Swahili John


/1 Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. 
Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. 
Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa 
pasipo yeye. 
Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. 
Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda. 
Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane. 
Ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga; Alikuja ili kwa ujumbe wake 
watu wote wapate kuamini. 
Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. 
Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. 
Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini 
ulimwengu haukumtambua. 
Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. 
Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa 
Mungu. 
Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za 
kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao. 
Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu; Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu 
wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. 
Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja 
wakati niliposema: [Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, 
maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."]. 
Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo. 
Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa 
njia ya Kristo. 
Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule; Mwana wa pekee aliye sawa na 
Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu. 
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu 
walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?" 
Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye 
Kristo." 
Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, 
"La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, 
"La!". 
Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, 
ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma." 
Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: 
[Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."]. 
Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo. 
Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, 
mbona wabatiza?" 
Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, 
msiyemjua bado. 
Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu 
vyake." 
Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane 
alikuwa anabatiza. 
Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa 
Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!. 
Huyu ndiye niliyesema juu yake: [Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu 
zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!]. 
Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa 
Israeli wapate kumjua." 
Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka 
mbinguni na kutua juu yake. 
Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa 
ameniambia: [Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa 
juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.]. 
Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu." 
Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili. 
Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa 
Mungu." 
Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu. 
Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, 
"Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?" 
Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona 
mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo; Ilikuwa yapata saa kumi 
jioni. 
Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia 
Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu. 
Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" 
(maana yake Kristo). 
Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu; Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe 
ni Simoni mwana wa Yohane; Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, 
"Mwamba."). 
Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya; Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, 
"Nifuate." 
Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro. 
Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose 
aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika 
habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti." 
Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" 
Filipo akamwambia, "Njoo uone." 
Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni 
Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake." 
Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa 
chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona." 
Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu; Wewe ni Mfalme 
wa Israeli!". 
Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya 
mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya." 
Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na 
malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu." 

/2 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya; Mama yake Yesu 
alikuwapo. 
Naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. 
Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!". 
Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya; Saa yangu bado." 
Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni." 
Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua 
kiasi cha madebe mawili au matatu; Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi 
ya Kiyahudi ya kutawadha. 
Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu. 
Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu." 
Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai; Yeye 
hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua); Mkuu wa 
karamu akamwita bwana arusi. 
Akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa 
ile hafifu; Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!". 
Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu 
wake; nao wanafunzi wake wakamwamini. 
Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi 
wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache. 
Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda 
Yerusalemu. 
Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha 
walikuwa wamekaa kwenye meza zao. 
Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo 
na ng'ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao. 
Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa; Msiifanye 
nyumba ya Baba yangu kuwa soko!". 
Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba 
yako waniua." 
Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba 
unayo haki kufanya mambo haya?" 
Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu." 
Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na 
sita; Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?" 
Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake. 
Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa 
amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema 
Yesu. 
Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini 
walipoona ishara alizozifanya. 
Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote. 
Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote 
yaliyomo mioyoni mwao. 

/3 Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake 
Nikodemo. 
Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni 
mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara 
unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye." 
Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme 
wa Mungu." 
Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni 
mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!". 
Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi 
kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu. 
Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho. 
Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya. 
Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka 
wala unakokwenda; Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho." 
Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?" 
Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya?. 
Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini 
ninyi hamkubali ujumbe wetu. 
Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini 
nikiwaambieni mambo ya mbinguni?. 
Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye 
ameshuka kutoka mbinguni. 
"Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa 
Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo. 
Ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele. 
Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili 
kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 
Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe 
ulimwengu. 
"Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu 
hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu. 
Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda 
giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu. 
Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana 
hapendi matendo yake maovu yamulikwe. 
Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake 
yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu." 
Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake; Alikaa huko 
pamoja nao kwa muda, akibatiza watu. 
Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko 
kulikuwa na maji mengi; Watu walimwendea, naye akawabatiza. 
(Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.). 
Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu 
desturi za kutawadha. 
Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu 
aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa 
naye anabatiza, na watu wote wanamwendea." 
Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu. 
Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: [Mimi siye Kristo, lakini 
nimetumwa ili nimtangulie!]. 
Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na 
kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema; Ndivyo furaha yangu 
ilivyokamilishwa. 
Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue. 
"Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na 
huongea mambo ya kidunia; Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko 
wote. 
Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe 
wake. 
Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli. 
Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo 
Roho wake bila kipimo. 
Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote. 
Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa 
milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake." 

/4 Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi 
wengi kuliko Yohane. 
(Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.). 
Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya. 
Na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria. 
Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo 
alikuwa amempa mwanawe, Yosefu. 
Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa 
safari, akaketi kando ya kisima; Ilikuwa yapata saa sita mchana. 
Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji; Yesu akamwambia, "Nipatie 
maji ninywe." 
(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.). 
Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! 
Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria 
katika matumizi ya vitu.). 
Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: 
[Nipatie maji ninywe,] ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai." 
Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho 
kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?. 
Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi 
kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya 
kisima hiki." 
Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 
Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele; Maji 
nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima 
wa milele." 
Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; 
nisije tena mpaka hapa kuteka maji." 
Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa." 
Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, 
kwamba huna mume. 
Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako; Hapo 
umesema kweli." 
Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii. 
Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa 
kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu." 
Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya 
mlima huu, wala kule Yerusalemu. 
Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo 
tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi. 
Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, 
watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba 
anaotaka. 
Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake." 
Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja; 
Atakapokuja atatujulisha kila kitu." 
Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye." 
Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke; 
Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na 
mwanamke?" 
Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu. 
"Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa 
yeye ndiye Kristo?" 
Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu. 
Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula." 
Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi." 
Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?" 
Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na 
kuitimiza kazi yake. 
Ninyi mwasema: [Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!] Lakini mimi 
nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa. 
Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa 
milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja. 
Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: [Mmoja hupanda na mwingine huvuna.]. 
Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya 
kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao." 
Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo 
mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya." 
Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili. 
Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake. 
Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi 
wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu." 
Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya. 
Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi 
yake." 
Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha; Maana nao pia 
walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko 
Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo. 
Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji 
kuwa divai; Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko 
Kafarnaumu. 
Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika 
Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa 
mahututi. 
Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!". 
Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa." 
Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya 
Yesu, akaenda zake. 
Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba 
mwanawe alikuwa mzima. 
Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba 
mchana, homa ilimwacha." 
Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: 
"Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote. 
Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda 
Galilaya. 

/5 Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda 
Yerusalemu. 
Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa 
la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye 
matao. 
Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza; 
Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe. 
Maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua; Mtu 
yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona 
ugonjwa wowote aliokuwa nao. 
Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka 
thelathini na minane. 
Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo 
kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?" 
Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati 
yanapotibuliwa; Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia." 
Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee." 
Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea; Jambo hili lilifanyika 
siku ya Sabato. 
Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, 
si halali kubeba mkeka wako." 
Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: [Chukua 
mkeka wako, tembea."]. 
Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: [Chukua mkeka wako, tembea,] ni 
nani?" 
Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka 
mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu. 
Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa 
umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi." 
Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye 
aliyemponya. 
Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza 
kumdhulumu. 
Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya 
kazi." 
Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya 
kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa 
alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu. 
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; 
anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya; Maana kile anachofanya 
Baba, Mwana hukifanya vilevile. 
Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena 
atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu. 
Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa 
uzima wale anaopenda. 
Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana. 
Ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba; Asiyemheshimu 
Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma. 
"Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao 
uzima wa milele; Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na 
kuingia katika uzima. 
Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia 
sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi. 
Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa 
asili ya uhai. 
Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu. 
Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini 
wataisikia sauti yake. 
Nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda 
maovu watafufuka na kuhukumiwa. 
"Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe; Mimi nina hukumu kama 
ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki; Nia yangu si 
kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma. 
Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli. 
Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote 
anayosema juu yangu ni ya kweli. 
Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli. 
Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili 
mpate kuokolewa. 
Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari 
kufurahia mwanga huo kwa kitambo. 
Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane; 
Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo 
zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma. 
Naye Baba aliyenituma hunishuhudia; Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, 
wala kuuona uso wake. 
Na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma. 
Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata 
uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!. 
Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima. 
"Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu. 
Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu. 
Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine 
akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea. 
Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi 
wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?. 
Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba; Mose ambaye ninyi mmemtumainia 
ndiye atakayewashtaki. 
Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu 
yangu. 
Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?" 

/6 Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au Ziwa Tiberia). 
Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara 
alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. 
Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake. 
Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia. 
Basi, Yesu na alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia 
Filipo, "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?" 
(Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.). 
Filipo akamjibu, "Mikate ya denari mia mbili za fedha haiwatoshi watu hawa 
hata kama ila mmoja atapata kipande kidogo tu!". 
Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia. 
"Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; 
lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?" 
Yesu akasema, "Waketisheni watu." Palikuwa na nyasi tele mahali hapo; Basi, 
watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano. 
Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa 
wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri 
alivyotaka. 
Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kusanyeni vipande 
vilivyobaki visipotee." 
Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu 
waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili. 
Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, "Hakika huyu ndiye 
nabii anayekuja ulimwenguni." 
Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, 
akaenda mlimani peke yake. 
Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani. 
Wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu; Giza lilikuwa limeingia, na 
Yesu alikuwa hajawafikia bado. 
Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma. 
Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona 
Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana. 
Yesu akawaambia, "Ni mimi, msiogope!". 
Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu 
walipokuwa wanakwenda. 
Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua 
kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja 
na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao. 
Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile 
mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu. 
Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali 
hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta. 
Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, "Mwalimu, 
ulifika lini hapa?" 
Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, 
bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba. 
Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa 
ajili ya uzima wa milele; Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni 
chakula hicho." 
Wao wakamwuliza, "Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?" 
Yesu akawajibu, "Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule 
aliyemtuma." 
Hapo wakamwambia, "Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya 
kitu gani?. 
Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: [Aliwalisha 
mkate kutoka mbinguni."]. 
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; 
Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni. 
Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu 
uzima." 
Basi, wakamwambia, "Mheshimiwa, tupe daima mkate huo." 
Yesu akawaambia, "Mimi ndimi mkate wa uzima; Anayekuja kwangu hataona njaa; 
anayeniamini hataona kiu kamwe. 
Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini. 
Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja 
kwangu. 
Kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila 
kutimiza matakwa ya yule aliyenituma. 
Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale 
alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho. 
Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe 
na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho." 
Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: "Mimi ni mkate 
ulioshuka kutoka mbinguni." 
Wakasema, "Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! 
Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?" 
Yesu akawaambia, "Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi. 
Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami 
nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho. 
Manabii wameandika: [Watu wote watafundishwa na Mungu.] Kila mtu anayemsikia 
Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu. 
Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa 
Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. 
Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele. 
Mimi ni mkate wa uzima. 
Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa. 
Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa. 
Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni; Mtu yeyote akila mkate huu 
ataishi milele; Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya 
uzima wa ulimwengu." 
Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao. 
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa 
damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu. 
Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami 
nitamfufua siku ya mwisho. 
Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 
Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani 
yake. 
Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye 
mimi ataishi pia kwa sababu yangu. 
Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu 
zetu, wakafa; Aulaye mkate huu ataishi milele." 
Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu. 
Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, "Haya ni mambo magumu! 
Nani awezaye kuyasikiliza?" 
Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung'unika 
juu ya jambo hilo, akawauliza, "Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka?. 
Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa 
kwanza?. 
Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi; Maneno niliyowaambieni ni 
Roho, ni uzima. 
Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini." (Yesu alisema hivyo kwani alijua 
tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.). 
Kisha akasema, "Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu 
asipowezeshwa na Baba yangu." 
Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane naye tena. 
Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, "Je, nanyi pia mwataka kwenda 
zenu?" 
Simoni Petro akamjibu, "Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo 
uzima wa milele. 
Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu." 
Yesu akawaambia, "Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja 
wenu ni Ibilisi!". 
Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa 
ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili. 

/7 Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; Hakutaka kutembea 
mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumwua. 
Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 
Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako 
wazione kazi unazozifanya. 
Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu; Maadam unafanya 
mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu." 
(Hata ndugu zake hawakumwamini!). 
Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado; Lakini kwenu ninyi 
kila wakati unafaa. 
Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi 
nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu. 
Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo; Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa 
yangu ifaayo haijafika." 
Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya. 
Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini 
hakuenda kwa hadhara bali kwa siri. 
Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: 
"Yuko wapi?" 
Kulikuwa na minong'ono mingi katika umati wa watu; Baadhi yao walisema, "Ni 
mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu." 
Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa 
viongozi wa Wayahudi. 
Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza 
kufundisha. 
Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma 
shuleni?" 
Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye 
aliyenituma. 
Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu 
yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe. 
Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta 
sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote. 
Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika 
Sheria; Kwa nini mnataka kuniua?" 
Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?" 
Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia. 
Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri; (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa 
Mose, bali ilitoka kwa mababu); Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato. 
Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose 
isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa 
siku ya Sabato?. 
Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki." 
Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si 
huyu?. 
Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno; 
Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?. 
Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua 
alikotoka mtu huyu!". 
Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati 
mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu 
mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui. 
Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma." 
Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata 
kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado. 
Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, "Je, Kristo akija 
atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?" 
Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu; Basi, wao 
pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni. 
Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule 
aliyenituma. 
Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika." 
Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda wapi ambapo 
hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na 
kuwafundisha Wagiriki?. 
Ana maana gani anaposema: [Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali 
nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?"]. 
Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum; Yesu alisimama, akasema 
kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe. 
Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: [Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye 
uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!"]. 
(Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea; Wakati 
huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.). 
Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu 
huyu ndiye yule nabii!". 
Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je, 
yawezekana Kristo akatoka Galilaya?. 
Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: [Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, 
na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!"]. 
Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu. 
Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata. 
Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, 
"Kwa nini hamkumleta?" 
Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu 
huyu!". 
Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?. 
Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo 
aliyemwamini?. 
Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!". 
Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu; Basi, 
yeye akawaambia. 
"Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya 
nini?" 
Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko 
Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!". 
Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake. 

/8 Lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni. 
Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni; Watu wote wakamwendea, 
naye akaketi akawa anawafundisha. 
Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa 
katika uzinzi; Wakamsimamisha katikati yao. 
Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi. 
Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe; Basi, wewe 
wasemaje?" 
Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki; Lakini Yesu akainama 
chini, akaandika ardhini kwa kidole. 
Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni 
mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe." 
Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini. 
Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee; Yesu 
akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale. 
Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna 
hata mmoja aliyekuhukumu?" 
Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, 
"Wala mimi sikuhukumu; Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena." 
Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu; 
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima." 
Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi 
wako si halali." 
Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli 
kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda; Lakini ninyi hamjui 
nilikotoka wala ninakokwenda. 
Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu. 
Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba 
aliyenituma yuko pamoja nami. 
Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali. 
Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia." 
Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi 
wala hamumjui Baba; Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia." 
Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha 
Hekaluni; Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa 
haijafika bado. 
Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika 
dhambi zenu; Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika." 
Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: [Niendako 
ninyi hamwezi kufika?"]. 
Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni 
wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. 
Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu; Kama msipoamini kwamba 
[Mimi ndimi], mtakufa katika dhambi zenu." 
Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo!. 
Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; Lakini yule aliyenituma ni kweli; 
nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake." 
Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba. 
Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo 
mtakapojua kwamba [Mimi ndimi], na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila 
nasema tu yale Baba aliyonifundisha. 
Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya 
daima yale yanayompendeza." 
Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini. 
Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia 
mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu. 
Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru." 
Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa 
wa mtu yeyote yule; Una maana gani unaposema: [mtakuwa huru?"]. 
Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa 
dhambi. 
Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu. 
Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli. 
Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu; Hata hivyo, mnataka kuniua kwa 
sababu hamuyakubali mafundisho yangu. 
Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale 
aliyowaambieni baba yenu." 
Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa 
watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu. 
Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka 
kuniua; Abrahamu hakufanya hivyo!. 
Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si 
watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu." 
Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi 
nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa; Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila 
yeye alinituma. 
Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe 
wangu. 
Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba 
yenu; Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani 
ukweli haumo ndani yake; Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya 
maumbile, maana yeye ni mwon go na baba wa uongo.
Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini. 
Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema 
ukweli, kwa nini hamniamini?. 
Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu; Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu 
ninyi si (watu wa) Mungu." 
Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena 
una pepo?" 
Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi 
hamniheshimu. 
Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu
huo, naye ni hakimu. 
Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele." 
Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! 
Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, [Anayeuzingatia 
ujumbe wangu hatakufa milele!]. 
Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na 
manabii walikufa; Wewe unajifanya kuwa nani?" 
Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; Baba yangu 
ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza. 
Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua; Na, nikisema simjui, nitakuwa 
mwongo kama ninyi; Mimi namjua na ninashika neno lake. 
Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi." 
Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona 
Abrahamu?" 
Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko." 
Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni. 

/9 Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa. 
Basi, wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, 
ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?" 
Yesu akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala 
dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane 
ikifanya kazi ndani yake. 
Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana 
usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi. 
Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu." 
Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule 
kipofu machoni. 
Akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina hili ni 
"aliyetumwa"); Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona. 
Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini 
mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?" 
Baadhi yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana naye." 
Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!". 
Basi, wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?" 
Naye akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na 
kuniambia: [Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.] Basi, mimi nikaenda, 
nikanawa, nikapata kuona." 
Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi sijui!". 
Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo. 
Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya 
Sabato. 
Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia, 
"Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona." 
Baadhi ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki 
sheria ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya 
ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao. 
Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua macho, 
wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!". 
Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na 
sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake. 
Basi, wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema 
alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?" 
Wazazi wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa 
kipofu. 
Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho; 
Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe." 
Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani 
viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu 
ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi. 
Ndiyo maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni." 
Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya 
Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi." 
Yeye akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui; Lakini kitu kimoja najua: 
Nilikuwa kipofu, na sasa naona." 
Basi, wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?" 
Huyo mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini 
mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?" 
Lakini wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa 
Mose. 
Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka 
wapi!". 
Naye akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, 
lakini amenifumbua macho yangu!. 
Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote 
mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake. 
Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu 
aliyezaliwa kipofu. 
Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!". 
Wao wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje 
kutufundisha sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali. 
Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, 
"Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?" 
Huyo mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini." 
Yesu akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa." 
Basi, huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia. 
Yesu akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate 
kuona, na wale wanaoona wawe vipofu." 
Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, 
"Je, sisi pia ni vipofu?" 
Yesu akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi 
mwasema: [Sisi tunaona], na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado. 

/10 Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la 
kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo 
ni mwizi na mnyang'anyi. 
Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo. 
Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita 
kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje. 
Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti 
yake. 
Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti 
yake." 
Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia. 
Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo. 
Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo 
hawakuwasikiliza. 
Mimi ni mlango; Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, 
na kupata malisho. 
Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu; Mimi nimekuja mpate kuwa na 
uzima--uzima kamili. 
"Mimi ni mchungaji mwema; Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo 
wake. 
Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona 
mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia; Kisha mbwa mwitu huwakamata 
na kuwatawanya. 
Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu. 
Mimi ni mchungaji mwema; Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi. 
Kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba; Mimi nayatoa maisha yangu kwa 
ajili yao. 
Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu; Inanibidi kuwaleta hao 
pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. 
"Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena. 
Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu 
mwenyewe; Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena; Hivi ndivyo Baba 
alivyoniamuru nifanye." 
Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya. 
Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?" 
Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo; Je, pepo anaweza kuyafumbua 
macho ya vipofu?" 
Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku; Wakati huo ulikuwa wa 
baridi. 
Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni. 
Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka 
lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi." 
Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki; Kazi ninazozifanya mimi kwa 
jina la Baba yangu zinanishuhudia. 
Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu. 
Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata. 
Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu 
atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu. 
Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye 
kuwatoa mikononi mwake Baba. 
Mimi na Baba, tu mmoja." 
Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie. 
Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba; Ni ipi kati ya 
hizo inayowafanya mnipige mawe?" 
Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu 
ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu." 
Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: [Mimi nimesema, ninyi ni 
miungu?]. 
Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko 
Matakatifu yasema ukweli daima. 
Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: 
[Unakufuru], eti kwa sababu nilisema: [Mimi ni Mwana wa Mungu?]. 
Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini. 
Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi 
mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake." 
Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao. 
Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, 
akakaa huko. 
Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote; Lakini yale 
yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa." 
Watu wengi mahali hapo wakamwamini. 

/11 Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa; (Kijiji 
cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake. 
Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake; 
Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.). 
Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!". 
Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili 
ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe." 
Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro. 
Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo 
alipokuwa kwa siku mbili zaidi. 
Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!". 
Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi 
walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?" 
Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana 
hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu. 
Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake." 
Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, 
lakini mimi nitakwenda kumwamsha." 
Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona." 
Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa 
amesema juu ya kifo cha Lazaro. 
Basi, Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa. 
Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini; Haya, 
twendeni kwake." 
Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe 
pamoja naye!". 
Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne. 
Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu. 
Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha 
kaka yao. 
Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini 
Maria alibaki nyumbani. 
Martha akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!. 
Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa." 
Yesu akamwambia, "Kaka yako atafufuka." 
Martha akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho." 
Yesu akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima; Anayeniamini mimi hata kama 
anakufa, ataishi. 
Na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe; Je, waamini hayo?" 
Martha akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa 
Mungu, yule ajaye ulimwenguni." 
Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia 
faraghani, "Mwalimu yuko hapa, anakuita." 
Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu. 
Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha 
alipomlaki. 
Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona 
ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata; Walidhani alikuwa anakwenda 
kaburini kuomboleza. 
Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, 
akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!". 
Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, 
alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni. 
Kisha akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone." 
Yesu akalia machozi. 
Basi, Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!". 
Lakini baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza 
kumfanya Lazaro asife?" 
Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini; Kaburi lenyewe 
lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe. 
Yesu akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa, 
akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!". 
Yesu akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?" 
Basi, wakaliondoa lile jiwe; Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, 
"Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza. 
Najua kwamba unanisikiliza daima; Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa 
waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma." 
Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: "Lazaro! Toka nje!". 
Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na 
uso wake umefunikwa; Yesu akawaambia, "Mfungueni, mkamwache aende zake." 
Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho 
alichokifanya Yesu wakamwamini. 
Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo 
alilofanya Yesu. 
Kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, 
wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno. 
Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu 
letu na taifa letu!". 
Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, 
akawaambia, "Ninyi hamjui kitu!. 
Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko 
taifa zima liangamizwe?" 
Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu 
mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao. 
Na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu 
waliotawanyika. 
Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu. 
Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, 
akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu; Akakaa huko pamoja 
na wanafunzi wake. 
Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda 
Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo. 
Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni 
wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au 
sivyo?" 
Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali 
aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni. 

/12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi 
Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu. 
Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia; Lazaro 
alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu. 
Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, 
akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake; Nyumba yote ikajaa harufu 
ya marashi. 
Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti 
Yesu, akasema. 
"Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa 
maskini?" 
Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu 
alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka 
katika hiyo hazina. 
Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku 
ya mazishi yangu. 
Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote." 
Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania; Basi, wakafika huko si 
tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu 
alimfufua kutoka wafu. 
Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro. 
Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini 
Yesu. 
Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu 
alikuwa njiani kuja Yerusalemu. 
Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti 
wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana; Abarikiwe mfalme wa 
Israeli." 
Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko. 
"Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda." 
Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha 
tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na 
kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. 
Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka 
kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia. 
Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa 
amefanya ishara hiyo. 
Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, 
ulimwengu wote unamfuata." 
Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu 
kuabudu wakati wa sikukuu hiyo. 
Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, 
"Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu." 
Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu. 
Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!. 
Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika 
udongo na kufa; Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi. 
Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika 
ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele. 
Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi 
ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa; Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu 
atampa heshima. 
"Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: [Baba, usiruhusu saa 
hii inifikie]? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii. 
Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, 
na nitalitukuza tena." 
Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao 
walisema, "Malaika ameongea naye!". 
Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa 
ajili yenu. 
Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu 
atapinduliwa. 
Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu." 
(Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani). 
Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo 
atadumu milele; Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? 
Huyo Mwana wa Mtu ni nani?" 
Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi; Tembeeni mngali mnao 
huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako. 
Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya 
kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao. 
Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini. 
Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe 
wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?" 
Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema. 
"Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, 
wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate 
kuwaponya." 
Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari 
zake. 
Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu; Lakini kwa sababu 
ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na 
sunagogi. 
Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu. 
Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila 
anamwamini pia yule aliyenituma. 
Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma. 
Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki 
gizani. 
Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja 
kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa. 
Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu 
wake siku ya mwisho. 
Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye 
aliyeniamuru niseme nini na niongee nini. 
Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele; Basi, mimi nasema tu yale 
Baba aliyoniagiza niyaseme." 

/13 Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka; Yesu alijua kwamba saa yake ya 
kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika; Alikuwa amewapenda 
daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!. 
Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni; Ibilisi 
alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu. 
Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa 
ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu. 
Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na 
kujifunga kiunoni. 
Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na 
kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia. 
Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu 
mimi?" 
Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye." 
Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha 
hutakuwa na uhusiano nami tena." 
Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na 
kichwa pia." 
Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana 
amekwisha takata mwili wote; Ninyi mmetakata, lakini si nyote." 
(Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, 
lakini si nyote."). 
Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, 
"Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?. 
Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi. 
Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia 
mnapaswa kuoshana miguu. 
Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni. 
Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si 
mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma. 
Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza. 
"Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote; Mimi nawajua wale niliowachagua; Lakini 
lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: [Yule aliyeshiriki chakula changu 
amegeuka kunishambulia.]. 
Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate 
kuamini kuwa mimi ndimi. 
Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na 
anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma." 
Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli 
nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!". 
Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani. 
Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu 
na Yesu. 
Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani." 
Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?" 
Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, 
ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa 
Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti. 
Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia; Basi Yesu 
akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!". 
Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini 
alikuwa amemwambia hivyo. 
Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao 
walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, 
au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini. 
Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara; Na 
ilikuwa usiku. 
Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye 
Mungu ametukuzwa ndani yake. 
Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu 
ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara. 
"Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu; Mtanitafuta, lakini sasa 
nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: [Niendako ninyi hamwezi 
kwenda!]. 
Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. 
Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu." 
Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako 
huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye." 
Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa 
ajili yako!". 
Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, 
kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!". 

/14 Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu; Mwaminini Mungu, niaminini na 
mimi pia. 
Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni; 
Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. 
Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili 
nanyi muwe pale nilipo mimi. 
Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda." 
Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo 
njia?" 
Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima; Hakuna awezaye kwenda kwa 
Baba ila kwa kupitia kwangu. 
Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia; Na tangu sasa, mnamjua, tena 
mmekwisha mwona." 
Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka." 
Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? 
Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba; Unawezaje basi, kusema: [Tuonyeshe 
Baba?]. 
Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno 
ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu 
anafanya kazi yake. 
Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko 
ndani yangu; Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya. 
Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, 
atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba. 
Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya 
Mwana. 
Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni. 
"Mkinipenda mtazishika amri zangu. 
Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi 
milele. 
Yeye ni Roho wa kweli; Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona 
wala kumjua; Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu. 
"Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu. 
Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa 
mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai. 
Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani 
yangu, nami ndani yenu. 
Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; Naye anipendaye 
mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake." 
Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha 
kwetu na si kwa ulimwengu?" 
Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, 
nasi tutakuja kwake na kukaa naye. 
Asiyenipenda hashiki maneno yangu; Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake 
Baba aliyenituma. 
"Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi. 
Lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, 
atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni. 
"Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu; Siwapi ninyi kama vile ulimwengu 
ufanyavyo; Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike. 
Mlikwisha sikia nikiwaambieni: [Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.] 
Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni 
mkuu kuliko mimi. 
Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini. 
Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja; 
Kwangu mimi hawezi kitu. 
Lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya 
kila kitu kama Baba alivyoniamuru; Simameni, tutoke hapa!". 

/15 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 
Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo 
hulisafisha lipate kuzaa zaidi. 
Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni. 
Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu; Tawi haliwezi peke yake kuzaa 
matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda 
msipokaa ndani yangu. 
"Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake; Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, 
huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote. 
Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata 
likakauka; Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue. 
Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote 
mtakacho nanyi mtapewa. 
Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu. 
Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi; Kaeni katika pendo 
langu. 
Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika 
amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. 
Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu 
ikamilike. 
Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi. 
Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya 
rafiki zake. 
Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru. 
Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake; 
Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo 
nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu. 
Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae 
matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho 
kwa jina langu. 
Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni. 
"Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla 
haujawachukia ninyi. 
Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu 
wake; Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka 
ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni. 
Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake; Ikiwa 
wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, 
watalishika na lenu pia. 
Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui 
yeye aliyenituma. 
Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi 
kujitetea kwamba hawana dhambi. 
Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia. 
Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya 
wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, 
wakamchukia na Baba yangu pia. 
Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: [Wamenichukia 
bure!]. 
"Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa 
kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi. 
Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo. 

/16 "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu. 
Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao; Tena, wakati unakuja ambapo kila 
atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu. 
Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi. 
Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba 
niliwaambieni; "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa 
pamoja nanyi. 
Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu 
anayeniuliza: [Unakwenda wapi?]. 
Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu. 
Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana 
nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu; Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu. 
Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, 
uadilifu na hukumu ya Mungu. 
Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini. 
Kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena. 
Kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa. 
"Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. 
Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana 
hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na 
atasema mambo yatakayokuwa yanakuja. 
Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 
Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho 
Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu. 
"Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena 
mtaniona!". 
Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: [Bado 
kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?] 
Tena anasema: [Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"]. 
Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: [Bado kitambo kidogo?] 
Hatuelewi anaongelea nini." 
Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya 
yale niliyosema: [Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo 
kidogo tena mtaniona?]. 
Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: 
mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 
Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; 
lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha 
kwamba mtu amezaliwa duniani. 
Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha 
mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu. 
Siku hiyo hamtaniomba chochote; Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba 
Baba kwa jina langu, atawapeni. 
Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu; Ombeni nanyi mtapata ili furaha 
yenu ikamilike. 
"Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo; Lakini wakati utakuja ambapo sitasema 
tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba. 
Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa 
niaba yenu. 
Maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na 
mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 
Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na 
kurudi kwa Baba." 
Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila 
kutumia mafumbo. 
Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na 
mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu." 
Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa?. 
Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu 
kwake, nami nitaachwa peke yangu; Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana 
Baba yu pamoja nami. 
Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami; 
Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda 
ulimwengu!". 

/17 Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, "Baba, saa 
imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza. 
Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wote 
hao uliompa. 
Na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na 
kumjua Yesu Kristo uliyemtuma. 
Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa nifanye. 
Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa 
ulimwengu. 
"Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani; Walikuwa watu 
wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako. 
Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako. 
Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa nao wameupokea; wanajua kwamba kweli 
nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma. 
"Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea hao ulionipa, maana ni wako. 
Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana ndani 
yao. 
Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni; Baba 
Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe 
kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja. 
Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa; Mimi 
nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule 
aliyelazimika kupotea ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia. 
Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze 
kushiriki kikamilifu furaha yangu. 
Mimi nimewapa neno lako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa 
ulimwengu kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 
Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu. 
Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu. 
Waweke wakfu kwa ukweli; neno lako ni ukweli. 
Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni. 
Na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu 
katika ukweli. 
"Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe 
wao. 
Naomba ili wote wawe kitu kimoja; Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe 
ulivyo ndani yangu nami ndani yako; Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu 
upate kuamini kwamba wewe ulinituma. 
Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi 
tulivyo mmoja. 
Mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu 
kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda 
wao kama unavyonipenda mimi. 
"Baba! Nataka wao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu 
wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu. 
Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua; Hawa nao wanajua kwamba 
wewe ulinituma. 
Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao 
kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao." 

/18 Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, pamoja na 
wanafunzi wake; Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo 
pamoja na wanafunzi wake. 
Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana 
na wanafunzi wake huko. 
Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na 
Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha. 
Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, "Mnamtafuta 
nani?" 
Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu akawaambia, "Mimi ndiye." Msaliti Yuda 
alikuwa amesimama hapo pamoja nao. 
Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi nyuma, wakaanguka chini. 
Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?" Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!". 
Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye; Basi, kama 
mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao." 
(Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: "Wale ulionipa sikumpoteza 
hata mmoja."). 
Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia 
mtumishi wa Kuhani Mkuu; Mtumishi huyo aliitwa Malko. 
Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako alani; Je, nisinywe kikombe 
alichonipa Baba?" 
Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, 
wakamfunga. 
Na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye 
alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo. 
Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja 
afe kwa ajili ya taifa. 
Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu; Huyo mwanafunzi 
mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu 
ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu. 
Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango; Basi, huyo mwanafunzi 
mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, 
mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani. 
Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je, nawe pia ni mmoja wa 
wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si mimi!". 
Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, 
wakawa wanaota moto; Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto. 
Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake. 
Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima hadharani; Kila mara nimefundisha 
katika masunagogi na Hekaluni, mahali wakutanikiapo Wayahudi wote; na wala 
sijasema chochote kwa siri. 
Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia; Wao wanajua 
nilivyosema." 
Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi 
akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?" 
Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema 
vema, mbona wanipiga?" 
Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani Mkuu Kayafa. 
Petro alikuwa hapo akiota moto; Basi, wakamwuliza, "Je, nawe pia si mmoja wa 
wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema, "Si mimi!". 
Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, 
akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?" 
Petro akakana tena; mara jogoo akawika. 
Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu; Ilikuwa alfajiri, 
nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa najisi. 
Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu ya mtu 
huyu?" 
Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako." 
Pilato akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na 
Sheria yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote." 
(Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa kifo 
gani.). 
Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati wewe 
ndiye Mfalme wa Wayahudi?" 
Yesu akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia habari zangu?" 
Pilato akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta 
kwangu; Umefanya nini?" 
Yesu akamjibu, "Ufalme wangu si wa ulimwengu huu; Kama ufalme wangu ungekuwa 
wa ulimwengu huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa 
Wayahudi; Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa." 
Hapo Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu, "Wewe umesema 
kwamba mimi ni Mfalme; Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo 
nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli; Kila mtu wa ukweli 
hunisikiliza." 
Pilato akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha sema hayo, 
aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia yoyote kwake. 
Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka; 
Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?" 
Hapo wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba alikuwa 
mnyang'anyi. 

/19 Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko. 
Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la 
rangi ya zambarau. 
Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: "Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!" 
Wakampiga makofi. 
Pilato akatoka tena nje, akawaambia, "Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua 
kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake." 
Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau; 
Pilato akawaambia, "Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo." 
Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaaza sauti: "Msulubishe! 
Msulubishe!" Pilato akawaambia, "Mchukueni basi, ninyi wenyewe mkamsulubishe, 
kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake." 
Wayahudi wakamjibu, "Sisi tunayo Sheria, na kufuatana na Sheria hiyo, ni 
lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu." 
Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa. 
Basi, akaingia tena ndani ya ikulu, akamwuliza Yesu, "Umetoka wapi wewe?" 
Lakini Yesu hakumjibu neno. 
Hivyo Pilato akamwambia, "Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya 
kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?" 
Yesu akamjibu, "Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu; 
Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi." 
Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi 
wakapiga kelele: "Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu 
anayejifanya kuwa Mfalme humpinga Kaisari!". 
Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha 
hukumu, mahali paitwapo: "Sakafu ya Mawe" (kwa Kiebrania, Gabatha). 
Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka; Pilato akawaambia 
Wayahudi, "Tazameni, Mfalme wenu!". 
Wao wakapaaza sauti: "Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!" Makuhani wakuu wakajibu, 
"Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!". 
Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe; Basi, wakamchukua 
Yesu. 
Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo "Fuvu la 
Kichwa", (kwa Kiebrania Golgotha). 
Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine 
wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye 
Yesu katikati. 
Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba; Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: 
"Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi." 
Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu 
palikuwa karibu na mji; Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, 
Kilatini, na Kigiriki. 
Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, "Usiandike: [Mfalme wa Wayahudi], ila 
[Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi."]. 
Pilato akajibu, "Niliyoandika, nimeandika!". 
Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa 
mafungu manne, fungu moja kwa kila askari; Walichukua pia na kanzu yake; kanzu 
hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono. 
Basi, hao askari wakashauriana: "Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya 
nani." Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: 
"Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura." Basi, ndivyo 
walivyofanya hao askari. 
Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama 
yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene. 
Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi 
aliyempenda, akamwambia mama yake: "Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao." 
Halafu akamwambia yule mwanafunzi: "Tazama, huyo ndiye mama yako." Na tangu 
saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake. 
Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate 
kutimia, akasema, "Naona kiu." 
Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki; Basi, wakachovya sifongo katika hiyo 
siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni. 
Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, "Yametimia!" Kisha akainama kichwa, 
akatoa roho. 
Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio; Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani 
siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi 
walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe. 
Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa 
pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu. 
Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja 
miguu. 
Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji. 
(Naye aliyeona tukio hilo ametoa habari zake ili nanyi mpate kuamini; Na hayo 
aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli.). 
Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: "Hapana hata mfupa wake 
mmoja utakaovunjwa." 
Tena Maandiko mengine yanasema: "Watamtazama yule waliyemtoboa."
Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Armathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya 
kuuchukua mwili wa Yesu; (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, 
maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi); Basi, Pilato akamruhusu; Hivyo Yosefu 
alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu.
Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa 
amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini. 
Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana 
na desturi ya Wayahudi katika kuzika. 
Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo 
kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake. 
Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile 
kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo. 

/20 Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene 
alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi. 
Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu 
alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui 
walikomweka." 
Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini. 
Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi 
kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 
Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani. 
Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda. 
Na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani; Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja 
na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake. 
Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia 
ndani, akaona, akaaamini. 
(Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa 
lazima afufuke kutoka wafu). 
Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani. 
Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia; Huku akiwa bado analia, 
aliinama na kuchungulia kaburini. 
Akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu
ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni. 
Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini unalia?" Naye akawaambia, 
"Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!". 
Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini 
asitambue ya kuwa ni Yesu. 
Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?" Maria, akidhani 
kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, "Mheshimiwa, kama ni wewe 
umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua." 
Yesu akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, 
"Raboni" (yaani "Mwalimu"). 
Yesu akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba; Lakini nenda kwa 
ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na 
Mungu wenu." 
Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona 
Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo. 
Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili; Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja 
ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi 
wa Wayahudi; Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, "Amani kwenu!". 
Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake; Basi, hao 
wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana. 
Yesu akawaambia tena, "Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami 
nawatuma ninyi." 
Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, "Pokeeni Roho Mtakatifu. 
Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi." 
Thoma mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati 
Yesu alipokuja. 
Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, "Tumemwona Bwana." Thoma akawaambia, 
"Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika 
kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki." 
Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na 
Thoma alikuwa pamoja nao; Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, 
akasimama kati yao, akasema, "Amani kwenu!". 
Kisha akamwambia Thoma, "Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete
mkono wako ukautie ubavuni mwangu; Usiwe na mashaka, ila amini!". 
Thoma akamjibu, "Bwana wangu na Mungu wangu!". 
Yesu akamwambia, "Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao 
hawajaona, lakini wameamini." 
Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo 
hazikuandikwa katika kitabu hiki. 
Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa 
Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uzima kwa nguvu ya jina lake. 

/21 Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia; 
Aliwatokea hivi. 
Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, 
wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote 
pamoja. 
Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi 
tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo 
hawakupata chochote. 
Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi 
hawakujua kwamba alikuwa yeye. 
Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, 
"La! Hatujapata kitu." 
Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." 
Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki. 
Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni 
Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa 
amelivaa), akarukia majini. 
Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu 
uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja 
kutoka ukingoni. 
Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa 
samaki na mkate. 
Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua." 
Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa 
umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu; Na ingawa walikuwa wengi 
hivyo wavu haukukatika. 
Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu 
kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana. 
Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki. 
Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka 
kutoka wafu. 
Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, 
wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba 
mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu." 
Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro 
akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza 
kondoo wangu." 
Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro 
akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, 
"Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, 
"Tunza kondoo wangu!. 
Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote 
ulikotaka; Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine 
atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda." 
(Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) 
Kisha akamwambia, "Nifuate." 
Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata 
(Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu 
sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?"). 
Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?" 
Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe 
nifuate mimi." 
Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi; 
Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki 
mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?" 
Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika; Nasi twajua kwamba 
aliyoyasema ni kweli. 
Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja 
baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu 
ambavyo vingeandikwa.