaba, akaileta sadaka ya Bwana; na kila mtu, aliyeona kwake mti wa mshita kwa kazi yo yote ya huo utumishi, akauleta. 25 Na wanawake wote waliokuwa na mioyo ya hekima, walisokota kwa mikono yao, nao wakaleta hizo walizokuwa wamezisokota, nguo za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na hizo nyuzi nyekundu, na hiyo nguo ya kitani nzuri. 26 Na wanawake wote ambao mioyo yao iliwahimiza katika hekima wakasokota hizo singa za mbuzi. 27 Na hao wakuu wakavileta vile vito vya shohamu, na vito vya kutiwa, kwa hiyo naivera, na kwa hicho kifuko cha kifuani, 28 na viungo vya manukato, na mafuta; kwa hiyo taa, na kwa hayo mafuta ya kutiwa, na kwa huo uvumba mzuri. 29 Wana wa Israeli wakaleta sadaka za kumpa Bwana kwa moyo wa kupenda; wote, waume kwa wake, ambao mioyo yao iliwafanya kuwa wapenda kuleta kwa hiyo kazi, ambayo Bwana aliamuru ifanywe kwa mkono wa Musa. 30 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli, Angalieni, Bwana amemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; 31 naye amemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na akili, na ujuzi, na kazi ya ustadi kila aina; 32 na kuvumbua kazi za werevu, na kufanya kazi ya dhahabu, na fedha, na shaba, 33 na kukata vito vya kutilia, na kuchora miti, atumike katika kazi za werevu kila aina. 34 Naye amemtilia moyoni mwake ili apate kufundisha, yeye, na Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. 35 Amewajaza watu hao akili za moyoni, ili watumike katika kazi kila aina, ya mwenye kuchora mawe, na kazi ya werevu, na ya mwenye kutia taraza, katika nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri, na ya mwenye kufuma nguo; ya hao wafanyao kazi yo yote, na ya wenye kuvumbua kazi za werevu.

Kutoka 36

1 Basi Bezaleli na Oholiabu watatenda kazi, na kila mtu mwenye moyo wa hekima, ambaye Bwana amemtia akili na hekima ili ajue kufanya kazi hiyo yote kwa huo utumishi wa mahali patakatifu, kama hayo yote Bwana aliyoyaagiza. 2 Basi Musa akawaita Bezaleli na Oholiabu, na kila mtu aliyekuwa na moyo wa akili, ambaye Bwana alimtia moyoni mwake hekima, kila mtu ambaye moyo wake ulimhimiza ili aende kuifanya kazi hiyo; 3 nao wakapokea mkononi mwa Musa matoleo yote, ambayo hao wana wa Israeli walikuwa wameyaleta kwa ajili ya huo utumishi wa mahali patakatifu, ili wapafanye. Kisha wakamletea matoleo kila siku asubuhi kwa moyo wa kupenda. 4 Na hao watu wote wenye hekima, waliotumika katika kazi yote ya mahali patakatifu, wakaenda kila mtu kutoka katika kazi yake aliyokuwa akiifanya; 5 nao wakasema na Musa, na kumwambia, Watu waleta vitu vingi sana zaidi ya hivyo vitoshavyo kwa ajili ya utumishi wa hiyo kazi, ambayo Bwana aliagiza ifanywe. 6 Basi Musa akatoa amri, nao wakatangaza mbiu katika marago yote, wakisema, Wasifanye kazi tena, mtu mume wala mwanamke, kwa ajili ya matoleo kwa mahali patakatifu. Basi watu wakazuiwa wasilete tena. 7 Kwani vile vitu walivyokuwa navyo vilikuwa vyatosha kwa kuifanya kazi hiyo yote, kisha vilizidi. 8 Basi kila mtu mwenye moyo wa hekima miongoni mwa hao waliofanya kazi, akaifanya hiyo maskani ya mapazia kumi; ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, na nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu; pamoja na makerubi, kazi ya fundi stadi; ndivyo alivyoyafanya. 9 Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa ishirini na nane, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; mapazia yote yalikuwa ya kipimo kimoja. 10 Naye akaunganisha mapazia matano hili na hili; na mapazia matano mengine akayaunganisha hili na hili. 11 Kisha akafanya matanzi ya rangi ya samawi katika ncha za pazia moja, katika upindo wa kiungo chake; akafanya vivyo katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili. 12 Akafanya matanzi hamsini katika pazia moja, na matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililokuwa katika kiungo cha pili; hayo matanzi yalikuwa yakabiliana hili na hili. 13 Kisha akafanya vifungo hamsini vya dhahabu, na kuyaunganya hayo mapazia hili na hili kwa vile vifungo; hivi ile maskani ilikuwa ni moja. 14 Kisha akafanya vifuniko vya singa za mbuzi kuwa hema ya kuifunika hiyo maskani; akafanya mapazia kumi na moja. 15 Urefu wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa thelathini, na upana wa kila pazia ulikuwa ni dhiraa nne; hayo mapazia yote kumi na moja yalikuwa ya kipimo kimoja. 16 Naye akaunganya mapazia matano mbali, na mapazia sita mbali. 17 Kisha akafanya matanzi hamsini katika upindo wa pazia lililo upande wa nje katika kile kiungo, naye akafanya matanzi hamsini katika ncha ya pazia lililokuwa upande wa nje katika kiungo cha pili. 18 Kisha akafanya vifungo hamsini vya shaba aiunganye ile hema pamoja, ili iwe hema moja. 19 Kisha akafanya kifuniko kwa ajili ya hiyo hema cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu; tena juu yake akafanya kifuniko cha ngozi za pomboo. 20 Kisha akafanya mbao za mti wa mshita kwa hiyo maskani, zilizosimama. 21 Urefu wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa kumi, na upana wa kila ubao ulikuwa ni dhiraa moja na nusu. 22 Kila ubao ulikuwa na ndimi mbili, zilizounganywa pamoja; ndivyo alivyozifanya hizo mbao zote za maskani. 23 Naye akazifanya hizo mbao kwa ajili ya hiyo maskani; mbao ishirini kwa upande wa kusini kuelekea kusini; 24 naye akafanya matako ya fedha arobaini yawe chini ya hizo mbao ishirini; matako mawili chini ya ubao mmoja kwa hizo ndimi zake mbili, na matako mawili chini ya ubao mwingine kwa ndimi zake mbili. 25 Na kwa upande wa pili wa maskani upande wa kaskazini, akafanya mbao ishirini, 26 na matako yake ya fedha arobaini; matako mawili chini ya ubao mmoja, na matako mawili chini ya ubao mwingine. 27 Na kwa upande wa nyuma wa hiyo maskani kuelekea magharibi akafanya mbao sita. 28 Naye akafanya mbao mbili kwa pembe za maskani upande wa nyuma. 29 Nazo zilikuwa mbao pacha upande wa chini, vivyo zilishikamana pamoja hata ncha ya juu kufikilia pete ya kwanza; ndivyo alivyofanya zote mbili katika hizo pembe mbili. 30 Hivyo zilikuwa mbao nane, na matako yake ya fedha, matako kumi na sita, matako mawili chini ya kila ubao. 31 Kisha akafanya mataruma ya miti ya mshita; matano kwa mbao za upande mmoja wa maskani; 32 na mataruma matano kwa mbao za upande wa pili wa maskani, na mataruma matano kwa hizo mbao za maskani zilizokuwa upande wa nyuma kuelekea magharibi. 33 Naye akalifanya hilo taruma la katikati lipenye kati ya hizo mbao kutoka upande huu hata upande huu. 34 Naye akazifunika hizo mbao dhahabu, akazifanya zile pete zake za dhahabu ziwe mahali pa hayo mataruma, akayafunika dhahabu hayo mataruma. 35 Kisha akafanya hilo pazia la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri zilizosokotwa; akatia na makerubi kazi ya fundi stadi, ndivyo alivyofanya. 36 Naye akafanya kwa ajili yake nguzo nne za mti wa mshita, akazifunika dhahabu; na kulabu zake zilikuwa za dhahabu; naye akasubu kwa ajili yake matako manne ya fedha. 37 Kisha akafanya pazia la sitara kwa ajili ya mlango wa Hema, la nguo ya rangi ya samawi, na ya rangi ya zambarau, na nyekundu, na nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kazi ya mwenye kutia taraza, 38 na nguzo zake tano pamoja na kulabu zake; naye akavifunika dhahabu vichwa vyake na vifungo vyake; na matako yake matano yalikuwa ya shaba.

Kutoka 37

1 Kisha Bezaleli akalifanya lile sanduku la mti wa mshita, urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa moja na nusu; 2 akalifunika dhahabu safi, ndani na nje, akafanya na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote. 3 Naye akasubu pete nne za dhahabu kwa ajili yake, katika miguu yake minne; pete mbili upande wake mmoja na pete mbili upande wake wa pili. 4 Akafanya na miti ya kulichukulia, ya mti wa mshita akaifunika dhahabu. 5 Naye akaitia hiyo miti katika zile pete zilizokuwa ubavuni mwa sanduku, ili kulichukua hilo sanduku. 6 Kisha akafanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake ulikuwa dhiraa mbili na nusu na upana wake ulikuwa dhiraa moja na nusu. 7 Kisha akafanya makerubi mawili ya dhahabu; akayafanya ya kazi ya kufua, yawe katika miisho miwili ya kiti cha rehema; 8 kerubi moja mwisho huu, na kerubi moja mwisho huu; alifanya hayo makerubi mawili ya kitu kimoja na hicho kiti cha rehema katika miisho yake miwili. 9 Na hayo makerubi yakayanyosha mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zilikuwa zaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zilikuwa zikielekea kiti cha rehema. 10 Kisha akafanya hiyo meza ya mti wa mshita; urefu wake ulikuwa ni dhiraa mbili, na upana wake ulikuwa ni dhiraa moja, na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa moja na nusu; 11 naye akaifunika dhahabu safi, akaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote. 12 Kisha akaifanyia upapi wa upana wa shibiri kuizunguka pande zote, akauzungushia ukingo wa urembo wa dhahabu ule upapi. 13 Naye akasubu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, akavitia vile vikuku katika pembe nne, katika miguu yake minne. 14 Vile vikuku vilikuwa karibu na ule upapi, ili viwe mahali pa kutilia ile miti, ya kuichukulia meza. 15 Naye akaifanya hiyo miti ya kuichukulia, ya mti wa mshita, akaifunika dhahabu, ili kuichukua hiyo meza. 16 Kisha, vile vyombo vilivyokuwa juu ya meza, sahani zake, na miiko yake, na bakuli zake, na makopo yake ya kumiminia, akavifanya vya dhahabu safi. 17 Kisha akakifanya kile kinara cha taa cha dhahabu safi, akakifanya kile kinara cha taa cha kazi ya kufua, tako lake, na mti wake; vikombe vyake, na matovu yake, na maua yake, vyote vilikuwa vya kitu kimoja nacho, 18 nacho kilikuwa na matawi sita yaliyotoka ubavuni mwake; matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu, na matawi matatu ya kinara yalikuwa upande huu; 19 vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi vilikuwa katika tawi moja, tovu na ua; na vikombe vitatu, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, katika tawi la pili, tovu na ua; yalikuwa ni vivyo hivyo yale matawi sita yaliyokuwa katika hicho kinara. 20 Katika kinara mlikuwa na vikombe vinne, vilivyofanywa mfano wa maua ya mlozi, matovu yake na maua yake; 21 kisha chini ya matawi mawili mlikuwa na tovu iliyokuwa ya kitu kimoja nacho, na chini ya matawi mawili mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho, tena chini ya matawi mawili hayo mengine mlikuwa na tovu ya kitu kimoja nacho; kwa ajili ya hayo matawi sita, yaliyotokana nacho. 22 Hayo matovu yake na matawi yake yalikuwa ya kitu kimoja nacho; kinara hicho kizima chote pia ni kazi moja ya kufua ya dhahabu safi. 23 Kisha akafanya taa zake saba, na makoleo yake, na visahani vyake, vya dhahabu safi. 24 Akakifanya cha talanta moja ya dhahabu safi, pamoja na vyombo vyake vyote. 25 Kisha akafanya hiyo madhabahu ya kufukizia uvumba ya mti wa mshita; urefu wake ulikuwa ni dhiraa moja, na upana wake ulikuwa ni dhiraa moja, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa ni dhiraa mbili; na pembe zake zilikuwa za kitu kimoja nayo. 26 Naye akaifunika dhahabu safi, upande wa juu, na mbavu zake pande zote, na hizo pembe zake; akaifanyia na ukingo wa dhahabu kuizunguka pande zote. 27 Naye akaifanyia vikuku viwili vya dhahabu na kuvitia chini ya ukingo wake, katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili, viwe ni mahali pa hiyo miti ya kuichukulia. 28 Kisha akafanya hiyo miti kwa mti wa mshita, na kuifunika dhahabu. 29 Kisha akayafanya hayo mafuta matakatifu ya kutiwa, na ule uvumba safi wa viungo vya manukato vizuri, kwa kuandama kazi ya mtengezaji manukato.

Kutoka 38

1 Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu. 2 Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba. 3 Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba. 4 Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu. 5 Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia. 6 Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba. 7 Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao. 8 Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania. 9 Naye akafanya ule ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua ya ua ilikuwa ya nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia; 10 nguzo zake zilikuwa ishirini, na matako yake yalikuwa ishirini, yalikuwa ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 11 Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia vivyo, nguzo zake ishirini na matako yake ishirini, yalikuwa ni ya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 12 Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na matako yake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 13 Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini. 14 Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na matako yake matatu; 15 ni vivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na matako yake matatu. 16 Chandarua za nguo zote za ule ua zilizouzunguka pande zote zilikuwa za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa. 17 Na matako ya zile nguzo yalikuwa ya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha. 18 Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wake dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua. 19 Na nguzo zake zilikuwa nne, na matako yake manne, yalikuwa ya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha. 20 Na vigungi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba. 21 Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani. 22 Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda, akafanya yote Bwana aliyomwagiza Musa. 23 Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri. 24 Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na kenda, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu. 25 Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu; 26 kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya watu waume sita mia na tatu elfu, na mia tano na hamsini (603,550). 27 Na hizo talanta mia za fedha zilikuwa kwa kusubu yale matako ya mahali patakatifu na matako ya hilo pazia; matako mia kwa hizo talanta mia, talanta moja tako moja. 28 Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake. 29 Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne. 30 Naye akafanya ya hiyo shaba matako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu, 31 na matako ya ua kuuzunguka pande zote, na matako ya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.

Kutoka 39

1 Na zile nyuzi za rangi ya samawi, na nyuzi za rangi ya zambarau, na nyekundu, wakafanya mavazi yaliyofumwa kwa ustadi sana kwa ajili ya kutumika katika mahali patakatifu, na kuyafanya hayo mavazi matakatifu ya Haruni, vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 2 Naye akaifanya hiyo naivera, ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. 3 Nao wakaifua hiyo dhahabu hata ikawa mabamba membamba sana, kisha wakaikata iwe nyuzi, ili wapate kuifuma pamoja na hizo nyuzi za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyuzi nyekundu na za kitani nzuri, kazi ya fundi stadi sana. 4 Nao wakafanya na vipande vya mabegani kwa ajili yake, vilivyoungwa pamoja; viliungwa pamoja kwa ncha zake mbili. 5 Na huo mshipi wa kazi ya werevu, uliokuwa juu yake ili kuifunga mahali pake; ulikuwa wa kitu kimoja, na wa kazi moja na naivera ya dhahabu, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 6 Nao wakavitengeza vile vito vya shohamu, vilivyotiwa katika vijalizo vya dhahabu, vilivyochorwa mfano wa kuchora kwake muhuri, kwa majina ya hao wana wa Israeli. 7 Naye akavitia katika vile vipande vya mabegani vya hiyo naivera, viwe vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 8 Naye akafanya kile kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi, kama hiyo kazi ya naivera; ya nyuzi za dhahabu, na za rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa. 9 Kilikuwa mraba; wakakifanya kile kifuko cha kifuani kwa kukikunja; urefu wake ulikuwa shibiri, na upana wake ulikuwa shibiri, tena kilikuwa ni cha kukunjwa. 10 Nao wakatia safu nne za vito ndani yake, safu moja ilikuwa ni akiki, na yakuti ya rangi ya manjano, na baharamani, vilikuwa ni safu ya kwanza. 11 Na safu ya pili ilikuwa zumaridi, na yakuti samawi, na almasi. 12 Na safu ya tatu ilikuwa ni hiakintho, na akiki nyekundu, na amethisto. 13 Na safu ya nne ilikuwa ni zabarajadi, na shohamu, na yaspi: vito hivyo vilikuwa vimetiwa katika vijalizo vya dhahabu, kila kimoja mahali pake. 14 Na hivyo vito vilikuwa vyaandama majina ya wana wa Israeli, kumi na mawili, sawasawa na majina yao; mfano wa kuchora muhuri, kila moja kwa jina lake, kwa zile kabila kumi na mbili. 15 Nao wakafanya katika kile kifuko cha kifuani mikufu mfano wa kamba, ya kazi ya kusokotwa ya dhahabu safi. 16 Nao wakafanya vijalizo viwili vya dhahabu, na pete mbili za dhahabu; nao wakazitia hizo pete mbili katika ncha mbili za hicho kifuko. 17 Nao wakaitia hiyo mikufu miwili iliyosokotwa katika hizo pete mbili zilizokuwa katika ncha mbili za hicho kifuko. 18 Na ncha hizo mbili nyingine, za hiyo mikufu miwili ya kusokotwa, wakazitia katika vile vijalizo viwili, na kuvitia katika vile vipande vya mabegani vya naivera, upande wa mbele. 19 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika ncha mbili za kifuko cha kifuani, katika ukingo wake, ulio upande wa naivera ulio ndani. 20 Nao wakafanya pete mbili za dhahabu, na kuzitia katika vile vipande viwili vya ile naivera chini yake, upande wa mbele, karibu na kifungo chake, juu ya huo mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi. 21 Nao wakakikaza kile kifuko kwa pete zake kwenye naivera kwa ukanda wa rangi ya samawi, ili kikae pale juu ya mshipi wa naivera uliosukwa kwa ustadi, na ya kwamba kifuko cha kifuani kisiachane na naivera; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 22 Naye akafanya hiyo joho ya naivera ya kazi ya kusuka, rangi ya samawi yote; 23 na hilo tundu lililokuwa katikati yake, mfano wa tundu lililo katika kanzu ya chuma, na utepe wake kulizunguka hilo tundu, ili lisipasuke. 24 Nao wakatia katika upindo wa joho makomamanga ya nyuzi za rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na rangi nyekundu, na kitani iliyosokotwa. 25 Nao wakafanya njuga za dhahabu safi, na kuzitia hizo njuga kati ya hayo makomamanga pande zote, kati ya hayo makomamanga; 26 njuga na komamanga, njuga na komamanga katika pindo za joho kuizunguka pande zote, ili kutumika kwa hiyo; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 27 Nao wakafanya hizo kanzu za nguo ya kitani nzuri ya kufumwa, kwa Haruni, na kwa wanawe 28 na hicho kilemba cha nguo ya kitani nzuri, na zile kofia nzuri za kitani, na hizo suruali za nguo ya kitani nzuri iliyosokotwa, 29 na huo mshipi wa nguo nzuri ya kitani iliyosokotwa, na rangi ya samawi, na rangi ya zambarau, na nyekundu, kazi ya fundi mwenye kutia taraza; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 30 Nao wakafanya hilo bamba la hiyo taji takatifu la dhahabu safi, na kuandika juu yake andiko, mfano wa kuchorwa kwa muhuri, MTAKATIFU KWA Bwana. 31 Nao wakatia ukanda wa rangi ya samawi ili kulifunga katika hicho kilemba upande wa juu; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 32 Basi ndivyo ilivyomalizwa kazi yote ya maskani ya hema ya kukutania; na wana wa Israeli walifanya kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya. 33 Nao wakamletea Musa hiyo maskani; yaani Hema, na vyombo vyake vyote, vifungo vyake, na mbao zake, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake; 34 na kifuniko chake cha ngozi za kondoo waume zilizotiwa rangi nyekundu, na kifuniko cha ngozi za pomboo, na pazia la sitara; 35 na sanduku la ushuhuda, na miti yake, na kiti cha rehema; 36 na meza, na vyombo vyake vyote, na mikate ya wonyesho; 37 na kinara cha taa safi, na taa zake, hizo taa za kuwekwa mahali pake, na vyombo vyake vyote, na mafuta ya taa, 38 na madhabahu ya dhahabu, na mafuta ya kutiwa, na uvumba mzuri, na pazia kwa mlango wa hema; 39 na madhabahu ya shaba, na wavu wake wa shaba, na miti yake, na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake; 40 na ukuta wa nguo wa ua, na nguzo zake na matako yake, na pazia la lango la ua, na kamba zake, na vigingi vyake, na vyombo vyote vya kutumiwa katika utumishi wa maskani, kwa hiyo hema ya kukutania, 41 na mavazi ya kazi nzuri kwa utumishi katika mahali patakatifu, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani. 42 Sawasawa na yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyoifanya hiyo kazi yote wana wa Israeli. 43 Musa akaiona hiyo kazi yote, na tazama, walikuwa wameimaliza; vile vile kama Bwana alivyoagiza, walikuwa wameifanya vivyo; basi Musa akawaombea heri.

Kutoka 40

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza utaisimamisha hiyo maskani ya hema ya kukutania. 3 Nawe utatia ndani yake sanduku la ushuhuda, nawe utalisitiri hilo sanduku kwa pazia. 4 Nawe utaleta meza na kuitia ndani, na kuviweka sawasawa vile vitu juu yake; kisha utakileta ndani kile kinara cha taa, na kuziwasha taa zake. 5 Kisha utaisimamisha madhabahu ya dhahabu kwa kufukizia uvumba mbele ya sanduku la ushuhuda, na kulitia pazia mlangoni mwa hiyo maskani. 6 Kisha utaweka madhabahu ya kuteketeza sadaka mbele ya mlango wa maskani ya hema ya kukutania. 7 Kisha utaliweka birika kati ya hema ya kukutania na hiyo madhabahu, nawe utatia maji ndani yake. 8 Kisha utausimamisha ukuta wa ua kuuzunguka pande zote, na kuitundika sitara ya lango la ua. 9 Kisha utayatwaa mafuta ya kutiwa, na kuitia mafuta hiyo maskani, na kila kitu kilicho ndani yake, na kuiweka iwe takatifu, na vyombo vyake vyote; nayo itakuwa takatifu. 10 Kisha utaitia mafuta madhabahu ya kuteketeza sadaka, na vyombo vyake vyote; na kuiweka takatifu madhabahu; na hiyo madhabahu itakuwa takatifu sana. 11 Kisha utalitia mafuta birika na tako lake, na kuliweka liwe takatifu. 12 Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji. 13 Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani. 14 Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao; 15 nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote. 16 Musa akafanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya. 17 Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi ile maskani ilisimamishwa. 18 Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake. 19 Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa. 20 Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku; 21 kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa. 22 Akaitia meza ndani ya hema ya kukutania, upande wa maskani ulioelekea kaskazini, nje ya pazia. 23 Akaipanga ile mikate juu yake mbele za Bwana; kama Bwana alivyomwamuru Musa. 24 Kisha akakitia kinara cha taa ndani ya hema ya kukutania, kuikabili ile meza, upande wa maskani ulioelekea kusini. 25 Kisha akaziwasha taa zake mbele za Bwana, kama Bwana alivyomwamuru Musa. 26 Akaitia madhabahu ya dhahabu ndani ya hema ya kukutania mbele ya pazia. 27 Akafukiza juu yake uvumba wa manukato kama Bwana alivyomwamuru Musa. 28 Akalitia pazia la mlango wa maskani. 29 Akaiweka madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mlangoni pa maskani ya kukutania, akatoa sadaka ya kuteketezwa juu yake, na sadaka ya unga; kama Bwana alivyomwamuru Musa. 30 Akaliweka birika kati ya hema ya kukutania na madhabahu, akatia maji ndani yake ya kuoshea. 31 Musa na Haruni, na wanawe wakanawa mikono yao na miguu yao ndani yake; 32 hapo walipoingia hema ya kukutania, na hapo walipoikaribia madhabahu walinawa kama Bwana alivyomwamuru Musa. 33 Akausimamisha ukuta wa ua kuizunguka maskani na madhabahu, akalitundika pazia la mlango wa ule ua. Basi Musa akaimaliza hiyo kazi. 34 Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. 35 Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. 36 Na hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote, 37 bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena. 38 Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana, na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku, mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.

Mambo ya Walawi 1

1 Bwana akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea Bwana matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo. 3 Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya Bwana. 4 Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. 5 Naye atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kando-kando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania 6 Kisha atachuna sadaka ya kuteketeza na kuikata vipande vyake. 7 Kisha wana wa Haruni, watatia moto juu ya madhabahu, na kuzipanga kuni juu ya moto, 8 kisha wana wa Haruni, makuhani, watazipanga kuni zilizo juu ya moto uliopo juu ya madhabahu; 9 lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana. 10 Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu. 11 Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za Bwana; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote. 12 Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu; 13 lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana. 14 Na matoleo yake atakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa, kwamba ni katika ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa. 15 Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu; 16 kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu; 17 kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.

Mambo ya Walawi 2

1 Na mtu atakapomtolea Bwana matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake; 2 kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana; 3 na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 4 Tena, utakapotoa matoleo ya sadaka ya unga uliookwa tanuuni, yatakuwa mikate isiyotiwa chachu, ya unga mwembamba uliokandwa na mafuta, au maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta. 5 Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga wa kaangoni, yatakuwa ya unga mwembamba usiotiwa chachu, uliokandwa na mafuta. 6 Utaukata-kata vipande, na kutia mafuta juu yake; ni sadaka ya unga. 7 Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga ya chunguni, yataandaliwa kwa unga mwembamba pamoja na mafuta. 8 Nawe utamletea Bwana sadaka ya unga iliyofanywa ya vitu hivyo; nayo italetwa kwa kuhani, naye ndiye atakayeisongeza madhabahuni. 9 Kisha kuhani atatwaa humo huo ukumbusho wa sadaka ya unga, naye atauteketeza juu ya madhabahu; ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana. 10 Na hicho kitakachosalia katika sadaka ya unga kitakuwa cha Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 11 Sadaka ya unga iwayo yote itakayosongezwa kwa Bwana isitiwe chachu kabisa; kwa kuwa hamtateketeza chachu, wala asali iwayo yote, kuwa ni sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 12 Vitu hivyo mtavisongeza kwa Bwana kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza. 13 Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote. 14 Nawe kwamba wamtolea Bwana sadaka ya unga ya malimbuko, utatoa hiyo ngano katika masuke yake iliyochomwa motoni, ngano iliyopondwa ya masuke mabichi, ndiyo utakayoleta kuwa sadaka ya unga ya malimbuko yako. 15 Nawe utatia mafuta juu yake, na kuweka ubani juu yake; ni sadaka ya unga. 16 Huyo kuhani atauteketeza ukumbusho wake, yaani, sehemu ya ngano iliyopondwa ya hiyo sadaka, na sehemu ya mafuta yake, pamoja na ule ubani wake wote; ni kafara ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

Mambo ya Walawi 3

1 Na matoleo yake kwamba ni sadaka za amani; kwamba asongeza katika ng'ombe, mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu mbele ya Bwana. 2 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemtoa, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote. 3 Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani, dhabihu kwa Bwana itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo juu ya matumbo, 4 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno, na hicho kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa. 5 Na wana wa Haruni watayateketeza kwa moto juu ya madhabahu, juu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo katika kuni zilizo juu ya moto; ni dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana. 6 Na matoleo yake kwa sadaka za amani atakayomchinjia Bwana, kwamba ni katika kundi la kondoo; mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu. 7 Kama akimtoa mwana-kondoo kuwa matoleo yake, ndipo atakapomtolea Bwana; 8 naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemsongeza, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote. 9 Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani dhabihu kwa Bwana, itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yake, na mkia wenye mafuta mzima, atauondoa kwa kuukata hapo karibu na mfupa wa maungoni; na mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo, 10 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa. 11 Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 12 Na matoleo yake, kwamba ni mbuzi, ndipo atakapomtoa mbele za Bwana; 13 naye ataweka mkono wake kichwani mwake, na kumchinja hapo mbele ya hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote. 14 Naye atasongeza katika sadaka hiyo matoleo yake, dhabihu kwa Bwana kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo, 15 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini pamoja na hizo figo mbili; hayo yote atayaondoa. 16 Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, iwe harufu ya kupendeza; mafuta yote ni ya Bwana. 17 Neno hili litakuwa amri ya daima, katika vizazi vyenu vyote, ndani ya nyumba zenu zote, ya kwamba hamtakula mafuta wala damu kabisa.

Mambo ya Walawi 4

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Haya, nena na wana wa Israeli, uwaambie, Kama mtu ye yote akifanya dhambi pasipo kukusudia, katika neno lo lote ambalo Bwana amelizuilia lisifanywe, na kutenda neno lo lote la maneno hayo; 3 kama kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu; ndipo na atoe kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya, na kumsongeza kwa Bwana ng'ombe mume mchanga mkamilifu, kuwa ni sadaka ya dhambi. 4 Naye atamleta huyo ng'ombe na kumweka mlangoni pa hiyo hema ya kukutania, mbele za Bwana; naye ataweka mkono wake kichwani mwake ng'ombe, na kumchinja huyo ng'ombe mbele za Bwana. 5 Kisha huyo kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng'ombe, na kuileta ndani ya hiyo hema ya kukutania; 6 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza damu mbele ya Bwana mara saba, mbele ya pazia la mahali patakatifu. 7 Kisha kuhani atatia baadhi ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba mzuri mbele ya Bwana iliyo ndani ya hema ya kukutania; kisha damu yote ya huyo ng'ombe ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyoko mlangoni pa hema ya kukutania. 8 Kisha mafuta yote ya huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi atayaondoa; mafuta yote yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo, 9 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo, hayo yote atayaondoa, 10 vile vile kama yanavyoondolewa katika ng'ombe wa kuchinjwa kwa sadaka za amani; kisha huyo kuhani atayateketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. 11 Kisha ngozi yake ng'ombe, na nyama yake yote, pamoja na kichwa chake, na pamoja na miguu yake, na matumbo yake, na mavi yake, 12 maana, huyo ng'ombe mzima atamchukua nje ya marago hata mahali safi, hapo wamwagapo majivu, naye atamchoma moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo majivu yamwagwapo. 13 Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na Bwana, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia; 14 hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania. 15 Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng'ombe mbele za Bwana; 16 kisha ng'ombe atachinjwa mbele za Bwana. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng'ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania; 17 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za Bwana, mbele ya pazia mara saba. 18 Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za Bwana, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania. 19 Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu. 20 Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng'ombe; kama alivyomfanyia huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa. 21 Kisha atamchukua huyo ng'ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng'ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano. 22 Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo Bwana, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia; 23 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu; 24 kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana; ni sadaka ya dhambi. 25 Kisha kuhani atatwaa katika damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza. 26 Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa. 27 Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia; 28 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. 29 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa. 30 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu. 31 Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa. 32 Naye akileta mwana-kondoo kuwa sadaka ya dhambi, ataleta wa kike mkamilifu. 33 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake sadaka ya dhambi, kisha atamchinja awe sadaka ya dhambi, mahali hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa. 34 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya kuteketezwa kwa kidole chake na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kisha damu yake yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu; 35 kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama mafuta ya mwana-kondoo yalivyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kwa desturi ya hizo sadaka za Bwana zilizosongezwa kwa njia ya moto; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.

Mambo ya Walawi 5

1 Na mtu awaye yote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe; 2 au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, kama ni mzoga wa mnyama wa nyikani aliye najisi, au kama ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au kama ni mzoga wa mdudu aliye najisi, naye jambo hilo linamfichamania, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake; 3 au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu uwao wote ambao kwa huo amepata unajisi, na jambo hilo linamfichamania, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia; 4 au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo; 5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa; 6 naye atamletea Bwana sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake. 7 Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea Bwana hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa. 8 Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamkongonyoa kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili; 9 kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi. 10 Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa. 11 Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi. 12 Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi. 13 Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa. 14 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 15 Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya Bwana; ndipo atakapomletea Bwana sadaka yake ya hatia, kondoo mume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia; 16 naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa. 17 Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake. 18 Naye ataleta kondoo mume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa. 19 Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za Bwana.

Mambo ya Walawi 6

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya Bwana, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe; 3 au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo; 4 ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye, 5 au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia. 6 Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa Bwana, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani; 7 na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo. 8 Bwana akanena na Musa na kumwambia, 9 Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike. 10 Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu. 11 Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi. 12 Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. 13 Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike. 14 Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za Bwana, mbele ya madhabahu. 15 Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa Bwana. 16 Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula. 17 Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia. 18 Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya Bwana yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu 19 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 20 Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea Bwana, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni. 21 Utaandaliwa kaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana. 22 Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa Bwana kwa amri ya milele. 23 Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe. 24 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 25 Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya hiyo sadaka ya dhambi ni hii; mahali hapo pachinjwapo sadaka ya kuteketezwa ndipo itakapochinjwa sadaka ya dhambi, mbele za Bwana; ni takatifu sana. 26 Huyo kuhani atakayeisongeza kwa ajili ya dhambi ndiye atakayeila; italiwa katika mahali patakatifu, katika ua wa hema ya kukutania. 27 Kila kitu kitakachoigusa nyama ya sadaka hiyo kitakuwa kitakatifu; tena itakapomwagika damu yake yo yote katika nguo yo yote, utaifua nguo hiyo iliyomwagiwa, katika mahali patakatifu. 28 Lakini hicho chombo cha udongo ambacho hiyo nyama ilipikwa ndani yake kitavunjwa; na kama ikipikwa katika chombo cha shaba, kitasuguliwa, na kuoshwa kwa maji. 29 Kila mwana mume miongoni mwa makuhani atakula katika hiyo; ni takatifu sana. 30 Wala haitaliwa sadaka ya dhambi yo yote, ambayo damu yake yo yote ililetwa ndani ya hema ya kukutania, ili kufanya upatanisho katika mahali patakatifu; itachomwa moto.

Mambo ya Walawi 7

1 Na sheria ya hiyo sadaka ya hatia ni hii; ni takatifu sana. 2 Wataichinja sadaka ya hatia pale pale waichinjapo sadaka ya kuteketezwa; na damu yake atainyunyiza katika madhabahu pande zote. 3 Katika sadaka hiyo atasongeza mafuta yake yote; yaani, mkia wake wenye mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo, 4 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na figo zake mbili, hayo yote atayaondoa; 5 na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kuwa dhabihu kwa Bwana kwa njia ya moto; ni sadaka ya hatia. 6 Kila mtu mume miongoni mwa makuhani atakula katika sadaka hiyo; italiwa katika mahali patakatifu; ni takatifu sana. 7 Kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo, na sadaka ya hatia ni vivyo; sheria yake ni moja; huyo kuhani afanyaye upatanisho kwayo, ndiye atakayekuwa nayo. 8 Tena kuhani atakayesongeza sadaka ya kuteketezwa ya mtu awaye yote, huyo kuhani atatwaa awe nayo ngozi ya huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa aliyemsongeza. 9 Na kila sadaka ya unga iliyookwa mekoni, na yote yaliyoandaliwa chunguni, au kaangoni, yote yatakuwa ya huyo kuhani aliyeyasongeza. 10 Na kila sadaka ya unga, kama umeandaliwa na mafuta, au kama ni mkavu, watautwaa wana wote wa Haruni kuutumia, kila mtu sawasawa. 11 Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa Bwana, ni hii. 12 Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta. 13 Ataleta matoleo yake, pamoja na mikate iliyotiwa chachu, na pamoja na sadaka zake za amani, kwa ajili ya shukrani. 14 Na katika hayo atasongeza kimoja katika kila toleo kiwe sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana; itakuwa ni ya kuhani atakayeinyunyiza hiyo damu ya sadaka za amani. 15 Na hiyo nyama ya sadaka zake za amani zilizochinjwa kwa ajili ya shukrani italiwa siku iyo hiyo ya matoleo yake; asisaze yo yote hata asubuhi. 16 Lakini kwamba hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa; 17 lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto. 18 Tena kama nyama yo yote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake. 19 Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila; 20 lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za Bwana, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. 21 Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu cho chote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yo yote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za Bwana, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. 22 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 23 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yo yote, ya ng'ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi. 24 Tena mafuta ya mnyama afaye mwenyewe, na mafuta ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, mna ruhusa kuyatumia kwa ajili ya matumizi mengine; lakini msiyale kabisa. 25 Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa Bwana kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake. 26 Tena msiile damu yo yote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote. 27 Mtu ye yote alaye damu, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. 28 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 29 Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa Bwana, atamletea Bwana matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani; 30 mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana. 31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe. 32 Mguu wa nyuma wa upande wa kuume mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka katika hizo sadaka zenu za amani. 33 Katika wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kuume kuwa sehemu yake. 34 Kwa maana, hicho kidari cha kutikiswa, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli. 35 Hii ndiyo sehemu ya Haruni, na sehemu ya wanawe, katika kutiwa mafuta kwao, katika hizo dhabihu zisongezwazo kwa Bwana kwa njia ya moto, siku hiyo aliyowaweka ili wamtumikie Bwana katika kazi ya ukuhani; 36 sehemu ambayo Bwana aliagiza wapewe na wana wa Israeli, siku hiyo aliyowatia mafuta. Ni haki yao ya milele katika vizazi vyao vyote. 37 Sheria ya sadaka ya kuteketezwa ni hii, na ya sadaka ya unga, na ya sadaka ya dhambi, na ya sadaka ya hatia, na ya kuwekwa wakfu, na ya sadaka za amani; 38 ambazo Bwana alimwagiza Musa katika mlima wa Sinai, siku hiyo aliyowaagiza wana wa Israeli wamtolee Bwana matoleo yao, huko katika jangwa la Sinai.

Mambo ya Walawi 8

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi, na kondoo waume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu; 3 kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania. 4 Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na Bwana; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania. 5 Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza Bwana kwamba lifanywe, ni hili. 6 Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji. 7 Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya mstadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi. 8 Kisha akamtia kile kifuko cha kifuani; akatia hizo Urimu na Thumimu katika hicho kifuko cha kifuani. 9 Akamvika na kile kilemba kichwani mwake; na juu ya kilemba, upande wa mbele, akakitia kile kipande cha dhahabu, hiyo taji takatifu; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 10 Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa. 11 Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa. 12 Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase. 13 Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 14 Kisha akamleta yule ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi. 15 Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake. 16 Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu. 17 Lakini huyo ng'ombe mwenyewe, na ngozi yake, na nyama yake, na mavi yake, akayachoma moto nje ya marago; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa. 18 Kisha akamsongeza yule kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo. 19 Kisha akamchinja; na Musa akainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote. 20 Kisha akamkata kondoo vipande vyake; na Musa akateketeza kichwa, na vile vipande, na mafuta. 21 Kisha akayaosha matumbo na miguu yake kwa maji; na Musa akamteketeza huyo kondoo wote juu ya madhabahu; ilikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza; ilikuwa ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 22 Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo. 23 Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume. 24 Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote. 25 Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume; 26 kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za Bwana, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume; 27 kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana. 28 Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto. 29 Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huku, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo mume wa kuwaweka wakfu; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 30 Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye. 31 Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila. 32 Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto. 33 Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hata siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba. 34 Vile vile kama vilivyotendeka siku ya leo, ni vivyo Bwana alivyoagiza kufanywa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 35 Nanyi mtakaa mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba mchana na usiku, na kuulinda ulinzi wa Bwana ili kwamba msife; kwani ndivyo nilivyoagizwa. 36 Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote Bwana aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.

Mambo ya Walawi 9

1 Basi ilikuwa siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, pamoja na wazee wa Israeli; 2 akamwambia Haruni, Twaa wewe mwana-ng'ombe mume awe sadaka ya dhambi, na kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa, wakamilifu, ukawasongeze mbele ya Bwana. 3 Nawe utawaambia wana wa Israeli, ukisema, Twaeni mbuzi mume awe sadaka ya dhambi; na mwana-ng'ombe, na mwana-kondoo, wote wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, kwa sadaka ya kuteketezwa; 4 na ng'ombe mume, na kondoo mume, kwa sadaka za amani, ili kuwachinja mbele za Bwana; na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta; kwa maana, Bwana hivi leo atawatokea. 5 Nao wakayaleta hayo yaliyoagizwa na Musa wakayaweka mbele ya hema ya kukutania; kisha mkutano wote ukakaribia wakasimama mbele za Bwana. 6 Kisha Musa akasema, Neno aliloliagiza Bwana kwamba mlifanye ni hili; na huo utukufu wa Bwana utawatokea. 7 Musa akamwambia Haruni, Ikaribie madhabahu, uitoe sadaka yako ya dhambi, na sadaka yako ya kuteketezwa, ukafanye upatanisho kwa ajili ya nafsi yako, na kwa ajili ya watu; nawe uitoe hiyo dhabihu ya watu, ukafanye upatanisho kwa ajili yao; kama Bwana alivyoagiza. 8 Basi Haruni akakaribia madhabahuni, akamchinja huyo mwana-ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliyekuwa kwa ajili ya nafsi yake. 9 Kisha wana wa Haruni wakamsongezea Haruni ile damu; naye akatia kidole chake katika damu, na kuitia katika pembe za madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu; 10 lakini mafuta, na figo, na kitambi kilichotoka katika ini ya hiyo sadaka ya dhambi, akaviteketeza juu ya madhabahu, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 11 Na nyama, na ngozi akazichoma moto nje ya marago. 12 Naye akaichinja sadaka ya kuteketezwa; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote. 13 Nao wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu. 14 Kisha akaosha matumbo, na miguu na kuiteketeza juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. 15 Kisha akaisongeza dhabihu ya watu, akamtwaa mbuzi wa sadaka ya dhambi aliyekuwa kwa hao watu, na kumchinja, na kumtoa kwa ajili ya dhambi kama yule wa kwanza. 16 Kisha akaisongeza sadaka ya kuteketezwa, na kuitoa sawasawa na sheria. 17 Kisha akaisongeza sadaka ya unga, na kutwaa konzi humo, na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi. 18 Huyo ng'ombe mume naye akamchinja, na huyo kondoo mume pia, dhabihu ya sadaka za amani, zilizokuwa kwa ajili ya watu; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote, 19 na mafuta ya ng'ombe; na ya kondoo, mkia wake wa mafuta, na hayo yafunikayo matumbo, na figo zake, na kitambi cha ini; 20 nao wakayaweka hayo mafuta juu ya vidari, naye akayateketeza mafuta juu ya madhabahu; 21 na vile vidari, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume, Haruni akavitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana; kama Musa alivyoagiza. 22 Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani. 23 Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa Bwana ukawatokea watu wote. 24 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Mambo ya Walawi 10

1 Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya Bwana, ambao yeye hakuwaagiza. 2 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, nao ukawala, nao wakafa mbele za Bwana. 3 Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo Bwana alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya. 4 Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago. 5 Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema. 6 Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavao yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya hicho kichomo alichowasha Bwana. 7 Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya Bwana ya juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa. 8 Kisha Bwana akanena na Haruni, na kumwambia, 9 Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; 10 kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi; 11 tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo Bwana amewaambia kwa mkono wa Musa. 12 Kisha Musa akanena na Haruni, na Eleazari, na Ithamari, hao wanawe waliobaki, Twaeni hiyo sadaka ya unga iliyosalia katika kafara za Bwana zilizotolewa kwa moto, mkaile pasipo kutiwa chachu, pale karibu na madhabahu; kwa kuwa ni takatifu sana; 13 nanyi mtaila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni haki yako, na haki ya wanao, katika hizo kafara zisongezwazo kwa Bwana kwa moto; kwani ni hivyo nilivyoagizwa. 14 Na kidari cha kutikiswa, na mguu wa kuinuliwa, mtavila katika mahali palipo safi; wewe, na wanao, na binti zako pamoja nawe; kwa maana vimetolewa kuwa ni haki yako, na haki ya wanao, katika zile kafara za sadaka za amani za wana wa Israeli. 15 Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama Bwana alivyoagiza. 16 Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuchomwa moto; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia, 17 Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana? 18 Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza. 19 Haruni akamwambia Musa, Angalia, hivi leo wamesongeza sadaka yao ya dhambi, na sadaka yao ya kuteketezwa, mbele za Bwana; kisha mambo kama haya yamenipata; tena kama ningalikula hiyo sadaka ya dhambi hivi leo, je! Lingekuwa ni jambo la kupendeza mbele za macho ya Bwana? 20 Naye Musa aliposikia hayo, yakampendeza.

Mambo ya Walawi 11

1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi. 3 Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala. 4 Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 5 Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 6 Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. 7 Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. 8 Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu. 9 Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao. 10 Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu, 11 watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu. 12 Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu. 13 Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu; 14 na mwewe, na kozi kwa aina zake, 15 na kila kunguru kwa aina zake; 16 na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake; 17 na bundi, na mnandi, na bundi mkubwa; 18 na mumbi, na mwari, na mderi; 19 na korongo, na koikoi kwa aina zake, na hudihudi, na popo. 20 Tena vyote vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne, hivi ni machukizo kwenu. 21 Pamoja na hayo, hivi vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne ni halali kula, hao walio na miguu mirefu, ya kurukia juu ya nchi; 22 katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na nzige kuu kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake. 23 Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu. 24 Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni; 25 na mtu awaye yote atakayechukua cho chote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni. 26 Kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, naye hana kwato mbili, wala hacheui, huyo ni najisi kwenu; kila agusaye wanyama hao atakuwa ni najisi. 27 Tena kila mnyama aendaye kwa vitanga vyake, katika hao wanyama wote waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu; awaye yote atakayegusa mizoga yao, atakuwa ni najisi hata jioni. 28 Na huyo atakayechukua mzoga wa wanyama hao atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni; hao ni najisi kwenu 29 Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake, 30 na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi. 31 Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni. 32 Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi. 33 Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa. 34 Kila chakula kilichomo, ambacho ni kuliwa, hicho ambacho maji hutumiwa juu yake, kitakuwa ni najisi; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi. 35 Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande cho chote cha mizoga yao kitakuwa najisi; kwamba ni tanuru, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu. 36 Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi. 37 Na kipande cho chote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa zitakazopandwa, zitakuwa safi. 38 Lakini kwamba hizo mbegu zilitiwa maji na cho chote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu. 39 Kama akifa mnyama awaye yote, ambaye mna ruhusa kumla, yeye anayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hata jioni. 40 Na yeye atakayekula nyama ya mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; yeye atakayeuchukua mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni. 41 Na kila kitu kitambaacho juu ya nchi ni machukizo; hakitaliwa. 42 Kila aendaye kwa tumbo lake, na kila aendaye kwa miguu minne, na kila aendaye kwa miguu mingi, maana, ni vyote vyenye kutambaa vitambaavyo juu ya nchi, hamtavila, kwa kuwa ni machukizo. 43 Msifanye nafsi zenu kuwa ni chukizo kwa kitu cho chote chenye kutambaa, kitambaacho, wala msifanye nafsi zenu kuwa ni najisi kwa vitu hivyo, mkajipatia uchafu kwa hivyo. 44 Kwa kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi. 45 Kwa kuwa mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu. 46 Hii ndiyo sheria katika hao wanyama, na ndege, na kila kiumbe kilicho hai, kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi; 47 ili kupambanua kati ya hao walio najisi na hao walio safi, na kati ya kiumbe kilicho hai ambacho chaliwa, na hicho kilicho hai ambacho hakiliwi.

Mambo ya Walawi 12

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto mume, ndipo atakuwa yu najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi, ndivyo atakavyokuwa najisi. 3 Siku nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake. 4 Na huyo mwanamke atakaa katika damu ya kutakata kwake siku thelathini na tatu; asiguse kitu kilicho kitakatifu, wala asiingie mahali patakatifu, hata siku hizo za kutakata kwake zitakapotimia. 5 Lakini kwamba amezaa mtoto mke ndipo atakuwa najisi juma mbili, kama katika kutengwa kwake; naye atakaa katika damu ya kutakata kwake muda wa siku sitini na sita. 6 Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mwana, au kwa ajili ya binti, ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani; 7 na yeye atawasongeza mbele za Bwana, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika na jicho la damu yake. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, kwamba ni mtoto mume au mke. 8 Kama mali yake huyo mwanamke haimfikilii mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.

Mambo ya Walawi 13

1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king'aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo; 3 na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi. 4 Na hicho kipaku king'aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo; 5 kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena; 6 kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi. 7 Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani; 8 na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma. 9 Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani; 10 na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe, 11 ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi. 12 Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani; 13 ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi. 14 Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi. 15 Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma. 16 Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani, 17 na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi. 18 Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa, 19 na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo; 20 na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu. 21 Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; 22 na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo. 23 Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi. 24 Au mwili wa mtu ukiwa una mahali katika ngozi yake penye moto, na hiyo nyama iliyomea pale penye moto, kama kikiwa kipaku chekundu kidogo, au cheupe; 25 ndipo kuhani atapaangalia; na tazama, yakiwa malaika yaliyo katika kile kipaku yamegeuka kuwa meupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali penye moto; na kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma. 26 Lakini kuhani akipaangalia, na tazama, malaika meupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; 27 na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma. 28 Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili. 29 Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake, 30 ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu. 31 Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba; 32 na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, 33 ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena; 34 na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi. 35 Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake; 36 ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye yu najisi. 37 Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimeshangaa, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi. 38 Mtu, mume au mke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe; 39 ndipo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba hivyo, imetokea katika ngozi; yeye yu safi. 40 Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upaa, yu safi. 41 Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upaa wa kipaji; yu safi. 42 Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upaa, au kile kipaji kilicho na upaa, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upaa, au katika kipaji chake cha upaa. 43 Ndipo kuhani atamwangalia; na tazama, kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu-chekundu, katika kichwa chake chenye upaa, au katika kipaji chake cha upaa, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili; 44 yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake. 45 Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi. 46 Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago. 47 Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani; 48 likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi; 49 hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani; 50 na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba; 51 kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi. 52 Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto; 53 Na kama kuhani akitazama, na tazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu cho chote cha ngozi; 54 ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena; 55 kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; na tazama, ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, li najisi; utakichoma moto; ni uharibifu likiwa lina upaa ndani au nje. 56 Huyo kuhani akiangalia, na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa; 57 kisha, likionekana li vivyo katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utalichoma moto. 58 Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu cho chote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi. 59 Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Mambo ya Walawi 14

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani, 3 na huyo kuhani atatoka aende nje ya marago; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma; 4 ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo; 5 kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; 6 kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni; 7 kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani. 8 Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya marago, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba. 9 Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyushi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi. 10 Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta. 11 Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania; 12 kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; 13 kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana; 14 kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume; 15 kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto; 16 kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za Bwana; 17 na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia; 18 na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za Bwana. 19 Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa; 20 kisha kuhani ataisongeza hiyo sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, juu ya madhabahu na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi. 21 Tena kwamba ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta; 22 na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa. 23 Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za Bwana, kwa ajili ya kutakaswa kwake. 24 Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; 25 kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume; 26 kisha kuhani atamimina sehemu ya hayo mafuta katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto; 27 kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kuume mara saba mbele za Bwana; 28 kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia; 29 na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana. 30 Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata; 31 hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za Bwana. 32 Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo. 33 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 34 Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu; 35 ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu; 36 ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame; 37 naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta; 38 ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba; 39 siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba; 40 ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji; 41 naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu; 42 kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba. 43 Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa, 44 ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi. 45 Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu. 46 Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hata jioni. 47 Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake. 48 Tena kwamba kuhani akiingia ndani na kuangalia, na tazama, ikiwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba, baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atasema kwamba hiyo nyumba i safi, maana, pigo limepoa. 49 Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba; 50 naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; 51 kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba; 52 naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu; 53 lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi. 54 Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe; 55 na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba; 56 na kivimbe, na kikoko na kipaku king'aacho; 57 ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.

Mambo ya Walawi 15

1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu ye yote atakapokuwa na kisonono kimtokacho mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake. 3 Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake. 4 Kitanda cho chote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu cho chote ambacho akiketia kitakuwa najisi. 5 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 6 Na mtu atakayeketi katika kitu cho chote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 7 Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 8 Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa yu najisi hata jioni. 9 Na tandiko lo lote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi. 10 Mtu awaye yote atakayegusa kitu cho chote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hata jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 11 Na mtu ye yote atakayeguswa na mwenye kisonono, asipokuwa amenawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 12 Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwa-vunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini. 13 Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi. 14 Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege; 15 na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya kisonono chake. 16 Na mtu ye yote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 17 Na kila nguo, na kila ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni. 18 Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni. 19 Mwanamke ye yote, kama anatokwa na kitu, na kitu chake alichokuwa nacho mwilini mwake ni damu, ataketi katika kutengwa kwake muda wa siku saba; na mtu ye yote atakayemgusa atakuwa najisi hata jioni. 20 Na kitu cho chote akilaliacho katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho akiketia kitakuwa najisi. 21 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 22 Mtu ye yote atakayekigusa cho chote ambacho huyo mwanamke amekiketia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 23 Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni. 24 Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi. 25 Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi. 26 Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake. 27 Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 28 Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi. 29 Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania. 30 Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake. 31 Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao. 32 Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake yamtoka, akawa na unajisi kwa hiyo; 33 na ya mwanamke ambaye yu katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, kama ni mtu mume, kama ni mtu mke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi.

Mambo ya Walawi 16

1 Bwana akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za Bwana, wakafa; 2 Bwana akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema. 3 Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng'ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa. 4 Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa. 5 Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa. 6 Na Haruni atamtoa yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake. 7 Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania. 8 Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli. 9 Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Bwana, na kumtoa awe sadaka ya dhambi. 10 Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za Bwana ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli. 11 Na Haruni atamsongeza ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake. 12 Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia. 13 Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za Bwana, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa. 14 Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba. 15 Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, 16 naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. 17 Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. 18 Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. 19 Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke. 20 Naye akiisha kufanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, na hema ya kukutania, na madhabahu, atamleta yule mbuzi aliye hai. 21 Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari. 22 Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani. 23 Na Haruni ataingia katika hema ya kukutania, naye atavua mavazi yake ya kitani, aliyoyavaa alipoingia katika patakatifu, atayaacha humo; 24 naye ataosha mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na kuvaa nguo zake, na kutoka, na kusongeza sadaka ya kuteketezwa yake mwenyewe, na sadaka ya kuteketezwa ya watu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu. 25 Na mafuta ya sadaka ya dhambi atayateketeza juu ya madhabahu. 26 Na mtu yule amwachaye mbuzi wa Azazeli aende zake, ataosha nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia katika marago. 27 Na yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, na yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, ambao damu yao ililetwa ndani ifanye ukumbusho katika patakatifu, watachukuliwa nje ya marago; nao watachoma moto ngozi zao, na nyama yao, na mavi yao. 28 Na yeye awachomaye moto atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia maragoni. 29 Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajitaabisha roho zenu, msifanye kazi ya namna yo yote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu. 30 Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za Bwana. 31 Ni Sabato ya raha ya makini kwenu nanyi mtajitaabisha roho zenu; ni amri ya milele. 32 Na kuhani atakayetiwa mafuta na kuwekwa wakfu badala ya baba yake, ataufanya huo upatanisho, naye atayavaa mavazi ya kitani, yaani, yale mavazi matakatifu. 33 Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya hema ya kukutania, na kwa ajili ya madhabahu; naye atafanya upatanisho kwa ajili ya makuhani, na kwa ajili ya watu wote wa kusanyiko. 34 Na amri hii itakuwa amri ya milele kwenu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao zote, mara moja kila mwaka. Naye akafanya vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa.

Mambo ya Walawi 17

1 Bwana akamwambia Musa, akisema, 2 Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, ukawaambie; Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema, 3 Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng'ombe, au mwana-kondoo, au mbuzi, ndani ya marago, au atakayemchinja nje ya marago, 4 wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, ili amtoe kuwa matoleo kwa Bwana mbele ya hema ya Bwana; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; 5 ili kusudi wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, naam, wazilete kwa Bwana, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa Bwana. 6 Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za Bwana. 7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi. 8 Nawe utawaambia, Mtu awaye yote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu, 9 wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa Bwana basi mtu huyo atatengwa na watu wake. 10 Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. 11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. 12 Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu. 13 Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga. 14 Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali. 15 Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi. 16 Lakini kwamba hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapochukua uovu wake.

Mambo ya Walawi 18

1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 3 Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao. 4 Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 5 Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi Bwana. 6 Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana. 7 Utupu wa baba yako, wala utupu wa mama yako, usifunue, maana ndiye mama yako; usifunue utupu wake. 8 Utupu wa mke wa baba yako, usifunue; maana, ni utupu wa baba yako. 9 Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue. 10 Utupu wa binti ya mwanao mume, au wa binti ya binti yako, utupu wao hao usifunue; kwa kuwa ndio utupu wako mwenyewe. 11 Utupu wa binti ya mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, yeye ni umbu lako, usifunue utupu wake. 12 Usifunue utupu wa umbu lake baba yako; maana, yeye ni jamaa aliye karibu. 13 Usifunue utupu wa umbu la mama yako; maana, yeye ni jamaa ya mama yako ya karibu. 14 Usifunue utupu wa ndugu ya baba yako, usimkaribie mkewe huyo; yeye ni shangazi lako. 15 Usifunue utupu wa mkweo mwanamke; yeye ni mke wa mwanao; usifunue utupu wake huyo. 16 Usifunue utupu wa mke wa nduguyo; maana, ni utupu wa nduguyo. 17 Usifunue utupu wa mwanamke na binti yake; usimtwae binti ya mwanawe mume, au binti ya binti yake, ili kufunua utupu wake; hao ni jamaa ya karibu; ni uovu mkuu. 18 Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai. 19 Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake. 20 Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye. 21 Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi Bwana. 22 Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo. 23 Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko. 24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; 25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa. 26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu; 27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;) 28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu. 29 Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao. 30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Mambo ya Walawi 19

1 Bwana akanena na Musa, akamwambia, 2 Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. 3 Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 4 Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 5 Nanyi hapo mtakapomchinjia Bwana sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa. 6 Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. 7 Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; 8 lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha Bwana; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. 9 Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; 10 wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 11 Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. 12 Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. 13 Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. 14 Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. 15 Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. 16 Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi Bwana. 17 Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. 18 Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana. 19 Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja. 20 Tena mtu ye yote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mume, wala hakukombolewa kwa lo lote, wala hakupewa uhuru; wataadhibiwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru. 21 Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa Bwana, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia. 22 Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za Bwana, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya. 23 Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa. 24 Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani. 25 Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 26 Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. 27 Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu. 28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana. 29 Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu. 30 Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana. 31 Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 32 Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana. 33 Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu. 34 Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 35 Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo. 36 Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri. 37 Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi Bwana.

Mambo ya Walawi 20

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Tena uwaambie wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe. 3 Mimi nami nitamkazia uso wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na kulinajisi jina langu takatifu. 4 Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue; 5 ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao. 6 Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake. 7 Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 8 Nanyi zishikeni sheria zangu, na kuzitenda; Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi. 9 Kwa maana kila mtu amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama yake; damu yake itakuwa juu yake. 10 Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa. 11 Na mtu mume atakayelala pamoja na mke wa baba yake amefunua utupu wa baba yake; wote wawili hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao. 12 Na mtu mume akilala na mkwewe mwanamke wote wawili hakika watauawa; wamefanya yaliyo uchafuko; damu yao itakuwa juu yao. 13 Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao. 14 Tena mtu mume akimwoa mke pamoja na mama yake, ni uovu mkuu; watachomwa moto, yeye mume na hao wanawake pia; ili kwamba usiwe uovu kati yenu. 15 Tena mtu mume akilala na mnyama, hakika atauawa; nanyi mtamwua huyo mnyama. 16 Tena mwanamke akimkaribia mnyama ye yote, na kulala pamoja naye, mtamwua huyo mwanamke, na mnyama pia; hakika watauawa; damu yao itakuwa ni juu yao. 17 Tena mtu mume akimwoa umbu lake, binti ya baba yake, au binti ya mama yake, na kuuona utupu wake, na huyo mwanamke kauona utupu wake huyo mume; ni jambo la aibu; watakatiliwa mbali mbele ya macho ya wana wa watu wao; amefunua utupu wa umbu lake; naye atauchukua uovu wake. 18 Tena mtu mume akilala na mwanamke aliye na ugonjwa wake, na kufunua utupu wake; amelifunua jito la damu yake, naye mwanamke amefunua jito la damu yake; wote wawili watakatiliwa mbali na watu wao. 19 Usifunue utupu wa umbu la mama yako, wala umbu la baba yako; kwa kuwa huyo amefunua utupu wa jamaa yake ya karibu; watauchukua uovu wao. 20 Tena mtu mume akilala na mke wa mjomba wake, ameufunua utupu wa mjomba wake; watauchukua uovu wao; watakufa bila kuzaa mwana. 21 Tena mtu mume akimtwaa mke wa nduguye, ni uchafu; ameufunua utupu wa nduguye; hao watakuwa hawana wana. 22 Basi zishikeni amri zangu zote, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kukaa, isiwatapike. 23 Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia. 24 Lakini mimi nimewaambia ninyi, Mtairithi nchi yao, nami nitawapa ninyi kuimiliki; nchi iliyojaa maziwa na asali; mimi ni Bwana, Mungu wenu, niliyewatenga ninyi na mataifa. 25 Kwa ajili ya hayo mtapambanua kati ya mnyama aliye safi na mnyama aliye najisi, na kati ya ndege aliye tohara na ndege aliye najisi; nanyi msizifanye nafsi zenu kuwa machukizo kwa njia ya mnyama, au kwa njia ya ndege, au kwa njia ya kitu cho chote ambacho nchi imejaa nacho, niliowatenga nanyi kuwa ni najisi. 26 Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu. 27 Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.

Mambo ya Walawi 21

1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake; 2 isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume; 3 na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo. 4 Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi. 5 Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao. 6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za Bwana kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu. 7 Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake. 8 Kwa hiyo basi utamtakasa; kwa kuwa yeye husongeza chakula cha Mungu wako; atakuwa mtakatifu kwako wewe; kwa kuwa mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu. 9 Na binti ya kuhani ye yote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa moto. 10 Na yeye aliye kuhani mkuu katika nduguze, ambaye mafuta ya kutiwa yamemiminwa kichwani mwake, naye akawekwa wakfu ili ayavae hayo mavazi, yeye hataziacha wazi nywele za kichwa chake, wala hatazirarua nguo zake; 11 wala hataingia penye maiti, wala asijitie unajisi kwa ajili ya baba yake wala mama yake; 12 wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake u juu yake; mimi ndimi Bwana. 13 Naye atamwoa mwanamke katika ubikira wake. 14 Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe. 15 Naye asiwatie unajisi kizazi chake katika watu wake; kwa kuwa mimi ndimi Bwana nimtakasaye. 16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 17 Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. 18 Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili, 19 au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono, 20 au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu; 21 mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za Bwana kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. 22 Atakula chakula cha Mungu wake, katika hicho kilicho kitakatifu sana, na hicho kilicho kitakatifu. 23 Lakini hataingia ndani ya pazia, wala asikaribie madhabahu, kwa sababu ana kilema; ili kwamba asipanajisi patakatifu pangu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye. 24 Basi Musa akanena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote.

Mambo ya Walawi 22

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na Haruni na wanawe, ili wajitenge wenyewe na vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena kwamba wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi Bwana. 3 Waambie, Mtu ye yote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia Bwana, naye ana unajisi, mtu huyo atakatiliwa mbali asiwe mbele zangu; mimi ndimi Bwana. 4 Mtu ye yote wa kizazi cha Haruni aliye mwenye ukoma, au mwenye kisonono; yeye asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu awaye yote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka; 5 au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wo wote alio nao; 6 huyo mtu atakayegusa kitu cho chote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini. 7 Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake. 8 Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi Bwana. 9 Basi kwa hiyo watayashika mausia yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi Bwana niwatakasaye. 10 Mgeni awaye yote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu. 11 Lakini kwamba kuhani akinunua mtu ye yote, kwa kumnunua kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake. 12 Na binti ya kuhani kwamba ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu. 13 Lakini kwamba binti ya kuhani ni mjane, au kwamba ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuketi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni awaye yote asile katika chakula hicho. 14 Tena kama mtu ye yote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu. 15 Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa Bwana; 16 hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye. 17 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 18 Nena na Haruni na wanawe, na wana wa israeli wote, uwaambie, Mtu ye yote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mojawapo, au kama ni sadaka yo yote ya hiari, watakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa; 19 ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng'ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi. 20 Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu. 21 Na mtu awaye yote atakayemtolea Bwana dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng'ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote. 22 Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea Bwana wanyama hao, wala msiwasongeze kwa Bwana kwa njia ya moto juu ya madhabahu. 23 Ng'ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa. 24 Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee Bwana; wala msifanye hivi katika nchi yenu. 25 Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu. 26 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 27 Hapo ng'ombe, au kondoo, au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa Bwana kwa njia ya moto. 28 Tena kama ni ng'ombe, au kama ni kondoo, msimchinje huyo na mwanawe wote wawili kwa siku moja. 29 Tena mtakapomchinjia Bwana dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa. 30 Italiwa siku iyo hiyo; msisaze kitu chake hata asubuhi; mimi ndimi Bwana. 31 Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi Bwana. 32 Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi, 33 niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi Bwana.

Mambo ya Walawi 23

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za Bwana, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu. 3 Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote. 4 Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. 5 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana. 6 Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba. 7 Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi. 8 Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. 9 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu; 11 naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa. 12 Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. 13 Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini. 14 Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote. 15 Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba; 16 hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya. 17 Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa Bwana. 18 Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng'ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 19 Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani. 20 Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa Bwana, wawe wa huyo kuhani. 21 Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu. 22 Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 23 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 24 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu. 25 Msifanye kazi yo yote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto. 26 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 27 Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto. 28 Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za Bwana, Mungu wenu. 29 Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake. 30 Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake. 31 Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote. 32 Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu. 33 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 34 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa Bwana. 35 Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. 36 Mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi. 37 Sikukuu za Bwana ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee Bwana sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake; 38 zaidi ya hizo Sabato za Bwana, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa Bwana. 39 Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya Bwana muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa. 40 Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, muda wa siku saba. 41 Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa Bwana muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba. 42 Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda; 43 ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana Mungu wenu. 44 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za Bwana.

Mambo ya Walawi 24

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. 3 Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za Bwana daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu. 4 Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za Bwana daima. 5 Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja. 6 Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za Bwana. 7 Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto. 8 Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za Bwana daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele. 9 Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zisongezwazo kwa Bwana kwa moto, kwa amri ya milele. 10 Ikawa mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, ambaye babaye alikuwa Mmisri, akatokea kati ya wana wa Israeli; na huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, na Mwisraeli mmoja, wakapigana pamoja ndani ya marago; 11 kisha huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru hilo Jina, na kuapiza; nao wakamleta kwa Musa. Na jina la mamaye alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila ya Dani. 12 Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa Bwana. 13 Na Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 14 Mtoe huyo aliyeapiza nje ya marago; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe. 15 Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake. 16 Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa. 17 Na mtu ampigaye mtu hata akafa, lazima atauawa; 18 na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa; uhai kwa uhai. 19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo; 20 jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo. 21 Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa. 22 Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 23 Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya marago, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Mambo ya Walawi 25

1 Kisha Bwana akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya Bwana. 3 Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake; 4 lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa Bwana; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu. 5 Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi. 6 Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe; 7 na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao. 8 Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda. 9 Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote. 10 Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu, nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake. 11 Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa. 12 Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani. 13 Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake. 14 Tena kama ukimwuzia jirani yako cho chote, au kununua cho chote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe; 15 kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile, ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe. 16 Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo. 17 Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 18 Kwa sababu hii zitendeni amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzifanya; nanyi mtakaa katika hiyo nchi salama. 19 Nayo nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba, na kuketi humo salama. 20 Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu; 21 ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu. 22 Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani. 23 Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu. 24 Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu. 25 Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye. 26 Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa; 27 ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake. 28 Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake. 29 Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima. 30 Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile. 31 Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile. 32 Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote. 33 Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli. 34 Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima. 35 Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri. 36 Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe. 37 Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida. 38 Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu. 39 Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa; 40 kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile; 41 ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake. 42 Kwa kuwa hao ni watumishi wangu, niliowaleta watoke nchi ya Misri; wasiuzwe mfano wa watumwa. 43 Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako. 44 Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi. 45 Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu. 46 Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; lakini msitawale kwa nguvu juu ya ndugu zenu, hao wana wa Israeli, wenyewe kwa wenyewe. 47 Tena kama mgeni au mtu akaaye nawe akitajirika, na nduguyo amekuwa maskini karibu naye, akajiuza kwa huyo mgeni, au kwa huyo akaaye kwako, au kwa ukoo wa jamaa ya huyo mgeni; 48 baada ya kuuzwa aweza kukombolewa; mtu mmoja miongoni mwa ndugu zake ana ruhusa kumkomboa; 49 au mjomba wake, au mwana wa mjomba wake, ana ruhusa ya kumkomboa, au mtu awaye yote aliye karibu naye wa jamaa yake, ana ruhusa ya kumkomboa; au kwamba yeye mwenyewe amepata mali, ana ruhusa ya kujikomboa mwenyewe. 50 Naye atafanya hesabu na huyo aliyemnunua, tangu mwaka huo aliojiuza hata mwaka wa yubile; na ile bei ya kuuzwa kwake itakuwa kama hesabu ya hiyo miaka ilivyo; atakuwa pamoja naye kama majira ya mtumishi aliyeajiriwa yalivyo. 51 Kwamba ikali imesalia miaka mingi, kama hesabu yake ilivyo ndivyo atakavyolipa bei ya ukombozi wake, katika hiyo fedha ambayo alinunuliwa kwayo. 52 Tena kwamba imesalia miaka michache tu hata mwaka wa yubile, ndipo atafanya hesabu naye, kama hesabu ya miaka yake ilivyo, ndivyo atakavyolipa tena bei ya ukombozi wake. 53 Kama mtumishi aliyeajiriwa mwaka hata mwaka, ndivyo atakavyokuwa pamoja naye; asitawale juu yake kwa nguvu mbele ya macho yako. 54 Tena kwamba hakukombolewa kwa njia hizi mojawapo, ndipo atatoka katika mwaka wa yubile, yeye, na watoto wake pamoja naye. 55 Kwa kuwa wana wa Israeli ni watumishi; ni watumishi wangu niliowaleta watoke katika nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Mambo ya Walawi 26

1 Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 2 Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana. 3 Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya; 4 ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake. 5 Tena kupura nafaka kwenu kutaendelea hata wakati wa kuvuna zabibu, na kuvuna zabibu kutaendelea hata wakati wa kupanda mbegu; nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, na kuketi katika nchi yenu salama. 6 Nami nitawapa amani katika nchi, tena mtalala wala hapana atakayewatia hofu; nami nitawakomesha wanyama wabaya katika nchi yenu, wala hautapita upanga katika nchi yenu. 7 Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga. 8 Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga. 9 Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi. 10 Nanyi mtakula akiba ya zamani mliyoiweka siku nyingi, tena hayo ya zamani mtayatoa, ili myaweke yaliyo mapya. 11 Nami nitaiweka maskani yangu kati yenu; wala roho yangu haitawachukia. 12 Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu. 13 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa. 14 Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote; 15 nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu; 16 mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila. 17 Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye. 18 Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu. 19 Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba; 20 na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake. 21 Nanyi ikiwa mwaenenda kinyume changu, wala hamtaki kunisikiza; nitaleta mapigo mara saba zaidi juu yenu, kama dhambi zenu zilivyo. 22 Nami nitaleta wanyama wakali kati yenu, ambao watawanyang'anya watoto wenu, na kuwaharibu wanyama wenu wa kufugwa, na kuwapunguza muwe wachache hesabu yenu; na njia zenu zitakuwa ni ukiwa. 23 Tena kama hamtaki kurejezwa upya kwangu mimi kwa mambo haya, bali mwaendelea kunishikia kinyume; ndipo mimi nami nitaendelea kuwashikia ninyi kinyume; 24 nami nitawapiga, naam mimi, mara saba kwa ajili ya dhambi zenu. 25 Nami nitaleta upanga juu yenu, utakaopatiliza kisasi cha hilo agano; nanyi mtakutanishwa ndani ya miji yenu; nami nitaleta tauni kati yenu; nanyi mtatiwa mkononi mwa adui. 26 Hapo nitakapovunja tegemeo lenu la mkate, wanawake kumi wataoka mikate yenu katika tanuu moja, nao watawapa mikate yenu tena kwa kupima kwa mizani; nanyi mtakula, lakini hamtashiba. 27 Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume; 28 ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu. 29 Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila. 30 Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia. 31 Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo. 32 Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia. 33 Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo. 34 Hapo ndipo nchi itakapozifurahia Sabato zake, wakati itakapokuwa hali ya ukiwa, nanyi mtakapokuwa katika nchi ya adui zenu; ndipo nchi itakapopumzika, na kuzifurahia Sabato zake. 35 Wakati wote itakapokuwa na ukiwa, itapumzika; ni hayo mapumziko ambayo haikuwa nayo katika Sabato zenu, hapo mlipokaa katika nchi hiyo. 36 Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye. 37 Nao wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama mbele ya upanga, hapo ambapo hapana afukuzaye; wala hamtakuwa na nguvu za kusimama mbele ya adui zenu. 38 Nanyi mtaangamia kati ya mataifa, na nchi ya adui zenu itawameza. 39 Na watu wa kwenu watakaobaki watafifia kwa ajili ya uovu wao, katika hizo nchi za adui zenu; tena watafifia kwa ajili ya uovu wa baba zao, pamoja nao. 40 Nao wataukiri uovu wao, na uovu wa baba zao, katika maasi yao waliyoasi juu yangu, tena ya kuwa kwa sababu wameendelea kunishikia kinyume, 41 mimi nami nimeendelea kuwashikia kinyume wao, na kuwatia katika nchi ya adui zao; lakini hapo, kama mioyo yao isiyokuwa tohara ikinyenyekea, nao wakubali adhabu ya uovu wao; 42 ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo. 43 Nchi nayo itaachwa na wao, nayo itazifurahia Sabato zake, itakapokuwa ukiwa pasipokuwa na wao; nao wataikubali adhabu ya uovu wao; kwa sababu, naam, ni kwa sababu wamezikataa hukumu zangu, na roho zao zimezichukia amri zangu. 44 Lakini pamoja na hayo yote, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi, sitawatupa, wala sitawachukia, niwaangamize kabisa, na kulivunja agano langu pamoja nao; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao; 45 lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano la baba zao, niliowaleta watoke katika nchi ya Misri mbele ya macho ya mataifa, ili kwamba niwe Mungu wao; mimi ndimi Bwana. 46 Hizi ni amri na hukumu na sheria, Bwana alizozifanya kati ya yeye na hao wana wa Israeli katika huo mlima wa Sinai kwa mkono wa Musa.

Mambo ya Walawi 27

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtu atakapoondoa nadhiri, hizo nafsi za watu zitakuwa kwa Bwana, kama utakavyowahesabia wewe. 3 Na hesabu yako itakuwa kwa mtu mume, tokea aliye na umri wa miaka ishirini hata umri wa miaka sitini, hesabu yako itakuwa shekeli hamsini za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu. 4 Kama ni mwanamke, hesabu yako itakuwa shekeli thelathini. 5 Tena akiwa mwenye umri wa miaka mitano hata umri wa miaka ishirini, ndipo hesabu yako itakuwa shekeli ishirini kwa mwanamume, na shekeli kumi kwa mwanamke. 6 Tena akiwa mwenye umri wa mwezi mmoja hata umri wa miaka mitano, ndipo hesabu yako itakuwa shekeli tano za fedha kwa mwanamume, na hesabu yako itakuwa shekeli tatu za fedha kwa mwanamke. 7 Tena akiwa mwenye umri wa miaka sitini na kuzidi; kama ni mwanamume, hesabu yako itakuwa shekeli kumi na tano, na kwa mwanamke shekeli kumi. 8 Lakini kwamba ni maskini zaidi ya kuhesabu kwako, ndipo atawekwa mbele ya kuhani, na huyo kuhani atamtia kima; kama uwezo wake huyo aliyeweka nadhiri ulivyo, ndivyo kuhani atakavyomtia kima. 9 Tena kama ni mnyama wa namna ambayo watu husongeza kuwa sadaka kwa Bwana, kila mmoja katika wanyama hao atakayetolewa kwa Bwana, na mtu ye yote, atakuwa ni mtakatifu. 10 Yeye hatamgeuza, wala kumbadili mwema kwa mbaya, au mbaya kwa mwema; kwamba atabadili mnyama kwa mnyama ye yote, ndipo mnyama huyo na yule waliobadiliwa wote wawili watakuwa watakatifu. 11 Na kama ni mnyama ye yote asiye safi, wa namna ambayo hawamsongezi kwa Bwana, basi atamweka huyo mnyama mbele ya kuhani; 12 na kuhani atamtia kima, akiwa mwema akiwa mbaya; kama wewe kuhani utakavyomtia kima, ndivyo itakavyokuwa. 13 Lakini kwamba ataka kumkomboa kweli, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano juu ya hesabu yako. 14 Na mtu atakapoiweka nyumba yake iwe wakfu kwa Bwana ndipo kuhani ataihesabu kima chake hiyo nyumba, ikiwa njema ikiwa mbaya; kama kuhani atakavyoihesabu kima chake ndivyo itakavyokuwa. 15 Tena mtu huyo aliyeweka nyumba yake iwe wakfu kama akitaka kuikomboa, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano ya hiyo fedha ya hesabu yako, nayo itakuwa mali yake. 16 Tena kama mtu akiweka wakfu kwa Bwana sehemu ya shamba la milki yake, ndipo hesabu yako itakuwa kama kule kupanda kwake kulivyo; kupanda kwake homeri moja ya mbegu ya shayiri, kutahesabiwa kuwa ni shekeli hamsini za fedha. 17 Kwamba anaweka shamba lake liwe wakfu tangu mwaka wa yubile, litasimama vivyo kama hesabu yako ilivyo. 18 Lakini akiliweka shamba lake wakfu baada ya yubile, ndipo kuhani atamhesabia hiyo fedha kama hesabu ya miaka iliyobaki hata mwaka wa yubile, na kuhesabiwa kwako kutapunguzwa. 19 Na kama yeye aliyeliweka shamba wakfu akitaka kulikomboa kweli, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano ya hiyo fedha ya hesabu yako, nalo litathibitishwa kwake. 20 Lakini asipotaka kulikomboa shamba, au kama amemwuzia mtu mwingine hilo shamba, halitakombolewa tena kabisa; 21 ila hilo shamba litakuwa takatifu kwa Bwana litakapotoka katika yubile, kama ni shamba lililowekwa wakfu; litakuwa mali ya kuhani. 22 Tena kama akiweka wakfu kwa Bwana shamba ambalo amelinunua, ambalo si shamba la milki yake; 23 ndipo kuhani atamhesabia kima cha kuhesabu kwako hata mwaka wa yubile: naye atatoa siku hiyo kama hesabu yako, kuwa ni kitu kitakatifu kwa Bwana. 24 Mwaka wa yubile shamba hilo litarejea kwake huyo ambaye lilinunuliwa kwake, yaani, huyo ambaye nchi hiyo ni milki yake. 25 Na hesabu zako zote zitaandamana shekeli ya mahali patakatifu; gera ishirini zitakuwa shekeli moja. 26 Mzaliwa wa kwanza tu katika wanyama, aliyewekwa kuwa mzaliwa wa kwanza kwa Bwana, mtu awaye yote hatamweka kuwa mtakatifu; kama ni ng'ombe, kama ni kondoo, huyo ni wa Bwana. 27 Na kama ni wa mnyama asiye safi, ndipo atamkomboa kama hesabu yako ilivyo, naye ataongeza sehemu ya tano ya bei yake; au asipokombolewa, ndipo atauzwa kama hesabu yako ilivyo. 28 Pamoja na hayo, hakitauzwa wala kukombolewa kitu cho chote kilichowekwa wakfu, ambacho mtu amekiweka wakfu kwa Bwana, katika vitu vyote alivyo navyo, kama ni mtu, au mnyama, au kama ni shamba la milki yake; kila kitu kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Bwana. 29 Kila aliyewekwa wakfu, aliyewekwa wakfu na binadamu, hatakombolewa; sharti atauawa. 30 Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana. 31 Na kama mtu akitaka kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake. 32 Tena zaka yote ya ng'ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa Bwana. 33 Hataangalia kwamba ni mwema au kwamba ni mbaya, wala hatambadili; na kama akimbadili na yo yote, ndipo wote wawili, huyo na huyo waliobadiliwa watakuwa ni watakatifu; hatakombolewa. 34 Haya ndiyo maagizo, Bwana aliyomwagiza Musa kwa ajili ya wana wa Israeli katika mlima wa Sinai.

Hesabu 1

1 Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, hemani mwa kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri, akamwambia, 2 Fanyeni hesabu ya mkutano wote wa wana wa Israeli, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina ilivyo, kila mtu mume kichwa kwa kichwa; 3 tangu mwenye miaka ishirini umri wake, na zaidi, wote wawezao kutoka kwenenda vitani katika Israeli; wewe na Haruni mtawahesabu kwa kuandama majeshi yao. 4 Tena mtu mume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi; kila mmoja aliye kichwa cha nyumba ya baba zake. 5 Na majina ya hao waume watakaosimama pamoja nanyi ni haya; Wa Reubeni; Elisuri mwana wa Shedeuri. 6 Wa Simeoni; Shelumieli mwana wa Suri-shadai. 7 Wa Yuda; Nashoni mwana wa Aminadabu. 8 Wa Isakari; Nethaneli mwana wa Suari. 9 Wa Zabuloni; Eliabu mwana wa Heloni. 10 Katika wana wa Yusufu; wa Efraimu, Elishama mwana wa Amihudi; na wa Manase; Gamalieli mwana wa Pedasuri. 11 Wa Benyamini Abidani mwana wa Gideoni. 12 Wa Dani; Ahiezeri mwana wa Amishadai. 13 Wa Asheri; Pagieli mwana wa Okirani. 14 Wa Gadi; Eliasafu mwana wa Deueli. 15 Wa Naftali; Ahira mwana wa Enani. 16 Hao ndio walioitwa wa mkutano, wakuu wa kabila za baba zao; nao ndio vichwa vya wale maelfu ya Israeli. 17 Basi Musa na Haruni wakawatwaa hao watu waume waliotajwa majina yao; 18 nao waliukutanisha mkutano mzima, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, nao wakaonyesha ukoo wa vizazi vyao kwa kuandama jamaa zao, kwa nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, kichwa kwa kichwa. 19 Kama Bwana alivyomwagiza Musa, ndivyo alivyowahesabu huko katika bara ya Sinai. 20 Na wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mtu mume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi wote walioweza kwenda vitani; 21 wale waliohesabiwa katika kabila ya Reubeni, walikuwa watu arobaini na sita elfu na mia tano (46,500). 22 Katika wana wa Simeoni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, wale waliohesabiwa kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 23 wale waliohesabiwa katika kabila ya Simeoni, walikuwa watu hamsini na kenda elfu na mia tatu (59,300). 24 Katika wana wa Gadi, kwa kuandama vizazi vyao, jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 25 wale waliohesabiwa katika kabila ya Gadi, walikuwa watu arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini (45,650). 26 Katika wana wa Yuda, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 27 wale waliohesabiwa katika kabila ya Yuda, walikuwa watu sabini na nne elfu na mia sita (74,600). 28 Katika wana wa Isakari, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kwa hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 29 wale waliohesabiwa katika kabila ya Isakari, walikuwa watu hamsini na nne elfu na mia nne (54,400). 30 Katika wana wa Zabuloni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 31 wale waliohesabiwa katika kabila ya Zabuloni, walikuwa watu hamsini na saba elfu na mia nne (57,400). 32 Katika wana wa Yusufu, maana katika wana wa Efraimu, vizazi vyao kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani, 33 wale waliohesabiwa katika kabila ya Efraimu, walikuwa watu arobaini elfu na mia tano (40,500). 34 Katika wana wa Manase, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 35 wale waliohesabiwa katika kabila ya Manase, walikuwa watu thelathini na mbili elfu na mia mbili (32,200). 36 Katika wana wa Benyamini, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 37 wale waliohesabiwa katika kabila ya Benyamini, walikuwa watu thelathini na tano elfu na mia nne (35,400). 38 Katika wana wa Dani, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 39 wale waliohesabiwa katika kabila ya Dani, walikuwa watu sitini na mbili elfu na mia saba (62,700). 40 Katika wana wa Asheri, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 41 wale waliohesabiwa katika kabila ya Asheri, walikuwa watu arobaini na moja elfu na mia tano (41,500). 42 Katika wana wa Naftali, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 43 wale waliohesabiwa katika kabila ya Naftali, walikuwa watu hamsini na tatu elfu na mia nne (53,400). 44 Hao ndio waliohesabiwa, ambao Musa na Haruni na wale wakuu wa Israeli watu kumi na wawili waliwahesabu; walikuwa kila mmoja kwa ajili ya nyumba ya baba zake. 45 Basi hao wote waliohesabiwa katika wana wa israeli kwa kuandama nyumba za baba zao tangu umri wa miaka ishirini na zaidi; wote walioweza kwenda vitani katika Israeli; 46 hao wote waliohesabiwa walikuwa ni watu waume mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini (603,550). 47 Lakini Walawi kwa kuiandama kabila ya baba zao hawakuhesabiwa katika watu hao. 48 Kwa kuwa Bwana alinena na Musa, na kumwambia, 49 Hiyo kabila ya Lawi tu usiihesabu, wala usiitie hesabu yao katika wana wa Israeli; 50 lakini uwaweke Walawi wawe juu ya maskani ya ushahidi, na juu ya vyombo vyake vyote, na juu ya vitu vyake vyote; wao wataichukua hiyo maskani, na vyombo vyake vyote; nao wataitumikia, na kupanga hema zao kwa kuizunguka maskani pande zote. 51 Tena hapo maskani itakapokwenda mbele, Walawi wataishusha; tena hapo maskani itakaposimamishwa, Walawi wataisimamisha; na mgeni atakayekaribia atauawa. 52 Na wana wa Israeli watazipanga hema zao, kila mtu katika marago yake mwenyewe, kila mtu hapo ilipo beramu yake mwenyewe, kama majeshi yao yalivyo. 53 Lakini Walawi watapanga hema zao kuizunguka maskani ya ushahidi pande zote, ili zisiwe hasira juu ya mkutano wa wana wa Israeli; kisha Walawi wataulinda ulinzi wa hiyo maskani ya ushahidi. 54 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.

Hesabu 2

1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye beramu yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote. 3 Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa beramu ya marago ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. 4 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sabini na nne elfu na mia sita. 5 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari; 6 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na nne elfu na mia nne; 7 na kabila ya Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni; 8 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na saba elfu na mia nne. 9 Hao wote waliohesabiwa katika marago ya Yuda walikuwa mia na themanini na sita elfu na mia nne, kwa majeshi yao. Hao ndio watakaosafiri mbele. 10 Upande wa kusini kutakuwa na beramu ya marago ya Reubeni kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Reubeni atakuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. 11 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na sita elfu na mia tano. 12 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Simeoni; na mkuu wa wana wa Simeoni atakuwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai; 13 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na kenda elfu na mia tatu; 14 na kabila ya Gadi; na mkuu wa wana wa Gadi atakuwa Eliasafu mwana wa Deueli; 15 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini. 16 Wote waliohesabiwa katika marago ya Reubeni walikuwa mia na hamsini na moja elfu na mia nne na hamsini, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri mahali pa pili. 17 Ndipo hema ya kukutania itasafiri, pamoja na marago ya Walawi katikati ya marago yote; kama wapangavyo marago, watasafiri vivyo, kila mtu mahali pake, penye beramu zao. 18 Upande wa magharibi kutakuwa na beramu ya marago ya Efraimu kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Efraimu atakuwa Elishama mwana wa Amihudi. 19 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini elfu na mia tano. 20 Na karibu naye itakuwa kabila ya Manase; na mkuu wa wana wa Manase atakuwa Gamalieli mwana wa Pedasuri; 21 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na mbili elfu na mia mbili; 22 tena kabila ya Benyamini; na mkuu wa wana wa Benyamini atakuwa Abidani mwana wa Gideoni; 23 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na tano elfu na mia nne. 24 Wote waliohesabiwa katika marago ya Efraimu walikuwa mia na nane elfu na mia moja, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri katika mahali pa tatu. 25 Upande wa kaskazini kutakuwa na beramu ya marago ya Dani kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Dani atakuwa Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sitini na mbili elfu na mia saba. 27 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Asheri; na mkuu wa wana wa Asheri atakuwa Pagieli mwana wa Okrani; 28 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na moja elfu na mia tano; 29 kisha kabila ya Naftali; na mkuu wa wana wa Naftali atakuwa Ahira mwana wa Enani; 30 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na tatu elfu na mia nne. 31 Wote waliohesabiwa katika marago ya Dani walikuwa mia na hamsini na saba elfu na mia sita. Hao ndio watakaosafiri mwisho kwa kuandama beramu zao. 32 Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa nyumba za baba zao; wote waliohesabiwa katika marago kwa majeshi yao, walikuwa mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini. 33 Lakini Walawi hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 34 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyopanga penye beramu zao, na ndivyo walivyosafiri, kila mtu kwa jamaa zao, kwa nyumba za baba zao.

Hesabu 3

1 Basi vizazi vya Haruni na Musa, siku hiyo Bwana aliyosema na Musa katika mlima wa Sinai, ni hivi. 2 Tena majina ya hao wana wa Haruni ni haya; Nadabu mzaliwa wa kwanza, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. 3 Hayo ndiyo majina ya wana wa Haruni, hao makuhani waliotiwa mafuta, ambao aliwaweka wakfu ili wafanye kazi ya ukuhani. 4 Kisha Nadabu na Abihu walikufa mbele za Bwana, waliposongeza moto wa kigeni mbele za Bwana, katika bara ya Sinai, nao walikuwa hawana wana; na Eleazari na Ithamari wakafanya kazi ya ukuhani mbele ya uso wa Haruni baba yao. 5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 6 Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia. 7 Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani. 8 Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani. 9 Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli. 10 Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa. 11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 12 Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu; 13 kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi Bwana. 14 Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia, 15 Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu. 16 Basi Musa akawahesabu kama neno la Bwana kama alivyoagizwa. 17 Na wana wa Lawi walikuwa ni hawa kwa majina yao; Gershoni, na Kohathi, na Merari. 18 Na majina ya wana wa Gershoni kwa jamaa zao ni Libni na Shimei. 19 Na wana wa Kohathi kwa jamaa zao ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli. 20 Na wana wa Merari kwa jamaa zao ni Mahli, na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kwa nyumba za baba zao. 21 Katika Gershoni walikuwa jamaa ya Walibni, na jamaa ya Washimei, hawa ndio jamaa za Wagershoni. 22 Hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, hao waliohesabiwa kwao walikuwa saba elfu na mia tano. 23 Jamaa za Wagershoni watapanga rago nyuma ya maskani, upande wa magharibi. 24 Na mkuu wa nyumba ya baba zao Wagershoni atakuwa Eliasafu mwana wa Laeli. 25 Na ulinzi wa Wagershoni katika hema ya kukutania ni hiyo maskani, na Hema, na kifuniko chake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania, 26 na kuta za nguo za ua, na sitara ya mlango wa ua, iliyo karibu na maskani, na karibu na madhabahu pande zote, na kamba zake zitumiwazo kwa matumizi yake yote. 27 Na katika Kohathi ni jamaa ya Waamrami, na jamaa ya Waishari, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya hao Wauzieli; hizo ni jamaa za Wakohathi. 28 Kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita, wenye kuulinda ulinzi wa mahali patakatifu. 29 Jamaa za wana wa Kohathi watapanga rago upande wa kusini wa maskani. 30 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Wakohathi atakuwa Elisafani mwana wa Uzieli. 31 Na vitu watakavyovitunza ni hilo sanduku, na meza, na kinara cha taa, na madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu wavitumiavyo katika kutumika kwao, na pazia, na utumishi wake wote. 32 Na Eleazari mwana wa Haruni kuhani atakuwa mkuu wa hao wakuu wa Walawi, naye atawasimamia hao walindao ulinzi wa mahali patakatifu. 33 Katika Merari ni jamaa ya hao Wamahli, na jamaa ya Wamushi; hizo ni jamaa za Merari. 34 Na hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa sita elfu na mia mbili. 35 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hao watapanga rago upande wa maskani, wa kaskazini. 36 Na usimamizi walioamriwa wana wa Merari ulikuwa ni kutunza mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake, na vyombo vyake vyote, na utumishi wake wote; 37 na nguzo za ua zilizouzunguka, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake. 38 Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa. 39 Hao wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana, kwa jamaa zao, waume wote tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa ishirini na mbili elfu. 40 Kisha Bwana akamwambia Musa, Uwahesabu waume wote wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi uyahesabu majina yao. 41 Nawe utawatwaa Walawi kwa ajili yangu mimi (Mimi ndimi Bwana) badala ya hao wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli; na wanyama wa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli. 42 Musa akahesabu, kama Bwana alivyomwagiza, wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli. 43 Wazaliwa wa kwanza wote walio waume kwa hesabu ya majina, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, katika hao waliohesabiwa kwao, walikuwa ishirini na mbili elfu na mia mbili na sabini na watatu. 44 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 45 Uwatwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli, na wanyama wa Walawi badala ya wanyama wao; na hao Walawi watakuwa wangu mimi; mimi ndimi Bwana. 46 Tena kwa kuwakomboa hao watu mia mbili na sabini na watatu, wa hao wazaliwa wa kwanza wa Israeli, ambao wamezidi ile hesabu ya Walawi, 47 utatwaa shekeli tano kwa kichwa cha kila mtu kwa hiyo shekeli ya mahali patakatifu (shekeli ni gera ishirini); 48 na hizo fedha ambazo waliosalia wamekombolewa kwazo utampa Haruni na wanawe. 49 Basi Musa akawatoza fedha za ukombozi, hao waliozidi hesabu ya wale waliokombolewa na Walawi; 50 akatwaa hizo fedha kwa wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli; shekeli elfu moja na mia tatu na sitini na tano kwa shekeli ya mahali patakatifu; 51 kisha hizo fedha za ukombozi Musa akampa Haruni na wanawe, kama neno la Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 4

1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Katika wana wa Lawi uitenge hesabu ya wana wa Kohathi, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao, 3 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi hata umri wa miaka hamsini, wote waingiao katika utumishi huo, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania. 4 Huu ndio utumishi wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania, katika vile vyombo vitakatifu sana; 5 hapo watakapong'oa safari, Haruni ataingia ndani, na wanawe, nao watalishusha pazia la sitara, na kulifunika sanduku la ushahidi kwa hilo pazia; 6 kisha atatia juu yake ngozi za pomboo za kulifunikia, na kutandika juu yake nguo ya rangi ya samawi tupu, kisha watatia hiyo miti yake. 7 Tena juu ya meza ya mikate ya wonyesho watatandika nguo ya rangi ya samawi, na kuweka juu yake sahani, na miiko, na mabakuli, na vikombe vya kumiminia; na hiyo mikate ya daima itakuwa juu yake; 8 nao watatandika juu yake nguo ya rangi nyekundu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo za kuifunikia, na kuitia ile miti yake. 9 Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake; 10 nao watakitia, na vyombo vyake vyote, ndani ya ngozi ya pomboo, na kukitia juu ya miti ya kukichukulia 11 Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake; 12 kisha watavitwaa vile vyombo vyote vya utumishi wavitumiavyo katika mahali patakatifu, na kuvitia katika nguo ya rangi ya samawi, na kuvifunika kwa ngozi za pomboo, na kuvitia juu ya miti ya kuvichukulia. 13 Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake; 14 nao wataweka vyombo vyake vyote juu yake ambavyo wavitumia katika madhabahu, vyetezo, na nyuma, na miiko, na mabakuli, vyombo vyote vya hiyo madhabahu; nao watatandika juu yake ngozi za pomboo, na kutia miti yake mahali pake. 15 Na Haruni na wanawe watakapokwisha kupafunika mahali patakatifu, na vyombo vyote vya mahali patakatifu, hapo watakapong'oa kambi; baadaye, wana wa Kohathi watakuja kuvichukua; lakini wasiviguse vile vitu vitakatifu, wasife. Vyombo vile ni mzigo wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania. 16 Na ulinzi wake Eleazari mwana wa Haruni kuhani utakuwa ni kuyaangalia mafuta kwa nuru, na uvumba mzuri, na sadaka ya unga ya daima, na mafuta ya kupaka, tena ulinzi wa hiyo maskani yote, na wa vitu vyote vilivyo ndani yake, mahali patakatifu, na vyombo vyake. 17 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 18 Msiitenge kabisa kabila ya jamaa za Wakohathi katika hao Walawi; 19 lakini wafanyieni neno hili, ili kwamba wawe hai, wasife, hapo watakapovikaribia vile vitu vilivyo vitakatifu sana; Haruni na wanawe wataingia ndani, na kuwawekea kila mtu utumishi wake, na kila mtu mzigo wake; 20 lakini wasiingie wao kupaona mahali pale patakatifu, hata kwa dakika moja, ili wasife. 21 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 22 Fanya jumla ya wana wa Gershoni nao, kwa nyumba za baba zao, na jamaa zao; 23 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini utawahesabu; wote watakaoingia kutumika, ili kufanya kazi katika hema ya kukutania. 24 Huu ni utumishi wa jamaa za Wagershoni, katika kutumika na katika kuchukua mizigo; 25 wao watayachukua mapazia ya maskani, na hema ya kukutania, hizo nguo za kufunikia, na zile ngozi za pomboo za kufunikia zilizo juu yake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania; 26 na kuta za nguo za ua, na sitara ya ile nafasi ya kuingilia ya lango la ua, ulio karibu na maskani na madhabahu, kuzunguka pande zote, na kamba zake, na vyombo vyote vya utumishi wao, na yote yatakayotendeka kwavyo, watatumika katika hayo. 27 Utumishi wote wa wana wa Wagershoni, katika mzigo wao wote, na utumishi wao wote, utakuwa kwa amri ya Haruni na wanawe; nanyi mtawaagizia mzigo wao wote kuulinda. 28 Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Wagershoni katika hema kukutania; na ulinzi utakuwa chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani. 29 Katika habari ya wana wa Merari, utawahesabu kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao; 30 tangu aliyepata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, utawahesabu, kila atakayeingia katika huo utumishi, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania. 31 Na mausia ya mzigo wao ni haya, kwa utumishi wao wote katika hema ya kukutania; mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake; 32 na viguzo vya ua vya kuuzunguka pande zote, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake, na vyombo vyake vyote, pamoja na utumishi wake wote; nanyi mtawaagizia kila mtu kwa jina lake vile vyombo vya mzigo wao watakaoulinda. 33 Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Merari, kwa utumishi wao wote, katika hema ya kukutania, chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani. 34 Basi Musa na Haruni na hao wakuu wa mkutano wakawahesabu wana wa Kohathi kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao, 35 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi kwa kazi katika hema ya kukutania, 36 na waliohesabiwa kwao kwa jamaa zao, walikuwa elfu mbili na mia saba hamsini. 37 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za Wakohathi, wote waliotumika katika hema ya kukutania, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa. 38 Na hao waliohesabiwa katika wana wa Gershoni, kwa jamaa zao na nyumba zao baba zao, 39 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi, kwa kazi katika hema ya kukutania, 40 hata wale waliohesabiwa kwao, kwa jamaa zao na nyumba za baba zao, walikuwa elfu mbili na mia sita na thelathini. 41 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Gershoni, wote waliotumika katika hema ya kukutania, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana. 42 Na hao waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Merari, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao, 43 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi kwa kazi katika hema ya kukutania, 44 wale waliohesabiwa kwao, kwa jamaa zao, walikuwa elfu tatu na mia mbili. 45 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Merari, ambao Musa na; Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana, kwa mkono wa Musa. 46 Wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni na hao wakuu wa Israeli waliwahesabu, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao, 47 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila aliyeingia kufanya kazi ya utumishi, na kazi ya kuchukua mizigo katika hema ya kukutania, 48 hao waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu nane na mia tano themanini. 49 Kwa amri ya Bwana, walihesabiwa kwa mkono wa Musa, kila mtu kwa utumishi wake, na kama mzigo wake ulivyokuwa; ndivyo walivyohesabiwa na yeye, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 5

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waamrishe wana wa Israeli kwamba wamtoe kila mwenye ukoma maragoni, na kila mtu aliye na kisonono, na kila aliye najisi kwa ajili ya wafu; 3 mtawatoa nje wote, waume kwa wake, mtawaweka nje ya marago; ili wasiyatie unajisi marago yao, ambayo mimi naketi katikati yake. 4 Wana wa Israeli wakafanya vivyo, wakawatoa na kuwaweka nje ya marago; kama Bwana alivyonena na Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. 5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 6 Uwaambie wana wa Israeli, Mtu mume au mke atakapofanya dhambi yo yote, ifanywayo na binadamu, kumwasi Bwana, na mtu huyo akawa na hatia; 7 ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya; naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano, na kumpa huyo aliyemkosa. 8 Lakini kwamba mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye inampasa kurudishiwa kwa ajili ya hiyo hatia, kile kitakachorudishwa kwa Bwana kwa hiyo hatia kitakuwa cha kuhani, pamoja na kondoo mume wa upatanisho, ambaye kwa huyo utafanywa upatanisho kwa ajili yake. 9 Tena kila sadaka ya kuinuliwa, ya vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, watakavyosongeza kwa kuhani, itakuwa ni yake. 10 Tena vitu vilivyowekwa wakfu na mtu awaye yote, vitakuwa ni vya kuhani; kitu cho chote mtu atakachompa kuhani, kitakuwa chake. 11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 12 Nena na wana wa israeli, uwaambie, kama mke wa mtu ye yote akikengeuka, na kumkosa mumewe, 13 na mtu mume akalala naye kwa uasherati, na jambo hilo likamfichamania mumewe, likawa jambo lisilojulikana, na huyo mwanamke akawa najisi, wala hapana shahidi aliyeshuhudia juu yake, wala hakufumaniwa; 14 kisha mumewe akashikwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye akawa najisi huyo mwanamke; au kama akiingiwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye hakuwa na unajisi huyo mke; 15 ndipo huyo mume atamchukua mkewe, aende naye kwa kuhani, naye ataleta sadaka yake kwa ajili yake, yaani, sehemu ya kumi ya efa ya unga wa shayiri; asitie mafuta juu yake, wala asitie ubani juu yake; maana, ni sadaka ya unga ya wivu, ni sadaka ya unga ya ukumbusho ya kukumbukia uovu. 16 Basi kuhani atamleta mwanamke akaribie, na kumweka mbele za Bwana; 17 kisha kuhani atatwaa maji matakatifu katika chombo cha udongo; kisha kuhani atatwaa katika vumbi lililo pale chini ya maskani, na kulitia katika hayo maji; 18 kisha kuhani atamweka mwanamke mbele za Bwana, naye atazifungua nywele za kichwani mwa huyo mwanamke, kisha atampa hiyo sadaka ya unga ya ukumbusho mikononi mwake, ambayo ni sadaka ya unga ya wivu, naye kuhani atakuwa na hayo maji ya uchungu yaletayo laana mkononi mwake; 19 tena kuhani atamwapisha huyo mwanamke, naye atamwambia mwanamke, Kwamba hakulala mtu mume pamoja nawe, tena kwamba hukukengeuka kuandama uchafu, uli chini ya mumeo, maji haya ya uchungu yaletayo laana yasikudhuru; 20 lakini kwamba umekengeuka uli chini ya mumeo, na kwamba u hali ya unajisi, na mtu mume amelala nawe, asiyekuwa mumeo; 21 hapo ndipo kuhani atamwapisha mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, kisha kuhani atamwambia huyo mwanamke maneno haya, Bwana na akufanye wewe uwe laana na kiapo kati ya watu wako, hapo Bwana akufanyapo paja lako kupooza, na tumbo lako kuvimba; 22 na maji yaletayo laana yatakuingia matumboni mwako, na kukuvimbisha tumbo, na kukupoozesha paja lako; na mwanamke ataitika, Amina, Amina. 23 Kisha kuhani ataziandika laana hizo ndani ya kitabu, na kuzifuta katika maji ya uchungu; 24 kisha atamnywesha mwanamke hayo maji ya uchungu yaletayo laana; nayo maji yaletayo laana yataingia ndani yake, nayo yatageuka kuwa uchungu. 25 Kisha kuhani ataitwaa hiyo sadaka ya unga ya wivu, kwa kuiondoa mkononi mwa huyo mwanamke, naye ataitikisa sadaka ya unga mbele ya Bwana, na kuisongeza pale madhabahuni; 26 kisha kuhani atatwaa konzi moja ya sadaka ya unga, kuwa ni ukumbusho wake, na kuuteketeza madhabahuni, baadaye atamnywesha mwanamke hayo maji. 27 Kisha hapo atakapokwisha kumnywesha maji, ndipo itakapokuwa, kama amekuwa hali ya unajisi na kumkosa mumewe, hayo maji yaletayo laana yatamwingia ndani yake, nayo yatakuwa uchungu, na tumbo lake litavimba, na paja lake litapooza; na huyo mwanamke atakuwa laana kati ya watu wake. 28 Na kama mwanamke hakuwa na unajisi lakini yu safi; ndipo ataachiliwa, naye atazaa wana. 29 Hii ndiyo sheria ya wivu, mwanamke, ambaye yu chini ya mumewe, akikengeuka, na kupata unajisi; 30 au, roho ya wivu ikimwingia mtu mume, naye akamwonea wivu mkewe; ndipo atakapomweka huyo mwanamke mbele za Bwana, na kuhani atatenda juu yake sheria hii yote. 31 Na huyo mume atakuwa hana uovu, na mwanamke atauchukua uovu wake.

Hesabu 6

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana; 3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka. 4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda. 5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu. 6 Siku hizo zote ambazo alijiweka awe wa Bwana asikaribie maiti. 7 Hatajitia unajisi kwa ajili ya baba yake, wala kwa ajili ya mamaye, wala kwa nduguye mume, wala kwa umbu lake, wakifa wao; kwa sababu ya huku kujiweka kwa Mungu ni juu ya kichwa chake. 8 Siku zote za kujitenga kwake, yeye ni mtakatifu kwa Bwana 9 Na kama mtu ye yote akifa ghafla karibu naye, akajitia unajisi kichwa cha kutengwa kwake, ndipo atakinyoa kichwa siku hiyo ya kutakaswa kwake, atakinyoa siku ya saba. 10 Tena siku ya nane ataleta hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, aende nao kwa kuhani, hata mlangoni pa hema ya kukutania; 11 naye kuhani atasongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa sababu aliingia kosani kwa ajili ya mfu, naye atatakasa kichwa chake siku iyo hiyo. 12 Kisha ataziweka kwa Bwana hizo siku za kujitenga kwake, naye ataleta mwana-kondoo mume wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya hatia; lakini hizo siku za kwanza hazitahesabiwa, kwa kuwa kule kujitenga kwake kulitiwa unajisi. 13 Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania; 14 naye atasongeza sadaka yake kwa Bwana, mwana-kondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwana-kondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani, 15 na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa, iliyotiwa mafuta, pamoja na sadaka zake za unga, na sadaka zake za kinywaji. 16 Na kuhani atavisongeza mbele za Bwana, naye atasongeza sadaka yake ya dhambi, na sadaka yake ya kuteketezwa; 17 naye atamsongeza huyo kondoo mume kuwa dhabihu ya sadaka za amani kwa Bwana, pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu; kisha kuhani atasongeza sadaka ya unga nayo, na sadaka yake ya kinywaji. 18 Naye Mnadhiri atakinyoa kichwa cha kujitenga kwake, mlangoni pa hema ya kukutania, kisha atatwaa hizo nywele za kichwa cha kujitenga kwake, na kuzitia katika moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka za amani. 19 Kisha kuhani atautwaa mkono wa huyo kondoo mume uliotokoswa, na mkate mmoja usio chachu atautwaa kikapuni, na mkate mmoja wa kaki, naye ataitia mikononi mwa yule Mnadhiri, baada ya kunyoa kichwa cha kujitenga kwake; 20 naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kitu hicho ni kitakatifu kwa kuhani, pamoja na kidari cha kutikiswa, na paja la kuinuliwa; kisha baadaye Mnadhiri ana ruhusa kunywa divai. 21 Sheria ya Mnadhiri awekaye nadhiri ni hiyo, tena ni sheria ya sadaka yake atakayomtolea Bwana kwa ajili ya kujitenga kwake, pamoja na vitu vile ambavyo aweza kuvipata zaidi; kama nadhiri yake awekayo ilivyo, ndivyo impasavyo kufanya kwa kuiandama sheria ya kujitenga kwake. 22 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 23 Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; 24 Bwana akubarikie, na kukulinda; 25 Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; 26 Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani. 27 Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.

Hesabu 7

1 Ilikuwa siku hiyo Musa alipokwisha kuisimamisha maskani, na kuitia mafuta, na kuitakasa, na vyombo vyake vyote, na hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote, na kuvitia mafuta, na kuvitakasa; 2 ndipo wakuu wa Israeli, vichwa vya nyumba za baba zao, wakatoa matoleo; hao ndio wakuu wa kabila, hao ndio waliokuwa juu yao waliohesabiwa; 3 nao wakamletea Bwana matoleo yao, magari sita yenye mafuniko juu, na ng'ombe kumi na wawili; gari moja kwa wakuu wawili wawili, na ng'ombe mmoja kwa kila mkuu; nao wakayasongeza hapo mbele ya maskani. 4 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 5 Pokea mikononi mwao, ili kwamba viwe vya kutumiwa katika utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawapa Walawi vitu hivyo, kila mtu utampa kama utumishi wake ulivyo. 6 Basi Musa akapokea hayo magari, na ng'ombe, akawapa Walawi. 7 Wana wa Gershoni akawapa magari mawili na ng'ombe wanne, kama utumishi wao ulivyokuwa; 8 na wana wa Merari akawapa magari manne na ng'ombe wanane kama utumishi wao ulivyokuwa, chini ya mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni kuhani. 9 Lakini hakuwapa wana wa Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao wakavichukua mabegani mwao. 10 Kisha wale wakuu wakatoa matoleo kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, katika siku hiyo iliyotiwa mafuta, wakuu wakayatoa matoleo yao mbele ya madhabahu. 11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Watasongeza matoleo yao, kila mkuu kwa siku yake, kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu. 12 Basi aliyetoa matoleo yake siku ya kwanza ni Nashoni mwana wa Aminadabu, wa kabila ya Yuda; 13 na matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha uzani wake ni shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga; 14 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kimejaa uvumba; 15 ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mmoja mume, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 16 mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 17 na kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe waume wawili, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Nashoni mwana wa Aminadabu. 18 Siku ya pili Nethaneli mwana wa Suari, mkuu wa Isakari, alitoa; 19 yeye akasongeza matoleo yake, sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa ni sadaka ya unga; 20 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilikuwa kimejaa uvumba; 21 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 22 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 23 na kwa dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Nethaneli mwana wa Suari. 24 Siku ya tatu Eliabu mwana wa Heloni, mkuu wa wana wa Zabuloni; 25 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 26 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 27 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 28 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 29 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Eliabu mwana wa Heloni. 30 Siku ya nne Elisuri mwana wa Shedeuri, mkuu wa wana wa Reubeni; 31 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 32 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 33 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 34 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 35 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Elisuri mwana wa Shedeuri. 36 Siku ya tano Shelumieli mwana wa Suri-shadai, mkuu wa wana Simeoni; 37 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 38 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 39 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 40 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 41 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Shelumieli mwana wa Suri-shadai 42 Siku ya sita Eliasafu mwana wa Deueli, mkuu wa wana wa Gadi 43 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 44 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 45 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 46 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 47 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Eliasafu mwana wa Deueli. 48 Siku ya saba Elishama mwana wa Amihudi, mkuu wa wana wa Efraimu; 49 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 50 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 51 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 52 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 53 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Elishama mwana wa Amihudi. 54 Siku ya nane Gamalieli mwana wa Pedasuri, mkuu wa wana wa Manase; 55 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 56 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 57 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 58 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 59 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Gamalieli mwana wa Pedasuri. 60 Siku ya kenda Abidani mwana wa Gideoni, mkuu wa wana wa Benyamini; 61 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 62 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 63 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 64 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 65 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Abidani mwana wa Gideoni. 66 Siku ya kumi Ahiezeri mwana wa Amishadai, mkuu wa wana wa Dani; 67 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 68 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 69 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 70 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 71 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Ahiezeri mwana wa Amishadai. 72 Na siku ya kumi na moja Pagieli mwana wa Okrani, mkuu wa wana wa Asheri; 73 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 74 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 75 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 76 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 77 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Pagieli mwana wa Okrani. 78 Na siku ya kumi na mbili Ahira mwana wa Enani, mkuu wa wana wa Naftali; 79 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga; 80 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba; 81 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa; 82 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; 83 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Ahira mwana wa Enani. 84 Hayo ndiyo matoleo yaliyotolewa na wakuu wa Israeli kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, siku hiyo ilipotiwa mafuta; sahani za fedha kumi na mbili, na bakuli za fedha kumi na mbili, na vijiko vya dhahabu kumi na viwili; 85 kila sahani ya fedha uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na kila bakuli uzani wake ni shekeli sabini; fedha yote ya vile vyombo ilikuwa shekeli elfu mbili na mia nne, kwa shekeli ya mahali patakatifu; 86 na vijiko vya dhahabu vilivyojaa uvumba kumi na viwili, uzani wake kila kijiko shekeli kumi, kwa shekeli ya mahali patakatifu; dhahabu yote ya vile vijiko ilikuwa shekeli mia na ishirini; 87 ng'ombe wote waliokuwa wa sadaka ya kuteketezwa walikuwa ng'ombe waume kumi na wawili, na hao kondoo waume walikuwa kumi na wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza walikuwa kumi na wawili, pamoja na sadaka yao ya unga; na mbuzi waume wa sadaka ya dhambi ni kumi na wawili; 88 na ng'ombe wote waliokuwa wa dhabihu ya sadaka za amani ni ng'ombe waume ishirini na wanne, na hao kondoo waume walikuwa ni sitini, na hao mbuzi waume walikuwa ni sitini, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza walikuwa sitini. Hayo ndiyo matoleo yaliyotolewa kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, baada ya hiyo madhabahu kutiwa mafuta. 89 Kisha, Musa alipoingia ndani ya hema ya kukutania ili kunena na Mungu ndipo alipoisikia Sauti ikinena naye kutoka hapo juu ya kiti cha rehema, kilichokuwa juu ya sanduku la ushahidi, ikitoka kati ya yale makerubi mawili; naye akanena naye.

Hesabu 8

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na Haruni, ukamwambie, Utakapoziweka taa, hizo taa saba zitatoa nuru hapo mbele ya kinara cha taa. 3 Basi Haruni akafanya; akaziweka taa zake ili zitoe nuru hapo mbele ya kinara, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 4 Na hii ndiyo kazi ya hicho kinara cha taa, ilikuwa ni kazi ya ufuzi wa dhahabu; tangu tako lake hata maua yake kilikuwa ni kazi ya ufuzi; vile vile kama ule mfano Bwana aliokuwa amemwonyesha Musa, ndivyo alivyokifanya kinara. 5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 6 Watwae Walawi na kuwaondoa kati ya wana wa Israeli, kisha uwatakase. 7 Nawe utawafanyia mambo haya ili kuwatakasa; nyunyiza juu yao maji yatakasayo dhambi, nao wajinyoe kwa wembe mwili wote, kisha wazifue nguo zao, na kujitakasa. 8 Kisha na watwae ng'ombe mume mmoja mchanga, na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, nawe utatwaa ng'ombe mume mchanga mwingine kuwa sadaka ya dhambi. 9 Nawe utawahudhurisha Walawi mbele ya hema ya kukutania; nawe utaukutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli; 10 nawe utawahudhurisha Walawi mbele za Bwana; kisha wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi; 11 naye Haruni atawasongeza Walawi mbele za Bwana wawe sadaka ya kutikiswa, kwa ajili ya wana wa Israeli, ili wawe wenye kufanya utumishi wa Bwana. 12 Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya hao ng'ombe; nawe umtoe mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa Bwana, na huyo wa pili awe sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi. 13 Kisha utawaweka Walawi mbele ya Haruni, na mbele ya wanawe na kuwasongeza kwa Bwana wawe sadaka ya kutikiswa. 14 Ndivyo utakavyowatenga Walawi na kuwatoa katika wana wa Israeli; na Walawi watakuwa wangu. 15 Kisha baadaye Walawi wataingia ndani, ili wafanye utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawatakasa, na kuwasongeza wawe sadaka ya kutikiswa. 16 Kwa kuwa nimepewa kabisa mimi watu hawa kutoka katika wana wa Israeli; badala ya wote wafunguao mimba, maana, wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli wote, nimewatwaa wawe wangu. 17 Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama; siku hiyo niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli. 19 Nami nimempa Haruni hao Walawi wawe kipawa chake yeye na wanawe, kutoka kwa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa wana wa Israeli katika hema ya kukutania, kisha wafanye upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli; ili kusiwe na maradhi kati ya wana wa Israeli, hapo wana wa Israeli watakapopakaribia mahali patakatifu. 20 Basi Musa na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi mambo hayo; kama hayo yote Bwana aliyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia. 21 Walawi wakajitakasa na dhambi, nao wakafua nguo zao; kisha Haruni akawasongeza mbele za Bwana wawe sadaka ya kutikiswa; Haruni akafanya kwa ajili yao ili kuwatakasa. 22 Kisha baada ya hayo Walawi wakaingia ili wafanye utumishi wao ndani ya hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe; kama Bwana alivyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo walivyowafanyia. 23 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 24 Mambo yawapasayo hao Walawi ni haya; tangu waliopata umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi wataingia ndani ili watumike utumishi katika kazi ya hema ya kukutania; 25 tena tangu waliopata umri wa miaka hamsini wataacha kutumika huo utumishi, wasitumike tena; 26 lakini watatumika pamoja na ndugu zao katika hema ya kukutania, kushika ulinzi, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. Ndivyo utakavyowafanyia Walawi katika mambo ya ulinzi wao.

Hesabu 9

1 Kisha Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia, 2 Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa. 3 Siku ya kumi na nne ya mwezi huu, wakati wa jioni, mtaishika kwa wakati wake ulioagizwa; kwa amri zake zote, na kama hukumu zake zote zilivyo, ndivyo mtakavyoishika. 4 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli kwamba waishike sikukuu hiyo ya Pasaka; 5 Nao wakaishika Pasaka katika mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika bara ya Sinai vile vile kama hayo yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. 6 Basi walikuwako watu waume kadha wa kadha waliokuwa na unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu, hata wasiweze kuishika Pasaka siku hiyo; nao wakaenda mbele ya Musa na Haruni, siku hiyo hao watu wakamwambia, 7 Sisi tu hali ya unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu; nasi tumezuiwa kwa nini hata tusipate kumtolea Bwana matoleo kwa wakati wake ulioagizwa, kati ya wana wa Israeli? 8 Musa akawaambia, Ngojeni hapo; hata nipate sikiza Bwana atakaloagiza juu yenu. 9 Bwana akanena na Musa, akamwambia, 10 Nena na wana wa Israeli, kuwaambia, Mtu wa kwenu, au wa vizazi vyenu, ye yote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa Bwana; 11 mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika; watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu; 12 wasisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake; kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika. 13 Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea Bwana matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake. 14 Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa Bwana; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi. 15 Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi. 16 Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku. 17 Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao. 18 Kwa amri ya Bwana Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya Bwana walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao. 19 Na lile wingu lilipokawia juu ya maskani siku nyingi, ndipo wana wa Israeli walipolinda malinzi ya Bwana, wala hawakusafiri. 20 Na pengine lile wingu lilikaa juu ya maskani siku chache; ndipo kwa amri ya Bwana walikaa katika kambi yao, tena kwa amri ya Bwana walisafiri. 21 Na pengine lile wingu lilikaa tangu jioni hata asubuhi; na lile wingu lilipoinuliwa asubuhi walisafiri, au kama likikaa usiku na mchana pia, lilipoinuliwa lile wingu, ndipo waliposafiri. 22 Ikiwa lile wingu lilikawia, likikaa juu ya maskani siku mbili, au mwezi, au mwaka, wana wa Israeli walikaa katika kambi yao, wasisafiri; 23 bali lilipoinuliwa walisafiri. Kwa amri ya Bwana walipiga kambi yao, na kwa amri ya Bwana walisafiri; wakayalinda malinzi ya Bwana, kwa mkono wa Musa.

Hesabu 10

1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, 2 Jifanyie tarumbeta mbili za fedha; utazifanya za kazi ya ufuzi; nawe utazitumia kwa kuwaita mkutano wakutane, na kwa kusafiri kwao yale makambi. 3 Na hapo watakapozipiga hizo tarumbeta, mkutano wote utakukutanikia wewe, hapo mlangoni pa hema ya kukutania. 4 Nao wakipiga tarumbeta moja tu ndipo wakuu, walio vichwa vya maelfu ya Israeli, watakukutanikia wewe 5 Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha sana, marago yaliyoko upande wa mashariki yatasafiri. Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha ya pili, marago yaliyoko upande wa kusini watasafiri; 6 watapiga sauti ya kugutusha kwa ajili ya safari zao. 7 Lakini mkutano utakapokutanishwa pamoja mtapiga, lakini hamtapiga sauti ya kugutusha. 8 Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta; nazo zitakuwa kwenu ni amri ya milele katika vizazi vyenu vyote. 9 Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu. 10 Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 11 Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi. 12 Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani. 13 Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa. 14 Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake. 15 Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari. 16 Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni. 17 Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele. 18 Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. 19 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai. 20 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli. 21 Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao. 22 Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi. 23 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri. 24 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni. 25 Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani; 27 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani. 28 Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele. 29 Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo Bwana amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa Bwana ametamka mema juu ya Israeli. 30 Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe. 31 Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho. 32 Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote Bwana atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo. 33 Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa Bwana safari ya siku tatu; na sanduku la agano la Bwana likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. 34 Na wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini. 35 Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee Bwana, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao. 36 Tena hapo liliposimama, akasema, Ee Bwana, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Hesabu 11

1 Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. 2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma. 3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao. 4 Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule? 5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; 6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu. 7 Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. 8 Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. 9 Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. 10 Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika. 11 Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? 12 Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? 13 Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula. 14 Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. 15 Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu. 16 Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe. 17 Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako. 18 Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula. 19 Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; 20 lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani? 21 Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima. 22 Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha? 23 Bwana akamwambia Musa, Je! Mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo. 24 Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya Bwana; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema. 25 Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena. 26 Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini. 27 Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. 28 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze. 29 Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake. 30 Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli. 31 Kisha upepo ukavuma kutoka kwa Bwana, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi. 32 Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote. 33 Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za Bwana ziliwaka juu ya watu, Bwana akawapiga watu kwa pigo kuu mno. 34 Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani. 35 Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.

Hesabu 12

1 Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. 2 Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. 3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. 4 Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. 5 Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. 6 Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi,Bwana,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto. 7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; 8 Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? 9 Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. 10 Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. 11 Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi. 12 Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake. 13 Musa akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana. 14 Bwana akamwambia Musa, Je! Kama baba yake angalimtemea mate usoni tu, hangaliona aibu muda wa siku saba? Na afungwe nje ya kambi muda wa siku saba, kisha baada ya hayo ataletwa ndani tena. 15 Basi Miriamu alifungwa nje ya kambi muda wa siku saba; wala watu hawakusafiri hata Miriamu alipoletwa ndani tena. 16 Baada ya hayo watu wakasafiri kutoka Haserothi, wakapanga kambi katika nyika ya Parani.

Hesabu 13

1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, 2 Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao. 3 Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli. 4 Na majina yao ni haya; katika kabila ya Reubeni, Shamua mwana Zakuri. 5 Katika kabila ya Simeoni, Shafati mwana wa Hori. 6 Katika kabila ya Yuda, Kalebu mwana wa Yefune. 7 Katika kabila ya Isakari, Igali mwana wa Yusufu. 8 Katika kabila ya Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni 9 Katika kabila ya Benyamini, Palti mwana wa Rafu. 10 Katika kabila ya Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi. 11 Katika kabila ya Yusufu, yaani, katika kabila ya Manase, Gadi mwana wa Susi. 12 Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali. 13 Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli. 14 Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi. 15 Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki. 16 Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua. 17 Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani, 18 mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi; 19 na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome; 20 nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza. 21 Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi. 22 Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri. 23 Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini. 24 Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli. 25 Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini. 26 Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi. 27 Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. 28 Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. 29 Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani. 30 Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. 31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi. 32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 33 Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.

Hesabu 14

1 Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule. 2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. 3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri? 4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri. 5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli. 6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao; 7 wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8 Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope. 10 Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote. 11 Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao. 12 Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao. 13 Basi Musa akamwambia Bwana, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao; 14 kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe Bwana u kati ya watu hawa; maana, wewe Bwana waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku. 15 Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema, 16 Ni kwa sababu yeye Bwana hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani. 17 Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema, 18 Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne. 19 Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. 20 Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa; 21 lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa Bwana; 22 kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu; 23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona; 24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki. 25 Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu. 26 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 27 Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo. 28 Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; 29 mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia, 30 hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. 31 Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa. 32 Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili. 33 Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani. 34 Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu. 35 Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa. 36 Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi, 37 watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya Bwana. 38 Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi. 39 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaombolea sana. 40 Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali Bwana alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi. 41 Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyahalifu maagizo ya Bwana? Maana halitafanikiwa jambo hilo. 42 Msikwee, kwa kuwa Bwana hamo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu. 43 Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimwandame Bwana, kwa hiyo Bwana hatakuwa pamoja nanyi. 44 Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la agano la Bwana halikutoka humo maragoni, wala Musa hakutoka. 45 Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakatelemka, wakawapiga na kuwaangusha, hata kufikilia Horma.

Hesabu 15

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtakapoingia nchi yenu ya kukaa, niwapayo, 3 nanyi mwataka kumsongezea Bwana sadaka kwa moto, kwamba ni sadaka ya kuteketezwa, au dhabihu ya kuchinjwa, ili kuondoa nadhiri, au kuwa sadaka ya hiari, au katika sikukuu zenu zilizoamriwa, ili kumfanyia Bwana harufu ipendezayo, katika ng'ombe, au katika kondoo; 4 ndipo yeye atakayetoa matoleo yake na amtolee Bwana sadaka ya unga ya sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta; 5 na divai kwa sadaka ya kinywaji, robo ya hini, utaiandaa pamoja na sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa ajili ya kila mwana-kondoo. 6 Au kwa ajili ya kondoo mume, utaiandaa sadaka ya unga ya sehemu za kumi mbili za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na sehemu ya tatu ya hini ya mafuta; 7 na kwa sadaka ya kinywaji utasongeza sehemu ya tatu ya hini ya divai, kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana. 8 Tena hapo utakapomwandaa ng'ombe mume kwa sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa kuondoa nadhiri, au kwa sadaka za amani kwa Bwana; 9 ndipo utakapotoa, pamoja na huyo ng'ombe, sadaka ya unga ya sehemu za kumi tatu za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta. 10 Tena utasongeza nusu ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji, kwa sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana. 11 Ndivyo itakavyofanywa kwa kila ng'ombe, au kwa kila kondoo mume, au kwa kila mwana-kondoo mume, au kila mwana-mbuzi. 12 Kama hesabu ilivyo ya hao mtakaowaandaa, ndivyo mtakavyofanya kwa kila mmoja, sawasawa na hesabu yao. 13 Wote ambao wamezaliwa kwenu watafanya hayo yote kwa kuandama mfano huo, katika kusongeza sadaka kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana. 14 Tena kwamba mgeni amekaa kwenu, au mtu ye yote aliye kati yenu katika vizazi vyenu, naye yuataka kusongeza sadaka kwa moto, na harufu ya kupendeza kwa Bwana; kama ninyi mfanyavyo, na yeye atafanya vivyo. 15 Katika huo mkutano, kutakuwa na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye pamoja nanyi; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo, na mgeni atakuwa vivyo mbele za Bwana. 16 Itakuwa sheria moja na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye nanyi. 17 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 18 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi niwapelekayo, 19 ndipo itakapokuwa ya kwamba hapo mtakapokula katika chakula cha nchi hiyo, mtamsongezea Bwana sadaka ya kuinuliwa. 20 Katika unga wenu wa kwanza wa chenga-chenga mtasongeza mkate uwe sadaka ya kuinuliwa; vile vile kama mfanyavyo sadaka ya kuinuliwa ya sakafu ya kupuria nafaka, ndivyo mtakavyoiinua. 21 Malimbuko ya unga wenu mtampa Bwana sadaka ya kuinuliwa, katika vizazi vyenu. 22 Tena mtakapokosa, msiyashike maagizo hayo yote Bwana aliyomwambia Musa, 23 hayo yote Bwana aliyowaagiza kwa mkono wa Musa, tangu siku hiyo Bwana aliyoleta maagizo, na baadaye katika vizazi vyenu 24 ndipo itakapokuwa, kama ni kosa lililofanywa pasipo kujua, wala mkutano haukuwa na fahamu, ndipo mkutano wote utasongeza ng'ombe mume mmoja mdogo kuwa sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana, pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji, kama amri ilivyo, na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi. 25 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mkutano wote wa wana wa Israeli, nao watasamehewa; maana, lilikuwa ni kosa, nao wamekwisha leta matoleo yao, sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto, na sadaka yao ya dhambi pia wameileta mbele za Bwana kwa ajili ya kosa lao; 26 nao mkutano wote wa wana wa Israeli watasamehewa, na mgeni akaaye kati yao; maana, katika habari za hao wote jambo hilo lilitendeka pasipo kujua. 27 Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi. 28 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa. 29 Mtakuwa na sheria moja kwa huyo afanyaye neno lo lote pasipo kujua, kwa huyo aliyezaliwa kwenu kati ya wana wa Israeli, na kwa mgeni akaaye kati yao. 30 Lakini mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo amtukana Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake. 31 Kwa sababu amelidharau neno la Bwana, na kuyavunja maagizo yake; mtu huyo atakatiliwa mbali, uovu wake utakuwa juu yake. 32 Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya Sabato. 33 Hao waliomwona akikusanya kuni wakamleta kwa Musa na Haruni, na kwa mkutano wote. 34 Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa halijasemwa atakalotendwa. 35 Bwana akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote watampiga kwa mawe huko nje ya marago. 36 Basi mkutano wote wakampeleka nje ya marago, nao wakampiga kwa mawe, akafa; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 37 Kisha Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 38 Nena na wana wa Israeli, na kuwaagiza ya kwamba wajifanyie vishada katika ncha za nguo zao, katika vizazi vyao, tena ya kwamba watie katika kila kishada cha kila ncha nyuzi za rangi ya samawi; 39 nacho kitakuwa kwenu ni kishada, ili mpate kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya Bwana, na kuyafanya; tena kwamba msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na macho yenu wenyewe, ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza; 40 ili mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa Mungu wenu. 41 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Hesabu 16

1 Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni; 2 nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa; 3 nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana? 4 Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi; 5 kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake. 6 Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote; 7 vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi. 8 Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi; 9 Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia; 10 tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia? 11 Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia? 12 Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi; 13 je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa? 14 Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji. 15 Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao. 16 Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni; 17 mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake. 18 Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni. 19 Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote. 20 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 21 Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja. 22 Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote? 23 Bwana akasema na Musa, na kumwambia, 24 Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu. 25 Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye. 26 Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote. 27 Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo. 28 Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe. 29 Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi. 30 Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana 31 Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka; 32 nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote. 33 Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni. 34 Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi. 35 Kisha moto ukatoka kwa Bwana, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba. 36 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 37 Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu; 38 vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za Bwana, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli. 39 Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu; 40 viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za Bwana; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama Bwana alivyonena naye, kwa mkono wa Musa. 41 Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung'unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa Bwana. 42 Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa Bwana ukaonekana. 43 Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania. 44 Naye Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 45 Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi. 46 Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa Bwana; hiyo tauni imeanza. 47 Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu. 48 Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa. 49 Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora. 50 Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.

Hesabu 17

1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, 2 Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake. 3 Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao. 4 Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi. 5 Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu. 6 Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao. 7 Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana katika hema ya kukutania. 8 Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa malozi mabivu. 9 Kisha Musa akazileta nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za Bwana na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake. 10 Kisha Bwana akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung'uniko yao waliyoninung'unikia, ili wasife. 11 Basi Musa akafanya vivyo; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya. 12 Kisha wana wa Israeli wakanena na Musa, na kumwambia, Angalia, sisi twafa, twaangamia, sote twaangamia. 13 Kila mtu akaribiaye, aikaribiaye maskani ya Bwana, hufa; je! Tutakufa pia sote?

Hesabu 18

1 Bwana akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu. 2 Na ndugu zako nao, kabila ya Lawi, kabila ya baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungwe nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi. 3 Nao watashika ulinzi kwa amri yako, na ulinzi wa Hema yote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi. 4 Nao wataungwa nawe, na kuushika ulinzi wa hema ya kukutania, kwa ajili ya utumishi wote wa hema; na mgeni asiwakaribie ninyi. 5 Nanyi mtashika ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa madhabahu, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena. 6 Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa Bwana, waufanye utumishi wa hema ya kukutania. 7 Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa. 8 Kisha Bwana akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele. 9 Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao. 10 Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe. 11 Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo. 12 Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa Bwana, amekupa wewe hayo. 13 Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea Bwana, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo. 14 Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako. 15 Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea Bwana cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa. 16 Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini). 17 Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto, iwe harufu ya kupendeza. 18 Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako. 19 Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe. 20 Kisha Bwana akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli. 21 Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania. 22 Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa. 23 Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi. 24 Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote. 25 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 26 Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka. 27 Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu, kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kushindikia zabibu. 28 Hivyo ninyi nanyi mtasongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika zaka zenu zote, mpokeazo mikononi mwa wana wa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana. 29 Katika vipawa vyenu vyote mtasongeza kila sadaka ya kuinuliwa ya Bwana, ya wema wake wote, hiyo sehemu yake iliyowekwa takatifu. 30 Kwa ajili ya hayo utawaambia, Mtakapoinua humo hayo yaliyo mema, ndipo yatahesabiwa kuwa ya Walawi, kama kuongea kwake sakafu ya kupuria nafaka, na kama maongeo ya kinu cha kushindikia zabibu. 31 Nanyi mtakula hayo kila mahali, ninyi na watu wa nyumbani mwenu; kwa kuwa ni thawabu yenu badala ya utumishi wenu katika hema ya kukutania. 32 Nanyi hamtachukua dhambi kwa ajili yake, hapo mtakapokwisha kuinua humo hayo mema yake; lakini msivitie unajisi vile vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, ili msife.

Hesabu 19

1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, 2 Hii ndiyo amri ya sheria Bwana aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng'ombe mke mwekundu asiye na kipaku, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado; 3 nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake; 4 kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba; 5 kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng'ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto; 6 kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng'ombe. 7 Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hata jioni. 8 Na huyo aliyemchoma moto ng'ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni. 9 Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng'ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi. 10 Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng'ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao. 11 Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba; 12 naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi. 13 Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado. 14 Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba. 15 Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi. 16 Kisha mtu ye yote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba. 17 Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo; 18 kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi; 19 na yule aliye safi atamnyunyiza huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni. 20 Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa Bwana; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yu najisi. 21 Nayo itakuwa amri ya sikuzote kwao; na yeye anyunyizaye maji ya farakano atazifua nguo zake; naye ayagusaye hayo maji ya farakano atakuwa najisi hata jioni. 22 Na kitu cho chote atakachokigusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi; na mtu atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi hata jioni.

Hesabu 20

1 Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia bara ya Sini, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko. 2 Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni. 3 Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana! 4 Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu? 5 Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa. 6 Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea. 7 Bwana akasema na Musa, akinena, 8 Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao. 9 Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru. 10 Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu? 11 Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia. 12 Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa. 13 Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao. 14 Kisha Musa akatuma wajumbe kutoka Kadeshi wamwendee mfalme wa Edomu, na kusema, Ndugu yako Israeli asema, Wewe wazijua taabu zote zilizotupata; 15 jinsi baba zetu walivyotelemkia Misri, nasi tulikaa Misri muda mwingi, nao Wamisri walitutenda vibaya sana, na baba zetu pia; 16 tena tulipomlilia Bwana, akatusikiza sauti yetu, akamtuma malaika, na kututoa tutoke Misri; nasi tupo hapa Kadeshi, mji wa mpakani mwako mwa mwisho; 17 tafadhali utupe ruhusa tupite katika nchi yako; hatutapita katika mashamba, wala katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visimani; tutaifuata njia kuu ya mfalme, tusigeuke kwenda upande wa kuume, wala upande wa kushoto, hata tutakapopita mpaka wako. 18 Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga. 19 Wana wa Israeli wakamwambia, Tutakwea kwa njia kuu; tena kama tukinywa maji yako, mimi na wanyama wangu wa mifugo, ndipo nitakulipa thamani yake; nipe ruhusa nipite kwa miguu yangu wala sitaki neno lingine lo lote. 20 Akamwambia, Hutapita katika nchi yangu. Kisha Edomu akamtokea ili kupigana naye, na watu wengi, na kwa mkono wa nguvu. 21 Basi hivyo Edomu akakataa kumpa Israeli ruhusa kupita katika mipaka yake; kwa hivyo Israeli akageuka na kumwacha. 22 Kisha wakasafiri kutoka Kadeshi; wana wa Israeli, mkutano mzima, wakafikilia mlima wa Hori. 23 Bwana akanena na Musa na Haruni katika mlima wa Hori, karibu na mpaka wa nchi ya Edomu, akawaambia, 24 Haruni atakusanywa awe pamoja na watu wake; kwa kuwa hataingia katika nchi niliyowapa wana wa Israeli, kwa sababu mliasi kinyume cha neno langu hapo penye maji ya Meriba. 25 Uwatwae Haruni na mwanawe Eleazari uwalete juu ya mlima wa Hori; 26 umvue Haruni mavazi yake, ukamvike Eleazari mwanawe mavazi hayo; kisha Haruni atakusanywa kwa watu wake, naye atakufa huko. 27 Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza; wakakwea katika mlima wa Hori mbele ya macho ya mkutano wote. 28 Kisha Musa akamvua Haruni mavazi yake, akamvika mwanawe Eleazari mavazi hayo; Haruni akafa huko katika kilele cha mlima; Musa na Eleazari wakatelemka mlimani. 29 Na mkutano wote ulipoona ya kuwa Haruni amekufa, wakamwombolea Haruni muda wa siku thelathini, maana, nyumba yote ya Israeli ikamwombolea.

Hesabu 21

1 Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka. 2 Basi Israeli akaweka nadhiri kwa Bwana akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa. 3 Bwana akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma. 4 Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. 5 Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. 6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. 7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. 8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. 9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi. 10 Kisha wana wa Israeli wakasafiri, wakapanga marago Obothi. 11 Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika jangwa iliyoelekea Moabu, upande wa maawio ya jua. 12 Kutoka huko wakasafiri, wakapanga katika bonde la Zeredi. 13 Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori. 14 Kwa hiyo imesemwa katika chuo cha Vita vya Bwana, Wahebu katika Sufa, Na bonde za Arnoni, 15 Na matelemko ya hizo bonde Kwenye kutelemkia maskani ya Ari, Na kutegemea mpaka wa Moabu. 16 Kutoka huko wakasafiri kwenda Beeri; ni kisima ambacho Bwana alimwambia Musa, Uwakutanishe watu, nami nitawapa maji. 17 Ndipo Israeli wakaimba wimbo huu; Bubujika Ee kisima; kiimbieni; 18 Kisima walichokichimba wakuu, Ambacho wakuu wa watu wakakifukua, Kwa fimbo za enzi, kwa fimbo zao. 19 na kutoka Matana wakaenda Nahalieli; na kutoka Nahalieli wakaenda Bamothi; 20 na kutoka Bamothi wakaenda bondeni kwenye konde la Moabu, hata kilele cha Pisga, kielekeacho chini jangwani. 21 Kisha Israeli akatuma wajumbe kumwendea Sihoni mfalme wa Waamori, na kusema, 22 Nipe ruhusa nipite katika nchi yako; hatutageuka kando kwenda mashambani, wala kuingia katika mashamba ya mizabibu hatutakunywa maji ya visimani; tutakwenda kwa njia kuu ya mfalme, hata tutakapokuwa tumepita mpaka wako. 23 Lakini Sihoni hakukubali kumwacha Israeli kupita katika mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, akatoka aende kupigana na Israeli jangwani, akafika mpaka Yahasa; akapigana na Israeli. 24 Israeli wakampiga kwa makali ya upanga, na kuimiliki nchi yake, tangu mto wa Arnoni hata mto wa Yaboki, mpaka nchi ya wana wa Amoni; kwa kuwa mpaka wa wana wa Amoni ulikuwa una nguvu. 25 Basi Israeli wakaitwaa miji hiyo yote; Israeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, katika Heshboni, na miji yake yote. 26 Kwa kuwa Heshboni ulikuwa ni mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akipigana na mfalme wa Moabu wa mbele, na kumpokonya nchi yake yote mkononi mwake, mpaka mto wa Arnoni. 27 Kwa hiyo, hao wanenao kwa mithali wasema, Njoni Heshboni, Mji wa Sihoni na ujengwe na kuthibitishwa; 28 Maana, moto umetoka Heshboni, Umekuwa Ari ya Moabu, Mwali wa moto umetoka mji wa Sihoni; Wakuu wa mahali palipoinuka Arnoni 29 Ole wako Moabu! Umeangamia, enyi watu wa Kemoshi; Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi, Na binti zake waende utumwani, Wamwendee Sihoni mfalme wa Waamori. 30 Tumewapigia mishale; Heshboni umepotea mpaka Diboni, Nasi tumeharibu mpaka Nofa, Ifikiliayo Medeba. 31 Basi hivyo Israeli akaketi katika nchi ya Waamori. 32 Kisha Musa akapeleka watu ili kupeleleza Yazeri, nao wakaitwaa miji yake, wakawafukuza Waamori waliokuwamo. 33 Kisha wakageuka na kukwea kwa njia ya Bashani; na Ogu mfalme wa Bashani akaondoka apigane nao huko Edrei, yeye na watu wake wote. 34 Bwana akamwambia Musa, Usimche; kwa kuwa nimekwisha mtia mkononi mwako, na watu wake wote, na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni mfalme wa Waamori, aliyeketi Heshboni. 35 Basi wakampiga, na wanawe, na watu wake wote, hata wasisaze kwake mtu ye yote; nao wakaimiliki nchi yake.

Hesabu 22

1 Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko. 2 Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori. 3 Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli. 4 Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile. 5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi. 6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa. 7 Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki. 8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu. 9 Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe? 10 Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, 11 Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. 12 Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa. 13 Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi. 14 Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi. 15 Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza. 16 Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie; 17 maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa. 18 Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza. 19 Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi. 20 Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi. 21 Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu. 22 Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye. 23 Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani. 24 Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu. 25 Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili. 26 Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto. 27 Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake. 28 Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi? 29 Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi. 30 Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La! 31 Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi. 32 Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu, 33 punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai. 34 Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena. 35 Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki. 36 Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo. 37 Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi? 38 Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema. 39 Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi. 40 Balaki akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye. 41 Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.

Hesabu 23

1 Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba. 2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. 3 Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima. 4 Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. 5 Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya. 6 Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye. 7 Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli. 8 Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu? 9 Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa. 10 Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake. 11 Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa. 12 Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu? 13 Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko. 14 Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. 15 Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule. 16 Bwana akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi. 17 Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana amenena nini? 18 Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori; 19 Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza? 20 Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua. 21 Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao. 22 Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. 23 Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu! 24 Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa. 25 Balaki akamwambia Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa. 26 Lakini Balaamu akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno Bwana atakalolisema sina budi kulitenda? 27 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, Haya, njoo sasa, nikupeleke mahali pengine; labda Mungu ataridhia kwamba unilaanie watu hao huko. 28 Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini yake. 29 Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba. 30 Basi Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume juu ya kila madhabahu.

Hesabu 24

1 Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani. 2 Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia. 3 Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema; 4 Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho; 5 Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli! 6 Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji. 7 Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa. 8 Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake. 9 Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye. 10 Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi. 11 Basi sasa kimbilia mahali pako; naliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, Bwana amekuzuilia heshima. 12 Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema, 13 Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; Bwana atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi. 14 Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho. 15 Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema, 16 Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho, 17 Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia. 18 Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa. 19 Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini. 20 Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atafikilia uharibifu. 21 Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kitundu chako kimewekwa katika jabali. 22 Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hata Ashuru atakapokuchukua mateka. 23 Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya? 24 Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atafikilia uharibifu. 25 Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.

Hesabu 25

1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu; 2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao. 3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli. 4 Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli. 5 Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori. 6 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania. 7 Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake; 8 akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli. 9 Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao. 10 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia, 11 Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, kwa kuwa alikuwa na wivu kati yao kwa wivu wangu mimi, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu. 12 Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani; 13 tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya Mungu wake, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli. 14 Basi jina la Mwisraeli huyo aliyeuawa pamoja na yule mwanamke Mmidiani, aliitwa Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba zake, katika kabila la Simeoni. 15 Na jina la huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa, aliitwa Kozbi, binti Suri; naye alikuwa kichwa cha watu wa nyumba ya baba zake huko Midiani 16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 17 Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga; 18 kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.

Hesabu 26

1 Ikawa baada ya hilo pigo, Bwana akanena na Musa na Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, na kuwaambia, 2 Fanya jumla ya mkutano wote wa wana wa Israeli, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi, kwa nyumba za baba zao, hao wote katika Israeli wawezao kutoka kuenenda vitani. 3 Kisha Musa na Eleazari kuhani wakanena nao katika nchi tambarare za Moabu karibu na mto wa Yordani, huko Yeriko, wakawaambia, 4 Fanyeni jumla ya watu, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi; kama Bwana alivyomwagiza Musa na wana wa Israeli, hao waliotoka nchi ya Misri. 5 Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli, wana wa Reubeni; wa Hanoki, jamaa ya Wahanoki; na wa Palu, jamaa ya Wapalu; 6 na wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; na wa Karmi, jamaa ya Wakarmi. 7 Hizi ndizo jamaa za Wareubeni; na hao waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tatu elfu na mia saba na thelathini. 8 Na wana wa Palu; Eliabu. 9 Na wana wa Eliabu; Nemueli, na Dathani, na Abiramu. Hawa ndio Dathani na Abiramu waliochaguliwa na mkutano, ambao walishindana na Musa na Haruni katika mkutano wa Kora, hapo waliposhindana na Bwana; 10 nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza pamoja na Kora, mkutano huo ulipokufa; wakati moto ulipowateketeza watu mia mbili na hamsini, nao wakawa ishara. 11 Pamoja na hayo, hao wana wa Kora hawakufa. 12 Na wana wa Simeoni kwa jamaa zao; wa Yemueli, jamaa ya Wayemueli; wa Yamini, jamaa ya Wayamini; na Yakini, jamaa ya Wayakini; 13 wa Sohari, jamaa ya Wasohari; wa Shauli, jamaa ya Washauli. 14 Hizi ndizo jamaa za Wasimeoni, watu ishirini na mbili elfu na mia mbili. 15 Na wana wa Gadi kwa jamaa zao; wa Sifoni, jamaa ya Wasifoni; wa Hagi, jamaa ya Wahagi; wa Shuni, jamaa ya Washuni; 16 wa Ezboni, jamaa ya Waezboni; wa Eri, jamaa ya Waeri; 17 wa Arodi, jamaa ya Waarodi; wa Areli, jamaa ya Waareli. 18 Hizi ndizo jamaa za wana wa Gadi kama waliohesabiwa kwao, arobaini elfu na mia tano. 19 Na wana wa Yuda, Eri na Onani; na hao Eri na Onani wakafa katika nchi ya Kanaani. 20 Na wana wa Yuda kwa jamaa zao; wa Shela, jamaa ya Washela; wa Peresi, jamaa ya Waperesi; wa Zera, jamaa ya Wazera. 21 Na wana wa Peresi walikuwa; wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; wa Hamuli, jamaa ya Wahamuli. 22 Hizi ndizo jamaa za Yuda kama waliohesabiwa kwao, sabini na sita elfu na mia tano. 23 Na wana wa Isakari kwa jamaa zao; wa Tola, jamaa ya Watola; wa Puva, jamaa ya Wapuva; 24 wa Yashubu, jamaa ya Wayashubu; wa Shimroni, jamaa ya Washimroni. 25 Hizi ndizo jamaa za Isakari kama waliohesabiwa kwao, sitini na nne elfu na mia tatu. 26 Na wana wa Zabuloni kwa jamaa zao; wa Seredi, jamaa ya Waseredi; wa Eloni, jamaa ya Waeloni; wa Yaleeli, jamaa ya Wayaleeli. 27 Hizi ndizo jamaa za Wazabuloni kama waliohesabiwa kwao, sitini elfu na mia tano. 28 Na wana wa Yusufu kwa jamaa zao; Manase na Efraimu. 29 Wana wa Manase; wa Makiri, jamaa ya Wamakiri; na Makiri akamzaa Gileadi; wa Gileadi, jamaa ya Wagileadi. 30 Hawa ndio wana wa Gileadi; wa Abiezeri, jamaa ya Waabiezeri; wa Heleki, jamaa ya Waheleki; 31 na wa Asrieli, jamaa ya Waasrieli; na wa Shekemu, jamaa ya Washekemu; 32 na wa Shemida, jamaa ya Washemida; na wa Heferi, jamaa ya Waheferi. 33 Na Selofehadi mwana wa Heferi hakuwa na wana waume, isipokuwa wa kike; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya, Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. 34 Hizi ndizo jamaa za Manase; na waliohesabiwa kwao walikuwa ni hamsini na mbili elfu na mia saba. 35 Na wana wa Efraimu kwa jamaa zao; wa Shuthela, jamaa ya Washuthela; wa Beredi, jamaa ya Waberedi; wa Tahathi, jamaa ya Watahathi. 36 Na wana wa Shuthela ni hawa; wa Erani, jamaa ya Waerani. 37 Hizi ndizo jamaa za wana wa Efraimu kama waliohesabiwa kwao, thelathini na mbili elfu na mia tano. Hao ndio wana wa Yusufu kwa jamaa zao. 38 Na wana wa Benyamini kwa jamaa zao; wa Bela, jamaa ya Wabela; na wa Ashbeli, jamaa ya Waashbeli; wa Ahiramu, jamaa ya Waahiramu; 39 wa Shufamu, jamaa ya Washufamu; wa Hufamu, jamaa ya Wahufamu. 40 Na wana wa Bela walikuwa Ardi na Naamani; wa Ardi, jamaa ya Waardi; wa Naamani, jamaa ya Wanaamani. 41 Hao ndio wana wa Benyamini kwa jamaa zao; na waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita. 42 Na wana wa Dani ni hawa kwa jamaa zao; wa Shuhamu, jamaa ya Washuhamu. Hizi ndizo jamaa za Dani kwa jamaa zao. 43 Jamaa zote za Washuhamu, kama waliohesabiwa kwao, walikuwa sitini na nne elfu na mia nne. 44 Na wana wa Asheri kwa jamaa zao; wa Imna, jamaa ya Waimna; wa Ishvi jamaa ya Waishvi; wa Beria, jamaa ya Waberia. 45 Wa wana wa Beria; wa Heberi, jamaa ya Waheberi; wa Malkieli, jamaa ya Wamalkieli. 46 Na jina la binti wa Asheri aliitwa Sera. 47 Hizi ndizo jamaa za wana wa Asheri kama waliohesabiwa kwao, hamsini na tatu elfu na mia nne. 48 Na wana wa Naftali kwa jamaa zake; wa Yaseeli, jamaa ya Wayaseeli; na wa Guni, jamaa ya Waguni; 49 wa Yeseri, jamaa ya Wayeseri, wa Shilemu jamaa ya Washilemu. 50 Hizi ndizo jamaa za Naftali kwa jamaa zao; na waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tano elfu na mia nne. 51 Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli, mia sita na moja elfu, na mia saba na thelathini (601,730). 52 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 53 Watu hawa watagawanyiwa nchi hiyo iwe urithi wao, vile vile kama hesabu ya majina yao ilivyo. 54 Hao waliozidi hesabu yao utawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka hesabu yao, utawapa urithi kama upungufu wao; kila mtu kama watu wake walivyohesabiwa, ndivyo atakavyopewa urithi wake. 55 Lakini nchi itagawanywa kwa kura; kwa majina ya kabila za baba zao, ndivyo watakavyopata urithi. 56 Kama kura itakavyokuwa, ndivyo urithi wao utakavyogawanywa kati yao, hao wengi na hao wachache. 57 Na hao waliohesabiwa katika Walawi kwa jamaa zao ni hawa; wa Gershoni, jamaa ya Wagershoni; na wa Kohathi, jamaa ya Wakohathi; na wa Merari, jamaa ya Wamerari. 58 Hizi ndizo jamaa za Lawi; jamaa ya Walibni, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya Wamala, na jamaa ya Wamushi jamaa ya Wakora. Na Kohathi alimzaa Amramu. 59 Na jina la mke wa Amramu aliitwa Yokebedi, binti wa Lawi, ambaye alizaliwa kwake Lawi huko Misri; na huyo Yokebedi akamzalia Amramu Haruni, na Musa, na Miriamu umbu lao. 60 Tena kwake Haruni walizaliwa hawa, Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. 61 Tena Nadabu na Abihu wakafa, hapo waliposongeza moto wa kigeni mbele za Bwana. 62 Na hao waliohesabiwa kwao walikuwa ishirini na tatu elfu, kila mwanamume tangu huyo aliyepata umri wa mwezi mmoja, na zaidi; kwa kuwa hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli, kwa sababu hawakupewa urithi katika wana wa Israeli. 63 Hao ndio waliohesabiwa na Musa na Eleazari kuhani; ambao waliwahesabu wana wa Israeli katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko. 64 Lakini katika watu hao hapakuwa na mtu hata mmoja wa wale waliohesabiwa na Musa na Haruni kuhani; waliowahesabu wana wa Israeli katika bara ya Sinai. 65 Kwa kuwa Bwana alisema juu yao, Hapana budi watakufa nyikani. Napo hapakusalia mtu mmoja miongoni mwao, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

Hesabu 27

1 Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. 2 Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema, 3 Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha Bwana katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume. 4 Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu. 5 Basi Musa akaleta neno lao mbele ya Bwana 6 Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 7 Hao binti za Selofehadi wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba yao; nawe utawapa urithi wa baba yao. 8 Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo utampa binti yake urithi wake. 9 Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake. 10 Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake. 11 Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 12 Bwana akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli. 13 Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika; 14 kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.) 15 Musa akanena na Bwana akisema, 16 Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, 17 atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. 18 Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; 19 kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. 20 Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. 21 Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. 22 Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; 23 kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.

Hesabu 28

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao. 3 Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea Bwana; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote. 4 Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni; 5 pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa. 6 Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto. 7 Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia Bwana katika mahali hapo patakatifu. 8 Na mwana-kondoo wa pili utamsongeza wakati wa jioni; kama ile sadaka ya unga iliyosongezwa asubuhi, na kama sadaka yake ya kinywaji, ndivyo utakavyoisongeza, ni sadaka ya kusongezwa kwa moto, ni harufu ya kupendeza kwa Bwana. 9 Tena katika siku ya Sabato watasongezwa wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, pamoja na sehemu ya kumi mbili za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji; 10 hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila Sabato, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji. 11 Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba; 12 pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng'ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja; 13 na sehemu ya kumi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwana-kondoo; kuwa sadaka ya kuteketezwa ya harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto. 14 Tena sadaka zake za vinywaji zitakuwa nusu ya hini ya divai kwa ng'ombe, na sehemu ya tatu ya hini kwa kondoo mume, na robo ya hini kwa mwana-kondoo; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika miezi yote ya mwaka. 15 Tena mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa Bwana itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji. 16 Tena, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, ni pasaka ya Bwana. 17 Siku ya kumi na tano ya mwezi huo patakuwa na sikukuu; mkate usiotiwa chachu utaliwa muda wa siku saba. 18 Siku ya kwanza patakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi; 19 lakini mtaisongeza sadaka kwa njia ya moto, sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu; 20 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta; mtasongeza sehemu ya kumi tatu kwa ng'ombe mmoja, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume; 21 na sehemu ya kumi moja utasongeza kwa kila mwana-kondoo, wale wana-kondoo saba; 22 tena mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 23 Mtasongeza wanyama hao zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, iliyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote. 24 Mtasongeza sadaka kwa mfano huu kila siku muda wa siku saba, chakula cha sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana; itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji. 25 Na siku ya saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi. 26 Tena katika siku ya malimbuko, hapo mtakapomsongezea Bwana sadaka ya unga mpya katika sikukuu yenu ya majuma mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi; 27 lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; 28 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng'ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume, 29 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo, wa wale wana-kondoo saba; 30 na mbuzi mume mmoja, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu. 31 Zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, mtasongeza wanyama hao (watakuwa wakamilifu kwenu), pamoja na sadaka zake za vinywaji.

Hesabu 29

1 Tena mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi; ni siku ya kupiga tarumbeta kwenu. 2 Nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba; 3 pamoja na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa ng'ombe, sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume, 4 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; 5 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu; 6 zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya kuandama mwezi, na sadaka yake ya unga, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kama ilivyo amri yake, kuwa harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto. 7 Tena siku ya kumi ya huo mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; nanyi mtazitesa nafsi zenu, msifanye kazi yo yote ya utumishi 8 lakini mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza; ng'ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu; 9 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa huyo ng'ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa huyo kondoo, 10 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba; 11 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya dhambi ya upatanisho, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji. 12 Tena siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi, nanyi mtamfanyia Bwana sikukuu muda wa siku saba; 13 nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka isongezwayo kwa moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo kumi na watatu, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza kumi na wanne; wote watakuwa wakamilifu; 14 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng'ombe katika wale kumi na watatu na sehemu ya kumi mbili kwa kila kondoo katika hao kondoo waume wawili; 15 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo kumi na wanne; 16 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 17 Tena siku ya pili mtasongeza ng'ombe waume wadogo kumi na wawili, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza kumi na wanne wakamilifu; 18 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuandama hiyo amri; 19 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji. 20 Tena siku ya tatu mtasongeza ng'ombe waume kumi na mmoja, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne; 21 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 22 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 23 Tena siku ya nne mtasongeza ng'ombe waume kumi, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne; 24 na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 25 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji. 26 Tena siku ya tano mtasongeza ng'ombe waume kenda, na kondoo Waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne; 27 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 28 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 29 Tena siku ya sita mtasongeza ng'ombe waume wanane, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne; 30 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 31 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 32 Tena siku ya saba mtasongeza ng'ombe waume saba, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne; 33 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 34 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 35 Tena siku ya nane mtakuwa na kusanyiko la makini sana; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi; 36 lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kusongezwa kwa moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe mume mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba; 37 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa huyo ng'ombe, na kwa huyo kondoo mume, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri; 38 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji. 39 Sadaka hizo mtamsongezea Bwana katika sikukuu zenu zilizoamriwa, zaidi ya nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, kuwa sadaka zenu za kuteketezwa, na sadaka zenu za unga, na sadaka zenu za vinywaji, na sadaka zenu za amani. 40 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli vile vile kama hayo yote Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 30

1 Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana. 2 Mtu atakapomwekea Bwana nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake. 3 Tena mtu mke atakapomwekea Bwana nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake; 4 babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika. 5 Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na Bwana atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza. 6 Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; 7 na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika. 8 Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na Bwana atamsamehe 9 Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake. 10 Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo, 11 na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika. 12 Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na Bwana atamsamehe. 13 Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua. 14 Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake. 15 Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe. 16 Hizi ndizo amri, ambazo Bwana alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, ali nyumbani mwa babaye.

Hesabu 31

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Walipize kisasi wana wa Israeli juu ya Wamidiani; kisha baadaye utakusanywa uwe pamoja na watu wako. 3 Basi Musa akanena na watu, na kuwaambia, Wavikeni silaha watu miongoni mwenu waende vitani, ili waende kupigana na Midiani, wapate kumlipiza kisasi Bwana, juu ya Midiani. 4 Katika kila kabila mtatoa watu elfu, katika kabila zote za Israeli, nanyi mtawapeleka waende vitani. 5 Basi walitolewa katika maelfu ya Israeli, elfu moja ya kila kabila, watu waume kumi na mbili elfu walioandaliwa kwa vita. 6 Basi Musa akawapeleka, watu elfu wa kila kabila waende vitani, wao na Finehasi mwana wa Eleazari kuhani, waende vitani, na vile vyombo vya mahali patakatifu, na hizo tarumbeta za kupiga sauti za kugutusha mkononi mwake. 7 Nao wakapigana na Midiani kama Bwana alivyomwagiza Musa; nao wakamwua kila mume. 8 Nao wafalme wa Midiani wakawaua pamoja na watu wengine waliouawa; Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao wafalme watano wa Midiani; Balaamu mwana wa Beori naye wakamwua kwa upanga. 9 Wana wa Israeli wakawachukua mateka wanawake wa Midiani na watoto wao; na ng'ombe zao wote, na kondoo zao wote, na mali zao zote, wakachukua nyara. 10 Na miji yao yote, kila mahali walipokuwa wakikaa, na marago yao yote wakayateketeza kwa moto. 11 Nao wakatwaa hizo nyara zote, na mateka yote, ya wanadamu na ya wanyama. 12 Nao wakawaleta mateka ya wanadamu, na mateka ya wanyama, na hizo nyara, na kuyaweka mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wa wana wa Israeli, hapo maragoni katika nchi tambarare za Moabu, zilizo karibu na Yordani hapo Yeriko. 13 Basi Musa, na Eleazari kuhani, na wakuu wote wa huo mkutano, wakatoka nje kwenda kuwalaki nje ya marago. 14 Musa akawakasirikia majemadari wa jeshi, na hao maakida wa elfu elfu, na wakuu wa mia mia, hao waliorudi kutoka katika kupiga vita. 15 Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai? 16 Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana. 17 Basi kwa ajili hiyo mwueni kila mume katika hao watoto, na kila mwanamke aliyemjua mume kwa kulala pamoja naye. 18 Lakini hao watoto wote wa kike ambao hawakumjua mume kwa kulala pamoja naye, mtawaweka hai kwa ajili yenu. 19 Nanyi fanyeni matuo yenu nje ya marago muda wa siku saba; mtu awaye yote aliyemwua mtu, na awaye yote aliyemgusa mtu aliyeuawa, jitakaseni nafsi zenu siku ya tatu, na siku ya saba, ninyi na mateka yenu. 20 Na katika habari ya kila nguo, na kila kitu kilichofanywa cha ngozi, na kazi yote ya singa za mbuzi, na vyombo vyote vilivyofanywa vya mti, mtajitakasa wenyewe; 21 Kisha Eleazari kuhani akawaambia waume wa vita wote waliokwenda vitani, Hii ndiyo amri ya sheria Bwana aliyomwagiza Musa; 22 lakini dhahabu, na fedha, na shaba, na chuma, na bati, na risasi, 23 kila kitu kiwezacho kuuhimili moto, mtakipitisha katika moto, nacho kitakuwa safi, pamoja na haya kitatakaswa kwa hayo maji ya farakano; na kila kitu kisichouhimili moto mtakipitisha katika hayo maji. 24 Nanyi mtazifua nguo zenu siku ya saba, nanyi mtakuwa safi, kisha baadaye mtaingia maragoni. 25 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 26 Fanya jumla ya hayo mateka ya wanadamu, na ya wanyama pia, wewe, na Eleazari kuhani, na wakuu wa nyumba za baba za mkutano; 27 ukagawanye nyara mafungu mawili; kati ya watu waliozoea vita, waliotoka nje waende vitani, na huo mkutano wote; 28 kisha uwatoze hao watu wa vita waliotoka kwenda vitani sehemu kwa ajili ya Bwana; mmoja katika mia tano, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo; 29 twaa katika nusu yao, ukampe Eleazari kuhani, kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana. 30 Na katika hiyo nusu ya wana wa Israeli utatwaa mmoja atakayetolewa katika kila hamsini, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo, maana, katika wanyama wote, ukawape Walawi, hao walindao ulinzi wa maskani ya Bwana. 31 Musa na Eleazari kuhani wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa. 32 Basi masazo ya hizo nyara walizotwaa watu wa vita, zilikuwa ni kondoo mia sita na sabini na tano elfu, 33 na ng'ombe sabini na mbili elfu, 34 na punda sitini na moja elfu, 35 tena wanadamu jumla yao ilikuwa thelathini na mbili elfu, katika hao wanawake ambao hawakumjua mume kwa kulala pamoja naye. 36 Na hiyo nusu ambayo ilikuwa ni sehemu ya hao waliotoka kwenda vitani, hesabu yake ilikuwa kondoo mia tatu na thelathini na saba elfu na mia tano; 37 na kodi ya Bwana katika hao kondoo ilikuwa kondoo mia sita na sabini na watano. 38 Tena, ng'ombe walikuwa thelathini na sita elfu; na katika hao kodi ya Bwana ilikuwa ng'ombe sabini na wawili. 39 Na punda walikuwa thelathini elfuna mia tano, katika hao kodi ya Bwana ilikuwa punda sitini na mmoja. 40 Na wanadamu walikuwa watu kumi na sita elfu; katika hao sehemu ya Bwana ilikuwa ni watu thelathini na wawili. 41 Basi Musa akampa Eleazari kuhani hiyo sehemu, iliyokuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Musa. 42 Tena katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, ambayo Musa aliitenga na watu waliokwenda vitani, 43 (basi hiyo nusu ya mkutano ilikuwa ni kondoo mia tatu na thelathini na saba elfu na mia tano, 44 na ng'ombe thelathini na sita elfu, 45 na punda thelathini elfu, na mia tano, 46 na wanadamu kumi na sita elfu;) 47 na katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, Musa akatwaa mmoja aliyetolewa katika kila hamsini, wa binadamu na wa wanyama, akawapa Walawi, waliolinda ulinzi wa maskani ya Bwana; kama Bwana alivyomwagiza Musa. 48 Na majemadari waliokuwa juu ya elfu elfu za hiyo jeshi, na maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia, wakamkaribia Musa; 49 wakamwambia Musa wakisema, Sisi watumishi wako tumefanya jumla ya hesabu ya watu wa vita walio chini ya mikono yetu, na hapana hata mmoja aliyetupungukia. 50 Nasi tumeleta matoleo ya Bwana, aliyopata kila mtu, ya vyombo vya dhahabu, na mitali, na timbi, na pete za muhuri, na vipini, na vikuku, ili kuzifanyia upatanisho nafsi zetu mbele ya Bwana. 51 Musa na Eleazari kuhani wakapokea kwao hiyo dhahabu, maana, vile vyombo vyote vilivyofanyizwa. 52 Na dhahabu yote ya sadaka ya kuinuliwa waliyosongeza kwa Bwana, ya maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia, ilikuwa shekeli kumi na sita elfu na mia saba na hamsini. 53 (Kwa kuwa hao watu wa vita walikuwa wametwaa nyara, kila mtu nafsi yake.) 54 Basi Musa na Eleazari kuhani wakapokea hiyo dhahabu mikononi mwa hao maakida wa elfu elfu na wa mia mia, na kuileta ndani ya hema ya kukutania, ili iwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele za Bwana.

Hesabu 32

1 Basi wana wa Reubeni, na hao wana wa Gadi, walikuwa na wanyama wa mifugo wengi sana; nao walipoona nchi ya Yazeri, na nchi ya Gileadi, ya kuwa mahali hapo palikuwa ni mahali pa kuwafaa wanyama; 2 hao wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakamwendea Musa na Eleazari kuhani, na wakuu wa mkutano, wakanena nao, wakisema, 3 Atarothi, na Diboni, na Yazeri, na Nimra, na Heshboni, na Eleale, na Sebamu, na Nebo na Beoni, 4 nchi hiyo ambayo Bwana aliipiga mbele ya mkutano wa Israeli, ni nchi ifaayo kwa mfugo wa wanyama, nasi watumishi wako tuna wanyama. 5 Wakasema, Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, sisi watumishi wako na tupewe nchi hii iwe milki yetu; usituvushe mto wa Yordani. 6 Musa akawaambia wana wa Gadi na wana wa Reubeni, Je! Ndugu zenu waende vitani nanyi mtaketi hapa? 7 Mbona mwawavunja mioyo yao wana wa Israeli, wasivuke na kuingia nchi hiyo ambayo Bwana amewapa? 8 Ndivyo walivyofanya baba zenu, hapo nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea ili waende kuiangalia hiyo nchi. 9 Kwa kuwa walipokwea na kuingia bonde la Eshkoli, na kuiona nchi, wakawavunja mioyo wana wa Israeli, ili wasikwee kuingia nchi Bwana aliyowapa. 10 Na siku ile hasira za Bwana ziliwaka, naye akaapa, akisema, 11 Hakika yangu hapana mtu mmoja katika wale watu waliotoka Misri, tangu huyo aliyepata umri wa miaka ishirini, na zaidi, atakayeiona hiyo nchi niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa sababu hawakuniandama kwa moyo wote; 12 ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama Bwana kwa moyo wote. 13 Na hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa Bwana kikaisha angamia. 14 Na tazama, ninyi mmeinuka badala ya baba zenu, maongeo ya watu wenye dhambi, ili kuongeza tena hizo hasira kali za Bwana juu ya Israeli. 15 Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote. 16 Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu; 17 lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi. 18 Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake. 19 Kwa kuwa sisi hatutarithi pamoja nao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, huko mbele; kwa sababu urithi wetu umetuangukia upande huu wa Yordani kwa mashariki. 20 Basi Musa akawaambia, Kama mtafanya jambo hili; kama mtajivika silaha, ili kutangulia mbele ya Bwana mwende vitani, 21 tena kama kila mume wa kwenu mwenye kuchukua silaha atavuka Yordani mbele ya Bwana, hata atakapokuwa amekwisha watoa adui zake mbele yake, 22 na hiyo nchi kushindwa mbele za Bwana; ndipo baadaye mtarudi, nanyi mtakuwa hamna hatia mbele za Bwana, wala kwa Israeli; na nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana. 23 Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi. 24 Basi, jengeni miji kwa ajili ya watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya kondoo zenu; mkayafanye hayo mliotamka kwa vinywa vyenu. 25 Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo. 26 Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng'ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi; 27 lakini sisi watumishi wako tutavuka, kila mume aliyevaa silaha za vita, mbele za Bwana, tuende vitani, kama wewe bwana wangu usemavyo. 28 Basi Musa akamwagiza Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na wakuu wa nyumba za mababa za kabila za wana wa Israeli, katika habari za watu hao. 29 Musa akawaambia, Kwamba wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, watavuka Yordani pamoja nanyi, kila mtu aliyevaa silaha kwa vita, mbele za Bwana, nayo nchi itashindwa mbele yenu; ndipo mtawapa nchi ya Gileadi kuwa milki yao; 30 lakini ikiwa hawataki kuvuka pamoja nanyi, hali wamevaa silaha zao, ndipo watakuwa na milki zao kati yenu katika nchi ya Kanaani. 31 Wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakajibu na kusema, Kama Bwana alivyotuambia sisi watumishi wako, ndivyo tutakavyofanya. 32 Tutavuka, hali tumevaa silaha zetu, mbele za Bwana, kuingia nchi ya Kanaani, nayo milki ya urithi wetu itakuwa ng'ambo ya pili ya Yordani. 33 Basi Musa akawapa wao, maana, wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, mwana wa Yusufu, ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, hiyo nchi, kama miji yao ilivyokuwa, pamoja na mipaka yake, maana, miji ya hiyo nchi iliyozunguka kotekote. 34 Kisha wana wa Gadi wakajenga Diboni, na Atarothi, na Aroeri; 35 na Atrothi-shofani, na Yazeri, na Yogbeha; 36 na, Beth-nimra, na Beth-harani; miji yenye maboma, na mazizi ya kondoo. 37 Na wana wa Reubeni wakajenga Heshboni, na Eleale, na Kiriathaimu; 38 na Nebo, na Baal-meoni, (majina yake yalikuwa yamegeuzwa) na Sibma; nao wakaiita miji waliyoijenga majina mengine. 39 Na wana wa Makiri mwana wa Manase wakaenda Gileadi, na kuitwaa, na kuwapokonya Waamori waliokuwamo humo. 40 Basi Musa akampa Makiri, mwana wa Manase, Gileadi, naye akakaa humo. 41 Kisha Yairi mwana wa Manase akaenda na kuvitwaa vijiji vya Gileadi. Akaviita jina lake Hawoth-yairi. 42 Kisha Noba akaenda na kutwaa Kenathi na vijiji vyake, na kuita jina lake Noba, kwa kuandama jina lake mwenyewe.

Hesabu 33

1 Hizi ndizo safari za wana wa Israeli, hapo walipotoka nchi ya Misri kwa jeshi zao chini ya mkono wa Musa na Haruni. 2 Musa akaandika jinsi walivyotoka katika safari zao, kwa amri ya Bwana; na hizi ndizo safari zao kama kutoka kwao kulivyokuwa. 3 Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa mkono wa nguvu mbele ya macho ya Wamisri wote, 4 hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, Bwana aliokuwa amewapiga kati yao; Bwana akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo. 5 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapanga katika Sukothi. 6 Kisha wakasafiri kutoka Sukothi, wakapanga Ethamu, palipo katika mwisho wa nyika. 7 Wakasafiri kutoka Ethamu, na kurudi nyuma hata Pi-hahirothi palipokabili Baal-sefoni; wakapanga mbele ya Migdoli. 8 Wakasafiri kutoka hapo mbele ya Hahirothi, wakapita katikati ya bahari na kuingia jangwani; kisha wakaenda safari ya siku tatu katika nyika ya Ethamu, wakapanga Mara. 9 Wakasafiri kutoka Mara, wakafikilia Elimu; huko Elimu palikuwa na chemchemi za maji kumi na mbili, na mitende sabini; nao wakapanga hapo. 10 Wakasafiri kutoka Elimu wakapanga karibu na Bahari ya Shamu. 11 Wakasafiri kutoka Bahari ya Shamu, wakapanga katika nyika ya Sini. 12 Wakasafiri kutoka nyika ya Sini, wakapanga Dofka. 13 Wakasafiri kutoka Dofka, wakapanga Alushi. 14 Wakasafiri kutoka Alushi, wakapanga Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya watu kunywa. 15 Wakasafiri kutoka Refidimu, wakapanga katika nyika ya Sinai. 16 Wakasafiri kutoka nyika ya Sinai, wakapanga Kibroth-hataava. 17 Wakasafiri kutoka Kibroth-hataava, wakapanga Haserothi. 18 Wakasafiri kutoka Haserothi, wakapanga Rithma. 19 Wakasafiri kutoka Rithma, wakapanga Rimon-peresi. 20 Wakasafiri kutoka Rimon-peresi, wakapanga Libna. 21 Wakasafiri kutoka Libna, wakapanga Risa. 22 Wakasafiri kutoka Risa, wakapanga Keheletha. 23 Wakasafiri kutoka Keheletha, wakapanga katika mlima wa Sheferi 24 Wakasafiri kutoka huo mlima wa Sheferi, wakapanga Harada. 25 Wakasafiri kutoka Harada, wakapanga Makelothi. 26 Wakasafiri kutoka Makelothi, wakapanga Tahathi. 27 Wakasafiri kutoka Tahathi wakapanga Tera. 28 Wakasafiri kutoka Tera, wakapanga Mithka. 29 Wakasafiri kutoka Mithka, wakapanga Hashmona. 30 Wakasafiri kutoka Hashmona, wakapanga Moserothi. 31 Wakasafiri kutoka Moserothi, wakapanga Bene-yakani. 32 Wakasafiri kutoka Bene-yakani, wakapanga Hor-hagidgadi. 33 Wakasafiri kutoka Hor-hagidgadi, wakapanga Yotbatha. 34 Wakasafiri kutoka Yotbatha, wakapanga Abrona. 35 Wakasafiri kutoka Abrona, wakapanga Esion-geberi. 36 Wakasafiri kutoka Esion-geberi, wakapanga katika nyika ya Sini (ni Kadeshi). 37 Wakasafiri kutoka Kadeshi wakapanga katika mlima wa Hori, katika mpaka wa nchi ya Edomu, 38 Haruni akakwea mlima wa Hori, kwa amri ya Bwana, akafa hapo, katika mwaka wa arobaini baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, mwezi wa tano, siku ya kwanza ya mwezi. 39 Naye Haruni alikuwa mtu wa umri wa miaka mia na ishirini na mitatu hapo alipokufa katika mlima wa Hori. 40 Ndipo Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyekaa pande za Negebu katika nchi ya Kanaani akasikia habari za kuja kwao wana wa Israeli. 41 Nao wakasafiri kutoka mlima wa Hori, wakapanga Salmona. 42 Wakasafiri kutoka Salmona, wakapanga Punoni. 43 Wakasafiri kutoka Punoni, wakapanga Obothi. 44 Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika mpaka wa Moabu. 45 Wakasafiri kutoka Iye-abarimu, wakapanga Dibon-gadi. 46 Wakasafiri kutoka Dibon-gadi, wakapanga Almon-diblathaimu. 47 Wakasafiri kutoka Almon-diblathaimu, wakapanga katika milima ya Abarimu, kukabili Nebo. 48 Wakasafiri kutoka hiyo milima ya Abarimu, wakapanga katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko. 49 Wakapanga karibu na Yordani, tangu Beth-yeshimothi hata kufikilia Abel-shitimu katika nchi tambarare za Moabu. 50 Kisha Bwana akanena na Musa hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko, na kumwambia, 51 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, 52 ndipo mtakapowafukuza wenyeji wote wa hiyo nchi mbele yenu, nanyi mtayaharibu mawe yao yote yenye kuchorwa sanamu, na kuziharibu sanamu zao zote za kusubu, kuvunja-vunja mahali pao pote palipoinuka; 53 nanyi mtaishika hiyo nchi kuimiliki na kuketi humo; kwa kuwa mimi nimewapa ninyi hiyo nchi ili mwimiliki. 54 Nanyi mtairithi nchi kwa kufanya kura, kama jamaa zenu zilivyo; hao walio wengi mtawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka utawapa kama kupunguka kwao; mahali po pote kura itakapomwangukia mtu ye yote, mahali hapo ni pake; mtarithi kama kabila za baba zenu zilivyo. 55 Lakini kama hamtaki kuwafukuza wenyeji wa nchi watoke mbele yenu; ndipo hao ambao mtakaowasaza watakuwa kama sindano machoni mwenu, na kama miiba ubavuni mwenu, nao watawasumbua katika hiyo nchi ambayo mwakaa. 56 Kisha itakuwa, kama nilivyoazimia kuwatenda wao, ndivyo nitakavyowatenda ninyi.

Hesabu 34

1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 2 Waagize wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi ya Kanaani, (hii ndiyo nchi itakayowaangukia kuwa urithi, maana, hiyo nchi ya Kanaani kama mipaka yake ilivyo,) 3 ndipo upande wenu wa kusini utakuwa tangu bara ya Sini kupita kando ya Edomu, na mpaka wenu wa kusini utakuwa tangu mwisho wa Bahari ya Chumvi kuelekea mashariki; 4 kisha mpaka wenu utageuka kwenda upande wa kusini wa kukwelea kwake Akrabimu, kisha kupita kwendelea Sini; na kutokea kwake kutakuwa kuelekea upande wa kusini wa Kadesh-barnea; kisha utaendelea mpaka Hasar-adari, na kufikilia Azmoni; 5 kisha mpaka utageuka kutoka Azmoni kwendelea kijito cha Misri, na kutokea kwake kutakuwa hapo baharini. 6 Kisha mpaka wenu wa upande wa magharibi mtakuwa na bahari kubwa na mpaka wake; hii ndiyo mpaka wenu upande wa magharibi. 7 Kisha mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa ni huu; kutoka bahari kubwa mtajiandikia mlima wa Hori; 8 na kutoka mlima wa Hori mtaandika mpaka kuingilia kwake Hamathi; na kutokea kwake mpaka kutakuwa hapo Sedada; 9 tena mpaka utatokea hata Zifroni, na kutokea kwake kutakuwa hapo Hasarenani; huo ndio mpaka wenu wa upande wa kaskazini. 10 Kisha mtaandika mpaka wenu wa upande wa mashariki kutoka Hasarenani hata Shefamu; 11 kisha mpaka utatelemka kutoka Shefamu mpaka Ribla, upande wa mashariki wa Aini; kisha mpaka utatelemka na kufikilia upande wa bahari ya Kinerethi upande wa mashariki; 12 kisha mpaka utatelemkia Yordani, na kutokea kwake kutakuwa hapo katika Bahari ya Chumvi; hii ndiyo nchi yenu kama mipaka yake ilivyo kuizunguka pande zote. 13 Kisha Musa akawaagiza wana wa Israeli, akisema, Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, ambayo Bwana ameagiza wapewe watu wa zile kabila kenda, na nusu ya kabila; 14 kwa kuwa kabila ya wana wa Reubeni kwa nyumba za baba zao, na kabila ya wana wa Gadi kwa nyumba za baba zao, wamekwisha pata, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wamekwisha pata urithi wao; 15 hizo kabila mbili na nusu ya kabila wamekwisha pata urithi wao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo Yeriko, upande wa mashariki, kuelekea maawio ya jua. 16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 17 Haya ndiyo majina ya watu watakaowagawanyia nchi iwe urithi wenu; Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni. 18 Kisha mtamtwaa mkuu mmoja wa kila kabila, ili waigawanye nchi iwe urithi wenu. 19 Na majina ya watu hao ni haya; katika kabila ya Yuda, ni Kalebu mwana wa Yefune. 20 Na katika kabila ya wana wa Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi. 21 Katika kabila ya Benyamini, ni Elidadi mwana wa Kisloni. 22 Na katika kabila ya wana wa Dani, mkuu, Buki mwana wa Yogli. 23 Katika wana wa Yusufu; katika kabila ya wana wa Manase, mkuu, Hanieli mwana wa Efodi; 24 na katika kabila ya wana wa Efraimu, mkuu, Kemueli mwana wa Shiftani. 25 Na katika kabila ya wana wa Zabuloni, mkuu, Elisafani mwana wa Parnaki. 26 Na katika kabila ya wana wa Isakari, mkuu, Paltieli mwana wa Azani. 27 Na katika kabila ya wana wa Asheri, mkuu, Ahihudi mwana wa Shelomi. 28 Na katika kabila ya wana wa Naftali, mkuu, Pedaheli mwana wa Amihudi. 29 Hao ndio Bwana aliowaagiza wawagawanyie urithi wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani.

Hesabu 35

1 Kisha Bwana akanena na Musa katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko, akamwambia, 2 Uwaagize wana wa Israeli wawape Walawi miji wapate mahali pa kukaa, katika milki yao; pamoja na malisho yaliyoizunguka hiyo miji kotekote mtawapa Walawi. 3 Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote. 4 Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote. 5 Nanyi mtapima hapo nje ya mji upande wa mashariki dhiraa elfu mbili, na upande wa kusini dhiraa elfu mbili, na upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, huo mji ulio katikati. Hayo ndiyo yatakayokuwa kwao malisho ya miji. 6 Na hiyo miji mtakayowapa Walawi, itakuwa miji sita ya makimbilio, mtakayoweka kwa ajili ya mwenye kumwua mtu, ili akimbilie huko; pamoja na hiyo mtawapa miji arobaini na miwili zaidi. 7 Miji yote mtakayowapa hao Walawi jumla yake itakuwa miji arobaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na malisho yake. 8 Tena katika miji mtakayotoa ya hiyo milki ya wana wa Israeli, katika hao walio wengi mtatwaa miji mingi; na katika hao walio wachache mtatwaa miji michache; kila mtu kama ulivyo urithi wake atakaourithi, atawapa Walawi katika miji yake. 9 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, 10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani, 11 Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. 12 Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe. 13 Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio. 14 Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio. 15 Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko. 16 Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa. 17 Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa. 18 Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa. 19 Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua. 20 Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa; 21 au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye. 22 Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia, 23 au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara; 24 ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo; 25 nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu. 26 Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia; 27 na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu; 28 kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake. 29 Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote. 30 Mtu awaye yote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu hata akafa. 31 Tena, msipokee fidia kwa ajili ya uhai wa mwuaji, ambaye amekuwa na hatia ya mauti; Lakini lazima atauawa. 32 Tena hamtapokea fidia kwa ajili ya huyo aliyeukimbilia mji wake wa makimbilio, apate kwenda tena kuketi katika nchi, hata kifo cha kuhani mkuu. 33 Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga. 34 Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa kati ya wana wa Israeli.

Hesabu 36

1 Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli; 2 wakasema, Bwana alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na Bwana awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao. 3 Wakiolewa na watu wa wana wa hizo kabila nyingine za wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hiyo kabila watakayotiwa ndani yake itaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu. 4 Tena itakapokuwapo hiyo yubile ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hiyo kabila ambayo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila ya baba zetu. 5 Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la Bwana lilivyokuwa, akasema, Kabila ya wana wa Yusufu imenena yaliyo haki. 6 Bwana ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao. 7 Hivyo hapana urithi wo wote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya baba zake. 8 Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila yo yote katika wana wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila ya baba yake, ili wana wa Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake. 9 Hivyo hapatakuwa na urithi uwao wote utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa kabila za wana wa Israeli zitashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe. 10 Basi hao binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa; 11 kwa kuwa Mala, na Tirsa, na Hogla, na Milka, na Noa, binti za Selofehadi waliolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao. 12 Waliolewa katika jamaa za wana wa Manase, mwana wa Yusufu, na urithi wao ukakaa katika kabila ya jamaa ya baba yao. 13 Haya ndiyo maagizo na hukumu, ambayo Bwana aliwaagiza wana wa Israeli, kwa mkono wa Musa, hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko

Kumbukumbu la Torati 1

1 Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng'ambo ya Yordani barani, katika Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu. 2 Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea. 3 Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na Bwana ya kuwaamuru; 4 alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei; 5 ni ng'ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema, 6 Bwana, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha; 7 geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati. 8 Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao. 9 Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu. 10 Bwana, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi. 11 Bwana, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi. 12 Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na mateto yenu? 13 Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya kabila zenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu. 14 Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilonena ni jema la kufanya. 15 Basi nikatwaa vichwa vya kabila zenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, maakida ya elfu elfu, na maakida ya mia mia, na maakida ya hamsini hamsini, na maakida ya kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya kabila zenu. 16 Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye. 17 Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza. 18 Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya. 19 Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama Bwana, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea. 20 Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi Bwana, Mungu wetu. 21 Tazama, Bwana, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike. 22 Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia. 23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila. 24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza. 25 Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa Bwana, Mungu wetu, ni nchi njema. 26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la Bwana, Mungu wenu; 27 mkanung'unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu Bwana ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. 28 Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. 29 Ndipo nikawaambieni, Msifanye hofu, wala msiwache. 30 Bwana, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; 31 na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua Bwana, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa. 32 Lakini katika jambo hili hamkumwamini Bwana, Mungu wenu, 33 aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonyesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu. 34 Bwana akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema, 35 Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa, 36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata Bwana kwa kila neno. 37 Na Bwana alinikasirikia mimi kwa ajili yenu, akasema, Wala wewe hutaingia humo; 38 Yoshua mwana wa Nuni asimamaye mbele yako ndiye atakayeingia; mtie moyo; kwa kuwa yeye atawarithisha Israeli. 39 Tena, wadogo wenu, mliosema watakuwa mateka, na wana wenu, wasiokuwa leo na maarifa ya mabaya wala mema, ndio watakaoingia, nao ndio nitakaowapa, nao wataimiliki. 40 Na ninyi basi geukeni, mshike safari yenu, mwende jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu. 41 Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya Bwana, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na Bwana. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. 42 Bwana akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. 43 Basi niliwaambia, msinisikize, bali mliasi amri ya Bwana, mkajikinai, na kukwea mlimani. 44 Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma. 45 Mkarudi mkalia mbele za Bwana; Bwana asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu. 46 Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.

Kumbukumbu la Torati 2

1 Ndipo tukageuka, tukashika safari yetu kwenda jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu, kama alivyoniambia Bwana; tukawa kuizunguka milima ya Seiri siku nyingi. 2 Bwana akanena, akaniambia, 3 Mlivyouzunguka mlima huu vyatosha; geukeni upande wa kaskazini. 4 Nawe waagize watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa watu, uwaambie, Mtapita kati ya mpaka wa ndugu zenu wana wa Esau waketio Seiri; nao watawaogopa; basi jiangalieni nafsi zenu sana; 5 msitete nao; kwa maana sitawapa katika nchi yao kamwe, hata kiasi cha kukanyaga wayo wa mguu; kwa kuwa nimempa Esau milima ya Seiri kuwa milki yake. 6 Nunueni vyakula kwao kwa fedha, mpate kula; na maji nayo nunueni kwao kwa fedha, mpate kunywa. 7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, amekubarikia katika kazi yote ya mkono wako; amejua ulivyotembea katika jangwa kubwa hili; miaka arobaini hii alikuwa nawe Bwana, Mungu wako; hukukosa kitu. 8 Basi tukapita kando yao ndugu zetu wana wa Esau, waketio Seiri kutoka njia ya Araba, kutoka Elathi na kutoka Esion-geberi. Tukageuka tukapita njia ya bara ya Moabu. 9 Bwana akaniambia, usiwasumbue Wamoabi, wala usishindane nao katika mapigano; kwa kuwa sitakupa katika nchi yake kuimiliki; kwa sababu Ari nimewapa wana wa Lutu kuimiliki. 10 (Walioketi humo hapo kale ni Waemi, nao ni watu wakubwa, wengi, warefu, mfano wa Waanaki; 11 na hawa nao wadhaniwa kuwa majitu kama Waanaki;lakini Wamoabi huwaita Waemi. 12 Na Wahori nao walikuwa wakikaa Seiri hapo kale, lakini wana wa Esau waliwafuata; wakawaangamiza mbele yao, wakakaa badala yao; kama alivyofanya Israeli nchi ya milki yake aliyopewa na Bwana.) 13 Sasa basi ondokeni, mkakivuke kijito cha Zeredi. Nasi tukakivuka kile kijito cha Zeredi. 14 Na siku tulizokuwa tukienda kutoka Kadesh-barnea hata tulipovuka kijito cha Zeredi, zilikuwa ni miaka thelathini na minane; maana, hata walipokwisha kuangamizwa watu wa vita kutoka kati ya marago, kizazi chao chote, kama walivyoapiwa na Bwana. 15 Tena mkono wa Bwana ulikuwa juu yao ili kuwaangamiza, kuwatoa kati ya marago, hata walipokoma. 16 Basi ikawa, walipokwisha angamizwa kwa kufa watu wote wa vita kati ya watu, 17 Bwana aliniambia, akasema, 18 Hivi leo ivuke Ari, mpaka wa Moabu; 19 na utakaposongea kuwaelekea wana wa Amoni, usiwasumbue wana wa Amoni, wala usishindane nao; kwa kuwa sitakupa katika nchi ya hao wana wa Amoni kuwa milki yako; kwa sababu nimewapa wana wa Lutu iwe milki yao. 20 (Nchi hiyo nayo yadhaniwa kuwa ni nchi ya Warefai, hapo kale Warefai walikaa humo; lakini Waamoni huwaita Wazamzumi; 21 nao ni watu wengi, wakubwa, warefu, kama Waanaki; lakini Bwana aliwaangamiza mbele yao; wakawafuata wakakaa badala yao; 22 kama vile alivyowafanyia wana wa Esau, waliokaa Seiri, alipowaangamiza Wahori mbele yao; wakawafuata, wakakaa badala yao hata hivi leo; 23 na Waavi waliokuwa wakikaa katika vijiji mpaka Gaza waliangamizwa na Wakaftori waliotoka Kaftori, na hawa wakakaa badala yao.) 24 Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano. 25 Hivi leo nitaanza mimi kutia utisho wako na kuhofiwa kwako juu ya watu walio chini ya mbingu kila mahali, watakaosikia uvumi wako, na kutetemeka, na kuingiwa na uchungu kwa sababu yako. 26 Nikatuma wajumbe kutoka bara ya Kedemothi kwenda kwa Sihoni mfalme wa Heshboni na maneno ya amani, kusema. 27 Nipishe katikati ya nchi yako; nitakwenda kwa njia ya barabara, sitageuka kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto. 28 Nawe uniuzie chakula kwa fedha nile; unipe na maji kwa fedha, ninywe; ila unipishe katikati kwa miguu yangu, hayo tu; 29 kama walivyonifanyia hao wana wa Esau waketio Seiri, na hao Wamoabi waketio Ari; hata nivuke Yordani niingie nchi tupewayo na Bwana, Mungu wetu. 30 Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni hakutuacha kupitia kwake; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, alimfanya mgumu roho yake, akamtia ukaidi moyoni mwake, apate mtia mkononi mwako kama alivyo hivi leo. 31 Kisha Bwana akaniambia, Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako; anza kuimiliki, upate kuirithi nchi yake. 32 Ndipo Sihoni alipotutokea juu yetu yeye na watu wake wote, kupigana huko Yahasa. 33 Bwana, Mungu wetu, akamtoa mbele yetu, tukampiga yeye na wanawe, na watu wake wote. 34 Tukatwaa miji yake yote wakati huo, tukaharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na wadogo; tusimsaze hata mmoja; 35 ila ng'ombe zao tuliwatwaa kuwa mawindo yetu, pamoja na nyara za miji tuliyoitwaa. 36 Kutoka Aroeri iliyo katika ukingo wa bonde la Arnoni, na huo mji ulio ndani ya bonde, mpaka kufika Gileadi, hapakuwa na mji uliokuwa mrefu kutushinda; Bwana, Mungu wetu, aliiweka wazi yote mbele yetu; ila nchi ya wana wa Amoni hukuisongelea; 37 upande wote wa mto wa Yaboki, na miji ya nchi ile ya milimani, na kila mahali alipotukataza Bwana, Mungu wetu.

Kumbukumbu la Torati 3

1 Ndipo tukageuka, tukakwea njia ya Bashani; na Ogu, mfalme wa Bashani, akatutokea juu yetu, yeye na watu wake wote, kuja kupigana huko Edrei. 2 Bwana akaniambia, Usimwogope; kwa kuwa nimemtia mkononi mwako, yeye na watu wake wote na nchi yake; nawe utamtenda mfano wa ulivyomtenda Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni. 3 Basi Bwana, Mungu wetu, akamtia mikononi mwetu na Ogu mfalme wa Bashani, na watu wake wote; tukampiga, asisaziwe cho chote. 4 Tukatwaa miji yake yote wakati huo; hapakuwa na mji tusiotwaa kwao miji sitini, nchi yote ya Argobu, ndio ufalme wa Ogu ulio katika Bashani. 5 Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma marefu, na malango, na makomeo, pamoja na miji isiyokuwa na maboma, mingi sana. 6 Tukaiharibu kabisa, kama tulivyomfanya huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, kwa kuharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na watoto. 7 Lakini wanyama wote wa mji, na nyara za miji, tulitwaa kuwa mawindo yetu. 8 Tukaitwaa na nchi wakati huo, katika mikono ya hao wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ng'ambo ya Yordani, tokea bonde la Arnoni mpaka kilima cha Hermoni; 9 (na hiyo Hermoni Wasidoni huiita Sirioni, na Waamori huiita Seniri); 10 miji yote ya nchi tambarare, na Gileadi yote, na Bashani yote, mpaka Saleka na Edrei, nayo ni miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani. 11 (Kwani aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho je! Hakiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni mikono kenda,na upana wake mikono minne,kwa mfano wa mkono wa mtu) 12 Na nchi hiyo tuliitwaa ikawa milki yetu, wakati huo; tokea Aroeri iliyo kwenye bonde la Arnoni, na nusu ya nchi ya milima ya Gileadi, na miji iliyokuwamo, niliwapa Wareubeni na Wagadi; 13 na nchi ya Gileadi iliyobaki, na Bashani yote, maana huo ufalme wa Ogu niliwapa nusu ya kabila ya Manase; nchi yote ya Argobu, nayo ndiyo Bashani yote. (Na nchi hii yaitwa nchi ya Warefai. 14 Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.) 15 Na Makiri nilimpa Gileadi. 16 Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni; 17 na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya matelemko ya Pisga, upande wa mashariki. 18 Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii mwimiliki, basi vukeni ng'ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa. 19 Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa; 20 hata Bwana awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na Bwana, Mungu wenu, ng'ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa. 21 Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda Bwana, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda Bwana kila ufalme huko uvukiako. 22 Msiwache, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye. 23 Nikamnyenyekea Bwana wakati huo, nikamwambia, 24 Ee Bwana Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu? 25 Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng'ambo ya Jordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni. 26 Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; Bwana akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili. 27 Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani. 28 Lakini mwagize Yoshua umtie moyo mkuu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye. 29 Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.

Kumbukumbu la Torati 4

1 Na sasa, Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. 2 Msiliongeze neno niwaamurulo wala msilipunguze, mpate kuzishika amri za Bwana, Mungu wenu, niwaamuruzo. 3 Macho yenu yameona aliyoyatenda Bwana kwa sababu ya Baal-peori; maana wote waliomfuata Baal-peori, Bwana, Mungu wako, amewaangamiza kutoka kati yako. 4 Bali ninyi mlioambatana na Bwana, Mungu wenu, mnaishi kila mmoja wenu, hata leo. 5 Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. 6 Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. 7 Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? 8 Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. 9 Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako; 10 siku ile uliyosimama mbele za Bwana wako huko Horebu, Bwana aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao. 11 Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu. 12 Bwana akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu. 13 Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe. 14 Bwana akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki. 15 Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile Bwana aliyosema nanyi kutoka kati ya moto; 16 msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke, 17 mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni, 18 au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi; 19 tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo Bwana, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote. 20 Bali Bwana amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi. 21 Tena Bwana alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo Bwana, Mungu wenu, iwe urithi. 22 Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema. 23 Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la Bwana, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na Bwana, Mungu wenu, 24 kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu. 25 Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, na kumtia hasira; 26 nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa. 27 Na Bwana atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na Bwana. 28 Na huko mtatumikia miungu, kazi za mikono ya watu, miti na mawe, ambao hawaoni, wala hawasikii, hawali, wala hawanusi. 29 Lakini huko, kama mkimtafuta Bwana, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote. 30 Na wakati uwapo katika mashaka, ukiisha kupatwa na mambo haya yote, siku za mwisho, utamrudia Bwana, Mungu wako, na kuisikiza sauti yake; 31 kwa kuwa Bwana, Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia. 32 Maana uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? 33 Je! Watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? 34 Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu? 35 Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye. 36 Kutoka mbinguni amekusikizisha sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonyesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake toka kati ya moto. 37 Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi, 38 ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nchi yao iwe urithi, kama ilivyo leo. 39 Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. 40 Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele. 41 Ndipo Musa akabagua miji mitatu ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua; 42 ili kwamba amwuaye mtu apate kukimbilia huko, amwuaye jirani yake pasipo kujua, wala hakumchukia tangu hapo; ili apate kuishi akimbiliapo mmojawapo miji hiyo; 43 nayo ni hii, Beseri ya barani iliyo katika nchi tambarare, kwa Wareubeni; na Ramothi iliyo Gileadi, kwa Wagadi; na Golani iliyo Bashani, kwa Wamanase. 44 Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii; 45 haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri; 46 ng'ambo ya Yordani, katika bonde lililoelekea Beth-peori, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni ndiye aliyepigwa na Musa na wana wa Israeli, walipotoka Misri; 47 wakaishika nchi yake, ikawa milki yao, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, ndio wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa ng'ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua; 48 toka Aroeri, iliyo juu ya ukingoni pa bonde la Arnoni, hata mpaka mlima wa Sioni (nao ndio Hermoni), 49 na Araba yote iliyo ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, hata mpaka bahari ya Araba, chini ya matelemko ya Pisga.

Kumbukumbu la Torati 5

1 Musa akawaita Israeli wote, akawaambia, Enyi Israeli, zisikieni amri na hukumu ninenazo masikioni mwenu leo, mpate kujifunza na kuangalia kuzitenda. 2 Bwana, Mungu wetu, alifanya agano nasi katika Horebu. 3 Bwana hakufanya agano hili na baba zetu, bali na sisi, yaani, sisi sote tuliopo hapa, tu hai. 4 Bwana alisema nanyi uso kwa uso mlimani, toka kati ya moto; 5 (nami wakati ule nalisimama kati ya Bwana na ninyi, ili kuwaonyesha neno la Bwana; maana, mliogopa kwa sababu ya ule moto, wala hamkupanda mlimani); naye akasema, 6 Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 7 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 8 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi. 9 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 10 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. 11 Usilitaje bure Jina la Bwana, Mungu wako; maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia, mtu alitajaye jina lake bure. 12 Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru. 13 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 14 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako ye yote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vile vile kama wewe. 15 Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike sabato. 16 Waheshimu baba yako na mama yako; kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru, siku zako zipate kuzidi, nawe upate kufanikiwa katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. 17 Usiue. 18 Wala usizini. 19 Wala usiibe. 20 Wala usimshuhudie jirani yako uongo. 21 Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako. 22 Haya ndiyo maneno ambayo Bwana aliwaambia mkutano wenu wote mlimani kwa sauti kuu toka kati ya moto, na wingu, na giza kuu; wala hakuongeza neno. Akayaandika juu ya mbao mbili za mawe, akanipa. 23 Ikawa, mlipoisikia sauti ile toka kati ya giza, na wakati uo huo mlima ule ulikuwa ukiwaka moto, basi, mlinikaribia, naam, wakuu wote wa kabila zenu, na wazee wenu, 24 mkasema, Tazama, Bwana, Mungu wetu, ametuonyesha utukufu wake, na ukuu wake, nasi tunasikia sauti yake toka kati ya moto; mmeona leo ya kuwa Mungu husema na mwanadamu, naye akaishi. 25 Sasa basi, mbona tufe? Maana moto huu mkubwa utatuteketeza; tukiisikia tena sauti ya Bwana, Mungu wetu, tutakufa. 26 Maana katika wote wenye mwili ni nani aliyeisikia sauti ya Mungu aliye hai, akisema toka kati ya moto, kama vile sisi, asife? 27 Enenda karibu wewe, ukasikie yote atakayoyasema Bwana, Mungu wetu; ukatuambie yote atakayokuambia Bwana, Mungu wetu; nasi tutayasikia na kuyatenda. 28 Naye Bwana akasikia sauti ya maneno yenu mliyoniambia; Bwana akaniambia, Nimesikia sauti ya maneno ya watu hawa waliyokuambia; wamesema vema yote waliyosema. 29 Laiti wangekuwa na moyo kama huu ndani yao sikuzote, wa kunicha, na kushika amri zangu zote sikuzote, wapate kufanikiwa wao na watoto wao milele! 30 Enda uwaambie, Rudini hemani mwenu. 31 Lakini wewe, simama hapa karibu nami, nami nitanena nawe sheria zote, na amri na hukumu, utakazowafunza, wapate kuzifanya katika nchi niwapayo kuimiliki. 32 Tunzeni basi, mtende kama mlivyoamriwa na Bwana, Mungu wenu; msikengeuke kwa mkono wa kuume wala wa kushoto. 33 Endeni njia yote aliyowaagiza Bwana, Mungu wenu, mpate kuwa hai, na kufanikiwa, mkafanye siku zenu kuwa nyingi katika nchi mtakayoimiliki.

Kumbukumbu la Torati 6

1 Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru Bwana, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki; 2 upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. 3 Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. 4 Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. 5 Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. 6 Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; 7 nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. 8 Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. 9 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. 10 Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, 11 na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; 12 ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. 13 Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. 14 Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; 15 kwani Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya Bwana, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi. 16 Msimjaribu Bwana, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. 17 Zishikeni kwa bidii sheria za Bwana, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza. 18 Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa Bwana; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia baba zako, 19 ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema Bwana. 20 Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N'nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza Bwana, Mungu wetu? 21 Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; Bwana, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; 22 Bwana akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; 23 akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu. 24 Bwana akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche Bwana, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. 25 Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya Bwana, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.

Kumbukumbu la Torati 7

1 Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; 2 wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao; 3 binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake. 4 Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. 5 Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. 6 Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi. 7 Bwana hakuwapenda ninyi, wala hakuwachagua ninyi, kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote; 8 bali kwa sababu Bwana anawapenda, na kwa sababu alitaka kuutimiza uapo wake aliowaapia baba zenu, ndiyo sababu Bwana akawatoa kwa mkono wa nguvu, akawakomboa katika nyumba ya utumwa, katika mkono wa Farao, mfalme wa Misri. 9 Basi jueni ya kuwa Bwana, Mungu wenu, ndiye Mungu; Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu; 10 naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao, kuwaangamiza. Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake. 11 Basi zishike amri, na sheria, na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende. 12 Na itakuwa, kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi, na kuzishika na kuzitenda, basi Bwana, Mungu wako, atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako; 13 naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena ataubarikia uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, nafaka zako na divai yako, na mafuta yako, maongeo ya ng'ombe zako, na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atakupa. 14 Utabarikiwa kuliko mataifa yote; hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu; wala kati ya wanyama wenu wa mifugo. 15 Na Bwana atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao. 16 Nawe angamiza mataifa yote atakayokupa Bwana, Mungu wako; jicho lako lisiwahurumie, wala usiitumikie miungu yao; kwani litakuwa ni mtego kwako jambo hilo. 17 Nawe kama ukisema moyoni mwako, Mataifa haya ni mengi kunipita mimi; nitawatoaje katika milki yao? 18 Usiwaogope; kumbuka sana Bwana, Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote; 19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyoka, aliokutolea nje Bwana, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya Bwana, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa. 20 Tena Bwana, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako. 21 Usiingiwe na kicho kwa sababu yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu katikati yako, Mungu mkuu, mwenye utisho. 22 Naye Bwana, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu. 23 Ila Bwana, Mungu wako, atawatoa mbele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa. 24 Na wafalme wao atakutilia mkononi mwako, nawe utalipoteza jina lao litoke chini ya mbingu; hapana mtu atakayeweza kusimama mbele yako, hata utakapokwisha kuwaangamiza. 25 Sanamu za kuchonga za miungu yao mtaziteketeza kwa moto; usitamani fedha wala dhahabu iliyo juu yao, wala usiitwae iwe yako usije ukanaswa nayo; kwa maana ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako; 26 na machukizo usitie ndani ya nyumba yako, usije wewe kuwa kitu cha haramu mfano wake; ukichukie kabisa, na kukikataa kabisa; kwa kuwa ni kitu kilichoharimishwa.

Kumbukumbu la Torati 8

1 Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki. 2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo. 3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana. 4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini. 5 Nawe fikiri moyoni mwako, ya kuwa kama vile baba amrudivyo mwanawe, ndivyo Bwana, Mungu wako, akurudivyo. 6 Nawe uzishike amri za Bwana, Mungu wako, upate kwenda katika njia zake, na kumcha. 7 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuakuingiza katika nchi nzuri, nchi yenye vijito vya maji, na chemchemi, na visima, vibubujikavyo katika mabonde na milima; 8 nchi ya ngano na shayiri, na mizabibu, na mitini, na mikomamanga; nchi ya mizeituni yenye mafuta, na asali; 9 nchi utakayokula mikate humo, pasina shida, hutapungukiwa na kitu ndani yake; nchi ambayo mawe yake ni chuma, na milima yake yafukuka shaba. 10 Nawe utakula ushibe, utamshukuru Bwana, Mungu wako, kwa nchi nzuri aliyokupa. 11 Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo. 12 Angalia, utakapokuwa umekula na kushiba, na kujenga nyumba nzuri na kukaa ndani yake; 13 na makundi yako ya ng'ombe na kondoo yatakapoongezeka, na fedha yako na dhahabu yako itakapoongezeka, na kila kitu ulicho nacho kitakapoongezeka; 14 basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau Bwana, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa; 15 aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji; aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, 16 aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako; apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. 17 Hapo usiseme moyoni mwako, Nguvu zangu na uwezo wa mkono wangu ndio ulionipatia utajiri huo. 18 Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo. 19 Lakini itakuwa, kama ukimsahau Bwana, Mungu wako, na kuiandama miungu mingine, na kuitumikia na kuiabudu, nawashuhudia leo ya kuwa mtaangamia bila shaka. 20 Kama vile mataifa yale ambayo Bwana anawaangamiza mbele yenu, ndivyo mtakavyoangamia; kwa sababu hamkutaka kuisikiliza sauti ya Bwana, Mungu wenu.

Kumbukumbu la Torati 9

1 Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni, 2 watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? 3 Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana. 4 Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako. 5 Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. 6 Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu. 7 Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana 8 Tena mlimkasirisha Bwana katika Horebu, Bwana akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza. 9 Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. 10 Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano. 11 Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Bwana alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano. 12 Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. 13 Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; 14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao. 15 Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. 16 Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru Bwana. 17 Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu. 18 Nikaanguka nchi mbele za Bwana siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kwa kumkasirisha. 19 Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia Bwana kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiza wakati huo nao. 20 Bwana akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo. 21 Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani. 22 Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia Bwana hasira. 23 Na wakati alipowatuma Bwana kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya Bwana, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake. 24 Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi. 25 Ndipo nikaanguka nchi mbele za Bwana siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa Bwana alisema atawaangamiza. 26 Nikamwomba Bwana, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu. 27 Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao; 28 isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani. 29 Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka.

Kumbukumbu la Torati 10

1 Wakati ule Bwana akaniambia, Chonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, kisha uje kwangu huku mlimani, ukajifanyie na sanduku la mti. 2 Nami nitaandika juu ya hizo mbao maneno hayo yaliyokuwa juu ya mbao za kwanza, ulizozivunja, nawe uzitie ndani ya hilo sanduku. 3 Basi nikafanya sanduku la mti wa mshita, nikachonga mbao mbili za mawe mfano wa zile za kwanza, nikakwea mle mlimani, na zile mbao mbili mkononi mwangu. 4 Naye akaandika juu ya mbao mfano wa maandiko ya kwanza, zile amri kumi, alizowaambia Bwana huko mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano; Bwana akanipa. 5 Basi nikageuka nikashuka kutoka mlimani, nikazitia mbao ndani ya sanduku nililofanya; nazo zimo humo kama alivyoniamuru Bwana. 6 (Wana wa Israeli wakasafiri kutoka visima vya Bene-Yaakani kwenda Mosera; Haruni akafa huko, akazikwa huko; na Eleazari mwanawe alitumika utumishi wa ukuhani badala yake. 7 Wakasafiri kutoka huko kwenda Gudgoda; wakatoka Gudgoda wakaenda Yotbatha, nayo ni nchi ya vijito vya maji. 8 Na wakati huo Bwana aliitenga kabila ya Lawi ili walichukue lile sanduku la agano la Bwana, wasimame mbele ya Bwana kwa kumtumikia, na kuwabarikia watu kwa jina lake, hata hivi leo. 9 Ndipo asiwe na fungu Lawi, wala urithi pamoja na nduguze; Bwana ndiye urithi wake, kwa mfano wa vile alivyomwambia Bwana, Mungu wako.) 10 Nikakaa mle mlimani kama hapo kwanza, siku arobaini usiku na mchana; Bwana akanisikiza wakati huo nao; asitake Bwana kukuangamiza. 11 Bwana akaniambia, Ondoka, ushike safari yako mbele ya watu; nao wataingia waimiliki nchi, niliyowaapia baba zao ya kuwa nitawapa. 12 Na sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; 13 kuzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri? 14 Tazama, mbingu ni mali za Bwana, Mungu wako, na mbingu za mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo. 15 Tena, Bwana aliwafurahia baba zako, na kuwapenda, akawachagua wazao wao baada yao, naam, na ninyi zaidi ya mataifa yote kama hivi leo. 16 Basi, zitahirini govi za mioyo yenu, wala msiwe na shingo ngumu. 17 Kwa maana Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa. 18 Huwafanyia yatima na mjane hukumu ya haki, naye humpenda mgeni, akimpa chakula na mavazi. 19 Basi, mpendeni mgeni, kwa sababu ninyi wenyewe mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. 20 Mche Bwana, Mungu wako, umtumikie yeye; ambatana naye, na kuapa kwa jina lake. 21 Yeye ndiye fahari yako, na yeye ndiye Mungu wako, aliyekutendea mambo haya makubwa, ya kutisha, uliyoyaona kwa macho yako. 22 Baba zako walishukia Misri na watu sabini; na sasa Bwana, Mungu wako, amekufanya kama nyota za mbinguni kwa wingi.

Kumbukumbu la Torati 11

1 Kwa ajili hii mpende Bwana, Mungu wako, na kushika sikuzote mausia yake, na amri zake, na hukumu zake, na maagizo yake. 2 Nanyi leo jueni; kwa kuwa sisemi sasa na vijana vyenu, ambao hawakujua, wala hawakuona adhabu ya Bwana, Mungu wenu, ukuu wake, na mkono wake wa nguvu, na mkono wake ulionyoka, 3 na ishara zake, na kazi zake alizomfanya Farao mfalme wa Misri, na nchi yake yote, katikati ya Misri; 4 na alivyolifanya jeshi la Misri, farasi zao, na magari yao; na alivyowafunikiza maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwaandamia, na alivyowaangamiza Bwana hata hivi leo; 5 na mambo aliyowafanyia ninyi barani, hata mkaja mahali hapa; 6 na alivyowafanya Dathani, na Abiramu, wana wa Eliabu mwana wa Reubeni; nchi ilivyofunua kinywa chake, ikawameza, na walio nyumbani mwao, na mahema yao, na kila kitu kilichokuwa hai kikiwafuata, katikati ya Israeli yote; 7 lakini macho yenu yameiona kazi kubwa ya Bwana aliyoifanya, yote. 8 Kwa hiyo yaangalieni maagizo yote niwaagizayo leo, mpate kuwa na nguvu, na kuingia mkaimiliki nchi mwivukiayo kuimiliki; 9 nanyi mpate kuzifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, ya kuwa atawapa wao na kizazi chao, nchi imiminikayo maziwa na asali 10 Kwa kuwa nchi mwingiayo kuimiliki, si mfano wa nchi ya Misri mlikotoka, uliyokuwa ukipanda mbegu zako humo na kuinywesheleza kwa mguu wako, kama shamba la mboga; 11 lakini nchi mwivukiayo kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua ya mbinguni; 12 nayo ni nchi itunzwayo na Bwana, Mungu wako; macho ya Bwana Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka. 13 Tena itakuwa, mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote, 14 ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako. 15 Nami nitakupa nyasi katika mavue yako kulisha wanyama wako wa mifugo, nawe utakula na kushiba. 16 Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu; 17 hasira za Bwana zikawaka juu yenu, naye akafunga mbingu kusiwe na mvua, wala nchi isitoe matunda yake; mkaangamia kwa upesi mtoke katika nchi nzuri awapayo Bwana. 18 Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu. 19 Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. 20 Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako; 21 ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi Bwana aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi. 22 Kwa kuwa kwamba mtayashika kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye; 23 ndipo Bwana atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuwapita ninyi. 24 Kila mahali mtakapokanyaga kwa nyayo za miguu yenu patakuwa penu; tokea hilo jangwa, na Lebanoni, na tokea mto wa Frati, mpaka bahari ya magharibi, itakuwa ndiyo mipaka yenu. 25 Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; Bwana, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia. 26 Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; 27 baraka ni hapo mtakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo; 28 na laana ni hapo msiposikiza maagizo ya Bwana, Mungu wenu, mkikengeuka katika njia niwaagizayo leo, kwa kuandama miungu mingine msiyoijua. 29 Tena itakuwa, atakapokuleta Bwana, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali. 30 Je! Haiwi ng'ambo ya Yordani? Nyuma ya njia ya machweo ya jua, katika nchi ya Wakanaani waketio katika Araba kuelekea Gilgali, kando ya hiyo mialoni ya More? 31 Kwani ninyi mtavuka Yordani mwingie kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, nanyi muimiliki na kuketi humo. 32 Nanyi angalieni mzifanye amri na hukumu zote niwawekeazo leo mbele yenu.

Kumbukumbu la Torati 12

1 Hizi ndizo amri na hukumu mtakazotunza kuzifanya katika nchi aliyokupa Bwana, Mungu wa baba zako, uimiliki, siku zote mtakazoishi juu ya nchi. 2 Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; 3 nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo. 4 Wala msimfanyie hivyo Bwana, Mungu wenu. 5 Lakini mahali atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; 6 pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo; 7 na huko mtakula mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi furahini katika yote mtakayotia mikono yenu, ninyi na wa nyumbani mwenu, aliyokubarikia Bwana, Mungu wako. 8 Msifanye kwa kufuata mambo yote tuyafanyayo hapa leo, kila mtu kama aonavyo vema machoni pake; 9 kwani hamjafikilia bado katika raha na urithi akupao Bwana, Mungu wako. 10 Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha Bwana, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama; 11 wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana. 12 Nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu. 13 Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo; 14 bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo. 15 Pamoja na haya waweza kuchinja nyama na kula ndani ya malango yako yote, kwa kufuata yote yatamaniwayo na roho yako, kwa mfano wa baraka ya Bwana, Mungu wako, aliyokupa; aliye tohara na asiye tohara ana ruhusa kula katika nyama hiyo, kama ya paa na ya kulungu. 16 Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji. 17 Usile ndani ya malango yako zaka ya nafaka zako, wala ya divai yako, wala ya mafuta yako, wala wazaliwa wa kwanza wa makundi yako, ya ng'ombe wala ya kondoo, wala nadhiri zako uwekazo zo zote, wala sadaka zako za hiari, wala sadaka ya kuinuliwa ya mkono wako; 18 lakini hivyo mtakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, wewe, na mwanao mume na mke, na mtumwa wako mume na mke, na Mlawi aliye ndani ya malango yako; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako, katika yote utakayotia mkono wako. 19 Jilinde nafsi yako usimwache Mlawi siku zote uishizo katika nchi yako. 20 Bwana, Mungu wako, atakapoongeza mpaka wako, kama alivyokuahidi, nawe utakaposema, Nataka kula nyama, kwa kuwa roho yako yatamani kula nyama; waweza kula nyama, kwa kufuata yote inayotamani roho yako. 21 Na mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apaweke jina lake, pakiwa mbali nawe mno, ndipo utakapochinja katika kundi lako la ng'ombe na kondoo alilokupa Bwana kama nilivyokuagiza, nawe utakula ndani ya malango yako, kwa kufuata yote inayotamani roho yako. 22 Kama vile aliwavyo paa na kulungu, ndivyo utakavyoila nyama hii; asiyekuwa tohara na aliye tohara wataila pia. 23 Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama. 24 Usiile; imwage juu ya nchi kama maji. 25 Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa Bwana. 26 Ila vitu vyako vitakatifu ulivyo navyo, na nadhiri zako, uvitwae ukaende mahali atakapochagua Bwana; 27 nawe zisongeze sadaka zako za kuteketezwa, nyama na damu, juu ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako; na damu ya dhabihu zako uimwage juu ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako, na wewe utakula nyama yake. 28 Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa Bwana, Mungu wako. 29 Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa mbele yako, huko uingiako kuyamiliki, nawe ukawatwaa, na kuketi katika nchi yao; 30 ujiangalie, usije ukanaswa ukawafuata, wakiisha kuangamizwa mbele yako; wala usije ukauliza habari za miungu yao, ukisema, Mataifa haya waitumikiaje miungu yao? Nami nifanye vivyo. 31 Usimtende kama haya Bwana, Mungu wako; kwani kila yaliyo machukizo kwa Bwana, ayachukiayo yeye, wameifanyia miungu yao; kwa maana hata wana wao na binti zao huiteketezea hiyo miungu yao ndani ya moto. 32 Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze.

Kumbukumbu la Torati 13

1 Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, 2 ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; 3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote. 4 Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye. 5 Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya Bwana, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru Bwana, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako. 6 Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako; 7 katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; 8 usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche; 9 mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote. 10 Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na Bwana, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 11 Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako. 12 Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo Bwana, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa, 13 Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua; 14 ndipo nawe uulize na kutafuta, ukiuliza kwa bidii; nawe angalia, ikiwa kweli, na jambo lile halina shaka, kwamba machukizo mfano wa haya yafanyika katikati yako; 15 hakika yako uwapige wenyeji wa mji ule kwa makali ya upanga, kwa kuwaangamiza kabisa, pamoja na vitu vyote vilivyomo, na wanyama walio humo, kwa makali ya upanga. 16 Na nyara zake zote uzikusanyie katikati ya njia yake; na mji uuteketeze kwa moto, na nyara zake zote, kuwe sadaka kamili ya kuteketezwa kwa Bwana, Mungu wako; nao utakuwa magofu milele; usijengwe tena. 17 Kisishikamane na mkono wako kitu cho chote katika kitu kilichoharimishwa; ili ageuke Bwana na ukali wa hasira zake akurehemu, akuonee huruma, na kukufanya kuwa wengi, kama alivyowaapia baba zako; 18 utakaposikiza sauti ya Bwana, Mungu wako kwa kushika maagizo yake yote nikuagizayo leo, ufanye yaliyoelekea machoni pa Bwana, Mungu wako.

Kumbukumbu la Torati 14

1 Ninyi mmekuwa wana wa Bwana, Mungu wenu; msijitoje miili yenu, wala msifanye upaa katikati ya macho yenu kwa ajili ya aliyekufa. 2 Kwa kuwa u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, na Bwana amekuchagua kuwa watu wake hasa, kuliko mataifa yote yaliyo juu ya uso wa nchi. 3 Usile kitu cho chote kichukizacho. 4 Wanyama mtakaokula ni hawa ng'ombe, na kondoo, na mbuzi, 5 kulungu, na paa, na kongoni, na mbuzi wa mwitu, na paa mweupe, na pofu, na mbuzi wa mlima; 6 na kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, ukapasuka ukwato wake zikawa mbili, naye ni mnyama mwenye kucheua akatafuna tena, katika wanyama wote, ndiye mnyama mtakayemla. 7 Lakini, hawa msile katika wale wenye kucheua, na hao waliopasuliwa ukwato; ngamia, na sungura, na kwang'a, kwa kuwa hucheua, lakini hawakupasuliwa kwato, ni najisi kwenu; 8 na nguruwe, kwa kuwa amepasuliwa ukwato lakini hacheui, huyu ni najisi kwenu msile nyama zao, wala mizoga yao msiiguse. 9 Mtakula hawa katika wote walio majini; kila kilicho na mapezi na magamba mtakula; 10 na kila kisichokuwa na mapezi na magamba msile; ni najisi kwenu. 11 Mna ruhusa kula katika nyuni wote walio safi. 12 Lakini hawa msiwale; tai, na furukombe, na kipungu; 13 na kengewa, na kozi, na mwewe kwa aina zake; 14 na kila kunguru kwa aina zake; 15 na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake; 16 na bundi, na mumbi, na bundi mkubwa; 17 na mwari, na nderi, na mnandi; 18 na membe, na koikoi, kwa aina zake; na hudihudi, na popo. 19 Na wadudu wote watambaao wenye mabawa ni najisi kwenu; msiwale. 20 Mna ruhusa kula katika nyuni wote walio safi. 21 Msile nyamafu yo yote; waweza kumpa mgeni aliye ndani ya malango yako, ili apate kula; au kumliza mtu wa mataifa; kwa kuwa wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mamaye. 22 Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka. 23 Nawe utakula mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua apakalishe jina lake, zaka ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yako ya ng'ombe na ya kondoo; ili upate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wako, daima. 24 Na njia ikiwa ndefu mno nawe, usiweze kuzichukua kwa kuwa mahali ni mbali nawe mno atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, hapo atakapokubarikia Bwana, Mungu wako; 25 ndipo uzibadili ziwe fedha, na kufunga zile fedha uende nazo mkononi mwako, hata mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako; 26 na zile fedha zitumie kwa cho chote itakachotamani roho yako, ng'ombe, au kondoo, au divai, au kileo, au roho yako itakacho kwako cho chote; nawe utakula huko mbele za Bwana, Mungu wako; tena furahi, wewe na nyumba yako; 27 na Mlawi aliye ndani ya malango yako usimwache, kwani hana fungu wala urithi pamoja nawe. 28 Kila mwaka wa tatu, mwisho wake, toa fungu la kumi lote la maongeo yako ya mwaka huo, uliweke ndani ya malango yako; 29 na Mlawi kwa kuwa hana fungu wala urithi pamoja nawe, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako, na waje wale na kushiba; ili kwamba Bwana, Mungu wako, akubarikie katika kazi yote ya mkono wako uifanyayo.

Kumbukumbu la Torati 15

1 Kila miaka saba, mwisho wake, fanya maachilio. 2 Na jinsi ya maachilio ni hii, kila mkopeshaji na akiache alichomkopesha mwenziwe, wala asimlipize mwenziwe wala nduguye; kwa kuwa imepigwa mbiu ya maachilio ya Bwana. 3 Waweza kumtoza mgeni; lakini kila uwiacho kwa nduguyo mkono wako utamwachilia. 4 Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa Bwana atakubarikia kweli katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;) 5 kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya. 6 Kwani Bwana, Mungu wako, atakubarikia, kama alivyokuahidi; nawe utakopesha mataifa mengi, lakini hutakopa; tena utayatawala mataifa mengi, usitawaliwe na wao. 7 Kama akiwapo mtu maskini pamoja nawe, nduguzo mmojawapo, ndani ya malango yako mojawapo, katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, usifanye moyo wako kuwa mgumu, wala usimfumbie mkono wako nduguyo maskini; 8 lakini mfumbulie mkono wako kwa kweli, umkopeshe kwa kweli yatoshayo haja yake katika ahitajiayo. 9 Jitunze, msiwe na neno lisilofaa moyoni mwako, kusema, Umekaribia mwaka wa saba, mwaka wa maachilio; jicho lako likawa ovu juu ya nduguyo usimpe kitu; naye akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako. 10 Mpe kwa kweli, wala moyo wako usisikitike utakapompa; kwa kuwa atakubarikia Bwana, Mungu wako, kwa neno hili katika kazi yako yote, na katika kila utakalotia mkono wako. 11 Kwa maana maskini hawatakoma katika nchi milele; ndipo ninakuamuru na kukuambia, Mfumbulie kwa kweli mkono wako nduguyo, mhitaji wako, maskini wako, katika nchi yako. 12 Ikiwa nduguyo, mume wa Kiebrania, au mwanamke wa Kiebrania, akiuzwa kwako, naye amekutumikia miaka sita; basi mwaka wa saba mwache huru aondoke kwako. 13 Nawe utakapomwacha huru aondoke kwako, usimwache aende zake mikono mitupu; 14 umwangalie kwa wema katika kundi lako, na sakafu yako ya nafaka, na kinu chako cha divai; mpe kama alivyokubarikia Bwana, Mungu wako. 15 Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, akakukomboa Bwana, Mungu wako; kwa hiyo mimi nakuamuru neno hili hivi leo. 16 Hata itakuwa, akikuambia, Siondoki kwako; kwa sababu akupenda wewe na nyumba yako, kwa kuwa yu hali njema kwako; 17 ndipo utwae uma, uupenyeze katika sikio lake uingie katika ubao wa mlango, naye atakuwa mtumishi wako milele. Na kijakazi chako naye mfanye vivyo. 18 Wala usione ugumu, utakapomwacha huru kuondoka kwako; kwani amekutumikia miaka sita kwa ujira mara mbili wa mwajiriwa; na Bwana, Mungu wako, atakubarikia kwa yote utakayofanya. 19 Wazaliwa wa kwanza waume wote wazaliwao katika kundi lako la ng'ombe na la kondoo, uwatakase kwa Bwana, Mungu wako; usifanye kazi kwa mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wako, wala usimkate manyoya mzaliwa wa kwanza wa kundi lako la kondoo. 20 Utamla mbele za Bwana, Mungu wako, mwaka hata mwaka mahali atakapochagua Bwana, wewe na nyumba yako. 21 Lakini akiwa na kilema, akichechea, au akiwa kipofu, au mwenye kilema kibaya cho chote, usimsongezee Bwana, Mungu wako, sadaka. 22 Utamla ndani ya malango yako; wasio tohara na wenye tohara pia watakula, kama unavyokula paa na kulungu. 23 Pamoja na haya usile damu yake; uimwage nchi kama maji.

Kumbukumbu la Torati 16

1 Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie pasaka Bwana, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku Bwana; Mungu wako. 2 Nawe umchinjie pasaka Bwana, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua Bwana apakalishe jina lake. 3 Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako. 4 Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale cho chote usiku kucha hata asubuhi. 5 Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo Bwana, Mungu wako; 6 ila mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri. 7 Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako. 8 Siku sita utakula mikate isiyotiwa chachu; na siku ya saba na uwe mkutano mtukufu kwa Bwana, Mungu wako, usifanye kazi yo yote. 9 Jihesabie majuma saba; tangu wakati uanzao kutia mundu katika mmea utaanza kuhesabu majuma saba. 10 Nawe sikukuu ya majuma umfanyie Bwana, Mungu wako, kwa kutoa sadaka ya hiari ya mkono wako, utakayotoa kwa kadiri akubarikiavyo Bwana, Mungu wako; 11 nawe utafurahi mbele ya Bwana, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako, apakalishe jina lake. 12 Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa huko Misri; tena zishike amri hizi kwa kuzifanya. 13 Fanya sikukuu ya vibanda siku saba, utakapokwisha kuyakusanya yatokayo katika sakafu yako ya nafaka, na katika kinu chako cha divai; 14 nawe utafurahi katika sikukuu yako, wewe, na mwanao, na binti yako, na mtumwa wako, na mjakazi wako, na Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako. 15 Siku saba mfanyie sikukuu Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua Bwana; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, atakubarikia katika maongeo yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa. 16 Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu. 17 Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa. 18 Weka waamuzi na maakida katika malango yako yote akupayo Bwana, Mungu wako, kwa hesabu ya kabila zako; nao wawaamue watu kwa maamuzi ya haki. 19 Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; wala usitwae rushwa; kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. 20 Yaliyo haki kabisa ndiyo utakayoyafuata, ili upate kuishi na kuirithi nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. 21 Usipande mti uwao wote kuwa Ashera kwako kando ya madhabahu utakayofanya ya Bwana, Mungu wako. 22 Wala usisimamishe nguzo; ambayo Bwana, Mungu wako, aichukia.

Kumbukumbu la Torati 17

1 Usimchinjie Bwana, Mungu wako, ng'ombe wala kondoo aliye na kilema, wala neno ovu lo lote; kwa kuwa hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako. 2 Ikiwa ameonekana katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, upewayo na Bwana, Mungu wako, mtu mume au mke afanyaye yaliyo maovu machoni pa Bwana, Mungu wako, kwa kuvunja maagano yake, 3 naye amekwenda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, au jua, au mwezi, au vilivyo katika jeshi la mbinguni vyo vyote, nisivyoagiza mimi; 4 ukiambiwa hayo nawe umeyasikia, ndipo utafute kwa bidii, na tazama, ikiwa ni kweli lina hakika jambo lile, kuwa yafanywa machukizo kama hayo katika Israeli; 5 ndipo umchukue nje malangoni kwako, yule mtu mume, au yule mwanamke, aliyefanya jambo lile ovu; ukawapige kwa mawe, wafe. 6 Huyo atakayeuawa na auawe kwa midomo ya mashahidi wawili, au mashahidi watatu; asiuawe kwa mdomo wa shahidi mmoja. 7 Mikono ya wale mashahidi na iwe juu yake kwanza kwa kumwua, kisha mikono ya watu wote. Uondoe vivyo uovu katikati yako. 8 Ikiwa limezuka neno lililo zito kukupita wewe, katika maamuzi kati ya damu na damu, na kati ya daawa na daawa, na kati ya pigo na pigo, nayo yashindaniwa katika malango yako; ndipo nawe uondoke, ukwee uende mahali atakapochagua Bwana, Mungu wako; 9 uwaendee makuhani Walawi, na mwamuzi atakayekuwako siku hizo; uwaulize; nao watakuonyesha hukumu ya maamuzi; 10 nawe fanya sawasawa na hukumu watakayokuonyesha mahali hapo atakapochagua Bwana; nawe tunza kufanya kwa mfano wa yote watakayokufunza; 11 kwa mfano wa sheria watakayokufunza, na kwa mfano wa hukumu watakayokuambia, fanya vivyo; usigeuke katika hukumu watakayokuonyesha, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto. 12 Na mtu afanyaye kwa kujikinai, kwa kutomsikiza kuhani asimamaye hapo kwa kumtumikia Bwana, Mungu wako, au mwamuzi, na afe mtu huyo; nawe utauondoa uovu katika Israeli. 13 Na hao watu wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena kwa kujikinai. 14 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kando-kando yangu; 15 usiache kumweka yule atakayechaguliwa na Bwana, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako. 16 Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa Bwana amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile. 17 Wala asijizidishie wake, ili moyo wake usikengeuke; wala asifanye fedha zake na dhahabu kuwa nyingi mno. 18 Tena na iwe, zamani aketipo juu ya kiti cha ufalme wake, ajiandikie nakala ya torati hii katika chuo, kufuata hicho kilicho mbele ya makuhani Walawi; 19 na awe nayo, asome humo siku zote atakazoishi; ili apate kujifunza kumcha Bwana, Mungu wake, ayashike maneno yote ya torati hii na amri hizi, kwa kuyafanya; 20 moyo wake usije ukainuliwa juu ya ndugu zake, wala asikengeuke katika maagizo, kwa mkono wa kuume wala wa kushoto; ili apate kuzifanya siku zake kuwa nyingi katika ufalme wake, yeye na wanawe, katikati ya Israeli.

Kumbukumbu la Torati 18

1 Makuhani Walawi, kabila yote ya Lawi, wasiwe na fungu wala urithi pamoja na Israeli; watakula sadaka za Bwana zifanywazo kwa moto, na urithi wake. 2 Wala wasiwe na urithi kati ya ndugu zao; Bwana ndiye urithi wao, kama alivyowaambia. 3 Na hii itakuwa haki ya makuhani kwa watu hao wasongezao sadaka, ikiwa ni ng'ombe au kondoo wampe kuhani mkono, na mashavu mawili, na tumbo. 4 Malimbuko ya nafaka zako, na divai yako, na mafuta yako, na manyoya ya kwanza ya kondoo zako, umpe. 5 Kwani Bwana, Mungu wako, amemchagua katika kabila zako zote, asimame atumike kwa jina la Bwana, yeye na wanawe milele. 6 Na akija Mlawi atokaye katika malango yako mojawapo, katika Israeli yote alipokuwa akikaa, akaja kwa mapenzi yote ya nafsi yake mahali atakapochagua Bwana; 7 na atumike kwa jina la Bwana, Mungu wake, kama wafanyavyo ndugu zake wote, Walawi wasimamao huko mbele za Bwana. 8 Wawe na fungu sawasawa la kula, pamoja na haya yaliyomfikilia kwa kuuzwa urithi wa baba zake. 9 Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. 10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, 11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. 12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. 13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako. 14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo. 15 Bwana, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye. 16 Kama vile ulivyotaka kwa Bwana, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya Bwana, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa. 17 Bwana akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema. 18 Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru. 19 Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake. 20 Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa. 21 Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena Bwana? 22 Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope

Kumbukumbu la Torati 19

1 Bwana, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao; 2 itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki. 3 Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo Bwana, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko. 4 Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo; 5 kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai; 6 asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo. 7 Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu. 8 Na kama Bwana, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako; 9 nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda Bwana, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile; 10 isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako. 11 Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo; 12 ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumuua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa. 13 Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa. 14 Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki. 15 Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu. 16 Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe; 17 ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za Bwana, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo; 18 nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye; 19 ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. 20 Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako. 21 Wala jicho lako lisiwe na huruma; uzima kwa uzima, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu.

Kumbukumbu la Torati 20

1 Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa Bwana Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. 2 Na iwe, msongeapo mapiganoni, kuhani na akaribie na kusema na watu, 3 awaambie, Sikizeni, enyi Israeli, hivi leo mwasongea mapiganoni juu ya adui zenu mioyo yenu na isizime; msiche, wala msiteteme, wala msiingiwe na hofu kwa ajili ya wao; 4 kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi. 5 Na maakida na waseme na watu, na kuwaambia, Ni mtu gani aliye hapa aliyejenga nyumba mpya, wala hajaiweka wakfu? Aende akarudi nyumbani kwake, asije akafa mapiganoni, ikawekwa wakfu na mtu mwingine. 6 Ni mtu gani aliye hapa aliyepanda shamba la mizabibu, wala hajatumia matunda yake? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, yakatumiwa na mtu mwingine matunda yake. 7 Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine. 8 Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake. 9 Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu. 10 Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani. 11 Itakuwa utakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa, na kukutumikia. 12 Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru; 13 na Bwana, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga; 14 lakini wanawake na watoto, na wanyama wa miji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa Bwana, Mungu wako. 15 Utaifanyia vivyo miji yote iliyo mbali sana nawe, isiyokuwa miji ya mataifa haya. 16 Lakini katika miji ya mataifa haya akupayo Bwana, Mungu wako, kuwa urithi, usihifadhi kuwa hai kitu cho chote kipumzikacho; 17 lakini uwaangamize kabisa, Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, kama alivyokuamuru Bwana, Mungu wako; 18 wasije wakawafunza kufanya mfano wa machukizo yao yote, waliyoifanyia miungu yao; hivyo itakuwa ni makosa juu ya Bwana, Mungu wenu. 19 Wewe utakapohusuru mji siku nyingi kwa kufanya vita juu yake, upate kuutwaa, usiangamize miti yake kwa kupeleka shoka juu yake, kwani utaweza kula matunda yake; wala usiiteme, kwa maana huo mti wa kondeni, je! Ni mtu, hata ukauzuie? 20 Ila miti uijuayo si miti ya kuliwa iangamize, na kuitema; ukajenge maburuji juu ya mji ufanyao vita juu yako, hata uanguke.

Kumbukumbu la Torati 21

1 Aonekanapo mtu ameuawa katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, kuimiliki, amelala kondeni, wala haijulikani ni nani aliyempiga; 2 na watoke nje wazee wako na waamuzi wako, nao wapime hapo mpaka miji iliyomzunguka huyo aliyeuawa; 3 na iwe, mji ulio karibu na yule aliyeuawa, wale wazee wake mji huo watwae mtamba katika kundi la ng'ombe, ambaye hajafanya kazi, wala hajakokota jembe la nira; 4 wazee wa mji huo na wamshushe yule mtamba mpaka bonde lenye maji ya mtoni, lisilolimwa wala kupandwa, wakamvunje yule mtamba shingo yake humo bondeni; 5 nao makuhani wana wa Lawi wasongee karibu, kwa kuwa ndio aliowachagua Bwana, Mungu wako, wamtumikie, na kubariki katika jina la Bwana na kila neno lishindaniwalo, na kila pigo, litakuwa kwa kufuata maneno yao; 6 na wazee wote wa mji ule, ulio karibu sana na yule aliyeuawa, na waoshe mikono yao juu ya huyo mtamba aliyevunjwa shingo yake humo bondeni; 7 na wajibizane kwamba, Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuiona. 8 Ee Bwana, samehe watu wako Israeli, uliowakomboa, wala usiache damu ya asiye makosa ikakaa katikati ya watu wako Israeli. Na ile damu utasamehewa kwao. 9 Ndivyo utakavyoondoa damu ya asiye makosa katikati yako, utakapofanya yaliyo sawa machoni pa Bwana. 10 Utakapokwenda vitani kupigana juu ya adui zako, na Bwana, Mungu wako, awatiapo mikononi mwako, nawe uwachukuapo mateka, 11 ukaona kati ya mateka mwanamke mzuri, ukafanya tamaa kwake, ukawaza kumtwaa kuwa mkeo; 12 ndipo umchukue kwenu nyumbani kwako, naye atanyoa kichwa, akate na kucha; 13 avue na mavazi ya uteka wake akae nyumbani mwako, awakalie matanga babaye na mamaye mwezi mzima, kisha uingie kwake uwe mumewe, naye awe mkeo. 14 Tena utakapokuwa huna furaha naye, mpe ruhusa aende atakako; lakini usimwuze kabisa kwa fedha, usimfanye kama mtumwa, kwa kuwa ulimtweza. 15 Akiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; 16 ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu; 17 lakini amkubali mzaliwa wa kwanza mwana wa yule asiyempenda, kwa kumpa mafungu mawili katika vyote alivyo navyo; kwa maana ndiye mwanzo wa nguvu zake; haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye. 18 Mtu akiwa na mwana mkaidi, mshupavu, asiyetii sauti ya baba yake, wala sauti ya mama yake, nao wajapomwadhibu hawasikizi, 19 ndipo babaye na mamaye na wamkamate, na kumpeleka kwa wazee wa mji wake, katika lango la mahali pake; 20 wawaambie wazee wa mji wake, Huyu mwana wetu ni mkaidi, mshupavu, hasikizi sauti yetu; ni mwasherati, tena ni mlevi. 21 Waume wote wa mji wake na wamtupie mawe, afe; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako; na Israeli wote watasikia na kuogopa. 22 Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti; 23 mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi wako.

Kumbukumbu la Torati 22

1 Umwonapo ng'ombe wa nduguyo au kondoo wake akipotea, usijifiche kama usiyemwona; sharti utamrudisha kwa nduguyo. 2 Na kwamba yule nduguyo hayupo karibu nawe, au ukiwa humjui, umchukue kwenu nyumbani kwako, uwe naye hata aje nduguyo kumtafuta, nawe mrudishie. 3 Tena fanya vivyo kwa punda wake; tena fanya vivyo kwa mavazi yake; tena fanya vivyo kwa kila kitu kilichopotea cha nduguyo, kilichompotea ukakiona wewe; usijifiche kama usiyekiona. 4 Umwonapo punda wa nduguyo, au ng'ombe wake, ameanguka kando ya njia, usijifiche kama usiyemwona; sharti umsaidie kumwinua tena. 5 Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako. 6 Kiota cha ndege kikitukia kuwa mbele yako njiani, katika mti wo wote, au chini, chenye makinda au mayai, naye koo ameatamia juu ya makinda, au juu ya mayai, usimtwae yule koo pamoja na makinda; 7 sharti umwache yule koo aende zake, lakini makinda waweza kuyatwaa uwe nayo; ili upate kufanikiwa, ufanye siku zako kuwa nyingi. 8 Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko. 9 Usipande shamba lako la mizabibu aina mbili za mbegu; yasije yakaondolewa matunda yote, mbegu ulizopanda na maongeo ya mizabibu yako. 10 Usilime kwa ng'ombe na punda wakikokota jembe pamoja. 11 Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja. 12 Ujifanyizie vishada katika pembe nne za mavazi yako ya kujifunika. 13 Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia, 14 kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira; 15 ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni; 16 na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia; 17 angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji. 18 Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi, 19 wamtoze shekeli mia za fedha, wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli; naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote. 20 Lakini likiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; 21 na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. 22 Akifumaniwa mtu mume amelala na mwanamke aliyeolewa na mume, na wafe wote wawili, mtu mume aliyelala na mwanamke, na yule mwanamke naye; ndivyo utakavyoondoa uovu katika Israeli. 23 Pakiwa na kijana aliye mwanamwali ameposwa na mume, na mwanamume akimkuta mjini, akalala naye; 24 watoeni nje katika lango la mji ule, mkawapige kwa mawe hata wafe; yule kijana, kwa kuwa hakupiga ukelele, naye yu ndani ya mji; na yule mume, kwa kuwa amemtweza mke wa mwenzake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. 25 Lakini yule mtu mume kama akimkuta kondeni kijana aliyeposwa, naye mume akamtenza nguvu, akalala naye; yule mtu mume aliyelala naye na afe pekee; 26 lakini yule kijana usimfanye neno; hana dhambi yule kijana ipasayo kuuawa, kwa kuwa ni mfano wa mtu kumwondokea mwenzake akamwua, ni vivyo lilivyo jambo hili; 27 kwani alimkuta kondeni; yule kijana aliyeposwa akalia, pasiwe na mtu wa kumwokoa. 28 Mtu mume akimwona kijana aliye mwanamwali ambaye hajaposwa, akamshika na kulala naye, wakaonekana; 29 yule mtu mume aliyelala naye na ampe baba yake yule kijana shekeli hamsini za fedha, kisha na awe mkewe, kwa kuwa amemtweza; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote. 30 Mtu mume asimtwae mke wa baba yake, wala asifunue ncha ya mavazi ya baba yake.

Kumbukumbu la Torati 23

1 Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa Bwana. 2 Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa Bwana; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa Bwana. 3 Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa Bwana; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa Bwana milele; 4 kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize. 5 Lakini Bwana, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; Bwana, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda Bwana, Mungu wako. 6 Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele. 7 Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake. 8 Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa Bwana. 9 Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya. 10 Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo; 11 lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo. 12 Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje; 13nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho; 14 kwa kuwa Bwana. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha. 15 Usimrudishe kwa bwana wake mtumwa aliyejiponya kutoka kwa bwana wake kuja kwako; 16na akae nawe, katikati yako, ndani ya malango yako mojawapo, mahali atakapochagua palipo pema machoni pake; usimwonee. 17 Pasiwe na kahaba katika binti za Israeli, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israeli wanaume. 18 Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili. 19 Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula, riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba; 20 mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; ili Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika yote utiayo mkono wako, katika nchi uingiayo kuimiliki. 21 Utakapoweka nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako; nayo hivi itakuwa dhambi kwako. 22 Lakini ukijizuia usiweke nadhiri, haitakuwa dhambi kwako. 23 Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako. 24 Uingiapo katika shamba la mizabibu la jirani yako, utaweza kula zabibu za kukushibisha, kama upendavyo; ila usitie katika chombo chako. 25 Uingiapo katika mmea wa jirani yako waweza kuyapurura masuke kwa mkono wako; ila usisongeze mundu katika mmea wa jirani yako.

Kumbukumbu la Torati 24

1 Mtu akiisha kutwaa mke kwa kumwoa, asipopata kibali machoni mwake, kwa kuwa ameona neno ovu kwake, na amwandikie hati ya kumwacha, akamtilie mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake. 2 Naye akiisha kuondoka katika nyumba yake, ana ruhusa kwenda akawa mke wa mtu mwingine. 3 Na huyo mumewe wa sasa akimchukia, na kumwandikia hati ya kumwacha, na kumpa mkononi mwake, na kumtoa katika nyumba yake; au akifa yeye mumewe wa sasa, aliyemtwaa kuwa mkewe; 4 yule wa kwanza aliyemwacha asimtwae kuwa mkewe tena, akiisha kutiwa unajisi; kwa kuwa haya ni machukizo mbele za Bwana; kwa hiyo usiitie dhambini nchi, akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi. 5 Mtu atwaapo mke mpya, asiende vitani pamoja na jeshi, wala asipewe shughuli juu yake yo yote; akae faragha mwaka mmoja nyumbani mwake, apate mfurahisha mkewe aliyemtwaa. 6 Mtu awaye yote asitwae jiwe la kusagia, la juu wala la chini, kuwa rehani; kwani hivi ni kutwaa maisha ya mtu kuwa rehani. 7 Mtu akionekana anamwiba nduguze mmojawapo katika wana wa Israeli, akamfanya kama mtumwa, au kumwuza; na afe mwivi huyo; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako. 8 Angalia katika pigo la ukoma, utunze kwa bidii, kwa kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao. 9 Kumbukeni na Bwana, Mungu wako alivyomtenda Miriamu katika njia mlipotoka Misri. 10 Umkopeshapo jirani yako cho chote kikopeshwacho usiingie katika nyumba yake kwenda kutwaa rehani kwake. 11 Simama nje, yule umkopeshaye akuletee nje ile rehani. 12 Naye akiwa ni mtu maskini, usilale na rehani yake. 13 Sharti umrudishie rehani lichwapo jua, apate kulala na mavazi yake, na kukubarikia; nayo itakuwa ni haki kwako mbele za Bwana, Mungu wako. 14Usimwonee mtumishi mwenye ujira aliye maskini na uhitaji, kama ni wa nduguzo, au kama ni wageni wako mmojawapo walio katika nchi yako, ndani ya malango yako; 15 mpe ujira wake kwa siku yake, wala jua lisichwe juu yake; kwa maana ni maskini, moyo wake umeutumainia huo; asije akamlilia Bwana juu yako, ikawa ni dhambi kwako. 16 Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe. 17 Usipotoshe hukumu ya mgeni, wala ya yatima; wala usitwae mavazi ya mjane, yawe rehani; 18 bali kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika Misri, Bwana, Mungu wako, akakukomboa huko; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili. 19 Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako. 20 Utakapochuma matunda ya mizeituni yako, usirudi kuchuma mara ya pili; yaliyobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. 21 Uchumapo zabibu katika shamba lako la mizabibu, usichume mara ya pili; zilizobaki apewe mgeni, na yatima, na mjane. 22 Nawe kumbuka ya kuwa ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri; kwa hiyo nakuamuru kutenda neno hili.

Kumbukumbu la Torati 25

1 Pakiwa na mashindano kati ya watu, wakaenda maamuzini, na hao waamuzi wakawaamua; na wampe haki mwenye haki, na wamhukumie makosa yule mwovu; 2 na iwe, ikimpasa kupigwa yule mwovu, alazwe chini na mwamuzi, na kupigwa mbele ya uso wake, kwa kadiri ya uovu wake, kwa kuhesabu. 3 Aweza kumpiga fimbo arobaini asizidishe asije akaonekana nduguyo kuwa amedharauliwa kwako, azidishapo kwa kumpiga fimbo nyingi juu ya hizi. 4 Ng'ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa. 5 Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe. 6 Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli. 7 Na yule mtu kwamba hapendi kumtwaa mke wa nduguye, aende huyo mke wa nduguye langoni kwa wazee, akawaambie, Nduguye mume wangu yuakataa kumsimamishia nduguye jina katika Israeli, hataki kunitimizia yampasayo nduguye mume wangu. 8 Ndipo wamwite wazee wa mji wake waseme naye; naye akisimama na kusema, Sitaki mimi kumtwaa mwanamke huyu, 9 ndipo mke wa nduguye amkaribie mbele ya hao wazee, amvue kiatu chake mguuni mwake, na kumtemea mate ya uso; kisha atajibu yule mwanamke, aseme, Mume akataaye kumjengea nduguye nyumba yake na afanywe hivi. 10 Na jina lake katika Israeli liitwe, Nyumba ya mvuliwa kiatu. 11 Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake; 12 umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako. 13 Usiwe na mawe ya kupimia mbalimbali, kubwa na dogo, katika mfuko wako. 14 Usiwe na vipimo mbalimbali, kikubwa na kidogo, katika nyumba yako. 15 Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. 16 Kwa kuwa wote wayatendao mambo kama haya, wote watendao yasiyo haki, ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako. 17 Kumbuka aliyokufanya Amaleki katika njia mlipokuwa mkitoka Misri; 18 jinsi alivyokukuta katika njia, akapiga katika watu wako walioachwa nyuma, wote waliokuwa wanyonge nyuma yako, ulipokuwa umechoka na kuzimia; wala asimche Mungu. 19 Basi itakuwa, hapo atakapokwisha kukupumzisha Bwana, Mungu wako, katika adui zako wote walio kando-kando, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi uimiliki, ndipo uufute ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu; usisahau.

Kumbukumbu la Torati 26

1 Pakiwa na mashindano kati ya watu, wakaenda maamuzini, na hao waamuzi wakawaamua; na wampe haki mwenye haki, na wamhukumie makosa yule mwovu; 2 na iwe, ikimpasa kupigwa yule mwovu, alazwe chini na mwamuzi, na kupigwa mbele ya uso wake, kwa kadiri ya uovu wake, kwa kuhesabu. 3 Aweza kumpiga fimbo arobaini asizidishe asije akaonekana nduguyo kuwa amedharauliwa kwako, azidishapo kwa kumpiga fimbo nyingi juu ya hizi. 4 Ng'ombe apurapo nafaka usimfunge kinywa. 5 Watakapoketi pamoja mtu na nduguye, mmojawapo akafa, wala hana mwana wa kiume, mke wa yule aliyekufa asiolewe nje na mgeni; nduguye yule mumewe amwingilie amweke kwake awe mkewe, kumfanyia yampasayo nduguye mumewe. 6 Na iwe, yule mzaliwa wa kwanza atakayemzaa, amfuate nduguye aliyekufa kwa jina lake, lisije likafutwa jina lake katika Israeli. 7 Na yule mtu kwamba hapendi kumtwaa mke wa nduguye, aende huyo mke wa nduguye langoni kwa wazee, akawaambie, Nduguye mume wangu yuakataa kumsimamishia nduguye jina katika Israeli, hataki kunitimizia yampasayo nduguye mume wangu. 8 Ndipo wamwite wazee wa mji wake waseme naye; naye akisimama na kusema, Sitaki mimi kumtwaa mwanamke huyu, 9 ndipo mke wa nduguye amkaribie mbele ya hao wazee, amvue kiatu chake mguuni mwake, na kumtemea mate ya uso; kisha atajibu yule mwanamke, aseme, Mume akataaye kumjengea nduguye nyumba yake na afanywe hivi. 10 Na jina lake katika Israeli liitwe, Nyumba ya mvuliwa kiatu. 11 Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake; 12 umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako. 13 Usiwe na mawe ya kupimia mbalimbali, kubwa na dogo, katika mfuko wako. 14 Usiwe na vipimo mbalimbali, kikubwa na kidogo, katika nyumba yako. 15 Uwe na jiwe timilifu la haki, uwe na kipimo kitimilifu cha haki; zipate kuwa nyingi siku zako, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. 16 Kwa kuwa wote wayatendao mambo kama haya, wote watendao yasiyo haki, ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako. 17 Kumbuka aliyokufanya Amaleki katika njia mlipokuwa mkitoka Misri; 18 jinsi alivyokukuta katika njia, akapiga katika watu wako walioachwa nyuma, wote waliokuwa wanyonge nyuma yako, ulipokuwa umechoka na kuzimia; wala asimche Mungu. 19 Basi itakuwa, hapo atakapokwisha kukupumzisha Bwana, Mungu wako, katika adui zako wote walio kando-kando, katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi uimiliki, ndipo uufute ukumbuko wa Amaleki chini ya mbingu; usisahau.

Kumbukumbu la Torati 27

1 Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo. 2 Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo Bwana, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo, 3 uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi Bwana, Mungu wa baba zako. 4 Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo. 5 Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake. 6 Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake; 7 ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako. 8 Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana. 9 Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa Bwana, Mungu wako. 10 Basi isikize sauti ya Bwana, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo. 11 Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema, 12 Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini; 13 na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali. 14 Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu, 15 Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina. 16 Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina. 17 Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina. 18 Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina. 19 Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina. 20 Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina. 21 Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina. 22 Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina. 23 Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina. 24 Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina. 25 Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina. 26 Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina.

Kumbukumbu la Torati 28

1 Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; 2 na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako. 3 Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani. 4 Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. 5 Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga. 6 Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo. 7 Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba. 8 Bwana ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako. 9 Bwana atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya Bwana, Mungu wako, na kutembea katika njia zake. 10 Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la Bwana, nao watakuwa na hofu kwako. 11 Bwana atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako kwamba atakupa. 12 Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe. 13 Bwana atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya Bwana, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya; 14 msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia. 15 Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata. 16 Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani. 17 Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia. 18 Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako. 19 Utalaaniwa uingiapo, utalaaniwa na utokapo, 20 Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo. 21 Bwana atakuambatanisha na tauni, hata atakapokwisha kukuondoa katika nchi uingiayo kwa kuimiliki. 22 Bwana atakupiga kwa kifua kikuu, na kwa homa, na kwa kuwashwa, na kwa hari ya moto, na kwa upanga, na kwa ukaufu, na kwa koga; navyo vitakufukuza hata uangamie. 23 Na mbingu zako zilizo juu ya kichwa chako zitakuwa shaba, na nchi iliyo chini yako itakuwa chuma. 24 Bwana atafanya mvua ya nchi yako iwe vumbi na mchanga; itakujilia juu yako kutoka mbinguni hata uangamie. 25 Bwana atakufanya upigwe mbele ya adui zako; utawatokea juu yao kwa njia moja, lakini utakimbia mbele yao kwa njia saba; nawe utatupwa huko na huko katika falme zote za duniani. 26 Na mzoga wako utakuwa chakula cha ndege wote wa angani, na wanyama wote wa duniani, pasiwe na mtu wa kuwafukuza. 27 Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri, na kwa bawasiri, na kwa pele, na kwa kujikuna, ambayo hupati kupoa. 28 Bwana atakupiga kwa wazimu, na kwa upofu, na kwa bumbuazi la moyoni; 29 utakwenda kwa kupapasa-papasa mchana, kama apapasavyo kipofu gizani, wala hufanikiwi katika njia zako; nawe sikuzote utaonewa na kutekwa nyara, wala hapatakuwa na mtu wa kukuokoa. 30 Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake. 31 Ng'ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang'anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa. 32 Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako. 33 Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima; 34 hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona. 35 Bwana atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa. 36 Bwana atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe. 37 Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza Bwana. 38 Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila. 39 Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu. 40 Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika. 41 Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani. 42 Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo. 43 Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini. 44 Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia. 45 Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza; 46 nazo zitakuwa juu yako kwa ishara na ajabu, na juu ya uzao wako milele; 47 kwa kuwa hukumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa furaha na moyo wa kushukuru, kwa ajili ya ule wingi wa vitu vyote; 48 kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza. 49 Bwana atakuletea taifa juu yako kutoka mbali, kutoka ncha ya dunia, kama arukavyo tai; taifa usiloufahamu ulimi wake; 50 taifa lenye uso mkali, ambalo haliangalii uso wa mzee, wala halipendelei kijana; 51 naye atakula uzao wa ng'ombe wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako mpaka utakapokwisha kuangamizwa; wala hatakuachia nafaka, wala divai, wala mafuta, wala maongeo ya ng'ombe wako, wala wana-kondoo wako, hata atakapokwisha kukuangamiza. 52 Naye atakuhusuru katika malango yako yote, hata kuta zako ndefu, zenye maboma, ulizokuwa ukiziamini, zishuke, katika nchi yako yote kila upande; naye atakuhusuru katika malango yako yote kila upande, katika nchi yako yote aliyokupa Bwana, Mungu wako. 53 Nawe utakula uzao wa tumbo lako mwenyewe, nyama ya wana wako na binti zako aliokupa Bwana, Mungu wako; katika mazingirwa na katika mkazo utakaokazwa na adui zako. 54 Mtu mume kati yenu aliye mwororo na laini sana, jicho lake litakuwa ovu juu ya nduguye, na juu ya mke wa kifuani mwake, na juu ya masalio ya wanawe waliosalia naye; 55 hata asitake wao mmojawapo apewe katika nyama ya wanawe atakaowala, kwa kuwa hana kitu kilichomsalia kwake; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako yote. 56 Mwanamke kati yenu aliye mwororo na laini, ambaye hangehatirisha kuweka wayo wa mguu wake nchi kwa umalidadi na ulaini, jicho lake huyu litakuwa ovu juu ya mume wa kifuani mwake, na juu ya mwanawe, na juu ya binti yake, 57 na juu ya mchanga wake atokaye katikati ya miguu yake, na juu ya wanawe atakaowazaa; kwa kuwa atawala kwa siri, kwa uhitaji wa vitu vyote; katika mazingirwa na mkazo utakaokazwa na adui yako katika malango yako. 58 Kama hutaki kutunza kufanya maneno yote ya torati hii yaliyoandikwa katika kitabu hiki, upate kulicha jina hili la fahari na utisho, Bwana, MUNGU WAKO; 59 ndipo atakapofanya Bwana mapigo yako yawe ya ajabu, na mapigo ya uzao wako, mapigo makubwa kwa kweli, ya kudumu sana, na magonjwa mazito ya kudumu sana. 60 Naye atakurejezea maradhi yote ya Misri juu yako uliyokuwa ukiyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61 Tena kila ugonjwa, na kila pigo yasiyoandikwa katika kitabu cha torati hii, atakutia nayo Bwana juu yako, hata utakapokwisha kuangamizwa. 62 Nanyi mtasalia wachache kwa hesabu, ninyi mliokuwa mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi; kwa kuwa hukuisikiza sauti ya Bwana, Mungu wako. 63 Tena itakuwa, kama vile alivyokuwa akifurahi Bwana juu yenu kwa kuwatendea mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo atakavyofurahi Bwana juu yenu kwa kuwapoteza na kuwaangamiza; nanyi mtanyakuliwa katika hiyo nchi mwingiayo kuimiliki. 64 Bwana atakutawanya katika mataifa yote, tokea ncha hii ya dunia hata ncha hii ya dunia; nawe huko utatumikia miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako, nayo ni miti na mawe. 65 Wala katika mataifa hayo hutapata raha iwayo yote, wala hutakuwa na kituo cha wayo wa mguu wako; lakini Bwana atakupa huko moyo wa kutetema, na macho ya kuzimia, na roho ya kudhoofika; 66 na uzima wako utakuwa na wasiwasi mbele yako; nawe utakuwa na woga usiku na mchana, wala hutaamini kamwe maisha yako; 67 asubuhi utasema, Laiti ingekuwa jioni! Na jioni utasema, Laiti ingekuwa asubuhi! Kwa kicho cha moyo wako utakavyokucha, na kuona kwa macho yako utakavyoona. 68 Bwana atakurudisha tena Misri kwa merikebu, kwa njia ambayo nilikuambia, Hutaiona tena po pote; nanyi huko mtajiuza nafsi zenu kwa adui zenu kuwa watumwa na wajakazi, wala hapana atakayewanunua.

Kumbukumbu la Torati 29

1 Haya ndiyo maneno ya agano Bwana alilomwamuru Musa alifanye na wana wa Israeli katika nchi ya Moabu, pamoja na agano alilofanya nao Horebu. 2 Musa akawaita Israeli wote akawaambia, Mmeyaona yote Bwana aliyomfanya Farao katika nchi ya Misri mbele ya macho yenu, yeye na watumwa wake wote, na nchi yake yote; 3 yale majaribu makuu yaliyoyaona macho yako; hizo ishara, na ile miujiza mikuu; 4 lakini Bwana hakuwapa moyo wa kujua, wala macho ya kuona, wala masikio ya kusikia, hata leo hivi. 5 Nami miaka arobaini nimewaongoza jangwani; nguo zenu hazikuchakaa juu yenu, wala kiatu chako hakikuchakaa katika mguu wako. 6 Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu. 7 Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga; 8 tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi. 9 Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo. 10 Leo mmesimama nyote mbele za Bwana, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli, 11 vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako; 12 ili uingie katika agano la Bwana, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe Bwana, Mungu wako, hivi leo; 13 apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. 14 Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki; 15 ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya Bwana, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo; 16 (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao; 17 nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;) 18 asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache Bwana, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga; 19 ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu kwa kuangamiza mbichi na kavu; 20 Bwana hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya Bwana na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na Bwana atalifuta jina lake chini ya mbingu. 21 Bwana atamtenga kwa uovu, kutoka kabila zote za Israeli, kwa laana zote za agano lililoandikwa katika chuo hiki cha torati. 22 Na kizazi cha baadaye, wanenu watakaoinuka baada yenu, na mgeni atakayekuja kutoka nchi ya mbali, watasema, watakapoyaona mapigo ya nchi ile, na magonjwa aliyoitia Bwana; 23 ya kuwa nchi yake nzima ni kibiriti, na chumvi, na kuteketea, haipandwi, wala haizai, wala nyasi hazimei humo, kama mapinduko ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, aliyoipindua Bwana kwa ghadhabu yake na hasira zake; 24 mataifa yote watasema, Mbona Bwana ameifanyia hivi nchi hii? Ni nini maana yake hari ya hasira hizi kubwa? 25 Ndipo watakaposema watu, Ni kwa kuwa waliacha agano la Bwana, Mungu wa baba zao, alilofanya nao hapo alipowatoa katika nchi ya Misri; 26 wakaenda wakatumikia miungu mingine, wakaiabudu miungu wasiyoijua, asiyowapa yeye; 27 ndipo ikawashwa hasira ya Bwana juu ya nchi hii, kwa kuleta juu yake laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki; 28 Bwana akawang'oa katika nchi yao kwa hasira, na ghadhabu, na makamio makuu, akawatupa waende nchi nyingine, kama hivi leo. 29 Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu; lakini mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele, ili tuyafanye maneno yote ya sheria hii.

Kumbukumbu la Torati 30

1 Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako, 2 nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; 3 ndipo Bwana, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako. 4 Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa; 5 atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako. 6 Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai. 7 Na laana hizi zote Bwana, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa. 8 Nawe utarudi, uitii sauti ya Bwana, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo. 9 Na Bwana, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng'ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa Bwana atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako; 10 ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote. 11 Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. 12 Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya? 13 Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya? 14 Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya. 15 Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; 16 kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. 17 Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; 18 nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. 19 Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; 20 kumpenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.

Kumbukumbu la Torati 31

1 Musa akaenda akawaambia Waisraeli maneno haya yote. 2 Akawaambia, Mimi leo ni mwenye miaka mia na ishirini; siwezi tena kutoka na kuingia, na Bwana ameniambia, Hutavuka mto huu Yordani. 3 Bwana Mungu wako, ndiye atakayevuka mbele yako, atawaangamiza mataifa haya mbele yako, nawe utawamiliki; na Yoshua atavuka mbele yako, kama Bwana alivyonena. 4 Na Bwana atawatenda hao kama vile alivyowatenda Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao, ambao aliwaharibu. 5 Naye Bwana atawatia mikononi mwenu, nanyi mtawatenda kadiri ya amri ile niliyowaamuru. 6 Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha. 7 Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi Bwana aliyowaapia baba zao, ya kwamba atawapa; nawe utawarithisha. 8 Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike. 9 Musa akaiandika torati hii, akawapa makuhani, wana wa Lawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, na wazee wote wa Israeli. 10 Musa, akawaamuru, akasema, Mwisho wa kila mwaka wa saba, wakati wa maachilio, wakati ulioamriwa wa sikukuu ya vibanda, 11 Israeli wote wafikapo ili kuonekana mbele za Bwana, Mungu wako, mahali pale atakapopachagua, uisome torati hii mbele ya Israeli wote masikioni mwao. 12 Wakusanye watu, wanaume na wanawake na watoto, na mgeni wako aliyemo malangoni mwako wapate kusikia na kujifunza, na kumcha Bwana, Mungu wenu, na kuangalia kutenda maneno yote ya torati hii; 13 na watoto wao wasiojua, wapate kusikia na kujifunza kumcha Bwana, Mungu wenu, siku zote mtakazokaa katika nchi mnayoivukia Yordani ili kuimiliki. 14 Bwana akamwambia Musa, Tazama, siku zako za kufa zinakaribia, umwite Yoshua, nanyi mkajihudhurishe katika hema ya kukutania, ili nipate kumwagiza kazi. Musa na Yoshua wakaenda, wakajihudhurisha ndani ya hema ya kukutania. 15 Bwana akaonekana katika Hema katika nguzo ya wingu; na ile nguzo ya wingu ikasimama juu ya mlango wa Hema. 16 Bwana akamwambia Musa, Angalia, wewe utalala na baba zako; na watu hawa wataondoka, wataifuata kwa ukahaba miungu ya kigeni ya nchi waiendeayo kuwa kati yao, nao wataniacha mimi na kulivunja agano langu, nililofanya nao. 17 Ndipo hasira yangu itakapowaka juu yao siku hiyo, nami nitawaacha, nitawaficha uso wangu, nao wataliwa, tena watajiliwa na mambo maovu mengi na mashaka; hata waseme siku hiyo, Je! Kujiliwa kwetu na maovu haya si kwa sababu Mungu wetu hayumo kati yetu? 18 Nami nitawaficha uso wangu kwa kweli siku hiyo, kwa maovu yote waliyoyafanya, kwa kuigeukia hiyo miungu mingine. 19 Basi sasa jiandikieni wimbo huu, uwafundishe wana wa Israeli; kawatie vinywani mwao, ili uwe shahidi kwangu wimbo huu, juu ya wana wa Israeli. 20 Kwa kuwa nitakapokwisha kuwatia katika nchi niliyowaapia baba zao, imiminikayo maziwa na asali; nao watakapokwisha kula na kushiba, na kuwanda; ndipo watakapoigeukia hiyo miungu mingine, na kuitumikia, na kunidharau mimi, na kulivunja agano langu. 21 Tena itakuwa, wakiisha kujiliwa na mambo maovu mengi na mashaka, utashuhudia wimbo huu mbele yao kama shahidi, kwa maana hautasahauliwa katika vinywa vya uzao wao; kwani nayajua mawazo yao wayawazayo, hata sasa kabla sijawatia katika nchi niliyoapa. 22 Basi Musa akauandika wimbo huu siku iyo hiyo, akawafundisha wana wa Israeli. 23 Akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, Uwe hodari na moyo mkuu, kwa kuwa utawapeleka wana wa Israeli katika nchi niliyowaapia; nami nitakuwa pamoja nawe. 24 Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha, 25 ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la agano la Bwana akawaambia, 26 Twaeni chuo hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako. 27 Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi nikali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya Bwana; siuze nitakapokwisha kufa! 28 Nikutanishieni wazee wote wa kabila zenu, na maakida yenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao. 29 Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa Bwana kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu. 30 Musa akasema maneno ya wimbo huu masikioni mwa kusanyiko la wana wa Israeli hata yakaisha.

Kumbukumbu la Torati 32

1 Kumbukumbu la Torati, Chapter :Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu. 2 Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua, Maneno yangu yatatona-tona kama umande; Kama manyunyu juu ya majani mabichi; Kama matone ya mvua juu ya mimea. 3 Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. 4 Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili. 5 Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka. 6 Je! Mnamlipa Bwana hivi, Enyi watu wapumbavu na ujinga? Je! Yeye siye baba yako aliyekununua? Amekufanya, na kukuweka imara. 7 Kumbuka siku za kale, Tafakari miaka ya vizazi vingi; Mwulize baba yako, naye atakuonyesha; Wazee wako, nao watakuambia. 8 Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao, Alipowabagua wanadamu, Aliweka mipaka ya watu Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli. 9 Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. 10 Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho; 11 Mfano wa tai ataharikishaye kioto chake; Na kupapatika juu ya makinda yake, Alikunjua mbawa zake, akawatwaa, Akawachukua juu ya mbawa zake; 12 Bwana peke yake alimwongoza, Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. 13 Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka, Naye akala mazao ya mashamba; Akamnyonyesha asali iliyotoka jabalini, Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume; 14 Siagi ya ng'ombe, na maziwa ya kondoo, Pamoja na mafuta ya wana-kondoo, Kondoo waume wa Kibashani, na mbuzi, Na unono wa ngano iliyo nzuri; Ukanywa divai, damu ya mizabibu. 15 Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. 16 Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo. 17 Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa. 18 Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau. 19 Bwana akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake. 20 Akasema, Nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio imani ndani yao. 21 Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; Wamenikasirisha kwa ubatili wao; Nami nitawatia wivu kwa wasio watu, Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. 22 Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, Unateketea hata chini ya kuzimu, Unakula dunia pamoja na mazao yake, Unaunguza misingi ya milima. 23 Nitaweka madhara juu yao chunguchungu; Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe; 24 Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto, Na uharibifu mkali; Nitawapelekea meno ya wanyama wakali, Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini. 25 Nje upanga utawafifiliza Na ndani ya vyumba, utisho; Utaangamiza mvulana na msichana, Anyonyaye pamoja na mwenye mvi, 26 Nalisema, Ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu; 27 Isipokuwa naliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo, Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka, Wala Bwana hakuyafanya haya yote. 28 Maana hawa ni taifa wasio shauri, Wala fahamu hamna ndani yao. 29 Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao. 30 Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa? 31 Maana, Mwamba wao si kama Mwamba wetu, Hata adui zetu wenyewe ndivyo wahukumuvyo. 32 Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Sodoma, Nao ni wa mashamba ya Gomora; Zabibu zao ni zabibu za uchungu, Vichala vyao ni vichungu. 33 Mvinyo yao ni sumu ya majoka, Uchungu mkali wa nyoka. 34 Je! Haya hayakuwekwa akiba kwangu? Na kutiwa muhuri kati ya hazina yangu? 35 Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao; Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka. 36 Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumwa wake, Aonapo ya kuwa nguvu zao zimeondoka, Na ya kuwa habaki mtu, aliyefungwa wala asiyefungwa, 37 Naye atasema, Iko wapi miungu yao, Mwamba ule walioutumaini; 38 Uliokula shahamu za sadaka zao, Na kunywa divai ya sadaka zao za kinywaji? Na waondoke na kuwasaidia ninyi; Na wawe hao himaya yenu. 39 Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu, 40 Maana, nainua mkono wangu mbinguni, Na kusema, Kama Mimi niishivyo milele, 41 Nikiunoa upanga wangu wa umeme, Mkono wangu ukishika hukumu, Nitawatoza kisasi adui zangu, Nitawalipa wanaonichukia. 42 Nitailevya mishale yangu kwa damu, Na upanga wangu utakula nyama; Pamoja na damu ya waliouawa na waliotekwa nyara, Katika vichwa vya wakuu wa adui. 43 Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake; Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake, Atawatoza kisasi adui zake, Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake. 44 Musa akaja akasema maneno haya yote ya wimbo huu masikioni mwa watu, yeye na Yoshua, mwana wa Nuni. 45 Musa akamaliza kuwaambia Israeli wote maneno haya yote; 46 akawaambia, Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo nashuhudia kwenu hivi leo; nayo waamuruni watoto wenu, wayatunze na kuyafanya maneno yote ya torati hii. 47 Kwa maana si jambo lisilofaa kwenu; maana, ni maisha yenu, na kwa jambo hili mtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki. 48 Bwana akasema na Musa siku iyo hiyo, akamwambia, 49 Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki; 50 ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe pamoja na watu wake; 51 kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli. 52 Kwani utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli.

Kumbukumbu la Torati 33

1 Kumbukumbu la Torati, Chapter :Hii ndiyo baraka ya Musa, huyo mtu wa Mungu, aliyowabarikia wana wa Israeli kabla ya kufa kwake. 2 Akasema,Bwana alitoka Sinai,Akawaondokea kutoka Seiri;Aliangaza katika kilima cha Parani,Akaja Meribath-Kadeshi.Upande wake wa kuume Palikuwa na sheria ya moto-moto kwao. 3 Hakika awapenda hayo makabila ya watu; Watakatifu wake wote wamo mkononi mwako; Nao waliketi miguuni pako; Watapokea kila mmoja katika maneno yako. 4 Musa alituagiza torati, Ni urithi kwa mkutano wa Yakobo. 5 Akawa mfalme katika Yeshuruni, Walipokutanika wakuu wa watu, Makabila yote ya Israeli pamoja. 6 Reubeni na aishi, asife; Lakini watu wake na wawe wachache. 7 Na baraka ya Yuda ni hii; akasema, Isikize, Ee Bwana, sauti ya Yuda, Umlete ndani kwa watu wake; Alijitetea kwa mikono yake; Nawe utakuwa msaada juu ya adui zake. 8 Akamnena Lawi, Thumimu yako na Urimu yako vina mtakatifu wako, Uliyemjaribu huko Masa; Ukateta naye kwenye maji ya Meriba. 9 Aliyemtaja baba yake na mama yake, Mimi sikumwona; Wala nduguze hakuwakubali; Wala hakuwajua watoto wake mwenyewe; Maana wameliangalia neno lako, Wamelishika agano lako. 10 Watamfundisha Yakobo hukumu zako, Na Israeli torati yako, Wataweka uvumba mbele zako, Na sadaka nzima za kuteketezwa madhabahuni mwako. 11 Ee Bwana, ubariki mali zake, Utakabali kazi ya mikono yake; Uwapige viuno vyao waondokao juu yake, Na wenye kumchukia, wasiinuke tena. 12 Akamnena Benyamini, Mpenzi wa Bwana atakaa salama kwake; Yuamfunika mchana kutwa, Naye hukaa kati ya mabega yake. 13 Na Yusufu akamnena, Nchi yake na ibarikiwe na Bwana; Kwa vitu vya thamani vya mbinguni, kwa huo umande, Na kwa kilindi kilalacho chini, 14 Na kwa vitu vilivyo bora vya matunda ya jua, Na kwa vitu vilivyo bora vya maongeo ya miezi, 15 Na kwa vitu viteule vya milima ya kale, Na kwa vitu vilivyo bora vya vilima vya milele, 16 Na kwa vitu vilivyo bora vya nchi, na kujaa kwake, Na uradhi wake aliyekaa ndani ya kile kijiti; Na ije baraka juu ya kichwa chake Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake aliyetengwa na nduguze. 17 Mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe wake mume, enzi ni yake; Na pembe zake ni pembe za nyati; Kwa hizo atayasukuma mataifa yote, hata ncha za nchi; Nao ni makumi ya maelfu ya Efraimu, Nao ni maelfu ya Manase. 18 Na Zabuloni akamnena, Furahi Zabuloni, katika kutoka kwako; 19 Watayaita mataifa waje mlimani; Wakasongeze huko sadaka za haki; Kwa kuwa watanyonya wingi wa bahari, Na akiba zilizofichamana za mchangani. 20 Na Gadi akamnena, Na abarikiwe amwongezaye Gadi; Yeye hukaa kama simba mke, Hurarua mkono, naam, na utosi wa kichwa. 21 Akajichagulia sehemu ya kwanza, Kwani ndiko lilikowekwa fungu la mtoa-sheria; Akaja pamoja na wakuu wa watu, Akaitekeleza haki ya Bwana, Na hukumu zake kwa Israeli. 22 Na Dani akamnena, Dani ni mwana-simba, Arukaye kutoka Bashani. 23 Na Naftali akamnena, Ee Naftali, uliyeshiba fadhili, Uliyejawa na baraka ya Bwana; Umiliki magharibi na kusini. 24 Na Asheri akamnena, Na abarikiwe Asheri kwa watoto; Na akubaliwe katika nduguze, Na achovye mguu wake katika mafuta. 25 Makomeo yako yatakuwa ya chuma na shaba; Na kadiri ya siku zako ndivyo zitakavyokuwa nguvu zako. 26 Hapana aliyefanana na Mungu, Ee Yeshuruni, Ajaye amepanda juu ya mbingu ili akusaidie. Na juu ya mawingu katika utukufu wake. 27 Mungu wa milele ndiye makazi yako, Na mikono ya milele i chini yako. Na mbele yako amemsukumia mbali adui; Akasema, Angamiza. 28 Na Israeli anakaa salama, Chemchemi ya Yakobo peke yake, Katika nchi ya ngano na divai; Naam, mbingu zake zadondoza umande. 29 U heri, Israeli. Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na Bwana! Ndiye ngao ya msaada wako, Na upanga wa utukufu wako; Na adui zako watajitiisha chini yako, Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.

Kumbukumbu la Torati 34

1 Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. Bwana akamwonyesha nchi yote ya Gileadi hata Dani; 2 na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi; 3 na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari. 4 Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko. 5 Basi Musa, mtumishi wa Bwana, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la Bwana. 6 Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo. 7 Musa alikuwa mtu wa miaka mia na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka. 8 Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha. 9 Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa. 10 Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso; 11 katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; 12 na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.

Yoshua 1

1 Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, 2 Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli. 3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. 4 Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. 5 Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. 6 Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. 7 Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. 8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. 9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako. 10 Ndipo Yoshua akawaamuru maakida wa watu, akisema, 11 Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, mpate kuimiliki. 12 Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema, 13 Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa Bwana, akisema, Bwana, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii. 14 Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng'ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia; 15 hata Bwana atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwapeni ng'ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua. 16 Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda. 17 Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; Bwana, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa. 18 Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.

Yoshua 2

1 Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko. 2 Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi. 3 Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi. 4 Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka; 5 ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata. 6 Lakini yeye alikuwa amewapandisha darini, akawaficha kwa mabua ya kitani, aliyokuwa ameyatandika juu ya dari. 7 Basi hao watu wakawafuata kwa njia iendayo Yordani mpaka vivukoni; na mara wale watu waliowafuatia walipokwisha kutoka, wakalifunga lango. 8 Tena kabla hawajalala akawaendea juu darini, 9 akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu. 10 Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa. 11 Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini. 12 Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa Bwana, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu; 13 ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa. 14 Wale wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa ihisani na uaminifu. 15 Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani. 16 Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha enendeni zenu. 17 Wale wanaume wakamwambia, Sisi tunataka tusiwe na hatia kwa ajili ya kiapo hiki ulichotuapisha. 18 Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako. 19 Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu, mkono wa mtu ukimpata. 20 Lakini wewe ukitangaza habari yetu hii, ndipo tutakuwa hatuna hatia, katika kiapo hiki ulichotuapisha. 21 Naye akasema, Na iwe hivyo kama yalivyo maneno yenu. Akawatoa, nao wakaenda zao; naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani 22 Watu hao wakaenda, wakafika mlimani, wakakaa huko siku tatu, hata wale waliowafuatia walipokuwa wamerudi; na wale waliowafuatia wakawafuatia katika njia ile yote, lakini hawakuwaona. 23 Kisha wale watu wakarudi, wakatelemka mlimani, wakavuka, wakamwendea Yoshua, mwana wa Nuni, nao wakamwambia habari za mambo yote yaliyowapata. 24 Wakamwambia Yoshua, Hakika Bwana ameitia nchi yote katika mikono yetu; tena zaidi ya hayo wenyeji wa nchi wanayeyuka mbele yetu.

Yoshua 3

1 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka. 2 Ikawa baada ya siku tatu, maakida wakapita katikati ya marago, 3 wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata. 4 Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado. 5 Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu. 6 Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu. 7 Bwana akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa. 8 Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani. 9 Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu. 10 Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi. 11 Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani. 12 Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja. 13 Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu. 14 Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la agano wakatangulia mbele ya watu, 15 basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno), 16 ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko. 17 Na hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hata taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.

Yoshua 4

1 Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo Bwana akanena na Yoshua, akamwambia, 2 Haya, twaeni watu waume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, 3 kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende nayo mawe hayo, mkayaweke nchi kambini, hapo mtakapolala usiku huu. 4 Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa amewaweka tayari tangu hapo, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; 5 naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la Bwana, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli; 6 ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? 7 Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la Bwana; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele. 8 Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama Bwana alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya kabila za wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayaweka nchi kuko huko. 9 Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo. 10 Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hata mambo yote Bwana aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka. 11 Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la Bwana likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu. 12 Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia; 13 walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya Bwana, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko. 14 Siku ile Bwana alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake. 15 Kisha Bwana akanena na Yoshua, akamwambia, 16 Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani. 17 Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani. 18 Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kujaa na kuipita mipaka yake, kama yalivyokuwa hapo kwanza. 19 Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko. 20 Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali. 21 Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini? 22 Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu. 23 Kwa sababu Bwana, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hata mlipokwisha kuvuka kama Bwana, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka; 24 watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa Bwana, ya kuwa ni mkono wenye uweza, ili wamche Bwana, Mungu wenu, milele.

Yoshua 5

1 Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng'ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hata tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli. 2 Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. 3 Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. 4 Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri. 5 Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika bara njiani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa. 6 Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arobaini barani, hata hilo taifa zima, yaani, watu waume waendao vitani, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya Bwana; nao ndio Bwana aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo Bwana aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi ijaayo maziwa na asali. 7 Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawakutahiriwa, kwa maana walikuwa hawakuwatahiri njiani. 8 Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake maragoni, hata walipopoa. 9 Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Gilgali, hata hivi leo. 10 Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. 11 Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. 12 Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo. 13 Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? 14 Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la Bwana. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake? 15 Huyo amiri wa jeshi la Bwana akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya vivyo.

Yoshua 6

1 Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. 2 Bwana akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. 3 Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. 4 Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao. 5 Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. 6 Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana. 7 Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la Bwana. 8 Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za Bwana, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la Bwana likawafuata. 9 Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. 10 Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. 11 Basi akalipeleka sanduku la Bwana liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini. 12 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la Bwana. 13 Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la Bwana; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. 14 Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. 15 Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba. 16 Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana Bwana amewapeni mji huu. 17 Na mji huu utakuwa wakfu kwa Bwana, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. 18 Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha. 19 Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa Bwana; vitaletwa katika hazina ya Bwana. 20 Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. 21 Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga. 22 Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia. 23 Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. 24 Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya Bwana. 25 Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko. 26 Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo. 27 Basi Bwana alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.

Yoshua 7

1 Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana ikawaka juu ya wana wa Israeli. 2 Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. 3 Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu. 4 Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai. 5 Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji. 6 Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Bwana hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. 7 Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng'ambo ya Yordani 8 Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? 9 Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? 10 Bwana akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi? 11 Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe. 12 Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. 13 Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. 14 Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa Bwana itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa Bwana itakaribia mtu kwa mtu. 15 Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la Bwana, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli. 16 Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa. 17 Akazisogeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisogeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa. 18 Akawasogeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda akatwaliwa. 19 Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche. 20 Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya. 21 Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake. 22 Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake. 23 Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za Bwana. 24 Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori. 25 Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? Bwana atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe. 26 Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa ya mawe hata leo; naye Bwana akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo.

Yoshua 8

1 Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake; 2 nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma. 3 Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku. 4 Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote; 5 na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao; 6 nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao; 7 basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu. 8 Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la Bwana; angalieni, nimewaagiza. 9 Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu. 10 Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli. 11 Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai. 12 Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji. 13 Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde. 14 Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na watu waume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji. 15 Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika. 16 Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji. 17 Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli. 18 Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji. 19 Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji. 20 Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia. 21 Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai. 22 Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona. 23 Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua. 24 Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga. 25 Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai. 26 Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai. 27 Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la Bwana alilomwamuru Yoshua. 28 Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo. 29 Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo. 30 Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali. 31 Kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyowaamuru wana wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma; nao wakatoa juu yake sadaka za kuteketezwa kwa Bwana, na kuchinja sadaka za amani. 32 Akaandika huko juu ya mawe hayo nakala ya torati ya Musa, aliyoiandika mbele ya wana wa Israeli. 33 Na Israeli wote, na wazee wao, na maakida yao, na makadhi yao, wakasimama upande huu wa sanduku na upande huu, mbele ya makuhani Walawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, huyo aliyekuwa mgeni pamoja na huyo mzalia; nusu yao mbele ya mlima Gerizimu, na nusu yao mbele ya mlima Ebali, kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyoamuru, ili wawabarikie watu wa Israeli kwanza. 34 Na baadaye alisoma maneno yote ya torati, baraka na laana, sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati. 35 Hapakuwa na hata neno moja katika hayo aliyoamuru Musa, ambalo Yoshua hakulisoma mbele ya kusanyiko lote la Israeli, na mbele ya wanawake, na watoto, na wageni waliokaa nao.

Yoshua 9

1 Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo; 2 ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja. 3 Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai, 4 wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka; 5 na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga. 6 Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi. 7 Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi? 8 Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi? 9 Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la Bwana, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri, 10 na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng'ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi. 11 Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi. 12 Huu mkate wetu tuliutwaa ukali moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia koga; 13 na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimeraruka-raruka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana. 14 Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa Bwana. 15 Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia. 16 Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. 17 Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu. 18 Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung'unikia hao wakuu. 19 Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa. 20 Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia. 21 Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia. 22 Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu? 23 Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu. 24 Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo Bwana, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. 25 Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende vivyo. 26 Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue. 27 Siku iyo hiyo Yoshua akawafanya kuwa ni wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano, na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana, hata siku hii ya leo, katika mahali hapo atakapopachagua.

Yoshua 10

1 Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyoushika mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya vivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao; 2 ndipo wakacha mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa. 3 Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia, 4 Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli. 5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na jeshi zao zote, na kupanga marago yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita. 6 Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali maragoni, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; uje kwetu kwa upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu. 7 Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote. 8 Bwana akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. 9 Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. 10 Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. 11 Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. 12 Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. 13 Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. 14 Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye Bwana kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa Bwana alipiga vita kwa ajili ya Israeli. 15 Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka maragoni hapo Gilgali. 16 Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda. 17 Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wa hali ya kujificha ndani ya pango la Makeda 18 Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda; 19 lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu. 20 Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma, 21 ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua maragoni huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo. 22 Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango. 23 Nao wakafanya, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni. 24 Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao. 25 Yoshua akawaambia, Msiche, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo Bwana atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mwapigana nao. 26 Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wakitundikwa katika hiyo miti hata jioni. 27 Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawatelemsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo. 28 Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko. 29 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna; 30 Bwana akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko. 31 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapanga marago mbele yake na kupigana nao; 32 Bwana akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna. 33 Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja. 34 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Egloni; nao wakapanga marago mbele yake, na kupigana nao; 35 siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi. 36 Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Hebroni; nao wakapigana nao; 37 wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake. 38 Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao; 39 kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake. 40 Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya matelemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa wavuta pumzi, kama Bwana, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. 41 Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni. 42 Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa, wakati huo, kwa sababu yeye Bwana, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli, 43 Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata marago yao huko Gilgali.

Yoshua 11

1 Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu, 2 na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi zilizoinuka za Dori upande wa magharibi, 3 na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. 4 Nao wakatoka nje, wao na jeshi zao zote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana. 5 Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli. 6 Bwana akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; utawatema farasi zao, na magari yao utayapiga moto. 7 Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia. 8 Bwana akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia. 9 Yoshua akawafanyia vile vile kama Bwana alivyomwamuru; akawatema farasi zao, na magari yao akayapiga moto. 10 Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo kwanza ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote. 11 Nao wakawapiga wote pia waliokuwamo ndani ya Hazori kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa; hakusazwa hata mmoja aliyevuta pumzi; kisha akauteketeza Hazori kwa moto. 12 Tena miji yote ya wafalme hao, na wafalme wake wote, Yoshua akawatwaa, akawapiga kwa makali ya upanga, na kuwaangamiza kabisa; vile vile kama huyo Musa mtumishi wa Bwana alivyomwamuru. 13 Lakini katika habari ya miji hiyo iliyosimama katika vilima vyao, Israeli hawakuipiga moto miji hiyo, isipokuwa ni mji wa Hazori tu; mji huo Yoshua aliupiga moto. 14 Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi. 15 Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote Bwana aliyomwamuru Musa. 16 Hivyo Yoshua akatwaa nchi hiyo yote, hiyo nchi ya vilima, na nchi yote ya Negebu, na nchi yote ya Gosheni, na hiyo Shefela, na hiyo Araba na nchi ya vilima vilima ya Israeli, na hiyo nchi tambarare; 17 tangu kilima cha Halaki, kiendeleacho upande wa Seiri, mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni chini ya kilima cha Hermoni; naye akawatwaa wafalme wao wote, akawapiga, na kuwaua. 18 Yoshua akapiga vita siku nyingi na wafalme hao wote. 19 Haukuwapo mji hata mmoja uliofanya amani na wana wa Israeli, isipokuwa ni wale Wahivi wenye kukaa Gibeoni; wakaitwaa yote vitani. 20 Kwa kuwa lilikuwa ni la Bwana kuifanya mioyo yao kuwa migumu, hata wakatoka kupigana na Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, wasihurumiwe lakini apate kuwaangamiza, kama vile Bwana alivyomwamuru Musa. 21 Wakati huo Yoshua akaenda na kuwakatilia mbali hao Waanaki watoke nchi ya vilima, kutoka Hebroni, na kutoka Debiri, na kutoka Anabu, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Yuda, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Israeli; Yoshua akawaangamiza kabisa na miji yao. 22 Hawakusalia Waanaki hata mmoja katika nchi ya wana wa Israeli; isipokuwa katika Gaza, na katika Gathi, na katika Ashdodi walisalia. 23 Basi Yoshua akaitwaa hiyo nchi yote, sawasawa na hayo yote Bwana aliyokuwa amemwambia Musa; Yoshua naye akawapa Israeli kuwa ni urithi wao, sawasawa na walivyogawanyikana kwa kabila zao. Kisha nchi ikatulia isiwe na vita tena.

Yoshua 12

1 Basi hawa ndio wafalme wa nchi, ambao wana wa Israeli waliwapiga na kuimiliki nchi yao ng'ambo ya pili ya Yordani, upande wa maawio ya jua, kutoka bonde la Amoni mpaka mlima wa Hermoni, na nchi yote ya Araba upande wa mashariki; 2 Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekaa huko Heshboni, naye ndiye aliyetawala toka Aroeri, ulioko kando ya bonde la Arnoni, na toka huo mji ulio katikati ya bonde, na nusu ya Gileadi, hata kuufikilia mto wa Yaboki, mpaka wa hao wana wa Amoni; 3 na nchi ya Araba mpaka bahari ya Kinerethi, kuelekea mashariki, tena mpaka bahari ya Ataba, mpaka Bahari ya Chumvi, kwendea mashariki, njia ya kwendea Beth-yeshimothi; tena upande wa kusini, chini ya matelemko ya Pisga; 4 tena mpaka wa Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa wa hayo mabaki ya hao Warefai, aliyekaa Ashtarothi na Edrei, 5 naye alitawala katika mlima wa Hermoni, na katika Saleka, na katika Bashani yote, hata mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na nusu ya Gileadi, mpaka wa huyo Sihoni mfalme wa Heshboni. 6 Musa mtumishi wa Bwana na wana wa Israeli wakawapiga; naye Musa mtumishi wa Bwana akawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase iwe urithi wao. 7 Hawa ni wafalme wa hiyo nchi ambao Yoshua na wana wa Israeli waliwapiga ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa magharibi, kutoka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka kilima cha Halaki, kilichoelekea Seiri; Yoshua naye akawapa kabila za Israeli iwe milki yao sawasawa na magawanyo yao; 8 katika nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika nchi ya Araba, na katika matelemko, na katika bara, na katika Negebu; nchi ya Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi; 9 mfalme wa Yeriko, mmoja; mfalme wa Ai, ulio karibu na Betheli, mmoja; 10 mfalme wa Yerusalemu, mmoja; mfalme wa Hebroni, mmoja; 11 mfalme wa Yarmuthi, mmoja; na mfalme wa Lakishi, mmoja; 12 mfalme wa Egloni, mmoja; na mfalme wa Gezeri, mmoja; 13 mfalme wa Debiri, mmoja; na mfalme wa Gederi, mmoja; 14 mfalme wa Horma, mmoja; na mfalme wa Aradi, mmoja; 15 mfalme wa Libna, mmoja; na mfalme wa Adulamu, mmoja; 16 mfalme wa Makeda, mmoja; na mfalme wa Betheli, mmoja; 17 mfalme wa Tapua, mmoja; na mfalme wa Heferi, mmoja; 18 mfalme wa Afeka, mmoja; na mfalme wa Lasharoni, mmoja; 19 mfalme wa Madoni, mmoja; na mfalme wa Hazori, mmoja; 20 mfalme wa Shimron-meroni, mmoja; na mfalme wa Akshafu, mmoja; 21 mfalme wa Taanaki, mmoja; na mfalme wa Megido, mmoja; 22 na mfalme wa Kedeshi, mmoja; mfalme wa Yokneamu wa Karmeli, mmoja; 23 mfalme wa Dori katika kilima cha Dori, mmoja; na mfalme wa makabila katika Gilgali, mmoja; 24 na mfalme wa Tirsa, mmoja; wafalme hao wote walikuwa ni thelathini na mmoja.

Yoshua 13

1 Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, Bwana akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa. 2 Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote; 3 kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi, 4 upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori; 5 na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi; 6 na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru. 7 Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila kenda, na nusu ya kabila ya Manase. 8 Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa Bwana alivyowapa; 9 kutoka huko Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulio pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni; 10 na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni; 11 na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka; 12 ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza. 13 Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hata siku hii ya leo. 14 Lakini hakuwapa watu wa kabila ya Lawi urithi uwao wote; maana sadaka za Bwana, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia. 15 Musa akawapa kabila ya wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao. 16 Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba; 17 na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni; 18 na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi; 19 na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde; 20 na Beth-peori, na nchi za matelemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi; 21 na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao mashehe wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo. 22 Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua. 23 Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na mpaka wake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. 24 Musa akawapa kabila ya Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao. 25 Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba; 26 tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hata mpaka wa Debiri; 27 tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na mpaka wake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki. 28 Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. 29 Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila ya Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila ya wana wa Manase sawasawa na jamaa zao. 30 Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini; 31 na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao. 32 Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng'ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki. 33 Lakini Musa hakuwapa kabila ya Lawi urithi uwao wote; yeye Bwana, Mungu wa Israeli, ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.

Yoshua 14

1 Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa kabila za Israeli, waliwagawanyia, 2 kwa kuandama hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hizo kabila kenda, na hiyo nusu ya kabila. 3 Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hizo kabila mbili na nusu, ng'ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi uwao wote kati yao. 4 Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa kabila mbili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya wanyama wao wa mifugo, na kwa ajili ya riziki zao. 5 Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi. 6 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. 7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. 8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu. 9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu. 10 Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. 11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. 12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena. 13 Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake. 14 Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu. 15 Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.

Yoshua 15

1 Kura ya kabila ya wana wa Yuda kwa kuandama jamaa zao ilikuwa kufikilia hata mpaka wa Edomu, hata bara ya Sini upande wa kusini, huko mwisho upande wa kusini. 2 Mpaka wao wa kusini ulikuwa kutoka mwisho wa Bahari ya Chumvi, kutoka ile hori ielekeayo kusini; 3 nao ukaendelea upande wa kusini wa kukwea kwenda Akrabimu, kisha ukaendelea hata Sini, kisha ukaenda upande wa kusini wa Kadesh-barnea, kisha ukaendelea karibu na Hesroni, kisha ukafikilia Adari, na kuzunguka kwendea Karka; 4 kisha ukaendelea hata Azmoni, na kutokea hapo penye kijito cha Misri; na matokeo ya huo mpaka yalikuwa baharini; huu ndio mpaka wenu wa upande wa kusini. 5 Na mpaka wa upande wa mashariki ulikuwa Bahari ya Chumvi, hata mwisho wa mto wa Yordani. Na mpaka wa upande wa kaskazini ulikuwa kutoka pale penye hori ya baharini mwisho wa mto wa Yordani; 6 na huo mpaka ukaendelea hata Beth-hogla, kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Beth-araba; kisha mpaka ukaendelea hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni; 7 kisha mpaka ukaendelea hata Debiri kutoka bonde la Akori, vivyo ukaendelea upande wa kaskazini, kwa kuelekea Gilgali, iliyo mkabala wa kukwelea kwenda Adumimu, ulio upande wa kusini wa mto; kisha huo mpaka ukaendelea hata ukafikilia maji ya Enshemeshi, na matokeo yake yalikuwa hapo Enrogeli; 8 kisha mpaka ukaendelea karibu na bonde la mwana wa Hinomu, na kufikilia ubavuni mwa huyu Myebusi upande wa kusini (ndio Yerusalemu); kisha mpaka ukaendelea hata kilele cha mlima ulio pale mkabala wa bonde la Hinomu upande wa magharibi, lililo pale mwisho wa bonde la Warefai upande wa kaskazini; 9 kisha mpaka ulipigwa kutoka juu ya mlima huo hata kufikilia chemchemi ya maji ya Neftoa kisha ukatokea hata miji ya kilima cha Efroni; kisha mpaka ulipigwa hata kufikilia Baala (ndio Kiriath-yearimu); 10 kisha mpaka ukazunguka kutoka Baala kwendelea upande wa magharibi hata kilima Seiri, kisha ukaendelea hata upande wa mlima wa Yearimu upande wa kaskazini (huo ndio Kesaloni), kisha ukatelemkia Beth-shemeshi, na kwendelea karibu na Timna; 11 kisha mpaka ukatokea hata kufikilia upande wa Ekroni upande wa kaskazini; tena mpaka ulipigwa hata Shikroni, na kwendelea hata kilima cha Baala, kisha ukatokea hapo Yabneeli; na matokeo ya mpaka yalikuwa baharini. 12 Na mpaka wa upande wa magharibi ulifikilia hata bahari kubwa, na mpaka wake. Huo ndio mpaka wa wana wa Yuda kwa kuzunguka kote kote sawasawa na jamaa zao. 13 Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama Bwana alivyomwamuru Yoshua, maana ni Kiriath-arba, ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki (huo ndio Hebroni). 14 Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki. 15 Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi. 16 Kalebu akasema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe. 17 Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe. 18 Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Wataka nini? 19 Huyo mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa umeniweka katika nchi ya kusini, unipe na chemchemi za maji pia. Ndipo akampa chemchemi za maji ya juu, na chemchemi za maji ya chini. 20 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Yuda sawasawa na jamaa zao. 21 Miji ya mwisho ya kabila ya wana wa Yuda upande wa kuelekea mpaka wa Edomu katika nchi ya Negebu ilikuwa ni Kabseeli, na Ederi, na Yaguri; 22 na Kina, na Dimona, na Adada; 23 na Kedeshi, na Hazori, na Ithnani; 24 na Zifu, na Telemu, na Bealothi; 25 na Hazor-hadata, na Kerioth-hezroni (ndio Hazori); 26 na Amamu, na Shema, na Molada; 27 na Hasar-gada, na Heshmoni, na Bethpeleti; 28 na Hasarshuali, na Beer-sheba, na Biziothia; 29 na Baala, na Iyimu, na Esemu; 30 na Eltoladi, na Kesili, na Horma; 31 na Siklagi, na Madmana, na Sansana; 32 na Lebaothi, na Shilhimu, na Aini, na Rimoni; miji hiyo yote ni miji ishirini na kenda, pamoja na vijiji vyake. 33 Katika nchi ya Shefela, Eshtaoli, na Sora, na Ashna, 34 na Zanoa, na Enganimu, na Tapua, na Enamu; 35 na Yarmuthi, na Adulamu, na Soko, na Azeka; 36 na Shaarimu, na Adithaimu, na Gedera, na Gederothaimu miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. 37 Senani, na Hadasha, na Migdal-gadi; 38 na Dilani, na Mispe, na Yoktheeli; 39 na Lakishi, na Boskathi, na Egloni; 40 na Kaboni, na Lamasi, na Kithilishi; 41 na Gederothi, na Beth-dagoni, na Naama, na Makeda; miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake. 42 Libna, na Etheri, na Ashani; 43 na Yifta, na Ashna, na Nesibu; 44 na Keila, na Akizibu, na Maresha; miji kenda, pamoja na vijiji vyake. 45 Ekroni, pamoja na miji yake na vijiji vyake; 46 kutoka huko Ekroni mpaka baharini, yote iliyokuwa upande wa Ashdodi, pamoja na vijiji vyake. 47 Ashdodi, na miji yake na vijiji vyake; na Gaza, na miji yake na vijiji vyake; mpaka kijito cha Misri, na bahari kubwa, na mpaka wake. 48 Na katika nchi ya vilima, Shamiri, na Yatiri, na Soko; 49 na Dana, na Kiriath-sana (ambao ni Debiri); 50 na Anabu, na Eshtemoa, na Animu; 51 na Gosheni, na Holoni, na Gilo; miji kumi na mmoja, pamoja na vijiji vyake. 52 Arabu, na Duma, na Eshani; 53 na Yanumu, na Beth-tapua, na Afeka; 54 na Humta, na Kiriath-arba (ndio Hebroni), na Siori; miji kenda, pamoja na vijiji vyake. 55 Maoni, na Karmeli, na Zifu, na Yuta; 56 na Yezreeli, na Yokdeamu, na Zanoa; 57 na Kaini, na Gibea, na Timna; miji kumi, pamoja na vijiji vyake. 58 Halhuli, na Bethsuri, na Gedori; 59 na Maarathi, na Bethanothi, Eltekoni; miji sita, pamoja na vijiji vyake. 60 Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), na Raba; miji miwili, pamoja vijiji vyake. 61 Huko nyikani, Betharaba, na Midini, na Sekaka; 62 na Nibshani, na huo Mji wa Chumvi, na Engedi; miji sita, pamoja na vijiji vyake. 63 Tena katika habari ya Wayebusi, hao wenye kukaa Yerusalemu, wana wa Yuda hawakuweza kuwatoa; lakini hao Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Yuda huko Yerusalemu hata hivi leo.

Yoshua 16

1 Kura ya wana wa Yusufu ilianza kutoka mto wa Yordani hapo Yeriko, hapo penye maji ya Yeriko upande wa mashariki, maana, ni hiyo nyika, kukwea kutoka Yeriko kati ya hiyo nchi ya vilima mpaka Betheli; 2 kisha ikatoka huko Betheli kwendelea Luzu, kisha ikaendelea hata kuufikilia mpaka wa Waarki mpaka Atarothi; 3 kisha ikatelemkia upande wa magharibi hata kuufikilia mpaka wa Wayafleti, hata mpaka wa Beth-horoni ya chini, hata kufikilia Gezeri; na matokeo yake yalikuwa hapo baharini. 4 Na wana wa Yusufu, Manase na Efraimu, walitwaa urithi wao. 5 Na mpaka wa wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao ulikuwa hivi; mpaka na urithi wao upande wa mashariki ulikuwa ni Ataroth-adari, hata Beth-horoni wa juu; 6 kisha mpaka ukatokea kwendelea upande wa magharibi huko Mikmeta upande wa kaskazini; kisha mpaka ukazunguka kwendea upande wa mashariki hata Taanath-shilo, kisha ukaendelea upande wa mashariki wa Yanoa; 7 kisha ulitelemka kutoka Yanoa hata Atarothi, na Naara, kisha ukafikilia Yeriko, na kutokea hapo penye mto wa Yordani. 8 Kutoka hapo Tapua mpaka ukaendelea upande wa magharibi hata kijito cha Kana; na matokeo yake yalikuwa baharini. Huo ndio urithi wa hao wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao; 9 pamoja na ile miji iliyotengwa kwa ajili ya wana wa Efraimu katikati ya urithi wa hao wana wa Manase, miji yote pamoja na vijiji vyake. 10 Nao hawakuwatoa Wakanaani waliokuwa Wakikaa Gezeri; lakini hao Wakanaani waliketi kati ya Efraimu, hata hivi leo, wakawa watumishi wa kufanya kazi za shokoa.

Yoshua 17

1 Kisha hii ndiyo kura iliyoiangukia kabila ya Manase; maana, yeye alikuwa ni mzaliwa wa kwanza, wa Yusufu. Katika habari za Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, babaye Gileadi, kwa sababu alikuwa mtu wa vita, basi alikuwa na Gileadi na Bashani. 2 Na kura ilikuwa ni ya hao wana wa Manase waliosalia kwa kuandama jamaa zao; kwa wana wa Abiezeri, na kwa wana wa Heleki, na kwa wana wa Asrieli, na kwa wana wa Shekemu, na kwa wana wa Heferi, na kwa wana wa Shemida; hao ndio wana waume wa Manase, mwana wa Yusufu, kwa kuandama jamaa zao. 3 Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa. 4 Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, Bwana alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya Bwana akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao. 5 Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng'ambo ya Yordani; 6 kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia. 7 Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hata Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kuume, hata kuwafikilia wenyeji wa Entapua. 8 Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu. 9 Tena mpaka ulitelemkia mpaka kijito cha Kana, upande wa kusini wa hicho kijito; miji hiyo ilikuwa ya Efraimu kati ya miji ya Manase; na mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa hicho kijito, na matokeo yake yalikuwa baharini; 10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafikilia hata Asheri upande wa kaskazini, na kufikilia hata Isakari upande wa mashariki. 11 Tena Manase alikuwa na miji katika Isakari na katika Asheri, nayo ni hii, Bethsheani na vijiji vyake, na Ibleamu na miji yake, na wenyeji wa Dori na miji yake, na wenyeji wa Endori na miji yake, na wenyeji wa Taanaki na miji yake, na wenyeji wa Megido na miji yake, hata mahali patatu palipoinuka. 12 Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa miji hiyo; bali hao Wakanaani walijikaza ili wakae katika nchi hiyo. 13 Kisha ikawa, hapo hao wana wa Israeli walipokuwa wamepata nguvu zaidi, ndipo wakawatenza nguvu hao Wakanaani wafanye kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa. 14 Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu Bwana amenibarikia hata hivi sasa? 15 Yoshua akawaambia, Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi. 16 Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia. 17 Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu; 18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.

Yoshua 18

1 Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. 2 Zilisalia katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao. 3 Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi. 5 Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini. 6 Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya Bwana, Mungu wetu. 7 Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa Bwana ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa Bwana. 8 Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za Bwana huko Shilo. 9 Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika chuo, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua maragoni huko Shilo. 10 Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za Bwana katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao. 11 Kisha ilizuka kura ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa hiyo kura yao ukatokea kati ya wana wa Yuda na wana wa Yusufu. 12 Mpaka wao upande wa kaskazini ulikuwa kutoka mto wa Yordani; kisha mpaka ukaendelea kufikilia ubavuni mwa mji wa Yeriko upande wa kaskazini, kisha ukaendelea kati ya nchi ya vilima kwa kuelekea upande wa magharibi; na matokeo yake yalikuwa hapo penye nyika ya Bethaveni. 13 Kisha mpaka ukaendelea kutoka hapo na kufikilia mji wa Luzu, ubavuni mwa Luzu (ndio Betheli), kwa upande wa kusini; kisha mpaka ukatelemkia Ataroth-adari, karibu na mlima ulio upande wa kusini wa Beth-horoni wa chini. 14 Kisha mpaka uliendelea na kuzunguka upande wa magharibi wa kuelekea kusini, kutoka huo mlima ulio mkabala wa Beth-horoni upande wa kusini; na matokeo yake yalikuwa hapo Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), ni mji wa wana wa Yuda; huo ndio upande wa magharibi. 15 Na upande wa kusini ulikuwa ukitoka upande wa mwisho wa Kiriath-yearimu, na mpaka ukatokea upande wa magharibi, ukaendelea hata chemchemi ya maji, pale Neftoa; 16 kisha mpaka ulitelemka hata mwisho wa mlima ulio pale mkabala wa bonde la mwana wa Hinomu, lililo pale katika bonde la Warefai, upande wa kaskazini; nao ukatelemkia mpaka bonde la Hinomu, hata ubavuni mwa Myebusi upande wa kusini, kisha ukatelemka hata Enrogeli, 17 kisha ulipigwa upande wa kaskazini, nao ukatokea hapo Enshemeshi, ukatokea hata kufikilia Gelilothi, ambao ni mkabala wa makweleo ya Adumimu; kisha ulitelemka hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni; 18 kisha ukaendelea mbele ubavuni kuikabili Araba, upande wa kuelekea kaskazini, nao ukatelemka hata hiyo Araba; 19 kisha mpaka ukaendelea mbele ubavuni mwa Beth-hogla upande wa kaskazini; na matokeo ya mpaka yalikuwa katika ile hori ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, mwisho wa kusini wa mto wa Yordani; huo ndio mpaka wa upande wa kusini. 20 Na mto wa Yordani ulikuwa ndio mpaka wake upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini, kwa kuandama mipaka yake kwa kuuzunguka kote kote, sawasawa na jamaa zao. 21 Basi miji ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni Yeriko, na Beth-hogla, na Emek-kesisi, 22 na Bethiaraba, na Semaraimu, na Betheli; 23 na Avimu, na Para, na Ofra; 24 na Kefar-amoni, na Ofni, na Geba; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake; 25 na Gibeoni, na Rama, na Beerothi; 26 na Mispa, na Kefira, na Moza; 27 na Rekemu, na Irpeeli, na Tarala; 28 na Zela, na Elefu, na huyo Myebusi (ndio Yerusalemu), na Gibeathi, na Kiriathi; miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao. Yoshua, Chapter 1Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. 2 Zilisalia katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao. 3 Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi. 5 Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini. 6 Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya Bwana, Mungu wetu. 7 Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa Bwana ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa Bwana. 8 Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za Bwana huko Shilo. 9 Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika chuo, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua maragoni huko Shilo. 10 Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za Bwana katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao. 11 Kisha ilizuka kura ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa hiyo kura yao ukatokea kati ya wana wa Yuda na wana wa Yusufu. 12 Mpaka wao upande wa kaskazini ulikuwa kutoka mto wa Yordani; kisha mpaka ukaendelea kufikilia ubavuni mwa mji wa Yeriko upande wa kaskazini, kisha ukaendelea kati ya nchi ya vilima kwa kuelekea upande wa magharibi; na matokeo yake yalikuwa hapo penye nyika ya Bethaveni. 13 Kisha mpaka ukaendelea kutoka hapo na kufikilia mji wa Luzu, ubavuni mwa Luzu (ndio Betheli), kwa upande wa kusini; kisha mpaka ukatelemkia Ataroth-adari, karibu na mlima ulio upande wa kusini wa Beth-horoni wa chini. 14 Kisha mpaka uliendelea na kuzunguka upande wa magharibi wa kuelekea kusini, kutoka huo mlima ulio mkabala wa Beth-horoni upande wa kusini; na matokeo yake yalikuwa hapo Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), ni mji wa wana wa Yuda; huo ndio upande wa magharibi. 15 Na upande wa kusini ulikuwa ukitoka upande wa mwisho wa Kiriath-yearimu, na mpaka ukatokea upande wa magharibi, ukaendelea hata chemchemi ya maji, pale Neftoa; 16 kisha mpaka ulitelemka hata mwisho wa mlima ulio pale mkabala wa bonde la mwana wa Hinomu, lililo pale katika bonde la Warefai, upande wa kaskazini; nao ukatelemkia mpaka bonde la Hinomu, hata ubavuni mwa Myebusi upande wa kusini, kisha ukatelemka hata Enrogeli, 17 kisha ulipigwa upande wa kaskazini, nao ukatokea hapo Enshemeshi, ukatokea hata kufikilia Gelilothi, ambao ni mkabala wa makweleo ya Adumimu; kisha ulitelemka hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni; 18 kisha ukaendelea mbele ubavuni kuikabili Araba, upande wa kuelekea kaskazini, nao ukatelemka hata hiyo Araba; 19 kisha mpaka ukaendelea mbele ubavuni mwa Beth-hogla upande wa kaskazini; na matokeo ya mpaka yalikuwa katika ile hori ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, mwisho wa kusini wa mto wa Yordani; huo ndio mpaka wa upande wa kusini. 20 Na mto wa Yordani ulikuwa ndio mpaka wake upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini, kwa kuandama mipaka yake kwa kuuzunguka kote kote, sawasawa na jamaa zao. 21 Basi miji ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni Yeriko, na Beth-hogla, na Emek-kesisi, 22 na Bethiaraba, na Semaraimu, na Betheli; 23 na Avimu, na Para, na Ofra; 24 na Kefar-amoni, na Ofni, na Geba; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake; 25 na Gibeoni, na Rama, na Beerothi; 26 na Mispa, na Kefira, na Moza; 27 na Rekemu, na Irpeeli, na Tarala; 28 na Zela, na Elefu, na huyo Myebusi (ndio Yerusalemu), na Gibeathi, na Kiriathi; miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao.

Yoshua 19

1 Kisha kura ya pili ilitokea kwa ajili ya Simeoni, maana, kwa ajili ya hiyo kabila ya wana wa Simeoni, kwa kuandama jamaa zao; na urithi wao ulikuwa katikati ya urithi wa wana wa Yuda. 2 Miji waliyokuwa nayo katika urithi wao ni Beer-sheba, na Sheba, na Molada; 3 na Hasarshuali, na Bala, na Esemu; 4 na Eltoladi, na Bethuli, na Horma; 5 na Siklagi, na Bethmarkabothi, na Hasarsusa; 6 na Bethlebaothi, na Sharuheni; miji kumi na mitatu, pamoja na vijiji vyake; 7 na Aini, na Rimoni, na Etheri, na Ashani; miji minne, pamoja na vijiji vyake; 8 tena vijiji vyote vilivyozunguka miji hiyo kote kote mpaka Baalath-beeri, Rama wa Kusini. Huo ndio urithi wa kabila ya wana wa Simeoni kwa kuandama jamaa zao. 9 Huo urithi wa hao wana wa Simeoni ulitoka katika fungu la wana wa Yuda; kwa maana hilo fungu la wana wa Yuda lilikuwa ni kubwa mno kwao; kwa hiyo wana wa Simeoni walikuwa na urithi katikati ya urithi wao. 10 Kisha kura ya tatu ilitokea kwa ajili ya wana wa Zabuloni kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa urithi wao ulifikilia hata Saridi; 11 kisha mpaka wao ukakwea kwendelea upande wa magharibi, hata kufikilia Marala, nao ukafikilia hata Dabeshethi; nao ukafikilia kijito cha maji kilicho mkabala wa Yokneamu; 12 kisha ukazunguka kutoka Saridi kwendelea upande wa mashariki kwa kuelekea maawio ya jua hata kufikilia mpaka wa Kisiloth-ubori; kisha ukatokea hata Daberathi, kisha ukakwea kwendelea Yafia; 13 kutoka hapo ukaendelea kuelekea mashariki mpaka Gath-heferi, hata kufikilia Ethkasini; kisha ukatokea huko Rimoni ufikiliao hata Nea; 14 kisha mpaka uliizunguka nchi hiyo kwa upande wa kaskazini hata Hanathoni; kisha matokeo yake yalikuwa katika bonde la Iftaeli; 15 na Katathi, na Nahalali, na Shimroni, na Idala, na Bethlehemu; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake. 16 Huu ndio urithi wa wana wa Zabuloni kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake. 17 Kisha kura ya nne ilitokea kwa ajili ya Isakari, maana, ni kwa ajili ya wana wa Isakari kwa kuandama jamaa zao. 18 Na mpaka wao ulifikilia Yezreeli, na Kesulothi, na Shunemu; 19 na Hafaraimu, na Shioni, na Anaharathi; 20 na Rabithu, na Kishioni, na Ebesi; 21 na Remethi, na Enganimu, na Enhada, na Bethpasesi; 22 na mpaka ukafikilia hata Tabori, na Shahasuma na Bethshemeshi; na matokeo ya mpaka wao yalikuwa katika mto wa Yordani; miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake. 23 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Isakari kwa kuandama jamaa zao; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. 24 Kisha kura ya tano ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao. 25 Na mpaka wao ulikuwa ni Helkathi, na Hali, na Beteni, na Akishafu; 26 na Alameleki, na Amadi, na Mishali; nao ukafikilia hata Karmeli upande wa magharibi, tena ulifikilia hata Shihor-libnathi; 27 kisha ukazunguka kuelekea maawio ya jua mpaka Beth-dagoni, nao ukafikilia hata Zabuloni, tena mpaka bonde la Iftaeli upande wa kaskazini hata Bethemeki na Neyeli; kisha ukatokea hata Kabuli upande wa kushoto; 28 na Ebroni, na Rehobu, na Hamoni, na Kana, hata kufikilia Sidoni mkuu; 29 kisha mpaka ulizunguka kuelekea Rama, na mji wa Tiro ulio na boma; kisha mpaka ulizunguka kuelekea Hosa; na matokeo yake yalikuwa baharini katika nchi ya Akzibu; 30 na Uma pia, na Afeka, na Rehobu; miji ishirini na miwili, pamoja na vijiji vyake. 31 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake. 32 Kisha kura ya sita ikatokea kwa ajili ya wana wa Naftali, maana, ni kwa ajili ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao. 33 Na mpaka wao ulikuwa kutoka Helefu, tokea ule mwaloni ulio katika Saananimu, na Adami-nekebu, na Yabineeli, hata kufikilia Lakumu; na matokeo yake yalikuwa katika mto wa Yordani; 34 tena mpaka ulizunguka kwendelea upande wa magharibi hata Aznoth-tabori, tena kutoka hapo ukaendelea mpaka Hukoki; kisha ukafikilia hata Zabuloni upande wa kusini, tena ulifikilia hata Asheri upande wa magharibi, tena ulifikilia hata Yuda hapo katika mto wa Yordani kwa upande wa kuelekea maawio ya jua. 35 Na miji yenye boma ilikuwa ni hii, Sidimu, na Seri, na Hamathi, na Rakathi, na Kinerethi; 36 na Adama, na Rama, na Hazori; 37 na Kedeshi, na Edrei, na Enhasori; 38 na Ironi, na Migdal-eli, na Horemu, na Bethanathi, na Bethshemeshi; miji kumi na kenda, pamoja na vijiji vyake. 39 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao; miji hiyo pamoja na vijiji vyake. 40 Kisha kura ya saba ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Dani kwa kuandama jamaa zao. 41 Na mpaka wa urithi wao ulikuwa ni Sora, na Eshtaoli, na Irishemeshi; 42 na Shaalabini, na Aiyaloni, na Ithla; 43 na Eloni, na Timna, na Ekroni; 44 na Elteka, na Gibethoni, na Baalathi; 45 na Yehudi, na Bene-beraki, na Gathrimoni; 46 na Meyarkoni, na Rakoni, pamoja na huo mpaka uliokuwa mkabala wa Yafa. 47 Kisha mpaka wa wana wa Dani ulitokea kuwapita wao; kwa kuwa hao wana wa Dani wakakwea na kupigana na Leshemu, na kuutwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na kuumiliki, nao wakakaa humo, wakauita Dani, kwa kuliandama jina la huyo Dani mzee wao. 48 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Dani kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake. 49 Basi wakamaliza hiyo kazi yao ya kuigawanya nchi iwe urithi kwa kuandama mipaka yake; kisha wana wa Israeli wakampa Yoshua, mwana wa Nuni, urithi katikati yao; 50 sawasawa na ile amri ya Bwana wakampa mji alioutaka, maana, ni Timnath-sera katika nchi ya vilima ya Efraimu; naye akaujenga huo mji na kukaa mumo. 51 Hizi ndizo nchi, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua huyo mwana wa Nuni, pamoja na hao vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli, walizigawanya kwa njia ya kupiga kura, ziwe urithi, huko Shilo mbele ya Bwana, hapo mlangoni mwa hema ya kukutania. Basi hivyo wakamaliza kazi ya kuigawanya hiyo nchi.

Yoshua 20

1 Kisha Bwana akanena na Yoshua, na kumwambia, 2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa; 3 ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu. 4 Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao. 5 Na kama huyo mwenye kujilipiza kisasi cha damu akimwandamia, ndipo hawatamtoa huyo mwuaji kumtia mkononi mwake huyo; kwa sababu alimpiga mwenziwe naye hakujua, wala hakumchukia tangu hapo. 6 Naye atakaa katika mji huo, hata hapo atakaposimama mbele ya mkutano kuhukumiwa, hata kifo chake kuhani mkuu mwenye kuwapo siku hizo; ndipo yule mwuaji atarudi, na kuuendea mji wake mwenyewe, na nyumba yake mwenyewe, hata mji huo alioutoka hapo alipokimbia. 7 Nao wakaweka Kedeshi katika Galilaya katika nchi ya vilima ya Naftali, na Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-arba (ndio Hebroni) katika nchi ya vilima ya Yuda. 8 Tena ng'ambo ya pili ya Yordani pande za Yeriko upande wa kuelekea mashariki wakaweka Bezeri ulioko nyikani, katika nchi tambarare ya kabila ya Reubeni, na Ramothi katika Gileadi katika kabila ya Gadi, na Golani katika Bashani katika kabila ya Manase. 9 Miji hiyo ndiyo miji iliyoamriwa kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa ajili ya mgeni akaaye kati yao ugenini, ili kwamba mtu awaye yote atakayemwua mtu pasipo kukusudia apate kimbilia huko, asife kwa mkono wa mwenye kujilipiza kisasi cha damu, hata hapo atakapokuwa amekwisha simama mbele ya mkutano.

Yoshua 21

1 Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea Eleazari, kuhani, na Yoshua, mwana wa Nuni, na hao waliokuwa vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli; 2 wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye Bwana aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, pamoja na malisho yake kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo. 3 Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na malisho yake, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya Bwana. 4 Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila ya Yuda, na katika kabila ya Simeoni, na katika kabila ya Benyamini. 5 Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Efraimu, na katika kabila ya Dani, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, miji kumi. 6 Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Isakari, na katika kabila ya Asheri, na katika kabila ya Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase huko Bashani, miji kumi na mitatu. 7 Na wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao walipata katika kabila ya Reubeni, na katika kabila ya Gadi, na katika kabila ya Zabuloni, miji kumi na miwili. 8 Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na malisho yake, kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa. 9 Kisha wakawapa katika kabila ya wana wa Yuda, na katika kabila ya wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina; 10 nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao. 11 Nao wakawapa Kiriath-arba, huyo Arba alikuwa baba yake Anaki, (ndio Hebroni), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na malisho yake yaliyouzunguka pande zote. 12 Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake. 13 Kisha wakawapa wana wa Haruni kuhani Hebroni pamoja na malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake; 14 na Yatiri pamoja na malisho yake, na Eshtemoa pamoja na malisho yake; 15 na Holoni pamoja na malisho yake, na Debiri pamoja na malisho yake; 16 na Aini pamoja na malisho yake, na Yuta pamoja na malisho yake, na Bethshemeshi pamoja na malisho yake; miji kenda katika kabila hizo mbili. 17 Tena katika kabila ya Benyamini, Gibeoni pamoja na malisho yake, na Geba pamoja na malisho yake; 18 na Anathothi pamoja na malisho yake, na Almoni pamoja na malisho yake; miji minne. 19 Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake. 20 Na jamaa za wana wa Kohathi, Walawi, hao wana wengine wa Kohathi waliosalia, wao walikuwa na miji ya kura yao katika kabila ya Efraimu. 21 Nao wakawapa Shekemu pamoja na malisho yake, katika nchi ya vilima ya Efraimu, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Gezeri pamoja na malisho yake; 22 na Kibisaumu pamoja na malisho yake, na Beth-horoni pamoja na malisho yake, miji minne. 23 Tena katika kabila ya Dani Elteke pamoja na malisho yake, na Gibethoni pamoja na malisho yake; 24 na Aiyaloni pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji minne. 25 Tena katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Taanaki pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji miwili. 26 Miji yote ya jamaa za wana wa Kohathi waliosalia ilikuwa ni miji kumi, pamoja na malisho yake. 27 Tena wana wa Gershoni, katika jamaa za Walawi, waliwapa, katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Golani katika Bashani pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Beeshtera pamoja na malisho yake; miji miwili. 28 Tena katika kabila ya Isakari, Kishioni pamoja na malisho yake, na Daberathi pamoja na malisho yake; 29 na Yarmuthi pamoja na malisho yake, na Enganimu pamoja na malisho yake; miji minne. 30 Tena katika kabila ya Asheri, Mishali pamoja na malisho yake, na Abdoni pamoja na malisho yake; 31 na Helkathi pamoja na malisho yake, na Rehobu pamoja na malisho yake; miji minne. 32 Tena katika kabila ya Naftali, Kedeshi katika Galilaya pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Hamoth-dori pamoja na malisho yake, na Kartani pamoja na malisho yake; miji mitatu. 33 Miji yote ya Wagershoni kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake. 34 Tena jamaa za wana wa Merari, hao Walawi waliosalia, katika kabila ya Zabuloni, Yokneamu pamoja na malisho yake, na Karta pamoja na malisho yake, 35 na Dimna pamoja na malisho yake, na Nahalali pamoja na malisho yake; miji minne. 36 Tena katika kabila ya Reubeni, Bezeri pamoja na malisho yake, na Yahasa pamoja na malisho yake, 37 na Kedemothi pamoja na malisho yake, na Mefaathi pamoja na malisho yake; miji minne. 38 Tena katika kabila ya Gadi Ramothi katika Gileadi pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Mahanaimu pamoja na malisho yake; 39 na Heshboni pamoja na malisho yake, na Yazeri pamoja na malisho yake; jumla yake miji minne. 40 Miji hiyo yote ilikuwa ni miji ya wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao, ni hizo jamaa za Walawi zilizosalia; na kura yao ilikuwa ni miji kumi na miwili. 41 Miji yote ya Walawi iliyokuwa kati ya milki ya wana wa Israeli ilikuwa ni miji arobaini na minane, pamoja na malisho yake. 42 Miji hiyo kila mmoja ulikuwa pamoja na malisho yake, yaliyouzunguka pande zote; ndivyo ilivyokuwa katika miji hiyo yote. 43 Basi Bwana aliwapa Israeli nchi hiyo yote, ambayo aliapa kwamba atawapa baba zao; nao wakaimiliki, na kukaa mumo. 44 Kisha Bwana akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao. 45 Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo Bwana alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote.

Yoshua 22

1 Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, 2 naye akawaambia, Ninyi mmeyaandama hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa Bwana, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi; 3 hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya Bwana, Mungu wenu. 4 Na sasa yeye Bwana, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa Bwana, aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani. 5 Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa Bwana, aliwaamuru, kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote. 6 Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao. 7 Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng'ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia, 8 kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng'ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu. 9 Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya Bwana kwa mkono wa Musa. 10 Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa. 11 Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli. 12 Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao. 13 Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani; 14 na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli. 15 Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena, 16 Mkutano wote wa Bwana wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya Bwana? 17 Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa Bwana, 18 hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama Bwana? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi Bwana hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli. 19 Basi kwamba hiyo nchi ya milki yenu si tohara, ndipo ninyi vukeni na kuingia nchi ya milki yake Bwana, ambayo maskani ya Bwana inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi Bwana, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wetu. 20 Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake? 21 Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema, 22 Mungu, Mungu Bwana, naam, Mungu, Mungu Bwana, yeye yuajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya Bwana, (usituokoe hivi leo); 23 sisi kujijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumwandama Bwana; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye Bwana mwenyewe na alitake jambo hili; 24 au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hadhari sana, tena makusudi, huku tukisema, Katika siku zijazo wana wenu yamkini wakanena na wana wetu, na kusema, Ninyi mna nini na Bwana, yeye Mungu wa Israeli? 25 Kwa kuwa yeye Bwana ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati ya sisi na ninyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika Bwana; basi hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu wasimche Bwana. 26 Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote; 27 bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa Bwana mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika Bwana. 28 Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya Bwana, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi. 29 Mungu na atuzuie msimwasi Bwana, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya Bwana, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake. 30 Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana. 31 Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba Bwana yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya Bwana; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa Bwana. 32 Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari. 33 Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi. 34 Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye Bwana ndiye Mungu.

Yoshua 23

1 Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana, 2 Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu; 3 nanyi mmeona mambo yote ambayo Bwana, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi. 4 Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua. 5 Yeye Bwana, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama Bwana Mungu wenu, alivyowaambia. 6 Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto. 7 Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao; 8 bali shikamaneni na Bwana, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo. 9 Maana Bwana amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo. 10 Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana Bwana, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia. 11 Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu. 12 Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu; 13 jueni hakika ya kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi. 14 Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena Bwana, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa. 15 Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, Bwana, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika Bwana atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, Bwana Mungu wenu, aliyowapa. 16 Hapo mtakapolivunja agano la Bwana, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya Bwana itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.

Yoshua 24

1 Yoshua akawakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida wao nao wakahudhuria mbele za Mungu. 2 Yoshua akawaambia watu wote, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng'ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine. 3 Nami nikamtwaa Ibrahimu baba yenu toka ng'ambo ya Mto, nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani; nikaongeza uzao wake, nikampa Isaka. 4 Kisha nikampa huyo Isaka, Yakobo na Esau; nami nikampa Esau mlima Seiri aumiliki; Yakobo na watoto wake wakashuka Misri. 5 Kisha nikawatuma Musa na Haruni nikaipiga nchi ya Misri, kwa hayo yote niliyoyatenda kati yake; hatimaye nikawatoa ninyi. 6 Nikawatoa baba zenu watoke Misri; nanyi mkaifikilia bahari; Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka bahari ya Shamu. 7 Nao walipomlilia Bwana, akaweka giza kati ya ninyi na Wamisri, akaileta bahari juu yao, akawafunikiza; nayo macho yenu yaliyaona mambo niliyoyatenda huko Misri; kisha mkakaa jangwani siku nyingi. 8 Kisha nikawaleta na kuwaingiza katika nchi ya Waamori waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani; nao wakapigana nanyi; nikawatia mikononi mwenu, mkaimiliki nchi yao; nami nikawaangamiza mbele yenu. 9 Ndipo Balaki, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akainuka, akapigana na Israeli; tena akatuma watu akamwita Balaamu, mwana wa Beori, aje awalaani; 10 lakini sikukubali kumsikiliza Balaamu; kwa hiyo akafuliza kuwabarikia ninyi; basi nikawatoa katika mkono wake. 11 Nanyi mliuvuka Yordani, mkafika Yeriko; nao watu wa Yeriko wakapigana nanyi, Mwamori, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhiti, na Mgirgashi, na Mhivi, na Myebusi; nami nikawatia mikononi mwenu. 12 Nikatuma mavu mbele yenu, waliowafukuza mbele yenu hao wafalme wawili wa Waamori, si kwa upanga wako, wala kwa upinde wako. 13 Nami nimewapa ninyi nchi msiyoitendea kazi, na miji msiyoijenga, nanyi mmekaa humo; mnakula matunda ya mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda. 14 Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana. 15 Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana. 16 Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; 17 kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao. 18 Bwana ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana, maana yeye ndiye Mungu wetu. 19 Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia Bwana; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. 20 Kama mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema. 21 Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia Bwana. 22 Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua Bwana, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi. 23 Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa Bwana, Mungu wa Israeli. 24 Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, Bwana, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii. 25 Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu. 26 Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa Bwana. 27 Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya Bwana aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu. 28 Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake. 29 Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi. 30 Wakamzika katika mpaka wa urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. 31 Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana, aliyowatendea Israeli. 32 Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu. 33 Huyo Eleazari mwana wa Haruni naye akafa; wakamzika katika kilima cha Finehasi mwanawe, ambacho alipewa yeye katika nchi ya vilima ya Efraimu.

Waamuzi 1

1 Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao? 2 Bwana akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake. 3 Ndipo Yuda akamwambia Simeoni ndugu yake, Kwea wewe pamoja nami katika kura yangu, ili tupate kupigana na Wakanaani; kisha mimi nami nitakwenda pamoja nawe katika kura yako. Basi Simeoni akaenda pamoja naye. 4 Yuda akakwea; naye Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi. 5 Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi. 6 Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu. 7 Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko. 8 Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji. 9 Baadaye wana wa Yuda wakatelemka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi ya milimani, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela. 10 Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai. 11 Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.) 12 Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe. 13 Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa. 14 Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo? 15 Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini. 16 Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao. 17 Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma. 18 Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake. 19 Bwana alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma. 20 Kisha wakampa huyo Kalebu Hebroni, kama alivyonena Musa naye akawafukuza wale wana watatu wa Anaki. 21 Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mji wa Yerusalemu; bali Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Benyamini ndani ya Yerusalemu hata hivi leo. 22 Nyumba ya Yusufu nayo, wao nao walikwea kwenda juu ya Betheli; naye Bwana alikuwa pamoja nao. 23 Kisha mbari ya Yusufu wakatuma watu waende kuupeleleza Betheli. (Jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Luzu.) 24 Hao wapelelezi walimwona mtu atoka katika huo mji, wakamwambia, Tafadhali, utuonyeshe maingilio ya mji huu, nasi tutakutendea mema. 25 Basi akawaonyesha maingilio ya mji, nao wakaupiga huo mji kwa makali ya upanga; lakini huyo mtu walimwacha aende zake, na watu wote wa jamaa yake. 26 Huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akaliita jina la huo mji Luzu; nalo ndilo jina lake hata hivi leo. 27 Tena Manase hakuwatoa wenyeji wa Bethsheani na miji yake, wala hao waliokaa Taanaki na miji yake, wala hao waliokaa Dori na miji yake, wala hao waliokaa Ibleamu na miji yake, wala hao waliokaa Megido na miji yake; lakini hao Wakanaani walikuwa hawakukubali kuiacha nchi hiyo. 28 Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepata nguvu, ndipo walipowatia hao Wakanaani katika kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa. 29 Efraimu naye hakuwatoa Wakanaani waliokuwa wakikaa katika Gezeri; lakini Wakanaani walikaa ndani ya Gezeri kati yao. 30 Zabuloni naye hakuwatoa wenyeji wa Kitroni, wala hao waliokaa katika Nahalali; lakini Wakanaani walikaa kati yao, wakalazimishwa shokoa. 31 Asheri naye hakuwatoa wenyeji wa Aka, wala hao waliokaa Sidoni, wala hao wa Alabu, wala hao wa Akzibu, wala hao wa Helba, wala hao wa Afeka, wala hao wa Rehobu; 32 lakini Waasheri wakakaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; kwa kuwa hawakuwafukuza. 33 Naftali naye hakuwatoa wenyeji wa Bethshemeshi, wala hao waliokaa Bethanathi; lakini alikaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; pamoja na haya hao wenyeji wa Bethshemeshi, na wenyeji wa Bethanathi, wakawatumikia kazi ya shokoa. 34 Kisha Waamori waliwasukumiza wana wa Dani waende milimani; kwani hawakuwakubali kutelemkia bondeni; 35 lakini hao Waamori waliendelea kukaa katika kilima cha Heresi, na katika Aiyaloni, na katika Shaalbimu; pamoja na haya mkono wa hiyo nyumba ya Yusufu ulishinda, hata wakawalazimisha shokoa. 36 Mpaka wa Waamori ulikuwa tangu huko kupandia Akrabimu, tangu hilo jabali, na juu yake.

Waamuzi 2

1 Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi; 2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? 3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu. 4 Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia. 5 Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia Bwana sadaka huko. 6 Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi. 7 Watu hao wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya Bwana yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. 8 Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi. 9 Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. 10 Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli. 11 Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali. 12 Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika. 13 Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi. 14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao. 15 Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana. 16 Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara. 17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo. 18 Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua. 19 Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi. 20 Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu; 21 mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa; 22 ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda katika njia hiyo, au sivyo. 23 Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Waamuzi 3

1 Basi haya ndiyo mataifa ambao Bwana aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani; 2 ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule; 3 aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi. 4 Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za Bwana, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa. 5 Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi; 6 wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao. 7 Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakamsahau Bwana, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi. 8 Kwa hiyo hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane. 9 Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. 10 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu. 11 Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa. 12 Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za Bwana; naye Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana. 13 Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende. 14 Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane. 15 Lakini wana wa Israeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi. 16 Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la mkono wa kuume. 17 Kisha akamsongezea Egloni, mfalme wa Moabu, hiyo tunu; basi Egloni alikuwa ni mtu aliyewanda sana. 18 Naye hapo alipokuwa amekwisha kuisongeza hiyo tunu, akawapa ruhusa watu hao walioichukua tunu, wakaenda zao. 19 Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha. 20 Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake. 21 Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake; 22 hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma. 23 Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo. 24 Basi alipokuwa amekwisha toka nje, hao watumishi wake wakaenda; wakaona, na tazama, hiyo milango ya chumba ilikuwa imefungwa kwa ufunguo; nao wakasema, Hapana budi amejifunika miguu yake ndani ya chumba cha baridi. 25 Wakangoja hata wakatahayari; na tazama, hakuifungua milango ya chumba; basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka nchi, naye amekufa. 26 Naye Ehudi alikimbia hapo walipokuwa wakingoja, akapita huko kwenye sanamu, na kukimbilia Seira. 27 Ikawa, hapo alipofika akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, ndipo wana wa Israeli wakatelemka pamoja naye kutoka huko milimani, naye akawatangulia. 28 Akawaambia, Niandameni mimi; kwa kuwa Bwana amewatia adui zenu, Wamoabi, mikononi mwenu. Basi wakatelemka na kumfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha Wamoabi, wala hawakumwacha mtu kuvuka. 29 Wakati huo wakapiga katika Wamoabi watu waume wapata kama elfu kumi, ambao wote walikuwa wanene, na wote mashujaa; hakupona hata mtu mmoja. 30 Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini 31 Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng'ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.

Waamuzi 4

1 Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana. 2 Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake. 3 Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini. 4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. 5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue. 6 Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni? 7 Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako. 8 Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi. 9 Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi. 10 Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye. 11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi. 12 Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori. 13 Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia kenda, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni. 14 Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera katika mkono wako. Je! Bwana hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata. 15 Bwana akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu. 16 Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hata Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja. 17 Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni. 18 Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti. 19 Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika. 20 Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana. 21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa. 22 Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake. 23 Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo. 24 Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.

Waamuzi 5

1 Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema; 2 Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana. 3 Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli. 4 Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji. 5 Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli. 6 Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando. 7 Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli. 8 Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli? 9 Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini Bwana. 10 Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu. 11 Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya Bwana; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa Bwana waliposhuka malangoni. 12 Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu. 13 Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; Bwana alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa. 14 Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi. 15 Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. 16 Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni. 17 Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake. 18 Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni. 19 Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha. 20 Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera. 21 Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu. 22 Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu. 23 Ulaanini Merozi, alisema malaika wa Bwana, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia Bwana, Kumsaidia Bwana juu ya hao wenye nguvu. 24 Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani. 25 Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima. 26 Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake. 27 Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa. 28 Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia? 29 Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu. 30 Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka. 31 Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee Bwana.

Waamuzi 6

1 Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba 2 Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. 3 Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; 4 wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. 5 Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. 6 Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana. 7 Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani, 8 Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa; 9 nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao; 10 kisha niliwaambia, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu. 11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. 12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. 13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. 14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. 16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. 17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami. 18 Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi. 19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa. 20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo. 21 Ndipo malaika wa Bwana akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa Bwana akaondoka mbele ya macho yake. 22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso. 23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa. 24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri. 25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; 26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. 27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. 28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. 29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. 30 Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. 31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. 32 Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake. 33 Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. 34 Lakini roho ya Bwana ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata. 35 Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki. 36 Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema, 37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema. 38 Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji. 39 Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote. 40 Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.

Waamuzi 7

1 Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni. 2 Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa. 3 Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi. 4 Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda. 5 Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa. 6 Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji. 7 Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake. 8 Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni. 9 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako. 10 Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini; 11 nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini. 12 Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi. 13 Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini. 14 Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake. 15 Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu. 16 Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi. 17 Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika. 18 Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa Bwana, na kwa Gideoni. 19 Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao. 20 Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa Bwana na wa Gideoni. 21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza. 22 Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye Bwana akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi. 23 Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani. 24 Kisha Gideoni akapeleka wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, telemkeni juu ya Midiani, na kuyashika hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Basi watu waume wote wa Efraimu walikutana pamoja, wakayashika maji mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. 25 Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.

Waamuzi 8

1 Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? Hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana. 2 Lakini akawaambia, Je! Mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri? 3 Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo. 4 Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamepungukiwa na nguvu, lakini wawafuatia vivyo. 5 Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wanapungukiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani. 6 Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate? 7 Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo Bwana atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma. 8 Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu. 9 Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu. 10 Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga. 11 Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama. 12 Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote. 13 Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi. 14 Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba. 15 Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate? 16 Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo. 17 Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo. 18 Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme. 19 Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye Bwana alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi. 20 Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu. 21 Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao. 22 Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani. 23 Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye Bwana atatawala juu yenu. 24 Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.) 25 Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake. 26 Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao. 27 Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake. 28 Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni. 29 Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe. 30 Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi. 31 Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki. 32 Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri. 33 Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao. 34 Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka Bwana, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote; 35 wala hawakuifanyia mema nyumba ya Yerubaali, yaani Gideoni, kwa kuyafuata hayo mema yote aliyowafanyia Israeli.

Waamuzi 9

1 Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema, 2 Haya, neneni tafadhali masikioni mwa waume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo jema kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, watawale juu yenu, au kwamba mtu mmoja atawale juu yenu? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu. 3 Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu. 4 Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye. 5 Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha. 6 Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu. 7 Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi. 8 Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. 9 Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 10 Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. 11 Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? 12 Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. 13 Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? 14 Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu. 15 Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni. 16 Basi sasa ikiwa mmetenda kwa uaminifu na uelekevu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake; 17 (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatirisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani; 18 nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;) 19 basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi; 20 lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki. 21 Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye. 22 Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu. 23 Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu; 24 ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze. 25 Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang'anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa. 26 Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye. 27 Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki. 28 Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani? 29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje. 30 Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka. 31 Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako. 32 Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani; 33 kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi. 34 Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne. 35 Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia. 36 Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu. 37 Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu. 38 Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao. 39 Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki. 40 Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango. 41 Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu. 42 Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa. 43 Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga. 44 Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga. 45 Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi. 46 Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi. 47 Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja. 48 Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi. 49 Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake. 50 Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa. 51 Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji. 52 Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto. 53 Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake. 54 Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa. 55 Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake. 56 Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini; 57 uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

Waamuzi 10

1 Baada yake Abimeleki, akainuka Tola mwana wa Pua, mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, kuwaokoa Israeli; naye alikuwa akikaa Shamiri, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu. 2 Huyo akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na mitatu, akafa, akazikwa katika Shamiri. 3 Baada yake huyo akainuka Yairi, Mgileadi; naye akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na miwili. 4 Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi. 5 Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni. 6 Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye. 7 Hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni. 8 Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng'ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane. 9 Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana. 10 Ndipo wana wa Israeli wakamlilia Bwana, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali. 11 Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti? 12 Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao. 13 Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena. 14 Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu. 15 Wana wa Israeli wakamwambia Bwana Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu. 16 Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia Bwana; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli. 17 Wakati huo wana wa Amoni walikutana pamoja, wakapanga marago huko Gileadi. Wana wa Israeli nao wakajikusanya wakapanga marago Mispa. 18 Na hao watu, wakuu wa Gileadi, wakaambiana wao kwa wao, Je! Ni mtu yupi atakayeanza kupigana na wana wa Amoni? Yeye atakuwa ni kichwa juu ya wenyeji wote wa Gileadi.

Waamuzi 11

1 Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha. 2 Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine. 3 Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye. 4 Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli. 5 Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; 6 wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. 7 Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu? 8 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi. 9 Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu? 10 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye Bwana atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako. 11 Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya Bwana huko Mispa. 12 Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu? 13 Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata. 14 Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni; 15 akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni; 16 lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi; 17 ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi. 18 Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu. 19 Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu. 20 Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli. 21 Bwana, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo. 22 Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani. 23 Basi sasa yeye Bwana, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki? 24 Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye Bwana, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki. 25 Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao? 26 Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo? 27 Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye Bwana, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni. 28 Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea. 29 Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni. 30 Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, 31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. 32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake. 33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli. 34 Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye. 35 Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma. 36 Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia Bwana kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye Bwana amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni. 37 Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu. 38 Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani. 39 Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli, 40 kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka.

Waamuzi 12

1 Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako. 2 Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao. 3 Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, Bwana naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami? 4 Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, mnaokaa kati ya Efraimu, na kati ya Manase. 5 Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La; 6 ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu. 7 Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo. 8 Baada yake huyo, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. 9 Alikuwa na wana thelathini; na binti thelathini akawapeleka waende mahali pengine, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba. 10 Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu. 11 Baada yake huyo, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi. 12 Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni. 13 Baada yake huyo, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli. 14 Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wana-punda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane. 15 Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

Waamuzi 13

1 Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya Bwana, Bwana akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini. 2 Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto. 3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. 4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; 5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti. 6 Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake; 7 lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake. 8 Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa. 9 Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye. 10 Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile. 11 Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi. 12 Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini? 13 Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari. 14 Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze. 15 Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako. 16 Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea Bwana. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa Bwana. 17 Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza? 18 Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu? 19 Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea Bwana hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia. 20 Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi. 21 Lakini malaika wa Bwana hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa Bwana. 22 Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu. 23 Lakini mkewe akamwambia, Kama Bwana angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu. 24 Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. 25 Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.

Waamuzi 14

1 Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti. 2 Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe. 3 Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana. 4 Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la Bwana; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli. 5 Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. 6 Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya. 7 Basi akatelemka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana. 8 Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akageuka kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali. 9 Akatwaa asali mikononi mwake akaenda mbele, huku akila alipokuwa akienenda, akawafikilia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba. 10 Basi babaye akamtelemkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa vijana ndivyo walivyokuwa wakifanya. 11 Basi ikawa hapo walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye. 12 Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mwaweza kunionyesha katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo hapo nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini; 13 lakini msipoweza kunionyesha ndipo hapo ninyi mtanipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia. 14 Naye akawaambia, Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu. 15 Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atuonyeshe hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo? 16 Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, nami nikuambie wewe? 17 Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili. 18 Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali? Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba? Naye akawaambia, kwamba hamkulima na mtamba wangu,Hamngekitambua kitendawili changu. 19 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake. 20 Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.

Waamuzi 15

1 Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia. 2 Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake. 3 Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru. 4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili. 5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni. 6 Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto. 7 Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma. 8 Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu. 9 Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi. 10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi. 11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao. 12 Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia. 13 Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini. 14 Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. 15 Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; 16 Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu. 17 Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi. 18 Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa. 19 Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo. 20 Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.

Waamuzi 16

1 Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake. 2 Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua. 3 Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni. 4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila. 5 Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja. 6 Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe. 7 Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 8 Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo. 9 Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana. 10 Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani? 11 Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 12 Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi. 13 Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo. 14 Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung'oa ule msumari, na ule mtande. 15 Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi. 16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa. 17 Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu. 18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao. 19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka. 20 Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha. 21 Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. 22 Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake. 23 Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu. 24 Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu. 25 Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili. 26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea. 27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza. 28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili. 29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto. 30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake. 31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.

Waamuzi 17

1 Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, ambaye jina lake alikuwa akiitwa Mika. 2 Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizonyang'anywa, ambazo uliweka kiapo kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, mwanangu na abarikiwe na Bwana. 3 Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe. 4 Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika. 5 Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake. 6 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe. 7 Alikuwako mtu mmoja hirimu aliyetoka Bethlehemu-yuda, wa jamaa ya Yuda, aliyekuwa ni Mlawi, naye akakaa huko hali ya ugeni. 8 Mtu huyo akatoka katika huo mji, katika Bethlehemu-yuda, ili aende kukaa hali ya ugeni hapo atakapoona mahali; akafikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu katika safari yake, hata nyumba ya huyo Mika. 9 Mika akamwuliza, Watoka wapi wewe? Akamwambia, Mimi ni Mlawi wa Bethlehemu-yuda, nami naenda kukaa hali ya ugeni po pote nitakapoona mahali. 10 Mika akamwambia, kaa pamoja nami, uwe kwangu baba, tena kuhani, nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, na nguo ya kuvaa, na vyakula. Basi huyo Mlawi akaingia ndani. 11 Huyo Mlawi aliridhika kukaa na mtu huyo; kisha huyo hirimu akawa kwake kama wanawe mmojawapo. 12 Basi Mika akamweka wakfu huyo Mlawi, huyo hirimu, naye akawa kuhani wake, akakaa nyumbani mwa Mika. 13 Ndipo Mika akasema, Sasa najua ya kwamba Bwana atanitendea mema, kwa kuwa nina Mlawi kuwa kuhani wangu.

Waamuzi 18

1 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli. 2 Basi wana wa Dani wakatuma watu wa jamaa zao, watu watano katika hesabu yao yote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuiaua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hata nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko. 3 Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo hirimu, huyo Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Nawe wafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa? 4 Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake. 5 Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kwamba njia yetu tuiendeayo itafanikiwa. 6 Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea i mbele za Bwana. 7 Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote. 8 Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani? 9 Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo. 10 Hapo mtakapokwenda mtawafikilia watu wakaao salama salimini, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani. 11 Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli. 12 Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu. 13 Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika. 14 Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya. 15 Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake. 16 Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango. 17 Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita. 18 Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi? 19 Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli? 20 Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu. 21 Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao. 22 Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani. 23 Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii? 24 Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe? 25 Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako. 26 Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake. 27 Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao. 28 Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo. 29 Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Laisha. 30 Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila ya Wadani hata siku ya kuchukuliwa mateka hiyo nchi. 31 Basi wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga aliyoifanya Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.

Waamuzi 19

1 Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda. 2 Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne. 3 Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye. 4 Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko. 5 Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu. 6 Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi. 7 Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena. 8 Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili. 9 Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu. 10 Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye. 11 Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu. 12 Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea. 13 Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikilie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama. 14 Basi wakashika njia kwenda zao mbele; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini. 15 Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika njia kuu ya mji; kwa kuwa hapakuwa na mtu awaye yote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala. 16 Kisha, tazama, akatokea mtu mume mzee, atoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea hali ya ugeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini. 17 Naye alipovua macho yake, akamwona huyo mtu msafiri katika njia kuu ya mji; huyo mzee akamwuliza, Waenda wapi wewe? Nawe watoka wapi? 18 Akamwambia, Sisi twapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, twaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya Bwana wala hapana mtu anikaribishaye nyumbani mwake. 19 Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda zetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu cho chote. 20 Kisha huyo mzee alisema, Na iwe amani kwako; lakini na haya yaliyokupungukia na yawe juu yangu mimi lakini usilale njiani. 21 Basi akamtia ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa. 22 Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua. 23 Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu. 24 Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii. 25 Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake. 26 Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha. 27 Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria yake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa i pale kizingitini. 28 Akamwambia, Haya ondoka, twende zetu; lakini hakuna aliyemjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda mahali pake mwenyewe. 29 Naye alipokwisha kuingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria yake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli. 30 Basi ikawa, wote walioliona jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hata leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, mkanene.

Waamuzi 20

1 Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hata Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia Bwana huko Mispa. 2 Hao wakuu wa watu, maana wakuu wa kabila zote za Israeli, wakajihudhurisha katika huo mkutano wa watu wa Mungu, watu waume mia nne elfu waendao kwa miguu, wenye kutumia upanga. 3 Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulikuwaje kutendeka? 4 Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. 5 Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa. 6 Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli. 7 Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu. 8 Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake. 9 Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kwa kura kwenda kuupiga; 10 nasi tutatwaa watu kumi katika mia katika kabila zote za Israeli, na watu mia katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili kwamba, hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli. 11 Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja. 12 Kisha kabila za Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu? 13 Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili kwamba tupate kuwaua, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli. 14 Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli. 15 Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba. 16 Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose. 17 Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni watu waume mia nne elfu, wenye kutumia upanga; hao wote walikuwa ni watu wa vita. 18 Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? Bwana akawaambia, Yuda atakwea kwanza. 19 Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao juu ya Gibea. 20 Watu wa Israeli walitoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea. 21 Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakaangamiza hata nchi watu ishirini na mbili elfu katika Israeli siku hiyo. 22 Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza. 23 Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za Bwana hata jioni; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye. 24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili. 25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga. 26 Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana. 27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo, 28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako. 29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote. 30 Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya nyakati nyingine. 31 Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kupiga na kuua katika hao watu, wapata kama watu thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika hizo njia kuu, ambazo njia mojawapo huendelea Betheli, na njia ya pili huendelea Gibea, katika shamba. 32 Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu. 33 Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba. 34 Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakaja juu ya Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini hawakujua ya kuwa uovu ulikuwa karibu nao. 35 Bwana akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza watu waume ishirini na tano elfu na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga. 36 Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea. 37 Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na hao wenye kuvizia wakaenda wakaupiga huo mji wote kwa makali ya upanga. 38 Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji. 39 Nao watu wa Israeli walipogeuka katika vile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika vile vita vya kwanza. 40 Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, huo mji mzima ulikuwa wapaa juu katika moshi kwenda mbinguni. 41 Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walisitushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiliwa na uovu. 42 Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini vile vita vikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake. 43 Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyaga-kanyaga hapo walipopumzika, hata kufikilia Gibea upande wa maawio ya jua. 44 Wakaanguka watu wa Benyamini watu kumi na nane elfu, hao wote walikuwa ni watu waume mashujaa. 45 Kisha wakageuka na kukimbia upande wa nyika hata kulifikilia jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu watu waume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawapiga wengine wao watu elfu mbili. 46 Basi jumla ya watu wa Benyamini walioanguka siku ile walikuwa ni watu ishirini na tano elfu waliokuwa wanatumia upanga; wote hao walikuwa ni watu mashujaa. 47 Lakini watu waume mia sita wakageuka, wakakimbia upande wa nyikani mpaka jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne. 48 Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaitia moto.

Waamuzi 21

1 Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu awaye yote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini. 2 Basi hao watu wakafikilia Betheli, wakaketi kuko mbele ya Mungu hata jioni, nao wakainua sauti zao na kulia sana. 3 Wakasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, kwani jambo hili kuwa katika Israeli, ya kwamba hivi leo ni kabila moja limepunguka katika Israeli? 4 Kisha ikawa siku ya pili yake, hao watu wakaamka asubuhi na mapema, wakajenga madhabahu huko, wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. 5 Wana wa Israeli wakasema, Katika hizi kabila zote za Israeli ni ipi isiyofika katika mkutano kumkaribia Bwana? Kwa maana walikuwa wameweka kiapo kikuu katika habari za huyo asiyefika kumkaribia Bwana huko Mispa, huku wakisema, Hakika yake atauawa huyo. 6 Nao wana wa Israeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu yao Benyamini, wakasema, Kabila moja imekatiliwa mbali na Israeli hivi leo. 7 Tufanyeje sisi ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa tumeapa kwa Bwana ya kwamba hatutawapa binti zetu ili wawaoe? 8 Basi wakasema, Ni ipi katika kabila za Israeli ambayo haikufika mbele ya Bwana huko Mispa? Na tazama, hakuja mmoja maragoni aliyetoka Yabeshi gileadi aufikilie huo mkutano. 9 Kwa maana hapo watu walipohesabiwa, hakuwapo hata mtu mmoja katika wenyeji wa Yabesh-gileadi. 10 Basi mkutano walipeleka huko watu kumi na mbili elfu wa hao waliokuwa mashujaa sana, kisha wakawaamuru, wakisema, Endeni mkawapige wenyeji wa Yabesh-gileadi kwa makali ya upanga, na hata wanawake na watoto wadogo. 11 Na jambo mtakalotenda ni hili; mtamwangamiza kila mume kabisa, na kila mwanamke ambaye amelala na mume. 12 Nao wakapata katika wenyeji wa Yabesh-gileadi wanawali mia nne, ambao hawajamjua mtu mume kwa kulala naye; basi wakawaleta maragoni huko Shilo, ulioko katika nchi ya Kanaani. 13 Basi mkutano ukatuma watu na kunena na wana wa Benyamini waliokuwako huko katika jabali la Rimoni, wakawatangazia amani. 14 Basi Benyamini wakarudi wakati huo; nao wakawapa wale wanawake waliowaponya wali hai katika hao wanawake wa Yabesh-gileadi; lakini hawakuwatosha. 15 Nao watu wakaghairi kwa ajili ya Benyamini, kwa sababu Bwana alikuwa amefanya pengo katika hizo kabila za Israeli. 16 Ndipo hao wazee wa huo mkutano walisema, Je! Tufanyeje ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa wanawake wameangamizwa katika Benyamini? 17 Wakasema, Lazima kuwa urithi kwa hao wa Benyamini waliopona, isiwe kabila kufutika katika Israeli. 18 Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke. 19 Kisha wakasema, Angalieni, iko sikukuu ya Bwana mwaka baada ya mwaka katika Shilo, ulioko upande kaskazini wa Betheli, upande wa mashariki wa hiyo njia kuu iendeayo kutoka Betheli kwenda Shekemu, nao ni upande wa kusini wa Lebona. 20 Basi wakawaagiza hao wana wa Benyamini wakisema, Haya, endeni, mkaotee katika mashamba ya mizabibu, 21 mkaangalie, kisha tazameni, kwamba hao binti za Shilo watoka ili wacheze katika hiyo michezo, basi tokeni ninyi mizabibuni, nanyi kila mtu na amshike mkewe katika hao binti za Shilo, kisha rudini nchi ya Benyamini. 22 Kisha itakuwa, hapo baba zao au ndugu zao, watakapokuja kushitaki, sisi tutawaambia, Kwa ihisani yenu tupeni sisi; kwa kuwa hatukumtwalia kila mtu mkewe katika vita; wala ninyi hamkuwapa wao, au kama sivyo ninyi sasa mngekuwa na hatia. 23 Wana wa Benyamini wakafanya vivyo, wakajitwalia wake, sawasawa na hesabu yao, katika hao waliocheza, wakawachukua wakaenda nao; kisha wakaenda kuurudia urithi wao, na kuijenga miji na kuikaa. 24 Nao wana wa Israeli wakati huo wakaenda zao, kila mtu akaenda kwa kabila yake na kwa jamaa yake; nao wakatoka huko, waende kila mtu kuuendea urithi wake. 25 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.

Ruthu 1

1 Ikawa zamani za Waamuzi walipoamua, kulikuwa na njaa katika nchi. Akaondoka mtu mmoja wa Bethlehemu ya Yuda, akaenda kukaa katika nchi ya Moabu, yeye na mkewe na wanawe wawili. 2 Na jina la mtu huyo aliitwa Elimeleki, na jina la mkewe Naomi, na majina ya wanawe wawili Maloni na Kilioni, Waefrathi wa Bethlehemu ya Yuda. Wakafika nchi ya Moabu, wakakaa huko. 3 Akafa Elimeleki, mumewe Naomi; na yule mwanamke akasalia na wanawe wawili. 4 Nao wakaoa wake katika wanawake wa Moabu; na jina la mmoja aliitwa Orpa, na jina la wa pili Ruthuu. Wakakaa huko yapata miaka kumi. 5 Wakafa na Maloni na Kilioni wote wawili; na huyo mwanamke akawa amefiwa na wanawe wawili, na mumewe pia. 6 Ndipo alipoondoka, yeye na wakweze, ili kurudi kutoka nchi ya Moabu; maana huko katika nchi ya Moabu amesikia ya kwamba Bwana amewajilia watu wake na kuwapa chakula. 7 Basi akatoka pale alipokuwapo, na wakweze wawili pamoja naye; wakashika njia ili kurudi mpaka nchi ya Yuda. 8 Kisha Naomi akawaambia wakweze wawili, Nendeni sasa mkarejee kila mmoja nyumbani kwa mamaye; Bwana na awatendee mema ninyi, kama ninyi mlivyowatendea mema hao waliofariki na mimi pia. 9 Bwana na awajalie kuona raha kila mmoja nyumbani kwa mumewe. Kisha akawabusu; nao wakapaza sauti zao wakalia. 10 Wakamwambia, La, sivyo; lakini tutarudi pamoja nawe kwa watu wako. 11 Naye Naomi akasema, Enyi wanangu, mrejee; kwani kufuatana na mimi? Je! Mimi ninao watoto wa kiume tena tumboni mwangu, hata wawe waume zenu? 12 Enyi wanangu, mrejee; nendeni zenu; kwa kuwa mimi ni mzee, siwezi kupata mume tena. Kama ningesema, Natumaini; kama ningepata mume hata usiku huu, na kuzaa watoto wa kiume; 13 je! Mngesubiri hata watakapokuwa watu wazima? Mngejizuia msiwe na waume? La, sivyo, wanangu; maana ni vigumu kwangu kuliko kwenu, kwa sababu mkono wa Bwana umetoka juu yangu. 14 Nao wakapaza sauti zao, wakalia tena, na Orpa akambusu mkwewe, lakini Ruthuu akaambatana naye. 15 Naye akasema, Tazama, shemeji yako amerejea kwa watu wake, na kwa mungu wake; basi urejee wewe umfuate shemeji yako. 16 Naye Ruthuu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu; 17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami. 18 Basi alipomwona kuwa amekaza nia yake kufuatana naye, aliacha kusema naye. 19 Hivyo hao wakaendelea wote wawili hata walipofika Bethlehemu. Na ikawa walipofika Bethlehemu, mji wote ulitaharuki kwa habari zao. Nao wanawake wakasema, Je! Huyu ni Naomi? 20 Akawaambia, Msiniite Naomi niiteni Mara,kwa sababu Mwenyezi Mungu amenitenda mambo machungu sana. 21 Mimi nalitoka hali nimejaa, naye Bwana amenirudisha sina kitu, kwani kuniita Naomi, ikiwa Bwana ameshuhudia juu yangu, na Mwenyezi Mungu amenitesa? 22 Basi Naomi akarudi; pamoja na Ruthuu Mmoabi, mkwewe; ambao walirudi kutoka nchi ya Moabu; nao wakafika Bethlehemu mwanzo wa mavuno ya shayiri.

Ruthu 2

1 Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. 2 Naye Ruthuu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. 3 Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. 4 Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, Bwana akae nanyi. Nao wakamwitikia, Bwana na akubariki. 5 Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? 6 Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; 7 naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. 8 Basi Boazi akamwambia Ruthuu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. 9 Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. 10 Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? 11 Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. 12 Bwana akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. 13 Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. 14 Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. 15 Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. 16 Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. 17 Basi Ruthuu akaokota masazo kondeni hata jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. 18 Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonyesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa. 19 Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. 20 Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na Bwana, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. 21 Naye Ruthuu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na vijana wangu, hata watakapomaliza mavuno yangu yote. 22 Kisha Naomi akamwambia Ruthuu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, wala watu wasikukute katika konde linginelo lote. 23 Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hata mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.

Ruthu 3

1 Kisha Naomi akamwambia mkwewe, Je! Mwanangu, si vizuri nikutafutie raha, ili upate mema? 2 Basi na huyu Boazi, je! Siye wa mbari yetu, ambaye ulikuwapo pamoja na wasichana wake? Tazama, usiku wa leo atakuwa akipepeta shayiri pale ugani. 3 Basi wewe oga, ujipake mafuta ujivike mavazi yako, kisha uende kwenye uga; walakini usijionyeshe kwake mtu yule, ila atakapokwisha kula na kunywa. 4 Nayo itakuwa wakati atakapolala, utapaangalia mahali alalapo, nawe uingie, uifunue miguu yake ujilaze hapo; na yeye atakuambia utakalofanya. 5 Akamwambia, Hayo yote unenayo mimi nitayafanya. 6 Basi akashuka mpaka ugani; akafanya yote kama vile mkwewe alivyomwagiza. 7 Ikawa huyo Boazi alipokwisha kula na kunywa, na moyo wake umekunjuka, alikwenda kulala penye mwisho wa chungu ya nafaka; na huyo mwanamke akaja taratibu, akaifunua miguu yake, akajilaza papo hapo. 8 Na ikawa usiku wa manane yule mtu akasituka, akajigeuza; na kumbe! Yupo mwanamke amelala miguuni pake. 9 Akasema, Ama! Ni nani wewe? Akamjibu, Ni mimi, Ruthuu, mjakazi wako; uitande nguo yako juu ya mjakazi wako; kwa kuwa ndiwe wa jamaa aliye karibu. 10 Akamwambia, Mwanangu, ubarikiwe na Bwana; umezidi kuonyesha fadhili zako mwisho kuliko mwanzo, kwa vile usivyowafuata vijana, kama ni maskini kama ni matajiri. 11 Basi, mwanangu, usiogope; mimi nitakufanyia yote uyanenayo; kwa maana mji wote pia wa watu wangu wanakujua ya kwamba u mwanamke mwema. 12 Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi. 13 Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; Bwana aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi. 14 Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga. 15 Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini. 16 Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia. 17 Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu. 18 Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.

Ruthu 4

1 Basi Boazi akakwea kwenda mpaka langoni, akaketi pale; na tazama, yule mtu wa jamaa aliyekuwa karibu, ambaye Boazi amemnena, akapita. Naye akamwita, Haya! Wewe, karibu, uketi hapa. Naye akaja akaketi. 2 Kisha akatwaa watu kumi miongoni mwa wazee wa mji, akawaambia, Ninyi nanyi, ketini hapa. Wakaketi. 3 Kisha akamwambia yule jamaa, Huyu Naomi, aliyerudi hapa kutoka nchi ya Moabu, anauza sehemu ya ardhi aliyokuwa nayo ndugu yetu, Elimeleki; 4 nami ilikuwa nia yangu nikujulishe wewe, na kukuambia, Uinunue mbele ya hawa waliopo na mbele ya wazee wa watu wangu. Kama wewe utaikomboa, haya, uikomboe; lakini kama hutaikomboa, uniambie ili nijue mimi; kwa kuwa hakuna mtu wa kuikomboa ila wewe, na baada yako ni mimi. Naye akasema, Nitaikomboa mimi. 5 Ndipo Boazi aliposema, Siku ile utakapolinunua shamba mkononi mwa Naomi, unamnunua Ruthuu pia, huyu Mmoabi, mkewe marehemu, ili makusudi umwinulie marehemu jina katika urithi wake. 6 Basi yule jamaa aliyekuwa wa karibu akasema, Mimi sitaweza kulikomboa kwa nafsi yangu, nisije nikauharibu urithi wangu mwenyewe; basi haki yangu ya kulikomboa ujichukulie wewe, maana mimi sitaweza kulikomboa. 7 Basi hii ilikuwa desturi zamani za kale katika Israeli, kwa habari ya kukomboa na kubadiliana, ili kuyahakikisha yote; mtu huvua kiatu chake na kumpa mwenziwe; ndivyo walivyohakikisha neno katika Israeli. 8 Basi yule jamaa akamwambia Boazi, Wewe ujinunulie mwenyewe. Akavua kiatu chake. 9 Naye Boazi akawaambia wale wazee na watu wote, Leo hivi ninyi ni mashahidi ya kwamba mimi nimenunua yote yaliyokuwa ya Elimeleki, na yote yaliyokuwa ya Kilioni na Maloni, mkononi mwa Naomi. 10 Tena, huyu Ruthuu Mmoabi, mkewe Maloni, nimemnunua awe mke wangu, makusudi nipate kumwinulia marehemu jina katika urithi wake, jina lake marehemu lisikatike miongoni mwa ndugu zake, wala langoni pa mji wake; leo hivi ninyi ni mashahidi. 11 Na watu wote waliokuwapo langoni, na wale wazee, wakasema, Naam, sisi ni mashahidi. Bwana na amfanye mwanamke huyu aingiaye nyumbani mwako kuwa kama Raheli na kama Lea, wale wawili walioijenga nyumba ya Israeli. Nawe ufanikiwe katika Efrata, na kuwa mashuhuri katika Bethlehemu. 12 Nyumba yako na ifanane na nyumba yake Peresi, ambaye kwamba Tamari alimzalia Yuda, kwa wazao atakaokupa Bwana katika mwanamke huyu. 13 Basi Boazi akamtwaa Ruthuu, naye akawa mke wake; naye akaingia kwake, na Bwana akamjalia kuchukua mimba, naye akazaa mtoto wa kiume. 14 Nao wale wanawake wakamwambia Naomi, Na ahimidiwe Bwana, asiyekuacha leo hali huna wa jamaa aliye karibu; jina lake huyu na liwe kuu katika Israeli. 15 Naye atakurejezea uhai wako, na kukuangalia katika uzee wako; kwa maana mkweo, ambaye akupenda, naye anakufaa kuliko watoto saba, ndiye aliyemzaa. 16 Basi Naomi akamtwaa yule mtoto, akamweka kifuani pake, akawa mlezi wake. 17 Nao wale wanawake waliokuwa jirani zake wakampa jina, wakisema, Naomi amezaliwa mwana; wakamwita jina lake Obedi; yeye ndiye baba yake Yese, aliye baba yake Daudi. 18 Hivi ndivyo vizazi vya Peresi; Peresi alimzaa Hesroni; 19 na Hesroni akamzaa Ramu; na Ramu akamzaa Aminadabu; 20 na Aminadabu akamzaa Nashoni; na Nashoni akamzaa Salmoni; 21 na Salmoni akamzaa Boazi; na Boazi akamzaa Obedi; 22 na Obedi akamzaa Yese; na Yese akamzaa Daudi.

1 Samweli 1

1 Palikuwa na mtu mmoja wa Rama, Msufi, wa nchi ya milima milima ya Efraimu, jina lake akiitwa Elkana, mwana wa Yerohamu, mwana wa Elihu, mwana wa Tohu, mwana wa Sufu, Mwefraimu 2 naye alikuwa na wake wawili; jina lake mmoja akiitwa Hana, na jina lake wa pili aliitwa Penina; naye huyo Penina alikuwa na watoto, lakini Hana hakuwa na watoto. 3 Na mtu huyo alikuwa akikwea kutoka mjini kwake mwaka kwa mwaka, ili kuabudu, na kumtolea Bwana wa majeshi dhabihu katika Shilo. Na wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, makuhani wa Bwana, walikuwako huko. 4 Hata siku ile ilipofika Elkana alipotoa dhabihu, kumpa mkewe Penina sehemu, akawapa na watoto wake wote, waume kwa wake, sehemu zao; 5 lakini Hana humpa sehemu mara mbili; maana alimpenda Hana, ingawa Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 6 Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu Bwana alikuwa amemfunga tumbo. 7 Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa Bwana, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. 8 Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? 9 Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la Bwana. 10 Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba Bwana akalia sana. 11 Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe. 12 Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za Bwana, Eli akamwangalia kinywa chake. 13 Basi Hana alikuwa akinena moyoni mwake; midomo yake tu ilionekana kama anena, sauti yake isisikiwe; kwa hiyo huyo Eli alimdhania kuwa amelewa. 14 Ndipo Eli akamwambia, Je! Utakuwa mlevi hata lini? Achilia mbali divai yako. 15 Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana. 16 Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. 17 Ndipo Eli akajibu, akasema, Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba. 18 Naye akasema, Mjakazi wako na aone kibali machoni pako. Basi huyo mwanamke akaenda zake, naye akala chakula, wala uso wake haukukunjamana tena. 19 Wakaondoka asubuhi na mapema, wakasali mbele za Bwana, kisha wakarejea na kufika nyumbani kwao huko Rama; Elkana akamjua mkewe Hana; naye Bwana akamkumbuka. 20 Ikawa, wakati ulipowadia, Hana akachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; akamwita jina lake Samweli, akisema, Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana. 21 Kisha yule mtu, Elkana, na watu wote wa nyumbani mwake, wakakwea kwenda kumtolea Bwana dhabihu ya mwaka, na nadhiri yake. 22 Bali Hana hakukwea; maana alimwambia mumewe, Sitakwea mimi hata mtoto wangu atakapoachishwa maziwa, hapo ndipo nitakapomleta, ili ahudhurie mbele za Bwana, akae huko daima. 23 Elkana, mumewe, akamwambia, Haya, fanya uonavyo vema; ngoja hata utakapomwachisha maziwa; Bwana na alithibitishe neno lake tu. Basi yule mwanamke akangoja, akamnyonyesha mtoto wake, hata akamwachisha maziwa. 24 Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga,na chupa ya divai,akamleta nyumbani kwa BWANA,huko Shilo ;na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. 25 Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. 26 Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. 27 Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; 28 kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.

1 Samweli 2

1 Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana, Pembe yangu imetukuka katika Bwana, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; 2 Hakuna aliye mtakatifu kama Bwana; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. 3 Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani. 4 Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. 5 Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. 6 Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. 7 Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. 8 Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. 9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; 10 Washindanao na Bwana watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; Bwana ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake. 11 Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia Bwana mbele yake Eli, kuhani. 12 Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali Bwana, 13 wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu ye yote alipotoa dhabihu wakati wo wote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake; 14 naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko. 15 Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi. 16 Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu. 17 Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya Bwana. 18 Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za Bwana, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani. 19 Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka. 20 Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, Bwana na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa Bwana. Kisha wakaenda nyumbani kwao. 21 Naye Bwana akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za Bwana. 22 Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. 23 Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. 24 Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa Bwana. 25 Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana amekusudia kuwaua. 26 Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa Bwana, na kwa watu pia. 27 Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, Bwana asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao? 28 Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa mbari ya baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto? 29 Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema? 30 Kwa sababu hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nalisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa Bwana asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau watahesabiwa kuwa si kitu. 31 Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa mbari ya baba yako, hata nyumbani mwako hatakuwako mzee. 32 Nawe utalitazama teso la maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hatakuwako mzee milele. 33 Tena mtu wa kwako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa wapatapo kuwa watu wazima. 34 Na hii ndiyo ishara itakayokuwa kwako, itakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; watakufa wote wawili katika siku moja. 35 Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele. 36 Kisha itakuwa, ya kwamba kila mtu atakayesalia katika nyumba yako atakwenda kumsujudia, apate kipande kidogo cha fedha, na mkate mmoja; na kumwambia, Tafadhali unitie katika kazi mojawapo ya ukuhani, nipate kula kipande kidogo cha mkate.

1 Samweli 3

1 Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. 2 Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), 3 na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; 4 basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. 5 Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena. 6 Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. 7 Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. 8 Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. 9 Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. 10 Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. 11 Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha. 12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho. 13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia. 14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele. 15 Naye Samweli akalala hata asubuhi, akaifungua milango ya nyumba ya Bwana. Samweli akaogopa kumjulisha Eli maono hayo. 16 Basi Eli akamwita Samweli, akasema, Samweli, mwanangu. Naye akajibu, Mimi hapa. 17 Akamwuliza, Ni neno gani alilosema nawe? Nakusihi, usinifiche; Mungu akufanyie vivyo hivyo, na kuzidi, ukinificha lo lote katika hayo yote Bwana aliyosema nawe. 18 Basi Samweli akamwambia kila neno, asimfiche lo lote. Naye akasema, Ndiye Bwana; na afanye alionalo kuwa ni jema. 19 Samweli akakua, naye Bwana alikuwa pamoja naye, wala hakuliacha neno lake lo lote lianguke chini. 20 Nao Waisraeli wote, toka Dani mpaka Beer-sheba, walitambua ya kwamba huyo Samweli amewekwa kuwa nabii wa Bwana. 21 Naye Bwana akaonekana tena huko Shilo; kwa kuwa Bwana akajifunua kwa Samweli huko Shilo, kwa neno la Bwana. Nalo neno la Samweli likawajia Israeli wote.

1 Samweli 4

1 [Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani;wakatua karibu na Ebenezeri ,nao Wafilisti wakatua huko Afeki. 2 Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne. 3 Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. 4 Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. 5 Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. 6 Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la Bwana limefika kambini. 7 Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. 8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. 9 Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. 10 Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. 11 Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa. 12 Basi, mtu mmoja wa Benyamini akapiga mbio kutoka mle jeshini akafika Shilo siku ile ile, hali nguo zake zimeraruliwa, na mavumbi kichwani mwake. 13 Alipofika, tazama, Eli alikuwa ameketi kitini pake kando ya njia, akingojea; maana moyo wake ulitetemeka kwa ajili ya sanduku la Mungu. Na yule mtu alipoingia mjini, akatoa habari, mji wote ukalia. 14 Naye Eli aliposikia kelele za kile kilio, akasema, Maana yake nini kelele za kishindo hiki? Yule mtu akafanya haraka, akaenda, akamwambia Eli. 15 Basi Eli umri wake umepata miaka tisini na minane; na macho yake yamepofuka hata asiweze kuona. 16 Yule mtu akamwambia Eli, Mimi ndimi niliyetoka jeshini, nami leo hivi nimekimbia toka jeshini. Naye akasema, Yalikwendaje, mwanangu? 17 Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa. 18 Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini. 19 Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia. 20 Hata alipokuwa katika kufa, wale wanawake waliohudhuria karibu naye wakamwambia, Usiogope; kwa maana umezaa mtoto mwanamume. Walakini hakujibu, wala hakumtazama. 21 Akamwita mtoto, Ikabodi, akisema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; kwa sababu sanduku la Mungu lilikuwa limetwaliwa, na kwa sababu ya mkwewe na mumewe. 22 Naam, akasema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; maana sanduku la Mungu limetwaliwa. Print this page Top WordProject - "Hapo mwanzo kulikuwako Neno ..." - Contact * * * * * * *

1 Samweli 5

1 Basi Wafilisti walikuwa wamelichukua sanduku la Mungu, wakaenda nalo kutoka Eben-ezeri hata Ashdodi. 2 Wafilisti wakalichukua sanduku la Mungu, wakalitia katika nyumba ya Dagoni, wakaliweka karibu na Dagoni. 3 Na watu wa Ashdodi, walipoamka alfajiri siku ya pili, kumbe! Dagoni imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana. Wakaitwaa Dagoni, wakaisimamisha mahali pake tena. 4 Hata walipoamka kesho yake asubuhi, kumbe! Dagoni ilikuwa imeanguka chini kifudifudi, mbele ya sanduku la Bwana; na kichwa chake Dagoni na vitanga vya mikono yake vyote viwili vimekatika, vipo vimelala kizingitini; Dagoni ikasalia kiwiliwili chake tu. 5 Kwa hiyo makuhani wa Dagoni, na mtu awaye yote aingiaye nyumbani mwa Dagoni, hawakanyagi kizingiti cha nyumba ya Dagoni huko Ashdodi, hata leo. 6 Lakini mkono wa Bwana ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi, akawaharibu, akawapiga kwa majipu, huko Ashdodi na mipakani mwake. 7 Kisha hao watu wa Ashdodi, walipoona ilivyokuwa, walisema, Hilo sanduku la Mungu wa Israeli halitakaa kwetu; kwa maana mkono wake ni mzito juu yetu, na juu ya Dagoni, mungu wetu. 8 Basi wakatuma watu waende kuwakusanya kwao mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Mungu wa Israeli? Nao wakajibu, Sanduku la Mungu wa Israeli na lihamishwe liende Gathi. Wakalihamisha sanduku la Mungu wa Israeli. 9 Ikawa, walipokwisha lihamisha, mkono wa Bwana ulikuwa juu ya mji huo, kwa kuwafadhaisha sana; akawapiga watu wa mjini, wadogo kwa wakubwa, wakapatwa na majipu. 10 Basi, wakalipeleka sanduku la Mungu mpaka Ekroni. Ikawa, sanduku la Mungu lilipofika Ekroni, watu wa Ekroni walifanya kelele, wakasema, Wamelileta hilo sanduku la Mungu wa Israeli kwetu, hata kutuua sisi na watu wetu. 11 Kwa hiyo wakatuma watu waende kuwakusanya mashehe wote wa Wafilisti, wakasema, Liondoeni hilo sanduku la Mungu wa Israeli, liende tena mahali pake, ili lisituue sisi, wala watu wetu; kwa sababu kulikuwa na fadhaa kubwa sana mjini mwote; mkono wa Mungu ulikuwa mzito mno huko. 12 Na wale wasiokufa walipigwa kwa yale majipu; na kilio cha mji kikafika mbinguni.

1 Samweli 6

1 Basi, hilo sanduku la Bwana lilikuwamo katika nchi ya Wafilisti muda wa miezi saba. 2 Nao Wafilisti wakawaita makuhani na waaguzi, wakasema, Tulifanyieje sanduku la Bwana? Tuonyesheni jinsi tuwezavyo kulirudisha mahali pake. 3 Nao wakajibu, Mkilirudisha hilo sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe kitupu; lakini msikose kumpelekea na matoleo ya kosa; hivyo mtapona, tena mtafunuliwa ni kwa sababu gani mkono wake haukuondolewa kwenu. 4 Ndipo wakauliza, Na hayo matoleo ya kosa yatakuwa ya namna gani, hayo tutakayompelekea? Nao wakajibu, Na yawe majipu ya dhahabu matano, na panya wa dhahabu watano, sawasawa na idadi ya mashehe wa Wafilisti; kwa kuwa tauni moja ilikuwa juu yenu nyote, na juu ya mashehe wenu. 5 Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu. 6 Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao? 7 Basi sasa jifanyizieni gari jipya, mtwae na ng'ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng'ombe garini, na kuwaondoa ndama zao na kuwatia zizini; 8 kisha, litwaeni hilo sanduku la Bwana, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda. 9 Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni ajali iliyotupata. 10 Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng'ombe wawili wakamwao, wakawafunga garini, na ndama zao wakawafunga zizini; 11 kisha wakaliweka sanduku la Bwana juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. 12 Na hao ng'ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. 13 Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona. 14 Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng'ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. 15 Nao Walawi walilishusha sanduku la Bwana, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa Bwana. 16 Na hao mashehe watano wa Wafilisti, hapo walipokwisha kuyaona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo. 17 Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa Bwana; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja; 18 na panya wa dhahabu, kwa idadi ya miji yote ya Wafilisti, milki zao wale mashehe watano, miji yenye maboma na vijiji vya mashamba pia. Nalo lile jiwe kubwa, ambalo juu yake waliliweka sanduku la Bwana, liko hata hivi leo hapo kondeni pa Yoshua wa Beth-shemeshi. 19 Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa uuaji mkuu. 20 Nao watu wa Beth-shemeshi wakasema, Ni nani awezaye kusimama mbele za Bwana, huyu Mungu mtakatifu? Naye atapanda kwenda kwa nani kutoka kwetu? 21 Nao wakatuma wajumbe waende kwa wenyeji wa Kiriath-yearimu, kusema, Wafilisti wamelirudisha sanduku la Bwana; basi shukeni, mkalichukue kwenu.

1 Samweli 7

1 Na hao watu wa Kiriath-yearimu wakaja, wakalichukua sanduku la Bwana, wakalileta ndani ya nyumba ya Abinadabu huko kilimani, nao wakamtenga Eleazari, mwanawe, ili alilinde sanduku la Bwana. 2 Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea Bwana. 3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia Bwana kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee Bwana mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. 4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia Bwana peke yake. 5 Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa Bwana. 6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za Bwana; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia Bwana dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. 7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. 8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia Bwana, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. 9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea Bwana sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia Bwana kwa ajili ya Israeli; Bwana akamwitikia. 10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini Bwana akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli. 11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari. 12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia. 13 Hivyo Wafilisti walishindwa, wasiingie tena ndani ya mipaka ya Israeli; na mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Wafilisti siku zote za Samweli. 14 Nayo miji ile Wafilisti waliyokuwa wamewapokonya Waisraeli ilirudishwa tena kwa Israeli, tokea Ekroni mpaka Gathi; na Waisraeli wakauokoa mpaka wake mikononi mwa Wafilisti. Tena kulikuwa na amani kati ya Israeli na Waamori. 15 Naye huyo Samweli akawaamua Israeli siku zote za maisha yake. 16 Naye huenda mwaka kwa mwaka kuzunguka mpaka Betheli, na Gilgali, na Mispa; akawaamua Israeli mahali hapo pote. 17 Na kurudi kwake kulikuwa mpaka Rama; maana ndipo ilipokuwa nyumba yake; nako ndiko alikowaamua Israeli; na huko akamjengea Bwana madhabahu.

1 Samweli 8

1 Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. 2 Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. 3 Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. 4 Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; 5 wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. 6 Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba Bwana. 7 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. 8 Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe. 9 Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki. 10 Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya Bwana. 11 Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. 12 Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. 13 Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji. 14 Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. 15 Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake. 16 Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. 17 Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. 18 Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; Bwana asiwajibu siku ile. 19 Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; 20 ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu. 21 Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa Bwana. 22 Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.

1 Samweli 9

1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. 2 Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote. 3 Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao. 4 Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata. 5 Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi. 6 Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea. 7 Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini angalia, kama tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi? 8 Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina robo ya shekeli ya fedha; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu. 9 (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) 10 Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu. 11 Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko? 12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu; 13 mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hata yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibarikia dhabihu; kisha hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona. 14 Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu. 15 Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, 16 Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. 17 Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. 18 Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? 19 Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. 20 Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako? 21 Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila ya Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo? 22 Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini. 23 Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke akiba. 24 Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa akiba ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hata wakati uliokusudiwa, maana nalisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo. 25 Hata waliposhuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, akaongea na Sauli darini. 26 Nao wakaamka alfajiri; kisha ikawa, kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli darini, akisema, Inuka, nikupeleke kwenu. Basi Sauli akainuka, nao wakatoka wote wawili, yeye na Samweli. 27 Hata walipokuwa wakishuka mwisho wa mji, Samweli akamwambia Sauli, Mwambie mtumishi atangulie, (naye akatangulia), bali wewe simama hapa sasa, ili nikuambie neno la Mungu.

1 Samweli 10

1 Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! Bwana hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa Bwana, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa Bwana amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake. 2 Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? 3 Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; 4 nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. 5 Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; 6 na roho ya Bwana itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. 7 Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. 8 Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya. 9 Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. 10 Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. 11 Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? 12 Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n'nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? 13 Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu. 14 Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli. 15 Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje? 16 Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo. 17 Basi Samweli akawakusanya watu mbele za Bwana huko Mispa 18 akawaambia wana wa Israeli, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea; 19 lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za Bwana, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu. 20 Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa. 21 Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana. 22 Basi wakazidi kumwuliza Bwana, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye Bwana akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo. 23 Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu. 24 Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na Bwana, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi! 25 Kisha Samweli aliwaambia watu madaraka ya ufalme, akayaandika katika kitabu, akakiweka mbele za Bwana. Samweli akawaruhusu watu wote, waende kila mtu nyumbani kwake. 26 Sauli naye akaenda nyumbani kwake huko Gibea; na pamoja naye wakaenda kikosi cha watu, ambao Mungu alikuwa ameigusa mioyo yao. 27 Walakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je! Atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi.

1 Samweli 11

1 Ikawa, kama baada ya mwezi mmoja, Nahashi, Mwamoni ,akakwea na kupanga marago juu ya Yabesh-gileadi;na watu wote wa Yabeshi wakamwambia Nahashi, Fanya mapatano nasi,na sisi tutakutumikia. 2 Huyo Nahashi, Mwamoni, akawaambia, Kwa sharti hii mimi nitapatana nanyi, kila mtu ang'olewe jicho la kuume; na kwa jambo hilo nitawashutumu Waisraeli wote pia. 3 Basi wazee wa Yabeshi wakamjibu, Tuachie siku saba, ili tutume wajumbe waende mipakani mwote mwa Israeli; kisha, ikiwa hakuna atakayetuokoa, tutakutokea. 4 Hivyo wajumbe wakafika Gibea ya Sauli, wakasema maneno hayo masikioni mwa watu; na watu wote wakainua sauti zao wakalia. 5 Na tazama, Sauli akaja akifuata ng'ombe kutoka kondeni; naye Sauli akauliza, Watu hawa wana nini, hata wakalia? Wakamwambia maneno ya watu wale wa Yabeshi. 6 Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. 7 Naye akatwaa jozi ya ng'ombe, akawakata-kata vipande, kisha akavipeleka vile vipande mipakani mwote mwa Israeli kwa mikono ya wajumbe, kusema, Ye yote asiyetoka nyuma ya Sauli na Samweli, ng'ombe zake watatendwa vivi hivi. Basi utisho wa Bwana ukawaangukia wale watu, wakatoka kama mtu mmoja. 8 Naye akawahesabu huko Bezeki; Waisraeli walikuwa mia tatu elfu, na Wayuda thelathini elfu. 9 Nao wakawaambia hao wajumbe waliokuja, Waambieni watu wa Yabesh-gileadi, Kesho, wakati wa jua kali, mtapata wokovu. Basi wale wajumbe wakaenda, wakawaarifu watu wa Yabeshi; nao walifurahiwa. 10 Kwa hiyo watu wa Yabeshi walisema, Kesho tutawatokea, nanyi mtatufanyia yote myaonayo kuwa ni mema. 11 Ikawa, kesho yake, Sauli akawapanga watu katika vikosi vitatu; nao wakaingia katikati ya marago kwenye zamu ya asubuhi, wakawapiga Waamoni hata wakati wa jua kali; kisha ikawa wale waliosalia wakatawanyika, hata wasiachwe wawili wao pamoja. 12 Ndipo watu walipomwambia Samweli, Ni nani yule aliyesema, Je! Huyo Sauli atatutawala? Walete watu hao, ili tuwaue. 13 Lakini Sauli akasema, Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo Bwana amefanya wokovu katika Israeli. 14 Kisha Samweli akawaambia watu, Haya! Na twendeni mpaka Gilgali, ili tuuimarishe ufalme huko mara ya pili. 15 Nao watu wote wakaenda Gilgali; wakamtawaza Sauli mbele za Bwana huko Gilgali; wakachinja sadaka za amani mbele za Bwana; na huko Sauli na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.

1 Samweli 12

1 Kisha Samweli akawaambia Israeli wote, Angalieni, nimeisikiliza sauti yenu katika hayo yote mliyoniambia, nami nimemtawaza mfalme juu yenu. 2 Basi sasa, angalieni, mfalme anakwenda mbele yenu; na mimi ni mzee, mwenye mvi; tena, tazameni, wana wangu wapo pamoja nanyi; nami nimekwenda mbele yenu toka ujana wangu hata leo. 3 Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za Bwana, na mbele ya masihi wake,nalitwaa ng`ombe wa nani? au nalitwaa punda wa nani? au ni nani niliye mdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi. 4 Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote. 5 Akawaambia, Bwana ni shahidi juu yenu, na masihi 6 Samweli akawaambia watu, Ni yeye Bwana aliyewaweka Musa na Haruni, ndiye yeye aliyewatoa baba zenu kutoka nchi ya Misri. 7 Basi sasa simameni, ili niwahutubie mbele za Bwana, kwa kutaja matendo yote ya haki ya Bwana, aliyowatendea ninyi na baba zenu. 8 Yakobo alipokuwa ameingia Misri, na baba zenu walipomlilia Bwana, ndipo Bwana akawapeleka Musa na Haruni, nao wakawatoa baba zenu kutoka Misri, wakawakalisha mahali hapa. 9 Lakini wakamsahau Bwana, Mungu wao, naye akawauza na kuwatia katika mikono ya Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori, na katika mikono ya Wafilisti, na katika mikono ya mfalme wa Moabu, nao wakapigana nao. 10 Nao wakamlilia Bwana, wakasema, Tumefanya dhambi, kwa kuwa tumemwacha Bwana, na kuwatumikia Mabaali na Maashtorethi; lakini sasa utuokoe na mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia wewe. 11 Bwana akawatuma Yerubaali, na Baraka, na Yeftha, na Samweli, akawaokoa ninyi na mikono ya adui zenu pande zote, nanyi mkakaa salama. 12 Hata mlipomwona Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, amekuja kupigana nanyi, mliniambia, Sivyo, lakini mfalme atatutawala; ingawa Bwana, Mungu wenu, ni mfalme wenu. 13 Basi sasa, mtazameni mfalme mliyemchagua na kumtaka; tazameni, Bwana ameweka mfalme juu yenu. 14 Kama mkimcha Bwana, na kumtumikia, na kuisikia sauti yake, msiiasi amri ya Bwana, tena kama ninyi, na mfalme anayewatawala, mkimfuata Bwana, Mungu wenu, vema! 15 Bali msipoisikia sauti ya Bwana, mkiiasi amri ya Bwana, ndipo mkono wa Bwana utakuwa juu yenu, kama ulivyokuwa juu ya baba zenu. 16 Na sasa simameni, mkalione jambo hili kubwa, Bwana atakalolitenda mbele ya macho yenu. 17 Leo je! Si mavuno ya ngano? Nitamwomba Bwana, kwamba apeleke ngurumo na mvua; nanyi mtajua na kuona ya kuwa uovu wenu ni mwingi sana, mlioufanya machoni pa Bwana, kwa kujitakia mfalme. 18 Basi Samweli akamwomba Bwana, naye Bwana akapeleka ngurumo na mvua siku ile; nao watu wote wakamwogopa Bwana sana, na Samweli pia. 19 Watu wote wakamwambia Samweli, Utuombee sisi watumwa wako kwa Bwana, Mungu wako, tusije tukafa; maana tumeongeza dhambi zetu zote kwa uovu huu, wa kujitakia mfalme. 20 Samweli akawaambia, Msiogope; ni kweli mmeutenda uovu huu wote; lakini msigeuke na kuacha kumfuata Bwana, bali mtumikieni Bwana kwa mioyo yenu yote. 21 Wala msigeuke upande, maana, kufuata vitu vya ubatili, 22 visivyoweza kusaidia wala kuokoa, kwa kuwa havifai kitu. Maana Bwana hatawaacha watu wake kwa ajili ya jina lake kuu; kwa kuwa imempendeza Bwana kuwafanya ninyi kuwa watu wake mwenyewe. 23 Walakini mimi, hasha! Nisimtende Bwana dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka 24 Mcheni Bwana tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu. 25 Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.

1 Samweli 13

1 Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala;naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli. 2 Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake. 3 Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania. 4 Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali. 5 Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni. 6 Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wa katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika. 7 Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa akaliko huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka. 8 Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muhula uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye. 9 Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa. 10 Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu. 11 Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu naliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi; 12 basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za Bwana; kwa hiyo nalijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa. 13 Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya Bwana, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana Bwana angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele. 14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; Bwana amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye Bwana amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile Bwana alilokuamuru. 15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita. 16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi. 17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali; 18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika. 19 Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki; 20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake; 21 ila walikuwa na tupa za kunolea sululu, na miundu, na mauma, na mashoka; na kwa kuinoa michokoo. 22 Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu ye yote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo. 23 Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mwanya wa Mikmashi.

1 Samweli 14

1 Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye. 2 Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita; 3 na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Bwana huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. 4 Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene. 5 Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba. 6 Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini Bwana atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia Bwana asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache. 7 Naye huyo mchukua silaha akamjibu, Fanya yote yaliyomo moyoni mwako; angalia, mimi hapa ni pamoja nawe, moyo wangu ni kama moyo wako. 8 Ndipo Yonathani akasema, Tazama, sisi tutawavukia watu hawa, na kujidhihirisha kwao. 9 Nao wakituambia hivi, Ngojeni, hata sisi tuwafikilie; ndipo tusimame pale pale mahali petu, tusiwapandie. 10 Lakini wakisema hivi, Haya! Ninyi, tupandieni sisi; hapo ndipo tutakapopanda; kwa maana Bwana amewatia mikononi mwetu; na hii itakuwa ndiyo ishara kwetu. 11 Basi, hao wote wawili wakajidhihirisha mbele ya ngome ya Wafilisti, na wale Wafilisti wakasema, Kumbe! Wale Waebrania watoka katika mashimo walimojificha! 12 Nao watu wa ngomeni wakamjibu Yonathani na mchukua silaha zake, wakasema, Haya! Ninyi, pandeni juu hapa tulipo, na sisi tutawaonyesha jambo. Yonathani akamwambia yule aliyezichukua silaha, Haya! Panda nyuma yangu; kwa kuwa Bwana amewatia mikononi mwa Israeli. 13 Basi Yonathani akapanda kwa mikono na miguu yake, na mchukua silaha nyuma yake; na hao watu wakaanguka mbele ya Yonathani; na huyo mchukua silaha zake akawaua nyuma yake. 14 Na uuaji huo wa kwanza walioufanya Yonathani na mchukua silaha zake, ulipata kama watu ishirini, katika nafasi kama nusu ya kiwanja kiwezacho kulimwa katika siku nzima. 15 K